SURA YA 102
Mfalme Aingia Yerusalemu Akiwa Juu ya Mwanapunda
MATHAYO 21:1-11, 14-17 MARKO 11:1-11 LUKA 19:29-44 YOHANA 12:12-19
YESU AINGIA YERUSALEMU KWA VISHINDO
KUHARIBIWA KWA YERUSALEMU KWATABIRIWA
Siku inayofuata, Jumapili, Nisani 9, Yesu anaondoka Bethania akiwa na wanafunzi wake na kuelekea Yerusalemu. Wanapokaribia Bethfage, kwenye Mlima wa Mizeituni, Yesu anawaambia hivi wawili kati ya wanafunzi wake:
“Nendeni katika kijiji mtakachokiona, na mara moja mtamwona punda amefungwa, na mwanapunda akiwa pamoja naye. Wafungueni na kuniletea. Mtu yeyote akiwauliza, semeni, ‘Bwana anawahitaji.’ Na mara moja atawaruhusu mwachukue.”—Mathayo 21:2, 3.
Wanafunzi hawatambui kwamba maagizo ambayo Yesu anawapa yanahusiana na unabii wa Biblia. Hata hivyo, baadaye wanatambua kwamba unabii wa Zekaria unatimizwa. Alitabiri kwamba Mfalme aliyeahidiwa na Mungu angeingia Yerusalemu akiwa “mnyenyekevu na [akiwa] amepanda punda, [akiwa] amepanda mwanapunda dume, mwana wa punda jike.”—Zekaria 9:9.
Wanafunzi wanapofika Bethfage na kumchukua mwanapunda na mama yake, watu waliosimama hapo karibu wanauliza: “Kwa nini mnamfungua mwanapunda huyu?” (Marko 11:5) Lakini wanaposikia kwamba Bwana anawahitaji wanyama hao, wanawaruhusu wanafunzi wawapeleke kwa Yesu. Wanafunzi wanatandika mavazi yao ya nje juu ya punda na mwanapunda, lakini Yesu anapanda juu ya mwanapunda.
Umati unaongezeka kadiri Yesu anavyokaribia Yerusalemu. Watu wengi wanatandika mavazi yao barabarani. Wengine wanatandika “matawi ya miti waliyokata katika mashamba.” Wanapaza sauti: “Tunaomba umwokoe! Amebarikiwa yule anayekuja katika jina la Yehova! Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!” (Marko 11:8-10) Mafarisayo walio katika umati wanakasirika wanaposikia maneno hayo. Wanamwambia Yesu: “Mwalimu, wakemee wanafunzi wako.” Lakini Yesu anawajibu: “Ninawaambia, hata hawa wakinyamaza, mawe yatapaza sauti.”—Luka 19:39, 40.
Yesu anapotazama Yerusalemu anaanza kulia na kusema: “Kama wewe, naam wewe, ungefahamu leo mambo yanayokuletea amani—lakini sasa yamefichwa kutoka machoni pako.” Yerusalemu litapatwa na matokeo mabaya ya kukataa kutii kimakusudi. Yesu anatabiri: “Adui zako [watajenga] ngome yenye miti iliyochongoka kukuzunguka, nao watakuzingira kila upande. Watakuangusha chini wewe na watoto wako walio ndani yako, nao hawataacha jiwe juu ya jiwe lingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kukaguliwa kwako.” (Luka 19:42-44) Kama Yesu alivyosema, Yerusalemu linaharibiwa mwaka wa 70 W.K.
Yesu anapoingia Yerusalemu, ‘jiji lote linakuwa na msukosuko, na kuulizana: “Ni nani huyu?”’ Umati unaendelea kusema: “Huyu ndiye nabii Yesu, kutoka Nazareti ya Galilaya!” (Mathayo 21:10, 11) Wale walio katika umati ambao walimwona Yesu akimfufua Lazaro wanawaambia wengine kuhusu muujiza huo. Mafarisayo wanalalamika kwamba hawajafaulu hata kidogo. Wanaambiana: “Ulimwengu wote umemfuata.”—Yohana 12:18, 19.
Kama ilivyo desturi yake anapotembelea Yerusalemu, Yesu anaenda kufundisha hekaluni. Huko, anawaponya vipofu na vilema. Wakuu wa makuhani na waandishi wanapoona mambo anayofanya na kusikia wavulana hekaluni wakipaza sauti, wakisema: “Tunaomba umwokoe, Mwana wa Daudi!” wanakasirika. Viongozi wa kidini wanamuuliza Yesu: “Je, unasikia wanachosema?” Yesu anajibu: “Je, hamkusoma jambo hili, ‘Kutoka katika vinywa vya watoto wadogo na wanaonyonya, umetoa sifa’?”—Mathayo 21:15, 16.
Yesu anatazama vitu vilivyo hekaluni. Sasa, muda umesonga naye anaondoka pamoja na mitume wake. Kabla ya Nisani 10 kuanza, anarudi Bethania ambako analala Jumapili usiku.