Maisha na Huduma ya Yesu
Huduma Kwenye Hekalu Yakamilishwa
YESU anaonekana hekaluni mara ya mwisho. Kwa uhakika, anamalizia huduma yake ya peupe akiwa duniani, isipokuwa matukio ya kujaribiwa na kuuawa kwake siku tatu baadaye. Sasa aendelea kuwachambua vikali waandishi na Mafarisayo.
Yeye apaaza mshangao huu mara tatu zaidi: “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki!” Kwanza, apiga mbiu ya ole juu yao kwa sababu wao husafisha sana “sehemu ya nje ya kikombe na ya sahani, lakini kwa ndani wao wamejaa utekwa-nyara na ukosefu wa kiasi.” Kwa hiyo awashauri hivi: “Kwanza safidini sehemu ya ndani ya kikombe na ya sahani, ili kwamba sehemu ya nje pia ipate kuwa safi.”
Ndipo atamka ole juu ya waandishi na Mafarisayo kwa sababu ya ubovu wa ndani na kioza ambacho wao wajaribu kuficha kwa kuonyesha udini wa nje-nje. “Nyinyi mwashabihiana na makaburi yaliyopakwa chokaa,” yeye asema, “ambayo kwa nje huonekana kweli kweli kuwa na uzuri mwingi lakini ndani yamejaa mifupa ya wanadamu wafu na kila namna ya ukosefu wa usafi.”
Mwisho, unafiki wao wadhihirishwa katika nia yao ya kujengea manabii makaburi na kuyapamba ili kuvuta fikira kwenye matendo yao wenyewe ya fadhili. Hata hivyo, kama Yesu afunuavyo, wao “ni wana wa wale waliowaua manabii.” Kweli kweli, mtu yeyote ambaye athubutu kufunua unafiki wao yumo hatarini!
Akiendelea, Yesu atamka mashutumu yake yaliyo makali zaidi ya yote. “Manyoka, wazao wa vipiri,” yeye asema, “ni jinsi gani nyinyi mtakimbia kutoka hukumu ya Gehena?” Gehena ni bonde lenye kutumiwa kama tupio la takataka za Yerusalemu. Kwa hiyo Yesu anasema kwamba kwa kufuatia mwendo wao mwovu, waandishi na Mafarisayo watapata uharibifu wa milele.
Kwa habari ya wale ambao yeye awatuma wakiwa wawakilishi wake, Yesu asema hivi: “Baadhi yao nyinyi mtaua na kutundika, na baadhi yao nyinyi mtapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwanyanyasa kutoka jiji hadi jiji; kwamba ipate kuja juu yenu damu yote ya uadilifu iliyomwagwa duniani, kuanzia damu ya Abeli mwadilifu hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia [mwenye kuitwa Yehoyada katika 2 Nyakati], ambaye nyinyi mliua kimakusudi kati ya patakatifu na madhabahu. Kwa kweli mimi nasema kwa nyinyi, Mambo yote haya yatakuja juu ya kizazi hiki.”
Kwa sababu kwa moyo mkuu Zekaria aliwasuta vikali viongozi wa Israeli, “wao walitunga hila dhidi yake na wakamtupia mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Yehova.” Lakini, kama Yesu atabirivyo, Israeli watalipia damu yote hiyo ya uadilifu iliyomwagwa. Wao wailipia miaka 37 baadaye, katika 70 W.K., wakati majeshi ya Kiroma yaharibupo Yerusalemu na Wayahudi zaidi ya milioni moja waangamia.
Yesu afikiriapo hali hii yenye kuogopesha, asononeka. “Yerusalemu, Yerusalemu,” yeye apiga mbiu kwa mara nyingine, “ni mara ngapi mimi nilitaka kukusanya watoto wako pamoja, jinsi kuku hukusanya vifaranga wake pamoja chini ya mabawa yake! Lakini nyinyi watu hamkutaka hivyo. Tazameni! Mmeachiwa nyumba yenu ukiwa.”
Ndipo Yesu aongezea hivi: “Kuanzia sasa hamtaniona mimi kwa vyovyote mpaka mseme, ‘Mbarikiwa ni yeye ambaye aja katika jina la Yehova!’” Siku hiyo itakuwa wakati wa kuwapo kwa Kristo ajapo katika Ufalme wake wa kimbingu na watu wamwonapo kwa macho ya imani.
Sasa Yesu asonga kwenda mahali ambapo aweza kutazama makasha ya hazina katika hekalu na umati wa watu ukitumbukiza pesa humo. Matajiri watumbukiza sarafu nyingi. Lakini ndipo mjane maskini mmoja aja pale na kutumbukiza sarafu ndogo mbili za thamani ndogo sana.
Akiwaita wanafunzi wake kwake, Yesu asema: “Kwa kweli mimi nasema kwa nyinyi kwamba mjane maskini huyu alitumbukiza zaidi ya wote wale wenye kutumbukiza pesa ndani ya yale makasha ya hazina.” Ni lazima wao wawe washangaa yawezaje kuwa hivyo. Kwa hiyo Yesu aeleza hivi: “Wote walitumbukiza kutokana na ziada yao, lakini yeye, kutokana na mwambo wake, alitumbukiza chote alichokuwa nacho, maishilio yake yote.” Baada ya kusema mambo haya, Yesu aondoka kwenye hekalu kwa mara ya mwisho.
Wakistaajabia ukubwa na uzuri wa hekalu, wanafunzi wake wapaaza mshangao huu: “Mwalimu, ona! ni mawe ya namna gani na ni majengo ya namna gani!” Kweli kweli, yaripotiwa kwamba mawe hayo yana urefu wa zaidi ya meta 11, upana wa zaidi ya meta 5, na kimo cha zaidi ya meta 3!
“Je! nyinyi mwayaona majengo makubwa haya?” Yesu ajibu. “Kwa vyovyote hakuna jiwe ambalo litaachwa hapa juu ya jiwe na lisitupwe chini.”
Baada ya kusema mambo haya, Yesu na mitume wake wavuka Bonde la Kidroni na kupanda Mlima wa Mizeituni. Wakiwa huko waweza kulichungulia hekalu hilo zuri mno. Mathayo 23:25–24:3; Marko 12:41–13:3; Luka 21:1-6; 2 Nyakati 24:20-22, NW.
◆ Yesu afanya nini wakati wa ziara yake ya mwisho kwenye hekalu?
◆ Unafiki wa waandishi na Mafarisayo wadhihirishwaje?
◆ Ni nini kinachomaanishwa na “hukumu ya Gehena”?
◆ Kwa nini Yesu asema kwamba mjane alichanga zaidi ya matajiri?