SURA YA 22
Wanafunzi Wanne Watakuwa Wavuvi wa Watu
MATHAYO 4:13-22 MARKO 1:16-20 LUKA 5:1-11
YESU AWAITA WANAFUNZI WAANDAMANE NAYE WAKATI WOTE
WAVUVI WA SAMAKI WANAKUWA WAVU VI WA WATU
Baada ya watu wa Nazareti kujaribu kumuua Yesu, anahamia katika jiji la Kapernaumu, karibu na Bahari ya Galilaya, ambayo pia inaitwa “ziwa la Genesareti.” (Luka 5:1) Hilo linatimiza unabii wa kitabu cha Isaya kwamba watu wa Galilaya wanaokaa kando ya bahari wangeona nuru kuu.—Isaya 9:1, 2.
Naam, huko Galilaya, Yesu anaendelea kutangaza kwamba “Ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mathayo 4:17) Yesu anawakuta wanne kati ya wanafunzi wake. Hapo awali walikuwa wamesafiri pamoja naye, lakini waliporudi pamoja na Yesu kutoka Yudea, walirudia biashara yao ya kuvua samaki. (Yohana 1:35-42) Hata hivyo, sasa wanapaswa kuwa pamoja na Yesu wakati wote ili awazoeze kuendeleza huduma baada ya yeye kuondoka.
Yesu anapotembea kando ya bahari anamwona Simoni Petro, ndugu yake Andrea, na wavuvi wenzao wakitengeneza nyavu zao. Yesu anawakaribia, anaingia katika mashua ya Petro, na kumwomba asogee mbali na nchi kavu. Wanaposonga mbali kidogo na nchi kavu, Yesu anaketi na kuanza kufundisha umati uliokuwa umekusanyika ufuoni kuhusu Ufalme.
Baadaye, Yesu anamwambia Petro: “Peleka mashua mahali penye kina, kisha mshushe nyavu zenu, mvue samaki.” Petro anamjibu: “Mwalimu, tumejitahidi kuvua samaki usiku wote na hatukupata chochote, lakini nitazishusha nyavu kama ulivyoniagiza.”—Luka 5:4, 5.
Wanashusha nyavu na kuvua samaki wengi sana hivi kwamba nyavu zinaanza kukatika! Mara moja, wanaume hao wanawapungia mkono wenzao walio katika mashua iliyo hapo karibu ili waje kuwasaidia. Baada ya muda mfupi mashua zote mbili zinajaa samaki wengi sana hivi kwamba zinaanza kuzama. Petro anapoona hivyo, anaanguka mbele za Yesu na kusema: “Bwana ondoka kwangu, kwa sababu mimi ni mtu mwenye dhambi.” Yesu anamwambia: “Acha kuogopa. Kuanzia sasa utakuwa ukiwavua watu wakiwa hai.”—Luka 5:8, 10.
Yesu anawaambia Petro na Andrea: “Nifuateni, nami nitawafanya muwe wavuvi wa watu.” (Mathayo 4:19) Pia, anawaita wavuvi wengine wawili, Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo. Wao pia wanakubali bila kusitasita. Basi, wanaume hao wanne wanaacha biashara yao ya kuvua samaki na kuwa wanafunzi wa kwanza wa Yesu wanaoandamana naye wakati wote.