Ile Mishnah na Sheria ya Mungu kwa Musa
“TWAANZA na wazo la kwamba twajiunga na mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wakati mrefu juu ya vichwa tusivyoweza kufahamu kamwe . . . Sisi . . . twahisi kana kwamba tumo katika sebule ya wasafiri kwenye uwanja wa ndege ulio mbali sana. Twaelewa maneno wasemayo watu, lakini twatatanishwa na wamaanishayo na mahangaiko yao, zaidi ya yote, twatatanishwa na sauti zao zenye kuhimiza.” Hivyo ndivyo msomi Myahudi Jacob Neusner afafanuavyo hisia ambayo wasomaji huenda wakawa nayo wanaposoma Mishnah kwa mara ya kwanza. Neusner aongeza kusema hivi: “Mishnah haina mwanzo maalumu. Huisha ghafula.”
Katika kichapo A History of Judaism, Daniel Jeremy Silver aiita Mishnah “maandishi muhimu ya Dini ya Kiyahudi ya kirabi.” Kwa hakika, azidi kueleza hivi: “Mishnah ilichukua mahali pa Biblia ikiwa utaratibu mkuu wa masomo wa kuendeleza elimu [ya Kiyahudi].” Kwa nini kitabu chenye mtindo usio dhahiri kama huo kingepata kuwa cha maana hivyo?
Sehemu ya jibu yaweza kupatikana katika taarifa hii iliyotolewa katika Mishnah: “Musa alipokea Torati katika Sinai akaipitisha kwa Yoshua, Yoshua akaipitisha kwa wazee, nao wazee wakaipitisha kwa manabii. Nao manabii wakaipitisha kwa wanaume wa kusanyiko kubwa.” (Avot 1:1) Mishnah hudai kushughulika na habari ambazo Musa alikabidhiwa kwenye Mlima Sinai—sehemu isiyoandikwa ya Sheria ya Mungu kwa Waisraeli. Wanaume wa kusanyiko kubwa (walioitwa Sanhedrini baadaye) walionwa kuwa sehemu ya nasaba ndefu ya wasomi wenye hekima, au watu wenye hekima, waliopitisha kwa mdomo mafundisho fulani kutoka kizazi hadi kizazi mpaka yaliporekodiwa katika Mishnah. Lakini je, jambo hilo ni la hakika? Ni nani kwa hakika aliyeiandika Mishnah, na kwa nini? Je, yaliyomo yalitokana na Musa kwenye Sinai? Je, ina maana kwetu leo?
Dini ya Kiyahudi Bila Hekalu
Itikadi katika sheria ya kimungu ya mdomo iliyotolewa kwa kuongezea Sheria ya Musa iliyoandikwa haikujulikana wakati ambapo Maandiko yalikuwa yakiandikwa chini ya upulizio.a (Kutoka 34:27) Karne nyingi baadaye Mafarisayo walikuwa kile kikundi ndani ya Dini ya Kiyahudi kilichotokeza na kuendeleza dhana hiyo. Karne ya kwanza W.K., Masadukayo na Wayahudi wengine walipinga fundisho hilo lisilo la Kibiblia. Hata hivyo, maadamu hekalu huko Yerusalemu lilikuwa kitovu cha ibada ya Wayahudi, lile suala la sheria ya mdomo lilichukua mahali pa pili. Ibada kwenye hekalu ilikutolea kuwako kwa kila Myahudi muundo na kadiri fulani ya uthabiti.
Ingawa hivyo, mwaka wa 70 W.K., taifa la Kiyahudi lilikabili tatizo kubwa mno la kidini. Yerusalemu liliharibiwa na malejioni ya Roma, na Wayahudi zaidi ya milioni moja wakauawa. Hekalu, kitovu cha maisha yao ya kiroho, halikuwapo tena. Kuishi kulingana na Sheria ya Kimusa, iliyotaka dhabihu na utumishi wa kikuhani hekaluni, kulikuwa jambo lisilowezekana. Jiwe la msingi la Dini ya Kiyahudi lilikuwa limetoweka. Msomi wa Talmud, Adin Steinsaltz aandika hivi: “Ule uharibifu . . . mwaka wa 70 W.K. ulikuwa umefanya kujenga upya mfumo mzima wa maisha ya kidini uwe uhitaji wa hima.” Nao waliujenga upya.
Hata kabla ya kuharibiwa kwa hekalu, Yohanan Ben Zakkai, mwanafunzi aliyestahiwa wa kiongozi wa Kifarisayo, Hillel, alipewa ruhusa na Vespasian (ambaye karibuni angekuwa maliki) ahamishe kitovu cha kiroho cha Dini ya Kiyahudi na Sanhedrini kutoka Yerusalemu hadi Yavneh. Kama vile Steinsaltz aelezavyo, baada ya kuharibiwa kwa Yerusalemu, Yohanan Ben Zakkai “alikabili ugumu wa kuwaanzishia watu kitovu kipya na kuwasaidia wajirekebishe wafaane na hali mpya ambayo ililazimu bidii ya kidini igeuzwe kukaziwa jambo jingine kwa vile sasa Hekalu lilikuwa limetoweka.” Jambo hilo jipya la kukaziwa lilikuwa sheria ya mdomo.
Hekalu likiwa magofu, Masadukayo na mafarakano mengine ya Kiyahudi hayakutoa kibadala chochote chenye kusadikisha. Mafarisayo wakawa dini mashuhuri ya Kiyahudi, ikifyonza vile vikundi vyenye kupinga. Wakikazia muungano, wale marabi mashuhuri walikoma kujiita Mafarisayo, neno lililojaa vidokezi vya kifarakano na vya kufuata mwanadamu. Walikuja kujulikana tu kuwa marabi, “watu wenye hekima wa Israeli.” Watu hao wenye hekima wangebuni mfumo wao wa itikadi ili kuhifadhi dhana yao ya sheria za mdomo. Ungekuwa muundo wa kiroho ambao ungekuwa vigumu zaidi kushambuliwa na wanadamu kuliko vile hekalu.
Kuunganishwa kwa Sheria ya Mdomo
Ijapokuwa chuo cha kirabi katika Yavneh (umbali wa kilometa 40 magharibi ya Yerusalemu) kilikuwa sasa ndicho kitovu kikuu, vyuo vingine vyenye kufundisha sheria ya mdomo vilianza kuchipuka kotekote katika Israeli, na hata katika sehemu za mbali sana kama Babiloni na Roma. Hata hivyo, hilo lilitokeza tatizo. Steinsaltz aeleza hivi: “Maadamu watu wote wenye hekima walikusanyika pamoja, na ile kazi kuu ya usomi ilitekelezwa na kikundi kimoja cha wanaume [huko Yerusalemu], usare wa mapokeo ulihifadhiwa. Lakini ongezeko la walimu na kuanzishwa kwa shule zilizojitenga kulitokeza . . . mifanyizo zaidi na njia zaidi za usemi.”
Walimu wa sheria ya mdomo waliitwa Tannaim, neno ambalo limetokana na neno la msingi la Kiaramu linalomaanisha “kujifunza,” “kurudia,” au kufundisha.” Hilo lilikazia njia yao ya kujifunza na kufundisha sheria ya mdomo kwa kurudia na kukariri kwa juhudi nyingi. Ili kufanya kukariri kwa mapokeo kuwe rahisi, kila sheria au pokeo lilipunguzwa kuwa fungu la maneno mafupi, yenye maelezo machache. Kadiri maneno yalivyokuwa machache zaidi, ndivyo yalivyofaa zaidi. Mtindo wa kuandika wa kishairi ulitafutwa, na mafungu ya maneno yalikaririwa, au kuimbwa. Lakini, sheria hizo zilikosa utaratibu, na zilitofautiana sana kati ya walimu mbalimbali.
Rabi wa kwanza kuyatolea mfanyizo na muundo mahususi mapokeo mengi tofauti-tofauti ya mdomo alikuwa Akiba ben Joseph (karibu 50-135 W.K.). Kumhusu, Steinsaltz aandika hivi: “Watu walioishi siku yake walilinganisha utendaji wake na kazi ya kibarua ambaye huenda shambani na kurundika kikapuni mwake chochote kile apatacho bila utaratibu, kisha hurudi nyumbani na kupanga kila aina peke yake. Akiba alikuwa amejifunza habari nyingi zisizo na utaratibu, akaziainisha katika vikundi mbalimbali.”
Karne ya pili W.K.—miaka zaidi ya 60 baada ya kuharibiwa kwa Yerusalemu—uasi wa pili mkubwa wa Wayahudi dhidi ya Roma uliongozwa na Bar Kokhba. Kwa mara nyingine, uasi ulileta msiba. Akiba na wengi wa wanafunzi wake walikuwa miongoni mwa wahasiriwa milioni moja wa Kiyahudi. Matumaini yoyote ya kujenga upya hekalu yalivunjwa kwa kuwa Maliki Mroma, Hadrian, alitangaza kuwa ilikuwa marufuku Wayahudi kuingia Yerusalemu, ila tu siku ya ukumbusho wa kuharibiwa kwa hekalu.
Tannaim walioishi baada ya Akiba hawakuwa wameona hekalu lililokuwa Yerusalemu. Lakini utaratibu ulioundwa wa kujifunza mapokeo ya sheria ya mdomo ukawa “hekalu” lao, au kitovu chao cha ibada. Kazi iliyoanzishwa na Akiba na wanafunzi wake katika kuimarisha muundo huo wa sheria ya mdomo iliendelezwa na Tannaim wa mwisho, Judah ha-Nasi.
Kilichofanyiza Mishnah
Judah ha-Nasi alikuwa mzao wa Hillel na Gamaliel.b Kwa kuwa alizaliwa wakati wa uasi wa Bar Kokhba, alipata kuwa kiongozi wa jumuiya ya Wayahudi katika Israeli mwishoni mwa karne ya pili na mwanzoni mwa karne ya tatu W.K. Jina la cheo ha-Nasi lamaanisha “mkuu,” likionyesha hadhi aliyokuwa nayo machoni pa Wayahudi wenzake. Mara nyingi yeye hurejezewa kuwa tu Rabi. Judah ha-Nasi aliongoza chuo chake mwenyewe na Sanhedrini, mara ya kwanza katika Bet She’arim na baadaye katika Sepphoris huko Galilaya.
Aking’amua kwamba mapambano ya wakati ujao pamoja na Roma huenda yangehatarisha kule kupitishwa kwa sheria ya mdomo, Judah ha-Nasi aliazimia kuipa muundo ambao ungehakikisha kuhifadhiwa kwake. Aliwakusanya kwenye chuo chake wasomi wenye kutokeza zaidi. Kila hoja na pokeo la sheria ya mdomo zilijadiliwa. Mihtasari ya mazungumzo hayo iliunganishwa kuwa mafungu dhahiri yenye maneno machache ajabu, yakifuata utaratibu wa nadhari ya kishairi ya Kiebrania.
Mihtasari hiyo ilipangwa katika migawanyiko mikubwa sita, au Maagizo, kulingana na vichwa vikuu. Judah aligawanya hayo maagizo tena kuwa sehemu 63, au maandishi. Huo muundo mkubwa wa kiroho ulikuwa sasa umekamilika. Kufikia wakati huo, mapokeo hayo yalikuwa yakipitishwa kwa mdomo. Lakini ikiwa kama kinga ya ziada, hatua ya mwisho ya badiliko kubwa ilichukuliwa—ile ya kuandika kila jambo. Muundo huo mpya na wenye kuvutia ulioandikwa unaohifadhi sheria ya mdomo uliitwa Mishnah. Jina Mishnah hutokana na neno la msingi la Kiebrania sha·nahʹ, linalomaanisha “kurudia,” “kujifunza,” au “kufundisha.” Ni neno lilinganalo na lile la Kiaramu, tenaʼʹ, ambalo hutokeza neno tan·na·ʼimʹ, neno litumiwalo kuhusiana na walimu wa Mishnah.
Kusudi la Mishnah halikuwa kuanzisha muhtasari wa mwisho wa sheria ya Kiyahudi. Ilishughulikia zaidi sheria zisizo za kawaida, ikidhaniwa kwamba msomaji alijua kanuni za msingi. Kwa hakika, ilifanya muhtasari wa yale yaliyozungumziwa na kufundishwa katika vyuo vya kirabi wakati wa Judah ha-Nasi. Mishnah ilikusudiwa kuwa muhtasari wa sheria ya mdomo kwa ajili ya majadiliano zaidi, mfanyizo wa maneno machache, au muundo wa msingi, ili kujenga juu yake.
Badala ya kufunua lolote alilopewa Musa kwenye Mlima Sinai, Mishnah huandaa ufahamu wenye kina juu ya kukua kwa sheria ya mdomo, dhana ambayo ilianza na Mafarisayo. Habari iliyorekodiwa katika Mishnah hutoa nuru juu ya taarifa mbalimbali katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo na juu ya mazungumzo fulani kati ya Yesu Kristo na Mafarisayo. Hata hivyo, kuna uhitaji wa tahadhari kwa sababu mawazo yapatikanayo katika Mishnah hudhihirisha maoni ya Kiyahudi tangu karne ya pili W.K. Mishnah ni daraja kati ya kipindi cha hekalu la pili na Talmud.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi, ona ukurasa wa 8-11 wa ile broshua Je! Ulimwengu Usio na Vita Utakuwako Wakati Wowote?, iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Ona makala “Gamalieli—Alimfundisha Sauli wa Tarso,” katika Mnara wa Mlinzi la Julai 15, 1996.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Migawanyiko ya Mishnah
Mishnah imegawanywa katika Maagizo sita. Hayo yana vitabu vidogo 63, au maandishi, yaliyogawanywa katika sura na mishnayot, au mafungu (si mistari).
1. Zeraim (Sheria za Kilimo)
Maandishi haya hutia ndani mazungumzo juu ya sala zilizotolewa juu ya chakula na kuhusiana na kilimo. Pia yatia ndani sheria juu ya zaka, mafungu ya kikuhani, masazo ya mavuno, na miaka ya Sabato.
2. Moed (Pindi Takatifu, Misherehekeo)
Maandishi ya Agizo hili huzungumzia sheria zinazohusiana na Sabato, Siku ya Kufunika, na misherehekeo mingine.
3. Nashim (Sheria ya Wanawake, ya Ndoa)
Haya ni maandishi yanayozungumzia ndoa na talaka, nadhiri, wanadhiri, na visa vya kushukiwa kufanya uzinzi.
4. Nezikin (Sheria ya Madhara na ya Kiraia)
Maandishi katika Agizo hili huzungumzia habari yenye kuhusiana na sheria ya kiraia na ya rasilimali, mahakama na adhabu, utendaji wa Sanhedrini, ibada ya sanamu, viapo, na Maadili ya Wanaume Wenye Kuongoza (Avot).
5. Kodashim (Dhabihu)
Maandishi haya yazungumzia kanuni zihusianazo na matoleo ya wanyama na ya nafaka na huzungumzia vilevile vipimo vya hekalu.
6. Toharot (Desturi za Utakaso)
Agizo hili lina maandishi yanayozungumzia utakaso wa kidesturi, kuoga, kuosha mikono, maradhi ya ngozi, na uchafu wa vitu tofauti-tofauti.
[Sanduku katika ukurasa wa 28]
Mishnah na Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo
Mathayo 12:1, 2: “Kwenye majira hayo Yesu alienda akipita katikati ya mashamba ya nafaka siku ya sabato. Wanafunzi wake wakaona njaa na kuanza kukwanyua masuke ya nafaka na kula. Kwa kuona hilo Mafarisayo wakamwambia: ‘Tazama! Wanafunzi wako wanafanya lisiloruhusika kisheria kufanya siku ya sabato.’” Maandiko ya Kiebrania hayakatazi walilofanya wanafunzi wa Yesu. Lakini katika Mishnah twapata orodha ya utendaji mbalimbali 39 uliokatazwa na marabi siku ya Sabato.—Shabbat 7:2.
Mathayo 15:3: “Kwa kujibu [Yesu] akawaambia: ‘Ni kwa nini nyinyi pia hukiuka amri ya Mungu kwa sababu ya mapokeo yenu?’” Mishnah huthibitisha jambo hilo. (Sanhedrin 11:3) Twasoma hivi: “Mkazo mkubwa watiwa katika [kushika] maneno ya Waandishi kuliko katika [kushika] maneno ya Sheria [iliyoandikwa]. Ikiwa mtu alisema, ‘Hakuna wajibu wa kuvaa tepe hivi kwamba akiuka maneno ya Sheria, hastahili lawama; [lakini ikiwa alisema], ‘Zapaswa kuwa na migawanyiko mitano,’ hivi kwamba aongezea maneno ya Waandishi, astahili lawama.”—The Mishnah, cha Herbert Danby, ukurasa wa 400.
Waefeso 2:14: “Yeye [Yesu] ni amani yetu, yeye aliyefanya vile vikundi viwili vya watu kuwa kimoja na kuharibu ukuta wa katikati uliowatenganisha kwa ua.” Mishnah husema hivi: “Ndani ya jengo la Temple Mount palikuwa na ukuta wenye waya zilizokingamana, (Soreg), wenye urefu wa upana kumi wa mkono [sentimeta 74].” (Middot 2:3) Wasio Wayahudi walikatazwa kupita sehemu hiyo na kuingia katika nyua za ndani zaidi. Huenda ikawa mtume Paulo alirejezea ukuta huo katika njia ya kitamathali alipowaandikia Waefeso mwaka wa 60 au 61 W.K., ulipokuwa bado ukisimama. Huo ukuta wa mfano ulikuwa agano la Sheria, ambalo lilikuwa limetenganisha Wayahudi na Wasio Wayahudi kwa muda mrefu. Hata hivyo, kwa msingi wa kifo cha Kristo mwaka wa 33 W.K., ukuta huo ulibatilishwa.