Maisha Huduma ya Yesu
Mwanzo wa Siku ya Mambo Makubwa
YESU aondokapo Yerusalemu jioni ya Jumatatu, arudi Bethania juu ya mwinamo wa mashariki wa Mlima wa Mizeituni. Amemaliza siku mbili za huduma yake ya mwisho katika Yerusalemu. Bila shaka Yesu akaa tena usiku huo pamoja na Lazaro rafiki yake. Tangu alipowasili kutoka Yeriko siku ya Ijumaa, huu ndio usiku wake wa nne kuwa katika Bethania.
Sasa, asubuhi na mapema Jumanne, Nisani 11, yeye na wanafunzi wake wako njiani tena. Hii yathibitika kuwa siku ya mambo makubwa ya huduma ya Yesu, iliyo na shughuli nyingi zaidi kufikia hapo. Ndiyo siku ya mwisho ya kuonekana kwake hekaluni. Nayo ndiyo siku ya mwisho ya huduma yake ya peupe kabla ya kujaribiwa na kuuawa kwake.
Wao wafuata njia ile ile ya kupita juu ya Mlima wa Mizeituni kuelekea Yerusalemu. Kando ya njia hiyo kutoka Bethania, Petro aona mti ambao Yesu aliulaani asubuhi iliyotangulia. “Rabi, tazama,” yeye apaaza mshangao, “mti ulioulaani umenyauka.”
Lakini kwa nini Yesu akaua mti ule? Yeye aonyesha sababu aendeleapo kusema: “Amin, nawaambia, Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu [Mlima wa Mizeituni ambao wamesimama juu yao], Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.”
Kwa hiyo kwa kusababisha mti huo unyauke, Yesu anaandalia wanafunzi wake somo la kutumia kitu chenye kuonekana ili waone uhitaji wao wa kuwa na imani katika Mungu. Kama vile ambavyo ataarifu: “Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Lo, ni somo la maana kama nini kwao kujifunza, hasa kwa sababu ya mitihani ya kuogofya itakayokuja karibuni! Hata hivyo, kuna uhusiano mwingine kati ya kunyauka kwa mtini na ubora wa imani.
Taifa la Israeli, kama mtini huu, lina sura ya udanganyifu. Ingawa taifa hilo limo katika uhusiano wa agano pamoja na Mungu na huenda likaonekana kinje-nje kuwa lashika virekebi vyake, limethibitika kuwa bila imani, likiwa na utasa wa kukosa matunda mema. Kwa sababu ya ukosefu wa imani, hata limo katika hatua za kukataa Mwana wa Mungu mwenyewe! Kwa hiyo, kwa kusababisha mtini ule usiozaa unyauke, Yesu aonyesha kwa udhihirifu mwingi tokeo la mwisho kwa taifa hili lisilozaa matunda, lisilo na imani.
Punde si punde, Yesu na wanafunzi wake waingia Yerusalemu, na kama ilivyo desturi yao, waenda hekaluni, ambako Yesu aanza kufundisha. Wakuu wa makuhani na wanaume wazee wa watu, bila shaka wakifikiria kitendo ambacho Yesu alifanya siku iliyotangulia dhidi ya wavunja-pesa, wamtolea dai hili lenye ubishi: “Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii?”
Katika kujibu Yesu asema hivi: “Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?”
Makuhani na wanaume wazee waanza kushauriana miongoni mwao wenyewe watajibu jinsi gani. “Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini? Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii.”
Viongozi hawajui la kujibu. Kwa hiyo wamjibu Yesu hivi: “Hatujui.”
Yesu, naye, asema: “Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya.” Mathayo 21:19-27; Marko 11:19-33; Luka 20:1-8.
◆ Ni jambo gani la maana kuhusu Jumanne, Nisani 11?
◆ Yesu aandaa masomo gani asababishapo mtini unyauke?
◆ Yesu awajibuje wale wenye kuuliza yeye afanya mambo kwa mamlaka gani?