Kuna Wakati Ujao Gani kwa Kondoo na Mbuzi?
“Atatenganisha watu, kama vile mchungaji atenganishavyo kondoo na mbuzi.”—MATHAYO 25:32, NW.
1, 2. Kwa nini mfano wa kondoo na mbuzi utupendeze?
HAKIKA Yesu Kristo alikuwa Mwalimu mkubwa kupita wote duniani. (Yohana 7:46) Mojayapo njia zake za kufundisha ilikuwa kutumia mifano, au vielezi. (Mathayo 13:34, 35) Mifano hiyo ilikuwa sahili lakini yenye nguvu sana katika kujulisha kweli za ndani za kiroho na za kiunabii.
2 Katika mfano wa kondoo na mbuzi, Yesu alielekezea wakati wake wa kutenda katika fungu la kipekee: “Wakati Mwana wa binadamu awasilipo katika utukufu wake, na . . . ” (Mathayo 25:31, NW) Hili lapaswa litupendeze kwa sababu hicho ndicho kielezi ambacho Yesu amalizia katika kujibu lile swali: “Ni nini itakuwa ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?” (Mathayo 24:3, NW) Lakini hili lamaanisha nini kwetu?
3. Mapema katika maneno yake, Yesu alisema nini kingetukia mara tu baada ya dhiki kubwa kuanza?
3 Yesu alitabiri matukio makubwa ambayo yangetukia “mara baada ya” kufyatuka kwa dhiki kubwa, matukio tunayongoja. Alisema kwamba ndipo “ishara ya Mwana wa binadamu” itatokea. Hili litaathiri kabisa “makabila yote ya dunia” ambayo “yatamwona Mwana wa binadamu akija juu ya mawingu ya mbinguni na nguvu na utukufu mkubwa.” Mwana wa binadamu ataandamana na “malaika zake.” (Mathayo 24:21, 29-31, NW)a Vipi juu ya mfano wa kondoo na mbuzi? Biblia za kisasa huuweka katika sura ya 25, lakini huo ni sehemu ya jibu la Yesu, ukieleza mambo mengine zaidi kuhusu kuja kwake katika utukufu na kukazia hukumu yake juu ya “mataifa yote.”—Mathayo 25:32, NW.
Wahusika Katika Huu Mfano
4. Mfano wa kondoo na mbuzi wataja nini mwanzoni kuhusu Yesu, na ni nani pia wanaotajwa?
4 Yesu aanza huu mfano kwa kusema: “Wakati Mwana wa binadamu awasilipo.” Yaelekea unajua “Mwana wa binadamu” ni nani. Waandikaji wa Gospeli mara nyingi walitumia usemi huo kumhusu Yesu. Hata Yesu mwenyewe aliutumia hivyo, bila shaka akikumbuka ono la Danieli la “mtu kama mwana wa binadamu” akimwendea Mkale wa Siku ili kupokea “utawala na heshima na ufalme.” (Danieli 7:13, 14, NW; Mathayo 26:63, 64, NW; Marko 14:61, 62, NW) Ingawa Yesu ndiye mhusika-mkuu katika mfano huu, hayuko peke yake. Mapema katika maneno yake, kama yalivyonukuliwa katika Mathayo 24:30, 31, alisema kwamba Mwana wa binadamu ‘ajapo na nguvu na utukufu mkubwa,’ malaika zake watatimiza fungu muhimu. Vivyo hivyo, mfano wa kondoo na mbuzi waonyesha malaika wakiwa na Yesu aketipo ‘juu ya kiti cha ufalme chenye utukufu’ ili kuhukumu. (Linganisha Mathayo 16:27.) Lakini Hakimu na malaika zake wako mbinguni, basi, je, wanadamu wanazungumzwa katika huu mfano?
5. Tunaweza kutambulishaje “ndugu” za Yesu?
5 Kutazama huu mfano kwafunua vikundi vitatu tunavyohitaji kutambulisha. Mbali na kondoo na mbuzi, Mwana wa binadamu aongezea kikundi cha tatu ambacho kitambulisho chacho ni muhimu sana katika kutambulisha kondoo na mbuzi. Yesu akiita hiki kikundi cha tatu ndugu zake wa kiroho. (Mathayo 25:40, 45) Ni lazima wawe waabudu wa kweli, kwa kuwa Yesu alisema: “Ye yote atakayefanya mapenzi ya Baba yangu . . ., huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.” (Mathayo 12:50; Yohana 20:17) Kihususa, Paulo aliandika juu ya Wakristo walio sehemu ya “mbegu ya Abrahamu” na ambao ni wana wa Mungu. Yeye aliwaita hawa “ndugu” za Yesu na “washiriki wa wito wa kimbingu.”—Waebrania 2:9–3:1, NW; Wagalatia 3:26, 29, NW.
6. Ni nani walio “wadogo zaidi sana” wa ndugu za Yesu?
6 Kwa nini Yesu alitaja ‘mdogo zaidi sana’ wa ndugu zake? Maneno hayo yarudia maneno yale mitume walimsikia akisema hapo awali. Alipokuwa akilinganisha Yohana Mbatizaji, aliyekufa kabla ya Yesu na hivyo kuwa na tumaini la kidunia, pamoja na wale wanaopata uhai wa kimbingu, Yesu alisema: “Hakujainuliwa mkubwa zaidi ya Yohana Mbatizaji; lakini mtu ambaye ni mdogo zaidi katika ufalme wa mbingu ni mkubwa zaidi kuliko yeye.” (Mathayo 11:11, NW) Wengine wanaoenda mbinguni huenda walikuwa mashuhuri katika kutaniko, kama vile mitume, na wengine wakiwa si mashuhuri hivyo, lakini wote ni ndugu za Yesu wa kiroho. (Luka 16:10; 1 Wakorintho 15:9; Waefeso 3:8; Waebrania 8:11) Hivyo, hata kama wengine walionekana kuwa hawana umashuhuri duniani, wao walikuwa ndugu zake nao wangalipaswa kutendewa hivyo.
Ni Nani Walio Kondoo na Mbuzi?
7, 8. Yesu alisema nini kuhusu kondoo, basi tunaweza kukata kauli gani kuwahusu?
7 Twasoma kuhusu kuhukumiwa kwa kondoo: “[Yesu] atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu [“tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu,” NW]; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki [“waadilifu,” “NW”] watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo [“zaidi sana,” NW], mlinitendea mimi.”—Mathayo 25:34-40, italiki ni zetu.
8 Kwa wazi, kondoo wanaohukumiwa kustahili kuwa upande wa kuume wa Yesu wa heshima na upendeleo wanawakilisha jamii fulani ya wanadamu. (Waefeso 1:20; Waebrania 1:3) Wao walifanya nini na lini? Yesu alisema kwamba kwa fadhili, staha, na ukarimu, walimlisha, wakamnywesha, na kumvika, wakimsaidia alipokuwa mgonjwa au alipokuwa gerezani. Kondoo wasemapo kwamba hawakuwa wamefanya hivyo kwa Yesu binafsi, yeye asema kwamba wao waliwaunga mkono ndugu zake wa kiroho, wale mabaki wa Wakristo watiwa-mafuta, basi katika maana hiyo walimfanyia hayo.
9. Kwa nini huu mfano hauhusu Mileani?
9 Huu mfano hauhusu wakati wa Mileani, kwa kuwa wakati huo watiwa-mafuta hawatakuwa wanadamu wenye kupatwa na njaa, kiu, ugonjwa, au kufungwa gerezani. Lakini wengi wao wamejionea hayo katika umalizio wa mfumo huu wa mambo. Tangu Shetani atupwe duniani, amefanya mabaki kuwa shabaha yake maalumu ya ghadhabu yake, akifanya wadhihakiwe, wateswe, na kuuawa.—Ufunuo 12:17.
10, 11. (a) Kwa nini si jambo la akili kufikiri kwamba kondoo watia ndani kila mtu atendalo tendo moja la fadhili kwa ndugu za Yesu? (b) Kwa kufaa kondoo wanawakilisha nani?
10 Je, Yesu anasema kwamba kila mtu anayeonyesha fadhili fulani ndogo kwa mmojawapo ndugu zake, kama vile kumpa kipande cha mkate au gilasi ya maji, anastahili kuwa mmoja wa kondoo hawa? Ni kweli kwamba kuonyesha fadhili kama hizo kwaweza kuwa fadhili ya kibinadamu, lakini kwa kweli, yaonekana kuwa kuna mengi zaidi yanayohusika na kondoo wa huu mfano. Kwa kielelezo, Yesu hakuwa akirejezea wasioamini kuwapo kwa Mungu au makasisi ambao kwa kutukia waweza kufanya tendo moja la fadhili kwa mmojawapo wa ndugu zake. Kinyume cha hilo, mara mbili Yesu aliwaita kondoo “waadilifu.” (Mathayo 25:37, 46, NW) Kwa hiyo ni lazima kondoo wawe wale ambao kwa kipindi cha wakati wamesaidia—kuwaunga mkono kwa matendo—ndugu za Kristo na ambao wamedhihirisha imani kwa kadiri ya kupokea msimamo mwadilifu mbele ya Mungu.
11 Katika karne ambazo zimepita, wengi kama vile Abrahamu wamekuwa na msimamo mwadilifu. (Yakobo 2:21-23) Noa, Abrahamu, na waaminifu wengine wanatiwa miongoni mwa “kondoo wengine” ambao wataurithi uhai katika Paradiso chini ya Ufalme wa Mungu. Katika nyakati za majuzi mamilioni zaidi wamekubali ibada ya kweli wakiwa kondoo wengine nao wamekuja kuwa “kundi moja” na watiwa-mafuta. (Yohana 10:16; Ufunuo 7:9) Hawa wenye tumaini la kidunia huwatambua ndugu za Yesu kuwa mabalozi wa Ufalme na hivyo kuwasaidia—kihalisi na kiroho. Yesu huona kana kwamba ametendewa jambo ambalo kondoo wengine hutendea ndugu zake duniani. Watu kama hao wanaokuwa wangali hai anapokuja kuhukumu mataifa watahukumiwa kuwa kondoo.
12. Kwa nini kondoo huenda wakauliza ni jinsi gani walivyomtendea Yesu kwa fadhili?
12 Ikiwa kondoo wengine sasa wanahubiri habari njema pamoja na watiwa-mafuta na kuwasaidia, kwa nini waulize: “Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?” (Mathayo 25:37) Kwaweza kuwa na sababu kadhaa. Huu ni mfano tu. Kuupitia, Yesu aonyesha hangaiko lake la ndani kwa ndugu zake wa kiroho; yeye ahisi pamoja nao, akiteseka pamoja nao. Mapema Yesu alikuwa amesema: “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi; ampokea yeye aliyenituma.” (Mathayo 10:40) Katika kielezi hiki, Yesu aendeleza kanuni hiyo, akionyesha kwamba yale yanayofanywa (mazuri au mabaya) kwa ndugu zake hufika hata mbinguni; ni kana kwamba anafanyiwa hayo mbinguni. Pia, Yesu hapa alikazia kiwango cha Yehova cha kuhukumu, akielewesha wazi kwamba hukumu ya Mungu, iwe yenye upendeleo au ya adhabu, ni ya kweli na ya haki. Mbuzi hawawezi kutoa udhuru, ‘Laiti tungalikuona wewe binafsi.’
13. Kwa nini wenye mfano wa mbuzi huenda wakamwita Yesu “Bwana”?
13 Mara tuelewapo wakati hukumu hiyo inayotajwa katika huu mfano inapotolewa, twafahamu kwa wazi zaidi ni nani walio mbuzi. Utimizo wao ni wakati “ishara ya Mwana wa binadamu itakapoonekana mbinguni, na ndipo makabila yote ya dunia yatakapojipiga yenyewe kwa maombolezo, nayo yatamwona Mwana wa binadamu akija . . . na nguvu na utukufu mkubwa.” (Mathayo 24:29, 30, NW) Waokokaji wa dhiki juu ya Babiloni Mkubwa ambao waliwatendea ndugu za Mfalme kwa madharau wanaweza sasa kumwita huyo Hakimu kwa mafadhaiko kuwa “Bwana,” wakitumaini kuokoa uhai wao.—Mathayo 7:22, 23; linganisha Ufunuo 6:15-17.
14. Ni kwa msingi gani Yesu atahukumu kondoo na mbuzi?
14 Hata hivyo, hukumu ya Yesu haitategemea madai yenye mafadhaiko ya wale waliokuwa waenda-kanisa, wasioamini kuwapo kwa Mungu, au wengine. (2 Wathesalonike 1:8) Badala ya hivyo, hakimu atachunguza hali ya moyo na matendo yaliyopita ya watu kuelekea hata ‘mmoja wa wadogo zaidi sana wa ndugu zake.’ Ni kweli kwamba idadi ya Wakristo watiwa-mafuta wanaosalia duniani inapunguka. Hata hivyo, maadamu watiwa-mafuta, wakifanyiza “mtumwa mwaminifu mwenye akili,” waendeleapo kuandaa chakula na mwelekezo wa kiroho, wale wenye matazamio ya kuwa kondoo wana fursa ya kufanya mema kwa jamii ya mtumwa, kama vile ‘umati mkubwa wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha’ wamefanya.—Ufunuo 7:9, 14.
15. (a) Wengi wamejionyeshaje kuwa kama mbuzi? (b) Kwa nini tuepuke kusema kama mtu ni kondoo au mbuzi?
15 Ndugu za Kristo na mamilioni ya kondoo wengine ambao wameungana nao kuwa kundi moja wametendewaje? Huenda watu wengi binafsi hawajawashambulia wawakilishi wa Kristo, lakini pia hawajawatendea watu wake kwa upendo. Wakipendelea ulimwengu mwovu, watu wenye mfano wa mbuzi hukataa ujumbe wa Ufalme, iwe wausikia kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja. (1 Yohana 2:15-17) Bila shaka, katika uchanganuzi wa mwisho, Yesu ndiye amewekwa rasmi kutoa hukumu. Si juu yetu kuamua ni nani walio kondoo na ni nani walio mbuzi.—Marko 2:8; Luka 5:22; Yohana 2:24, 25; Warumi 14:10-12; 1 Wakorintho 4:5.
Kuna Wakati Ujao Gani kwa Kila Kikundi?
16, 17. Kondoo watakuwa na wakati ujao gani?
16 Yesu alitoa hukumu yake juu ya kondoo: “Njoni, nyinyi ambao mmebarikiwa na Baba yangu, rithini ufalme uliotayarishwa kwa ajili yenu tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu.” Huo ni mwaliko mchangamfu kama nini—“Njoni”! Wapate nini? Uhai udumuo milele, kama alivyoeleza katika umalizio wake: “Waadilifu [wataingia] katika uhai udumuo milele.”—Mathayo 25:34, 46, NW.
17 Katika mfano wa talanta, Yesu alionyesha kile kinachohitajika kwa wale watakaotawala pamoja naye mbinguni, lakini katika mfano huu yeye aonyesha kile kinachotazamiwa kwa raia wa Ufalme. (Mathayo 25:14-23) Hasa, kwa sababu ya kuunga mkono kwa moyo wote ndugu za Yesu, kondoo watarithi sehemu katika makao ya kidunia ya Ufalme wake. Wao watafurahia uhai katika dunia iliyo paradiso—tazamio ambalo Mungu aliwatayarishia “tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu” wa wanadamu wawezao kukombolewa.—Luka 11:50, 51, NW.
18, 19. (a) Yesu atatoa hukumu gani kwa mbuzi? (b) Tunaweza kuwaje na hakika kwamba mbuzi hawatakabili mateso ya milele?
18 Hukumu itekelezwayo juu ya mbuzi ni tofauti kama nini! “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo [“zaidi sana,” NW], hamkunitendea mimi.”—Mathayo 25:41-45.
19 Wanafunzi wa Biblia wajua kwamba hilo haliwezi kumaanisha kwamba nafsi zisizoweza kufa za wenye mfano wa mbuzi zitateseka katika moto wa milele. La, kwa kuwa wanadamu ni nafsi; hawana nafsi zisizoweza kufa. (Mwanzo 2:7; Mhubiri 9:5, 10; Ezekieli 18:4) Kwa kuhukumu mbuzi kwa “moto wa milele,” Hakimu anamaanisha uharibifu usio na tumaini la wakati ujao, ambao pia utakuwa mwisho wa daima wa Ibilisi na roho waovu wake. (Ufunuo 20:10, 14) Hivyo, Hakimu wa Yehova atoa hukumu hizo zilizo tofauti. Awaambia kondoo, “Njoni”; mbuzi, “Ondokeni kwangu.” Kondoo watarithi “uhai udumuo milele.” Mbuzi watapatwa na “kukatiliwa-mbali kudumuko milele.”—Mathayo 25:46, NW.b
Hilo Lamaanisha Nini Kwetu?
20, 21. (a) Wakristo wana kazi gani ya maana ya kufanya? (b) Ni mgawanyiko upi unaoendelea sasa? (c) Hali ya watu itakuwa nini wakati mfano wa kondoo na mbuzi uanzapo kutimizwa?
20 Wale mitume wanne waliosikia jibu la Yesu kuhusu ishara ya kuwapo kwake na ya umalizio wa mfumo walikuwa na mengi zaidi ya kufikiria. Wangehitaji kukesha na kulinda. (Mathayo 24:42) Pia wangehitaji kufanya kazi ya kutoa ushahidi inayotajwa katika Marko 13:10. Mashahidi wa Yehova wanafanya kwa bidii kazi hiyo leo.
21 Hata hivyo, uelewevu huu mpya wa mfano wa kondoo na mbuzi wamaanisha nini kwetu? Naam, tayari watu wanachukua misimamo. Wengine wamo katika ‘barabara pana iongozayo katika uharibifu,’ huku wengine wakijaribu kudumu katika ‘barabara yenye kufinyana iongozayo katika uhai.’ (Mathayo 7:13, 14, NW) Lakini wakati ambapo Yesu atatangaza hukumu ya mwisho juu ya kondoo na mbuzi wanaoonyeshwa katika huu mfano ungali mbele. Mwana wa binadamu ajapo katika fungu la Hakimu, yeye ataamua kwamba Wakristo wengi wa kweli—hasa “umati mkubwa” wa kondoo waliojiweka wakfu—watastahili kupita sehemu ya mwisho ya “dhiki kubwa” na kuingia katika ulimwengu mpya. Tazamio hilo lapaswa sasa kuwa chanzo cha shangwe. (Ufunuo 7:9, 14, NW) Kwa upande mwingine, halaiki ya watu kutoka kwa “mataifa yote” watakuwa wamejithibitisha kuwa mbuzi washupavu. Wao “[wataingia] katika kukatiliwa-mbali kudumuko milele.” Liwazo lililoje kwa dunia!
22, 23. Kwa kuwa utimizo wa huu mfano ungali mbele, kwa nini kazi yetu ya kuhubiri leo ni muhimu?
22 Ingawa kule kuhukumu kama kunavyofafanuliwa katika huu mfano kuko karibu sana, hata sasa jambo muhimu linatukia. Sisi Wakristo tunashiriki katika kazi ya kuokoa uhai ya kutangaza ujumbe unaotokeza mgawanyiko kati ya watu. (Mathayo 10:32-39) Paulo aliandika: “Kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?” (Warumi 10:13, 14) Huduma yetu ya hadharani inafikia watu katika nchi zaidi ya 230 kwa jina la Mungu na ujumbe wake wa wokovu. Ndugu za Kristo watiwa-mafuta wangali wakiongoza kazi hii. Kondoo wengine wapatao milioni tano wamejiunga nao sasa. Na watu duniani pote wanauitikia ujumbe unaotangazwa na ndugu za Yesu.
23 Wengi hupata ujumbe wetu tuhubiripo nyumba kwa nyumba au kivivi-hivi. Wengine huenda wakajifunza juu ya Mashahidi wa Yehova na kile tunachowakilisha katika njia tusizojua. Wakati wa hukumu ufikapo, Yesu atafikiria kwa kadiri gani ustahili wa kijumuiya na ustahili wa kifamilia? Hatujui, na hakuna haja ya kukisia. (Linganisha 1 Wakorintho 7:14.) Wengi sasa hupuuza kimakusudi, hudhihaki, au hushiriki moja kwa moja katika kuwanyanyasa watu wa Mungu. Hivyo, huu ni wakati muhimu; watu kama hao huenda wanaelekea kuwa wale ambao Yesu atahukumu kuwa mbuzi.—Mathayo 10:22; Yohana 15:20; 16:2, 3; Warumi 2:5, 6.
24. (a) Kwa nini ni jambo la maana kwa watu mmoja-mmoja kuitikia ifaavyo kuhubiri kwetu? (b) Funzo hili limekusaidia wewe binafsi kuwa na mtazamo gani kuelekea huduma yako?
24 Ingawa hivyo, kwa furaha wengi huitikia ifaavyo, hujifunza Neno la Mungu, na kuwa Mashahidi wa Yehova. Wengine ambao sasa wanaonekana kuwa wenye mfano wa mbuzi huenda wakabadilika na kuwa kama kondoo. Jambo kuu ni kwamba wale wanaoitikia na kuunga mkono kwa matendo mabaki ya ndugu za Kristo wanatoa uthibitisho sasa ambao utawawekea msingi wa kuwekwa kwenye mkono wa kuume wa Yesu aketipo, hivi karibuni, katika kiti chake cha ufalme ili kutoa hukumu. Hawa wanabarikiwa nao wataendelea kubarikiwa. Hivyo, huu mfano wapaswa kutuchochea kwenye utendaji wa bidii zaidi katika huduma ya Kikristo. Kabla ya kuchelewa mno, tunataka tufanye yote tuwezayo ili kutangaza habari njema ya Ufalme na hivyo kuwapa wengine fursa ya kuitikia. Kisha ni juu ya Yesu kutoa hukumu, ya adhabu au ya upendeleo.—Mathayo 25:46.
[Maelezo ya chinis]
a Ona Mnara wa Mlinzi la Februari 15, 1994, kurasa 16-21.
b El Evangelio de Mateo chaeleza: “Uhai udumuo milele ni uhai wa hakika; kinyume chao ni adhabu ya hakika. Kivumishi cha Kigiriki aionios hasa hakionyeshi kipindi cha wakati, bali hali. Adhabu ya hakika ni kifo cha milele.”—Profesa mstaafu Juan Mateos (Pontifical Biblical Institute, Rome) na Profesa Fernando Camacho (Kituo cha Kitheolojia, Seville), Madrid, Hispania, 1981.
Je, Wakumbuka?
◻ Ni milingano gani kati ya Mathayo 24:29-31, (NW) na Mathayo 25:31-33, NW, ionyeshayo kwamba mfano wa kondoo na mbuzi unahusu wakati ujao, nao ni lini?
◻ Ni nani walio “wadogo zaidi sana” wa ndugu za Yesu?
◻ Utumizi wa Yesu wa neno “waadilifu” watusaidiaje kutambulisha ni nani ambao hao wanawakilisha na ni nani ambao hawawakilishi?
◻ Ingawa huu mfano utatimizwa wakati ujao, kwa nini kuhubiri kwetu ni kwa maana sasa na kwenye hima?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa24]
ONA MILINGANO
Mathayo 24:29-31, NW Mathayo 25:31-33, NW
Baada ya dhiki kubwa Mwana wa binadamu yuaja
kuanza, Mwana wa binadamu awasili
Yuaja na utukufu mkubwa Awasili katika utukufu na kuketi katika
kiti chake cha ufalme chenye utukufu
Malaika wako pamoja naye Malaika wawasili pamoja naye
Makabila yote ya dunia Mataifa yote yakusanywa; mbuzi wahukumiwa
yamwona hatimaye (dhiki kubwa yaisha)
[Hisani]
Garo Nalbandian