Msanii Aliyepuuzwa Zaidi wa Wakati Wetu
“Asili ni usanii wa Mungu.”—Sir Thomas Browne, daktari wa karne ya 17.
LEONARDO DA VINCI, Rembrandt, van Gogh—haya ni majina yajulikanayo kwa mamilioni. Hata ingawa huenda hujapata kamwe kuona moja ya michoro yao ya awali, unawajua wanaume hawa kuwa wasanii wakuu. Usanii wao, umewafanya wakumbukwe daima.
Walidhihirisha kwenye vitambaa tabasamu iliyofichika, picha yenye kuathiri hisia kwa kina, mwono wa urembo ulio katika uumbaji, mambo ambayo bado yana uvutano kwenye uwezo wa kufikiri wa mtazamaji. Tunavutiwa na kile kilichowavutia—hata ingawa twaishi karne nyingi baada yao.
Huenda tusiwe wala wasanii wala wahakiki wa sanaa, lakini twaweza bado kutambua ubora wa kisanaa. Kama msanii ambaye tunavutiwa na kazi yake, sisi pia tuna utambuzi na uthamini kuelekea urembo. Uwezo wetu wa kutambua rangi, umbo, vigezo, na nuru huenda ukawa jambo tunalopuuza, lakini ni sehemu ya maisha zetu. Hakuna shaka kwamba sisi hupenda kupamba nyumba zetu na vitu au michoro ambayo hupendeza jicho. Ingawa upendezi hutofautiana, uwezo huu wa kutambua urembo ni zawadi iliyo na wengi wa jamii ya kibinadamu. Ni zawadi ambayo yaweza kutuvuta karibu zaidi na Muumba wetu.
Ile Zawadi ya Urembo
Uwezo wa kutambua urembo ni moja ya sifa nyingi ambazo hutofautisha wanadamu na wanyama. Kitabu Summa Artis—Historia General del Arte (Maandishi ya Kina ya Sanaa—Historia ya Jumla ya Sanaa) hutaja kwamba “mwanadamu aweza kufafanuliwa kuwa mnyama aliye na uwezo wa kutambua thamani ya urembo.” Kwa kuwa tunatofautiana na wanyama twaona uumbaji kwa njia tofauti. Je, mbwa hung’amua machweo yenye kupendeza?
Ni nani aliyetufanya hivyo? Biblia hueleza kwamba ‘Mungu akamwumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba.’ (Mwanzo 1:27) Si kwamba wazazi wetu wa kwanza walifanana na Mungu. Badala ya hivyo, Mungu aliwapa sifa alizo nazo yeye mwenyewe. Moja ya hizo ni uwezo wa kuthamini urembo.
Kwa taratibu isiyoweza kufahamika ubongo wa binadamu hutambua urembo. Kwanza kabisa, hisi zetu hupeleka habari kwenye ubongo kuhusu sauti, harufu, rangi, na maumbo ya vitu vinavyovutia uangalifu wetu. Lakini urembo ni zaidi tu ya jumla ya mipwito hiyo ya kielektrokemikali, ambayo hutuambia tu kile kinachotendeka karibu nasi. Hatuoni mti, ua, au ndege katika namna ileile mnyama anavyoona. Ingawa vitu hivi haviwezi kutupa manufaa yenye kutumika ya papo hapo, kwa vyovyote hivyo hutupa raha. Ubongo wetu hutuwezesha tutambue thamani yavyo ya kisanaa.
Uwezo huu hugusa hisia zetu na kuboresha maisha zetu. Mary anayeishi Hispania, akumbuka vizuri sana jioni moja ya Novemba miaka kadhaa iliyopita aliposimama kando ya ziwa lililo mbali sana na kutazama machweo. “Likipuruka kunielekea lilikuja kundi baada ya kundi la korongo wakiitana,” yeye asema. “Maelfu ya ndege yalisonga kwa mistari kuvuka anga jekundu kwa vigezo vya kibuibui. Safari yao ya kila mwaka ya uhamaji kutoka Urusi na Scandinavia iliwafikisha mahali hapa pa kupumzikia pa Kihispania. Ono hilo lilikuwa lenye kuvutia mno hivi kwamba lilinifanya nilie.”
Kwa Nini Tulipewa Zawadi ya Urembo?
Kwa watu wengi uwezo wa kutambua urembo huonyesha waziwazi kuwapo kwa Muumba mwenye upendo, ambaye ataka uumbaji wake wenye akili ufurahie sanaa yake. Ni jambo la akili na la kutosheleza kama nini kumpatia sifa Muumba mwenye upendo kwa ajili ya uwezo wetu wa kutambua urembo. Biblia hueleza kwamba “Mungu ni upendo,” na umaana halisi wa upendo ni kushiriki na wengine. (1 Yohana 4:8; Matendo 20:35) Yehova amependezwa na kushiriki usanii wake wa ubuni pamoja nasi. Ikiwa muziki wenye kupendeza haungesikiwa kamwe au mchoro wenye kuvutia haungeonekana kamwe, urembo wavyo ungepotea. Sanaa hubuniwa ili ishirikiwe na kufurahiwa—hiyo haifai kitu ikikosa watazamaji.
Ndiyo, Yehova aliumba vitu vyenye kuvutia kwa kusudi—ili watu wavishiriki na kuvifurahia. Kwa hakika, makao ya wazazi wetu wa kwanza yalikuwa bustani ya paradiso iliyoenea sana iliyoitwa Edeni—ambalo humaanisha “Raha.” Mungu hajajaza dunia kwa sanaa tu bali pia amewapa wanadamu uwezo wa kuitambua na kuithamini. Na jinsi kulivyo na urembo mwingi wa kutazama! Kama alivyoonelea Paul Davies, “nyakati fulani yaonekana kana kwamba asili ‘ilikuwa ikifanya jitihada ya kipekee’ ili kutokeza ulimwengu wote mzima wenye kupendeza na wenye mazao.” Twaona ulimwengu wote mzima ukipendeza na ukiwa na mazao hasa kwa sababu Yehova ‘amefanya jitihada ya kipekee’ kutuumba tukiwa na uwezo wa kuuchunguza na kuufurahia.
Haishangazi kwamba utambuzi wa urembo wa asili—na tamaa ya kuuiga—ni jambo la kawaida kwa tamaduni zote, kutoka wakale waliochora kwenye kuta za pango hadi wasanii. Maelfu ya miaka iliyopita, wakazi wa magharibi mwa Hispania walichora picha zilizo wazi sana za wanyama katika mapango ya Altamira, Cantabria. Zaidi ya karne moja iliyopita, wasanii walio wachoraji walitoka katika mahali pao pa kazi ili kujaribu kuchora maonyesho mangavu ya rangi katika shamba la maua au vigezo vinavyobadilika vya nuru katika maji. Hata watoto wadogo wanatambua kwa umakini vitu vyenye kupendeza. Kwa hakika, wengi wao wanapopewa kalamu za rangi na karatasi hupenda kuchora chochote wanachoona ambacho hunasa uwezo wao wa kufikiri.
Siku hizi, watu wazima wengi hupendelea kupiga picha ili kukumbuka mandhari yenye kuvutia ambayo iliwapendeza. Lakini hata bila kamera, akili zetu zaweza kukumbuka sura zenye urembo ambazo huenda tuliona miongo mingi iliyopita. Kwa wazi, Mungu ametufanya tukiwa na uwezo wa kufurahia makao yetu ya kidunia, ambayo ameyapamba kwa ubora wenye kupendeza. (Zaburi 115:16) Hata hivyo, kuna sababu nyingine, kwa nini Mungu alitupa uwezo wa kutambua urembo.
‘Sifa Zake Zaonwa Wazi’
Kuongeza uthamini wetu kwa sanaa iliyo katika asili, kwaweza kutusaidia kupata kumjua Muumba wetu, ambaye kazi ya mikono yake yatuzunguka. Katika pindi moja Yesu aliwaambia wanafunzi wake watazame kwa ukaribu maua ya porini yaliyokuwa yakikua kote katika Galilaya. “Fikirini maua ya mashamba,” yeye akasema, “jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.” (Mathayo 6:28, 29) Urembo wa ua la porini lisilo na umaana mkubwa waweza kutumika kutukumbusha kwamba Mungu hapuuzi mahitaji ya familia ya kibinadamu.
Yesu alisema pia kwamba unaweza kumjua mtu kwa “matunda,” au kazi zake. (Mathayo 7:16-20) Kwa hiyo, inapasa kutarajiwa tu kwamba kazi za uumbaji za Mungu zingetupa ufahamu wenye kina kuhusu utu wake. Ni nini baadhi ya ‘sifa zake ambazo zaonwa waziwazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu na kuendelea’?—Warumi 1:20, NW.
“Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako!” akapaaza sauti mtunga zaburi. “Kwa hekima umevifanya vyote pia.” (Zaburi 104:24) Hekima ya Mungu yaweza hata kutambuliwa katika rangi ambazo ametumia “kuchora” mimea na wanyama wa dunia. “Rangi huchangamsha moyo na macho,” wataja Fabris na Germani katika kitabu chao Colore, Disegno ed estetica nell’arte grafica (Rangi—Ubuni na Ubora katika Sanaa ya Kuchorwa). Rangi zenye upatano na zenye kutofautiana, ambazo hufurahisha macho na kuchangamsha moyo ziko kila mahali. Lakini labda zenye kutokeza kuliko zote ni zile rangi zinazotokezwa wakati kitu chenye kung’aa kinapogeuzwa-geuzwa—rangi kama zile za upinde wa mvua—ushuhuda wenye kutokeza wa ubuni wenye hekima.
Rangi zinazotokezwa wakati kitu chenye kung’aa kinapogeuzwa-geuzwa ni za kawaida hasa katika ndege-wavumi.a Ni nini kifanyacho manyoya yao yang’ae sana? Sehemu ya juu ya tatu ya manyoya yao ya kipekee huvunja nuru ya jua kuwa rangi tofauti-tofauti zilizo kama upinde—kama vile mche ufanyavyo. Majina ya kienyeji ya ndege-wavumi, kama vile yakuti, yakuti samawi, na zumaridi, kwa kufaa hushuhudia rangi zenye kung’aa nyekundu, buluu, na kijani kibichi ambazo hupamba ndege hawa walio kama johari. “Ni nini kusudi la urembo huu wenye fahari wa viumbe hawa wenye ubora unaovutia?” auliza Sara Godwin katika kitabu chake Hummingbirds. “Kwa kadiri sayansi iwezavyo kupambanua, hauna kusudi duniani ila kumduwaza mtazamaji,” yeye ajibu. Kwa hakika, hakuna msanii wa kibinadamu aliyepata kuwa na kibao cha kufanyizia rangi kama hicho!
Twaweza kutambua uweza wa Mungu katika maporomoko ya maji yenye kuvuma, kujaa na kupwa kwa maji ufuoni, mawimbi meupe yenye kutwanga fuo, au miti mirefu mno ya misitu inayopindwa na nguvu za upepo. Sanaa hii ya ajabu yaweza kuwa yenye kuvutia tu kama mandhari tulivu. Aliyekuwa mstadi wa asili Mmarekani John Muir wakati mmoja alifafanua hivi athari ya dhoruba kwa kikundi cha miti aina ya Douglas fir katika Sierra Nevada ya California:
“Ingawa ilikuwa michanga kwa kulinganishwa, ilikuwa na urefu wa futi 100, na vilele vyayo vinavyonyumbuka kwa urahisi na vilivyochanuka vilikuwa vikibembea na kuzunguka kwa mvurugo usioweza kudhibitiwa. . . . Vile vilele vyembamba vilipunga na kuvurumika kabisa katika mvua kubwa mno isiyo tulivu, vikipindika na kuzunguka nyuma na mbele, kuvurura, vikifuata vizingo vilivyonyooka na vilivyo tambarare visivyoweza kufafanuliwa.” Kama mtunga-zaburi alivyoandika maelfu ya miaka iliyopita, ‘upepo wa dhoruba humsifu Yehova’—hutupatia kiolezo cha uwezo wake upitao wa kawaida.—Zaburi 148:7, 8.
Ndege amejulikana kwa muda mrefu kuwa mfano wa upendo kwa Wajapani. Ni korongo mwenye kuvutia wa Kijapani, ambaye dansi zake zenye madoido za kutafuta uchumba zina madaha kama kikundi chochote cha kucheza dansi. Wachezaji hao wa kindege wanaheshimiwa sana hivi kwamba wameainishwa katika Japani kuwa “ukumbuko wa pekee wa asili.” Kwa kuwa korongo hukaa wawili-wawili kwa muda wote wa maisha yao na wanaweza kuishi kwa miaka 50 au zaidi, Wajapani huwaona kuwa mfano bora zaidi wa uaminifu wa ndoa.
Namna gani upendo wa Mungu? Kwa kupendeza, Biblia hulinganisha ulinzi wa Yehova wenye upendo kuelekea waaminifu wake na ule wa mzazi wa ndege atumiaye mabawa yake kufunika watoto wake kutokana na hali mbaya ya hewa. Kumbukumbu la Torati 32:11, husema juu ya tai “ataharikishaye kioto chake, na kupapatika juu ya makinda yake, akikunjua mbawa zake, akawatwaa, akawachukua juu ya mbawa zake.” Tai mzazi hufanya mambo haya ili kutia moyo makinda yaondoke kiotani na kupuruka. Ingawa huonekana mara chache sana, kuna visa vilivyoripotiwa vya tai wakisaidia makinda yao kwa kuwabeba juu ya mbawa zao.—Zaburi 17:8.
Tunapotazama kwa ukaribu ulimwengu wa asili unaotuzunguka, twaona kanuni fulani zikifanya kazi ambazo pia zafunua sehemu nyingine za utu wa Mungu.
Unamna-Namna Ndio Kikolezo cha Maisha
Unamna-namna katika kazi ya mikono ya Mungu ni jambo linaloonekana wazi mara moja. Unamna-namna wa mimea, ndege, wanyama, na wadudu ni wenye kushangaza. Hektari moja tu ya msitu wa kitropiki yaweza kuwa na spishi 300 tofauti za miti na spishi 41,000 za wadudu; kilometa tatu za mraba zaweza kuwa makao ya asili ya aina tofauti 1,500 za vipepeo; na mti mmoja waweza kuwa makao ya spishi 150 za mbawakawa! Na kama vile hakuna watu wawili wafananao kabisa, inaweza kusemwa vivyo hivyo kuhusu miti ya oki au simbamarara. Ujianzilishaji, sifa inayoheshimiwa miongoni mwa wasanii wa kibinadamu, ni sehemu muhimu sana ya asili.
Bila shaka, tumetaja kifupi tu sehemu chache za usanii wa asili. Kwa kuutazama kwa ukaribu zaidi, twaweza kutambua sehemu nyingine nyingi za utu wa Mungu. Lakini ili kufanya hilo, twahitaji kutumia uwezo wetu wa kisanaa wa kutambua na kuthamini tuliopewa na Mungu. Twaweza kujifunzaje kuthamini vema zaidi usanii wa Msanii mkuu kuliko wote?
[Maelezo ya Chini]
a Vipepeo wengi, kama vile mofo wa Amerika ya kitropiki wenye rangi zenye kutokeza za buluu, wana magamba yenye kutokeza rangi mbalimbali kwenye mabawa yao.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Twahitaji Kujua Ni Nani Aliyetuweka Hapa
Mtafsiri wa Biblia Ronald Knox wakati mmoja alijihusisha katika mazungumzo ya kitheolojia pamoja na mwanasayansi John Scott Haldane. “Katika ulimwengu wote mzima ulio na mamilioni ya sayari,” akasababu Haldane, “je, haielekei kwamba uhai wapaswa kuwa angalau kwa moja yazo?”
“Bwana,” akajibu Knox, “ikiwa wapelelezi wa Scotland Yard wangepata maiti katika mahali pa kuwekea mizigo pa gari lako, je, ungewaambia: ‘Kuna mamilioni ya mahali pa kuwekea mizigo ulimwenguni—kwa kweli lazima kuna mojapo palipo na maiti?’ Nafikiri bado watataka kujua ni nani aliyeiweka hapo.”—The Little, Brown Book of Anecdotes.
Zaidi ya kutosheleza udadisi wetu, kuna sababu nyingine kwa nini ni lazima tujue ni nani aliyetuweka hapa—ili tumpe Yeye sifa anayostahili. Msanii mwenye kipawa angeitikiaje ikiwa mhakiki mkaidi angefafanua mchoro wake kuwa aksidenti tu katika duka la rangi? Vivyo hivyo, ni suto lililoje tungekuwa tukimwekea Muumba wa ulimwengu wote mzima kwa kuelekezea sanaa yake kwa tukio la ghafula lisilotazamiwa?
[Hisani]
Kwa hisani ya ROE/Anglo-Australian Observatory, picha na David Malin
[Picha katika ukurasa wa 8]
Korongo wakiruka
Michoro ya pangoni katika Altamira, Hispania
[Picha katika ukurasa wa 9]
Dolfini, ndege-wavumi, na maporomoko ya maji vyote hufunua sehemu za utu wa Msanii Mkuu
[Hisani]
Godo-Foto
G. C. Kelley, Tucson, AZ
Godo-Foto