Maisha na Huduma ya Yesu
Kuingia kwa Kristo Katika Yerusalemu kwa Shangwe ya Ushindi
ASUBUHI inayofuata, Jumapili, Nisani 9, Yesu aondoka Bethania pamoja na wanafunzi wake na kusonga ng’ambo ya Mlima wa Mizeituni kuelekea Yerusalemu. Muda si muda, wao wakaribia Bethfage, iliyo juu ya Mlima wa Mizeituni. Yesu aagiza hivi wawili wa wanafunzi wake:
“Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana ana haja nao; na mara hiyo atawapeleka.”
Ingawa kwanza wanafunzi washindwa kutambua kwamba maagizo haya yana uhusiano na utimizo wa unabii wa Biblia, baadaye wao wang’amua kwamba kumbe yanao. Nabii Zekaria alitabiri kwamba Mfalme mwahidiwa wa Mungu angepanda kuingia Yerusalemu akiwa juu ya punda, naam, juu ya “mwana-punda, mtoto wa punda [juu ya mnyama aliyekua kikamili aliye mwana wa punda-jike, NW].” Mfalme Sulemani alikuwa vivyo hivyo amepanda mtoto wa punda akaenda kupakwa mafuta.
Wanafunzi waingiapo Bethfage na kuchukua mwana-punda huyo na mama yake, baadhi ya wenye kusimama hapo wasema: “Mnafanya nini?” Lakini waambiwapo kwamba wanyama wale ni kwa ajili ya Bwana, watu hao waacha wanafunzi wampelekee Yesu. Wanafunzi watandika mavazi yao ya nje juu ya yule punda-mama na juu ya mtoto wake, lakini Yesu ampanda mwana-punda.
Yesu apandapo kuelekea Yerusalemu, umati waongezeka. Walio wengi wa watu hao watandaza mavazi yao ya nje barabarani, hali wengine wakata matawi kutoka kwenye miti na kuyatandaza. “Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana [Yehova, NW],” wao wapaaza sauti. “Amani mbinguni, na utukufu huko juu”!
Mafarisayo fulani katika umati waudhiwa na mbiu hizi nao walalamikia Yesu hivi: “Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako.” Lakini Yesu ajibu hivi: “Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”
Yesu akaribiapo Yerusalemu, yeye aliona jiji na kuanza kulia juu yalo, akisema: “Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani! lakini sasa yamefichwa machoni pako.” Kwa sababu ya kukosa utii kimakusudi, ni lazima Yerusalemu ailipe bei ya kufanya hivyo, kama vile Yesu atabirivyo:
‘Adui zako [Waroma wakiwa chini ya Jenerali Tito watakujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe.’ Kwa kweli uharibifu huu wa Yerusalemu ukiotabiriwa na Yesu watukia miaka 37 baadaye, katika 70 W.K.
Majuma machache tu mapema kidogo, wengi katika umati walikuwa wameona Yesu akifufua Lazaro. Sasa hawa waendelea kuambia wengine kuhusu muujiza huo. Kwa hiyo Yesu aingiapo Yerusalemu, jiji zima laingiwa na kishindo. “Ni nani huyu?” watu wataka kujua. Na umati waendelee kusema hivi: “Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.” Wanapoona linalotendeka, Mafarisayo waomboleza kwamba wao wafanya kazi bure tu, kwa maana, kama wasemavyo: “Ulimwengu umekwenda nyuma yake.”
Kama ilivyo desturi yake katika ziara za kwenda Yerusalemu, Yesu aenda kwenye hekalu akafundishe. Huko vipofu na vilema wamjia yeye, naye awaponya! Wakuu wa makuhani na waandishi wakasirika waonapo mambo mazuri sana ambayo Yesu anafanya na wawasikiapo wavulana hekaluni wakipaaza sauti, “Hosana, Mwana wa Daudi [Okoa, twasali, Mwana wa Daudi,” NW]!” “Wasikia hawa wasemavyo?” wao wateta.
“Naam,” Yesu ajibu. “Hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?”
Yesu aendelea kufundisha, naye atazama-tazama vitu vyote vimzungukavyo hekaluni. Muda si muda mchana umesonga sana. Kwa hiyo yeye aondoka, pamoja na wale 12, naye arudi Bethania ule mwendo wa kilometa 3. Alala huko usiku wa Jumapili, labda nyumbani mwa Lazaro rafiki yake. Mathayo 21:1-11, 14-17; Marko 11:1-11; Luka 19:29-44; Yohana 12:12-19; Zekaria 9:9.
◆ Ni lini na jinsi gani Yesu aingia Yerusalemu akiwa Mfalme?
◆ Ni jambo muhimu kadiri gani kwamba umati wamsifu Yesu?
◆ Yesu ahisi jinsi gani aonapo Yerusalemu, naye atamka unabii gani?
◆ Ni jambo gani latendeka Yesu aendapo hekaluni?