Maisha na Huduma ya Yesu
Kufundisha kwa Mifano
YESU inaonekana yuko Kapernaumu wakati anapokemea Mafarisayo. Baadaye siku hiyo yeye anaondoka katika nyumba ile na kutembea kwenda kwenye Bahari ya Galilaya iliyo karibu, ambako umati wa watu unakusanyika. Kule anapanda mashua, aondoke mbali, anaanza kufundisha watu ufuoni juu ya Ufalme wa mbingu. Anafanya hivyo kupitia mfululizo wa mifano, kila mmoja ukiwa na kikao kinachofahamiwa sana na watu.
Kwanza, Yesu aeleza juu ya mpanzi anaye panda mbegu, mbegu fulani zinaanguka kando ya barabara na kuliwa na ndege. Mbegu nyingine zinaanguka juu ya udongo ambao chini yao pana mwamba. Kwa kuwa mizizi haina kina, mimea ile mipya inanyauka chini ya jua lenye kuichoma sana. Bado mbegu nyingine zinaanguka miongoni mwa miiba, ambayo inaisonga mimea wakati inapotokeza. Hatimaye, mbegu fulani zinaanguka juu ya udongo mzuri na kuzaa mara 100, nyingine mara 60, na nyingine mara 30.
Katika mfano mwingine Yesu anasema Ufalme wa Mungu ni kama wakati mtu anapopanda mbegu. Wakati siku zinapopita, huku mtu yule akiwa amelala na wakati ameamka, mbegu ile inakua. Mtu yule hajui ni jinsi gani. Inakua yenyewe tu na kuzaa nafaka. Wakati nafaka imeiva, mtu yule anaivuna.
Yesu anasimulia mfano wa tatu juu ya mtu anayepanda mbegu ya aina inayofaa, lakini huku yeye akiwa amelala adui anakuja na kupanda magugu miongoni mwa ngano. Watumishi wa mtu yule wanauliza kama inawapasa kung’oa magugu. Lakini yeye anajibu: ‘Hapana, mtang’oa kiasi fulani cha ngano mkifanya hivyo. Acheni vyote viwili vikue pamoja mpaka mavuno. Ndipo mimi nitawaambia wavunaji wachague-chague magugu na kuyateketeza na kuweka ngano katika ghala.’
Akiendelea na hotuba yake kwa umati katika ufuo wa bahari, Yesu anaandaa mifano miwili zaidi. Yeye anaeleza kwamba Ufalme wa mbingu ni kama punje ya haradali ambayo mtu anapanda. Ingawa hiyo ndiyo mbegu iliyo ndogo sana sana kati ya mbegu zote, yeye anasema, inamea na kuwa mboga iliyo kubwa zaidi ya mboga zote. Inakuwa mti ambao ndege wanaendea, wakipata makao miongoni mwa matawi yao.
Watu fulani leo wanapinga wakisema kwamba kuna mbegu zilizo ndogo sana kuliko mbegu za haradali. Lakini Yesu hatoi somo la elimu ya mimea. Kati ya mbegu ambazo Wagalilaya wa siku zake wanafahamu sana, mbegu ya haradali kwa kweli ndiyo iliyo ndogo zaidi ya zote. Kwa hiyo wao wanalithamini jambo la ukuzi wa ajabu sana ambao Yesu anafananisha.
Hatimaye, Yesu analinganisha Ufalme wa mbingu na chachu ambayo mwanamke amechukua na kuchanganya ndani ya vipimo vitatu vikubwa vya unga. Baada ya muda, yeye anasema, chachu hiyo inaenea kila sehemu ya kinyunya.
Baada ya kutoa mifano hiyo mitano, Yesu anaambia umati uende kisha yeye anarudia nyumba anamokaa. Baada ya muda mfupi mitume wake 12 na wengine walio pamoja nao wanaenda huko. Mathayo 13:1-9, 24-36; Marko 4:1-9, 26-32; Luka 8:1-8.
◆ Ni wakati gani na mahali gani ambapo Yesu alinena na umati wa watu kwa mifano?
◆ Ni mifano gani mitano ambayo Yesu aliambia umati?
◆ Kwa sababu gani Kristo akasema mbegu ya haradali ndiyo mbegu iliyo ndogo zaidi ya zote?