Sura ya 10
Ahadi ya Mkuu wa Amani
1. Wanadamu wamekabili nini tangu wakati wa Kaini?
MIAKA ipatayo elfu sita iliyopita, mtoto wa kwanza wa kibinadamu alizaliwa. Jina lake Kaini, na kuzaliwa kwake kulikuwa tukio la pekee. Wazazi wake, wala malaika, wala hata Muumba hawakuwa wameona mtoto wa kibinadamu. Kitoto hicho kilichozaliwa karibuni kingaliweza kuiletea tumaini jamii ya kibinadamu iliyohukumiwa adhabu. Basi lilikuwa jambo lenye kuvunja moyo kama nini, baada ya kuwa mtu mzima, akawa muuaji kimakusudi! (1 Yohana 3:12) Tangu wakati huo wanadamu wameshuhudia mauaji mengine mengi mno. Wanadamu, wenye hali ya kuelekea kutenda mabaya, hawana amani kati yao wenyewe wala kati yao na Mungu.—Mwanzo 6:5; Isaya 48:22.
2, 3. Yesu Kristo alifungua mataraja gani, nasi lazima tufanye nini ili kupokea baraka hizo?
2 Miaka elfu nne hivi baada ya kuzaliwa kwa Kaini, mtoto mwingine alizaliwa. Aliitwa Yesu, na kuzaliwa kwake pia kulikuwa tukio la pekee. Alizaliwa na bikira, kwa nguvu ya roho takatifu—katika historia yote, yeye peke yake ndiye aliyezaliwa hivyo. Alipozaliwa, umati wa malaika wenye shangwe walimwimbia Mungu sifa, wakisema: “Utukufu katika mahali pa juu kwa Mungu, na juu ya dunia amani miongoni mwa watu wa nia njema.” (Luka 2:13, 14) Yesu hakuwa muuaji hata kidogo, bali aliwawezesha wanadamu kuwa na amani pamoja na Mungu na kupata uhai udumuo milele.—Yohana 3:16; 1 Wakorintho 15:55.
3 Isaya alitabiri kuwa Yesu angeitwa “Mkuu wa Amani.” (Isaya 9:6, NW) Angetoa uhai wake mwenyewe kwa niaba ya wanadamu, hivyo akifanya msamaha wa dhambi uwezekane. (Isaya 53:11) Leo, amani pamoja na Mungu na msamaha wa dhambi zaweza kupatikana kwa msingi wa imani katika Yesu Kristo. Lakini baraka hizo haziji pasipo jitihada. (Wakolosai 1:21-23) Wanaozitaka sharti wajifunze kumtii Yehova Mungu. (1 Petro 3:11; linganisha Waebrania 5:8, 9.) Katika siku ya Isaya, Israeli na Yuda zafanya kinyume kabisa.
Kugeukia Roho Waovu
4, 5. Mambo yakoje katika siku ya Isaya, na wengine wamgeukia nani?
4 Kwa sababu ya kutotii kwao, watu wa siku ya Isaya wamo katika hali mbaya sana ya kiadili, shimo kubwa lenye giza la kiroho. Hata ufalme wa kusini wa Yuda, liliko hekalu la Mungu, hauna amani. Watu wa Yuda wametishwa na uvamizi wa Waashuri, na nyakati ngumu zawakabili, hayo yakiwa matokeo ya ukosefu wao wa uaminifu. Je, watafute msaada kwa nani? Kwa kusikitisha, wengi wamgeukia Shetani, wala si Yehova. Hasha! hawamwombi Shetani kwa jina. Badala yake, kama vile Mfalme Sauli wa zamani, wao wanawasiliana na roho, wakitafuta utatuzi wa matatizo yao kwa kujaribu kuwasiliana na wafu.—1 Samweli 28:1-20.
5 Hata wengine wao wanachangia kusitawi kwa zoea hilo. Isaya ataja uasi huo asemapo: “Wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi [“wawasiliani-roho au kwa wale wenye roho ya kutabiri,” “NW”]; waliao kama ndege na kunong’ona; je! haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? je! waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?” (Isaya 8:19) Wawasiliani-roho waweza kuhadaa watu, “[wakilia] kama ndege na kunong’ona.” Sauti hizo zisemwazo eti ni za roho za wafu, zaweza kutolewa na mwasiliani-roho aliye hai afanyaye ionekane kana kwamba zatokana na wafu. Ingawa hivyo, nyakati nyingine huenda roho waovu wakahusika moja kwa moja na kujifanya kuwa wafu, kama ambavyo huenda ilitukia Sauli alipotafuta habari kwa mchawi wa Endori.—1 Samweli 28:8-19.
6. Sababu gani Waisraeli ambao wamegeukia uwasiliani-roho ndio hasa wanaostahili kulaumiwa?
6 Mambo hayo yote yanatendeka katika Yuda licha ya kwamba Yehova amekataza zoea la kuwasiliana na roho. Chini ya Sheria ya Kimusa, ni kosa linalostahili kifo. (Mambo ya Walawi 19:31; 20:6, 27; Kumbukumbu la Torati 18:9-12) Kwa nini watu wa pekee wa Yehova wakiuka sheria kwa njia mbaya hivyo? Kwa sababu wameikataa Sheria ya Yehova na shauri lake nao ‘wamefanywa kuwa wagumu kwa nguvu ya udanganyifu ya dhambi.’ (Waebrania 3:13) “Mioyo yao imenenepa kama shahamu,” nao wametengwa na Mungu wao.—Zaburi 119:70.a
7. Wengi leo huigaje Waisraeli wa siku ya Isaya, na wakati ujao wa watu hao utakuwaje wasipotubu?
7 Labda wao wafikiri hivi, ‘Kwani Sheria ya Yehova ina faida gani tukabilipo shambulio la Waashuri hivi karibuni?’ Wanataka utatuzi wa haraka na ulio rahisi kwa msiba wao nao hawana nia ya kumngojea Yehova afanye mapenzi yake. Katika siku yetu pia, wengi huipuuza sheria ya Yehova na kugeukia wawasiliani-roho, nyota, na namna nyingine za mafumbo ili watatue matatizo yao. Hata hivyo, ni upumbavu kwa walio hai leo kutafuta majibu kwa wafu, kama vile ilivyokuwa zamani. Wakati ujao wa yeyote anayezoea mambo hayo bila kutubu utakuwa na “wauaji-kimakusudi na waasherati na . . . waabudu-sanamu na waongo wote.” Hawana matazamio yoyote ya kuishi wakati ujao.—Ufunuo 21:8.
“Sheria na Ushuhuda” wa Mungu
8. Ni nini “sheria na ushuhuda” tunazopaswa kuziendea leo ili kupata mwelekezo?
8 Sheria ya Yehova inayopiga marufuku uwasiliani-roho, pamoja na amri zake nyingine, haijafichika katika Yuda. Imehifadhiwa kwa maandishi. Leo Neno lake lililokamilika lapatikana kwa maandishi. Neno hilo ni Biblia, ambayo ina mkusanyo wa sheria na kanuni za Mungu na vilevile masimulizi ya jinsi Mungu alivyoshughulika na watu. Masimulizi hayo ya Biblia ya shughuli za Yehova huandaa ushuhuda, au uthibitisho, unaotufundisha utu na sifa za Yehova. Badala ya kuwaendea wafu, Waisraeli wapaswa kutafuta mwelekezo kutoka wapi? Isaya ajibu: “Kwa sheria na ushuhuda”! (Isaya 8:20a) Naam, wale wanaotaka ujuzi wa kweli wapaswa kuligeukia Neno la Mungu lililoandikwa.
9. Je, watenda-dhambi wasiotubu watapata faida yoyote kwa kunukuu Biblia mara kwa mara?
9 Huenda baadhi ya Waisraeli wanaopendezwa na uwasiliani-roho wakadai kuwa wanalistahi Neno la Mungu lililoandikwa. Lakini hayo ni madai tu nayo ni ya kinafiki. Isaya asema: “Ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” (Isaya 8:20b) Isaya arejezea neno gani hapa? Labda kwa neno: “Kwa sheria na ushuhuda.” Labda baadhi ya Waisraeli waasi-imani wanalirejezea Neno la Mungu, kama vile huenda waasi-imani na wengine leo wakanukuu Andiko. Lakini hayo ni maneno matupu tu. Kunukuu Andiko hakutatokeza “asubuhi [“nuru ya alfajiri,” NW],” au nuru ya Yehova, iwapo hakuandamani na kutenda mapenzi ya Yehova na kukataa mazoea yasiyo safi.b
“Si Njaa ya Kukosa Chakula”
10. Watu wa Yuda wanatesekaje kwa sababu ya kumkataa Yehova?
10 Kutomtii Yehova husababisha giza la akili. (Waefeso 4:17, 18) Watu wa Yuda wamekuwa vipofu kiroho, hawana uelewevu. (1 Wakorintho 2:14) Isaya afafanua hali yao: “Watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa.” (Isaya 8:21a) Kwa sababu taifa hilo limekosa uaminifu—hasa wakati wa utawala wa Mfalme Ahazi—kuendelea kwa Yuda ikiwa ufalme ulio huru kumetishwa. Adui wamelizingira taifa hilo. Jeshi la Ashuru lashambulia majiji ya Yuda, moja baada ya jingine. Adui aharibu nchi yenye kuzaa, hali inayotokeza uhaba wa chakula. Wengi “wamedhikika sana na kuwa na njaa.” Lakini njaa ya aina nyingine yaikumba nchi. Makumi kadhaa ya miaka mapema, Amosi alitabiri: “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA.” (Amosi 8:11) Yuda sasa yadhikika kwa njaa ya kiroho kama hiyo!
11. Je, Yuda itajifunza kutokana na nidhamu inayopokea?
11 Je, Yuda itajifunza na kumrudia Yehova? Je, watu wake wataacha kuwasiliana na roho na kuabudu sanamu nao warudi “kwa sheria na ushuhuda”? Yehova aona kimbele itikio lao: “Na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa [“kumlaani,” “BHN”] kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu.” (Isaya 8:21b) Naam, wengi watamlaumu mfalme wao wa kibinadamu kwa kuwasababishia hali hiyo. Hata wengine, kwa upumbavu, watamlaumu Yehova kwa maafa yao! (Linganisha Yeremia 44:15-18.) Leo, wengi huitikia vivyo hivyo, wakimlaumu Mungu kwa misiba isababishwayo na uovu wa binadamu.
12. (a) Kumwacha Mungu kumeleta nini kwa Yuda? (b) Ni maswali gani muhimu yanayozushwa?
12 Je, kumlaani Mungu kutawaletea wakazi wa Yuda amani? La. Isaya atabiri: “Wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapana changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.” (Isaya 8:22) Baada ya kuinua macho yao mbinguni ili wamlaumu Mungu, warudi kuiangalia nchi, wayarudia matazamio yao yasiyo na matumaini. Kumwacha kwao Mungu kumeleta maafa. (Mithali 19:3) Hata hivyo, namna gani juu ya ahadi za Mungu kwa Abrahamu, Isaka, na Yakobo? (Mwanzo 22:15-18; 28:14, 15) Je, Yehova atazipuuza? Je, Waashuri au mamlaka nyingine ya kijeshi zitakomesha nasaba ya kifalme waliyoahidiwa Yuda na Daudi? (Mwanzo 49:8-10; 2 Samweli 7:11-16) Je, Waisraeli watahukumiwa adhabu ya kukaa gizani milele?
Nchi ‘Yadharauliwa’
13. “Galilaya ya mataifa” ni nini, nayo yajaje “kudharauliwa”?
13 Isaya sasa agusia tukio moja kati ya matukio yenye maafa makubwa zaidi yanayowakumba wazao wa Abrahamu: “Yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.” (Isaya 9:1) Galilaya ni eneo katika ufalme wa kaskazini wa Israeli. Katika unabii wa Isaya eneo hilo latia ndani “nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali” na pia “njia ya bahari,” ambayo ni njia ya zamani iliyokuwa kandokando ya Bahari ya Galilaya na kufika kwenye Bahari ya Mediterania. Katika siku ya Isaya, eneo hilo laitwa “Galilaya ya mataifa,” labda kwa sababu wakazi katika mengi ya majiji yake ni watu wasio Waisraeli.c Nchi hiyo ‘yadharauliwaje’? Waashuri wapagani waishinda, wawapeleka Waisraeli uhamishoni, na kuleta wakazi wapagani katika eneo hilo, ambao si wazao wa Abrahamu. Basi ufalme wa kaskazini wa makabila kumi watoweka katika historia, na kutokuwa taifa dhahiri tena!—2 Wafalme 17:5, 6, 18, 23, 24.
14. “Dhiki” ya Yuda itakuwaje nyepesi kuliko ile ya ufalme wa makabila kumi?
14 Yuda pia imesongwa na Waashuri. Je, itatokomea katika “dhiki” kama ule ufalme wa makabila kumi uliowakilishwa na Zabuloni na Naftali? La. Katika “zamani za mwisho,” Yehova ataleta baraka katika eneo la ufalme wa kusini wa Yuda na hata katika nchi ambayo hapo awali ilitawaliwa na ufalme wa kaskazini. Jinsi gani?
15, 16. (a) Wakati unaoitwa “zamani za mwisho” ambapo hali itabadilika kwa “wilaya za Zebuloni na Naftali” ni upi? (b) Nchi iliyodharauliwa yapata kuheshimiwaje?
15 Mtume Mathayo ajibu swali hilo katika rekodi yake iliyopuliziwa ihusuyo huduma ya Yesu duniani. Akifafanua siku za mwanzo za huduma hiyo, Mathayo asema: “Baada ya kuondoka Nazareti, [Yesu] alikuja na kufanya makao katika Kapernaumu kando ya bahari katika wilaya za Zebuloni na Naftali, ili kupate kutimizwa lile lililosemwa kupitia Isaya nabii, akisema: ‘Ewe nchi ya Zebuloni na nchi ya Naftali, kando ya barabara ya bahari, katika upande ule mwingine wa Yordani, Galilaya ya mataifa! watu wenye kuketi katika giza waliona nuru kubwa, na kwa habari ya wale wenye kuketi katika mkoa wa kivuli cha kifo, nuru iliwazukia.’”—Mathayo 4:13-16.
16 Naam, “zamani za mwisho” alizotabiri Isaya ni wakati wa huduma ya Kristo duniani. Yesu alitumia wakati mwingi wa maisha yake duniani akiwa Galilaya. Alianza huduma yake katika wilaya ya Galilaya na kutangaza: “Ufalme wa mbingu umekaribia.” (Mathayo 4:17) Huko Galilaya, alitoa Mahubiri ya Mlimani yaliyo maarufu sana, akawachagua mitume wake, akafanya mwujiza wake wa kwanza, na kuonekana kwa wafuasi wapatao 500 baada ya ufufuo wake. (Mathayo 5:1–7:27; 28:16-20; Marko 3:13, 14; Yohana 2:8-11; 1 Wakorintho 15:6) Hivyo, Yesu alitimiza unabii wa Isaya kwa kuitukuza “nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali.” Bila shaka, Yesu hakuhudumia watu wa Galilaya peke yao. Kwa kuhubiri habari njema nchini kote, Yesu ‘alilifanya kuwa tukufu’ taifa lote la Israeli, kutia ndani Yuda.
“Nuru Kuu”
17. “Nuru kuu” yaangazaje katika Galilaya?
17 Hata hivyo, namna gani kuhusu mtajo wa Mathayo juu ya “nuru kubwa” katika Galilaya? Huo pia ulinukuliwa katika unabii wa Isaya. Isaya aliandika: “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza.” (Isaya 9:2) Kufikia karne ya kwanza W.K., nuru ya ile kweli ilikuwa imefichwa na mambo ya kipagani yasiyo ya kweli. Wayahudi waliokuwa viongozi wa kidini walikuwa wamelizidisha tatizo hilo kwa kushikilia mapokeo yao ya kidini ‘yaliyolibatilisha neno la Mungu.’ (Mathayo 15:6) Wanyenyekevu walionewa na kutatanishwa, huku wakifuata “viongozi vipofu.” (Mathayo 23:2-4, 16) Yesu Mesiya alipokuja, macho ya watu wengi wanyenyekevu yalifunguliwa kiajabu. (Yohana 1:9, 12) Kazi ya Yesu akiwa duniani na baraka zilizotokana na dhabihu yake zafananishwa ipasavyo na “nuru kuu” katika unabii wa Isaya.—Yohana 8:12.
18, 19. Kwa nini wale walioitikia nuru walikuwa na shangwe kuu?
18 Wale walioitikia nuru hiyo walikuwa na sababu nyingi za kufurahi. Isaya aliendelea: “Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, kama furaha ya wakati wa mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara.” (Isaya 9:3) Kuhubiri kwa Yesu na kule kwa wafuasi wake kulitokeza wenye moyo wa haki, walioonyesha hamu ya kumwabudu Yehova kwa roho na kweli. (Yohana 4:24) Katika muda unaopungua miaka minne, umati ulikubali Ukristo. Elfu tatu walibatizwa katika siku ya Pentekoste mwaka wa 33 W.K. Muda mfupi baadaye, “idadi ya wanaume ikawa karibu elfu tano.” (Matendo 2:41; 4:4) Wanafunzi walipozidi kudhihirisha nuru kwa bidii, “idadi ya wanafunzi ikafuliza kuzidi sana katika Yerusalemu; na umati mkubwa wa makuhani ukaanza kuwa mtiifu kwa imani.”—Matendo 6:7.
19 Sawa na wale wanaoshangilia kupata mavuno mengi au wanaofurahia kugawanya nyara yenye thamani baada ya ushindi mkubwa wa kijeshi, wafuasi wa Yesu walishangilia kwa sababu ya ongezeko. (Matendo 2:46, 47) Baadaye, Yehova aliifanya nuru ing’ae katika mataifa. (Matendo 14:27) Kwa hiyo watu wa jamii mbalimbali wakashangilia kwa sababu njia ya kumkaribia Yehova ilikuwa imefunguliwa kwao.—Matendo 13:48.
“Kama Katika Siku ya Midiani”
20. (a) Wamidiani walithibitikaje kuwa adui za Israeli, na Yehova alikomeshaje tisho lao? (b) Yesu atakomeshaje tisho la adui za watu wa Mungu “katika siku ya Midiani” ya wakati ujao?
20 Matokeo ya utendaji wa Mesiya ni ya kudumu, kama tuonavyo katika maneno yafuatayo ya Isaya: “Umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani.” (Isaya 9:4) Karne kadhaa kabla ya siku ya Isaya, Wamidiani walipanga njama na Wamoabi ili kushawishi Israeli watende dhambi. (Hesabu 25:1-9, 14-18; 31:15, 16) Baadaye, Wamidiani waliwatisha Waisraeli kwa kuvamia na kupora vijiji na mashamba yao kwa miaka saba. (Waamuzi 6:1-6) Ndipo Yehova, kupitia Gideoni mtumishi wake, akayashinda kabisa majeshi ya Midiani. Baada ya “siku [hiyo] ya Midiani,” hakuna uthibitisho uonyeshao kuwa watu wa Yehova waliteseka tena mikononi mwa Wamidiani. (Waamuzi 6:7-16; 8:28) Katika wakati ujao ulio karibu, Yesu Kristo, Gideoni mkuu, atawatwanga na kuwaua adui za watu wa Yehova leo. (Ufunuo 17:14; 19:11-21) Kisha, “kama katika siku ya Midiani,” ushindi kamili na udumuo milele utapatikana kwa nguvu za Yehova, wala si kwa uwezo wa binadamu. (Waamuzi 7:2-22) Watu wa Mungu hawatateseka tena kamwe chini ya nira ya uonevu!
21. Unabii wa Isaya waonyesha nini juu ya wakati ujao wa vita?
21 Wonyesho wa nguvu za Mungu si utukuzaji wa vita. Yesu aliyefufuliwa ndiye Mkuu wa Amani, naye ataleta amani ya milele kwa kuwaharibu adui zake. Isaya sasa asema juu ya zana za kijeshi kuharibiwa kabisa kwa moto: “Silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo [“kila buti ya akanyagaye kwa mtetemo,” “NW”], na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni.” (Isaya 9:5) Mitetemo inayosababishwa na kukanyaga kwa buti za wanajeshi walio mwendoni haitasikika tena kamwe. Yunifomu zenye damu za askari waliozoea vita hazitaonekana tena. Vita havitakuwapo tena kamwe!—Zaburi 46:9.
“Mshauri wa Ajabu”
22. Katika kitabu cha Isaya, Yesu apewa jina gani la unabii lenye maana nyingi?
22 Wakati wa kuzaliwa kwake kimwujiza, yeye aliyezaliwa ili awe Mesiya alipewa jina Yesu, limaanishalo “Yehova Ni Wokovu.” Lakini anayo majina mengine pia, majina ya unabii yanayoonyesha jukumu lake muhimu na cheo chake cha juu. Jina moja kati ya hayo ni Imanueli, limaanishalo “Pamoja Nasi Yuko Mungu.” (Isaya 7:14; linganisha Mathayo 1:23.) Isaya sasa afafanua jina jingine la unabii: “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme [“Mkuu,” “NW”] wa amani.” (Isaya 9:6) Fikiria maana kamili ya jina hilo la unabii lenye sehemu nyingi.
23, 24. (a) Yesu ni “Mshauri wa ajabu” kwa njia gani? (b) Washauri Wakristo leo waweza kuigaje kielelezo cha Yesu?
23 Mshauri ni mtu anayetoa shauri. Yesu Kristo alitoa mashauri ya ajabu alipokuwa duniani. Twasoma katika Biblia kuwa “umati ulishangaa juu ya njia yake ya kufundisha.” (Mathayo 7:28) Yeye ni Mshauri mwenye hekima na hisia-mwenzi, anayeelewa hali ya binadamu kwa njia ya pekee. Shauri lake si la kukemea na kutia adabu tu. Mara nyingi, hilo hutolewa kwa namna ya mafundisho na shauri lenye upendo. Shauri la Yesu ni la ajabu kwa sababu sikuzote lina hekima, ni kamilifu, nalo halina makosa. Lifuatwapo, huongoza kwenye uhai udumuo milele.—Yohana 6:68.
24 Shauri la Yesu halitokani tu na akili zake nyingi. Badala yake, asema: “Kile nifundishacho si changu, bali ni chake yeye aliyenituma.” (Yohana 7:16) Kama ilivyokuwa kwa habari ya Solomoni, Yehova Mungu ndiye Chanzo cha hekima ya Yesu. (1 Wafalme 3:7-14; Mathayo 12:42) Kielelezo cha Yesu chapasa kuwachochea walimu na washauri katika kutaniko la Kikristo kutegemeza mafundisho yao kwa Neno la Mungu sikuzote.—Mithali 21:30.
“Mungu Mwenye Nguvu” na “Baba wa Milele”
25. Jina “Mungu mwenye nguvu” latufahamisha nini juu ya Yesu wa mbinguni?
25 Yesu pia ni “Mungu mwenye nguvu” na “Baba wa milele.” Haimaanishi kuwa ananyakua mamlaka na cheo cha Yehova, aliye “Mungu Baba yetu.” (2 Wakorintho 1:2) Yesu “hakufikiria upokonyaji, yaani, kwamba yeye awe sawa na Mungu.” (Wafilipi 2:6) Yeye anaitwa Mungu Mwenye Nguvu, wala si Mungu Mweza Yote. Yesu hakujifanya kamwe kuwa Mungu Mweza Yote, kwa maana alisema kuhusu Baba yake kuwa “Mungu pekee wa kweli,” yaani, Mungu pekee apaswaye kuabudiwa. (Yohana 17:3; Ufunuo 4:11) Katika Maandiko, neno “mungu” laweza kumaanisha “mwenye uweza” au “mwenye nguvu.” (Kutoka 12:12; Zaburi 8:5; 2 Wakorintho 4:4) Kabla hajaja duniani, Yesu alikuwa “mungu,” “akiwako katika umbo la Mungu.” Baada ya ufufuo wake, alirudi kwenye cheo cha juu hata zaidi huko mbinguni. (Yohana 1:1; Wafilipi 2:6-11) Isitoshe, jina “mungu” lina maana nyingine zaidi. Waamuzi katika Israeli waliitwa “miungu”—wakati mmoja Yesu mwenyewe aliwaita hivyo. (Zaburi 82:6; Yohana 10:35) Yehova amemteua Yesu kuwa Hakimu, ambaye “akusudiwa kuhukumu walio hai na wafu.” (2 Timotheo 4:1; Yohana 5:30) Kwa wazi, yeye aitwa ipasavyo Mungu Mwenye Nguvu.
26. Kwa nini Yesu aweza kuitwa “Baba wa milele”?
26 Jina la cheo “Baba wa milele” larejezea nguvu na mamlaka ya Mfalme wa Kimesiya ya kuwapa binadamu tazamio la uhai wa milele duniani. (Yohana 11:25, 26) Urithi wa mzazi wetu wa kwanza, Adamu, ulikuwa kifo. Yesu, Adamu wa mwisho, “akawa roho ipayo uhai.” (1 Wakorintho 15:22, 45; Waroma 5:12, 18) Kama vile Yesu, Baba wa Milele, atakavyoishi milele, ndivyo wanadamu watiifu watakavyofurahia milele manufaa ya ubaba wake.—Waroma 6:9.
‘Mkuu wa Amani’
27, 28. Raia za ‘Mkuu wa amani’ wanapata manufaa gani za ajabu wakati huu na hata wakati ujao pia?
27 Mbali na uhai udumuo milele, mwanadamu pia huhitaji amani, pamoja na Mungu na vilevile pamoja na mwanadamu mwenzake. Hata leo, wale wanaojitiisha kwa utawala wa ‘Mkuu wa amani’ ‘wamefua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.’ (Isaya 2:2-4) Wao hawaweki chuki kwa sababu ya tofauti za kisiasa, kijamii, kiuchumi, au za maeneo. Wameungana katika ibada ya Mungu mmoja wa kweli, Yehova, nao hujitahidi kudumisha uhusiano wa amani pamoja na jirani zao, ndani na vilevile nje ya kutaniko.—Wagalatia 6:10; Waefeso 4:2, 3; 2 Timotheo 2:24.
28 Kwa wakati wa Mungu uliowekwa, Kristo ataleta amani thabiti, yenye kudumu na kuenea kotekote duniani. (Matendo 1:7) “Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe, katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; kuuthibitisha na kuutegemeza kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele.” (Isaya 9:7a) Yesu hatatumia njia za kimabavu ili kudhihirisha mamlaka yake akiwa Mkuu wa Amani. Raia zake hawatanyang’anywa hiari yao na kukandamizwa. Badala yake, yote atakayotekeleza yatakuwa “kwa hukumu na kwa haki.” Ni badiliko lenye kuburudisha kama nini!
29. Twapaswa kufanya nini iwapo twataka kufurahia baraka ya amani idumuyo milele?
29 Kwa kuzingatia maana ya ajabu ya jina la Yesu la unabii, umalizio wa Isaya kwa sehemu hii ya unabii wake unasisimua kwelikweli. Aandika: “Wivu [“Bidii,” “NW”] wa BWANA wa majeshi ndio utakaotenda hayo.” (Isaya 9:7b) Naam, Yehova hutenda kwa bidii. Hafanyi jambo lolote shingo upande. Twaweza kuwa na hakika ya kwamba lolote aahidilo, atalitimiza kikamili. Iwapo yeyote atamani kufurahia amani idumuyo milele, basi na amtumikie Yehova kwa moyo wote. Sawa na Yehova Mungu na Yesu, Mkuu wa Amani, watumishi wote wa Mungu na wawe “wenye bidii kwa kazi zilizo bora.”—Tito 2:14.
[Maelezo ya Chini]
a Wengi huamini kuwa Zaburi 119 iliandikwa na Hezekia kabla hajawa mfalme. Ikiwa hivyo, labda iliandikwa Isaya akiwa bado anatoa unabii.
b Usemi, “neno hili” katika Isaya 8:20 labda warejezea neno linalohusu wawasiliani-roho, lililonukuliwa katika Isaya 8:19. Ikiwa ndivyo ilivyo, Isaya amaanisha kwamba watu wanaochangia kusitawi kwa uwasiliani-roho katika Yuda wataendelea kuwasihi wengine waende kwa wawasiliani-roho na hivyo wasipate nuru ya Yehova.
c Wengine wamedokeza kuwa labda wakazi wa yale majiji 20 ya Galilaya ambayo Mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro hawakuwa Waisraeli.—1 Wafalme 9:10-13.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 122]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Korazini
Bethsaida
Kapernaumu
Uwanda wa Genesareti
Bahari ya Galilaya
Magadani
Tiberiasi
Mto Yordani
GADARA
Gadara
[Picha katika ukurasa wa 119]
Kuzaliwa kwa Kaini na kwa Yesu pia yalikuwa matukio ya pekee sana. Kule kuzaliwa kwa Yesu tu ndiko kulikokuwa na mwisho wenye furaha
[Picha katika ukurasa wa 121]
Kutakuwa na njaa iliyo mbaya sana kuliko ile njaa ya kukosa chakula na kiu ya kukosa maji
[Picha katika ukurasa wa 127]
Yesu alikuwa nuru nchini