SURA YA 109
Awashutumu Wapinzani wa Kidini
MATHAYO 22:41–23:24 MARKO 12:35-40 LUKA 20:41-47
KRISTO NI MWANA WA NANI?
YESU AWAFUNUA WAPINZANI WANAFIKI
Wapinzani wa kidini wanashindwa kumharibia sifa Yesu au kumnasa na kumkabidhi kwa Waroma. (Luka 20:20) Sasa wakiwa bado hekaluni Nisani 11, Yesu anawageukia na kuwaonyesha utambulisho wake halisi. Kwanza anawauliza: “Mna maoni gani kuhusu Kristo? Ni mwana wa nani?” (Mathayo 22:42) Ni wazi kwamba Kristo au Masihi, atatoka katika ukoo wa Daudi. Hivyo ndivyo wanavyojibu.—Mathayo 9:27; 12:23; Yohana 7:42.
Yesu anauliza: “Basi, kwa nini Daudi akiongozwa na roho anamwita Bwana, akisema, ‘Yehova alimwambia Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kuume mpaka niwaweke maadui wako chini ya miguu yako”’? Basi ikiwa Daudi anamwita Bwana, anawezaje kuwa mwanawe?”—Mathayo 22:43-45.
Mafarisayo wananyamaza, kwa kuwa wanatumaini kwamba mtu kutoka ukoo wa Daudi atawakomboa kutoka kwa utawala wa Roma. Lakini Yesu anatumia maneno ya Daudi katika Zaburi 110:1, 2, kuonyesha kwamba Masihi atakuwa zaidi ya mtawala wa kibinadamu. Yeye ndiye Bwana wa Daudi, na baada ya kukaa katika mkono wa kuume wa Mungu, atakuwa mtawala. Maneno ya Yesu yanawanyamazisha wapinzani wake.
Wanafunzi na wengine wengi wamekuwa wakisikiliza. Sasa Yesu anazungumza nao, akiwaonya kuhusu waandishi na Mafarisayo. Watu hao “wamejiketisha kwenye kiti cha Musa” ili kufundisha Sheria ya Mungu. Yesu anawaambia hivi wasikilizaji wake: “Fanyeni mambo yote wanayowaambia, lakini msitende kama wao, kwa maana wao husema lakini hawatendi mambo wanayosema.”—Mathayo 23:2, 3.
Kisha Yesu anatoa mifano kuhusu unafiki wao, akisema: “Wanapanua visanduku vyenye maandiko wanavyovaa kama ulinzi.” Baadhi ya Wayahudi walivaa kwenye paji la uso au mkononi visanduku hivyo vidogo vilivyokuwa na mafungu mafupi ya Sheria. Mafarisayo huongezea ukubwa wa visanduku vyao ili kujionyesha kwamba wana bidii ya kufuata Sheria. Pia, ‘wanarefusha pindo zenye nyuzi za mavazi yao.’ Waisraeli walipaswa kutengeneza pindo kwenye mavazi yao, lakini Mafarisayo wanahakikisha kwamba pindo zao ni ndefu sana. (Hesabu 15:38-40) Wanafanya mambo yote hayo “ili waonwe na watu.”—Mathayo 23:5.
Hata wanafunzi wa Yesu wanaweza kuathiriwa na tamaa ya umashuhuri, hivyo anawashauri hivi: “Msiitwe Rabi, kwa maana Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Zaidi ya hayo, msimwite mtu yeyote baba yenu duniani, kwa maana Baba yenu ni mmoja, Yule aliye mbinguni. Wala msiitwe viongozi, kwa maana Kiongozi wenu ni mmoja, Kristo.” Hivyo basi, wanafunzi wanapaswa kujionaje na kutendaje? Yesu anawaambia: “Aliye mkuu zaidi kati yenu lazima awe mhudumu wenu. Yeyote anayejiinua atanyenyekezwa, na yeyote anayejinyenyekeza atainuliwa.”—Mathayo 23:8-12.
Kisha Yesu anawatangazia ole waandishi na Mafarisayo wanafiki: “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu mnawafungia watu Ufalme wa mbinguni; kwa maana ninyi wenyewe hamwingii, na mnawazuia wale wanaotaka kuingia.”—Mathayo 23:13.
Yesu anawashutumu Mafarisayo kwa sababu hawathamini mambo ya kiroho, kama inavyoonyeshwa na maamuzi yao yasiyo na msingi. Kwa mfano, wanasema: “Yeyote akiapa kwa hekalu, si kitu; lakini yeyote akiapa kwa dhahabu ya hekalu, yuko chini ya wajibu.” Hivyo wanaonyesha jinsi walivyo vipofu kimaadili, kwa maana wanakazia zaidi dhahabu ya hekalu kuliko thamani ya kiroho ya mahali pa kumwabudu Yehova. Nao ‘wamepuuza mambo mazito zaidi ya Sheria, yaani, haki, rehema, na uaminifu.’—Mathayo 23:16, 23; Luka 11:42.
Yesu anawaita Mafarisayo hao “viongozi vipofu, ambao huchuja mbu lakini hummeza ngamia!” (Mathayo 23:24) Wanachuja mbu kutoka kwenye divai yao kwa sababu mdudu huyo si safi kisherehe. Lakini wanapopuuza mambo mazito ya Sheria ni kama wanammeza ngamia, ambaye pia ni mnyama asiye safi kisherehe, lakini mkubwa zaidi.—Mambo ya Walawi 11:4, 21-24.