Johari la Kutoka Gospeli ya Mathayo
YEHOVA MUNGU alimvuvia Mathayo aliyekuwa mkusanya kodi ili aandike usimulizi wa kusisimua juu ya uzaliwa, maisha, kifo, na ufufuo wa Yesu Kristo. Maandishi yaliyo katika hati-mkono kadhaa za baada ya karne ya kumi yanasema kwamba Gospeli hii iliandikwa karibu mwaka wa nane baada ya kupaa kwa Yesu (karibu 41 W.K.). Jambo hili halipingani na ushuhuda wa ndani, kwa kuwa usimulizi unamalizika huku Yesu akitoa utume wa kuwa wafanya-wanafunzi katika 33 W.K. wala hausemi lolote juu ya uharibifu wa Yerusalemu mikononi mwa Waroma katika 70 W.K.
Katika Historia Ecclesiastica (Historia ya Kimahubiri), Eusebio mwanahistoria wa karne ya nne ananukuu maneno ya Papiasi na Irenayo wa karne ya pili na Origeni wa karne ya tatu, wote hao wakimhesabu Mathayo kuwa mwandikaji wa Gospeli hii na kusema kwamba aliiandika katika Kiebrania. Je! kweli hiki kilikuwa Kiaramu? Si kulingana na hati zilizotajwa na George Howard, profesa wa dini kwenye Chuo Kikuu cha Georgia. Yeye aliandika hivi: “Dhana hii ilisababishwa hasa na imani ya kwamba Kiebrania katika siku za Yesu hakikuwa tena kikitumiwa katika Palestina bali Kiaramu kilikuwa kimechukua mahali pacho. Ugunduzi uliofuata wa Hati-Kunjo za Bahari ya Ufu, nyingi zazo zikiwa ni insha za Kiebrania, na pia ugunduzi wa hati nyingine za Kiebrania kutoka Palestina za tangu kipindi cha ujumla cha wakati wa Yesu, sasa unaonyesha kwamba katika karne ya kwanza Kiebrania kilikuwako kikiwa salama salimini.” Yaonekana wazi kwamba Mathayo aliandika Gospeli yake ili kunufaisha Wakristo Waebrania, lakini huenda akawa aliitafsiri pia katika Kigiriki cha watu wa kikawaida.
Twakuhimiza uisome Gospeli ya Mathayo. Tutazamapo baadhi ya johari zilizomo, angalia habari nyingine ndogo-ndogo zinazohusianishwa nayo ili kuuelewesha wazi usimulizi.
Uzaliwa na Huduma ya Mapema
Gospeli ya Mathayo yaanza na orodha ya vizazi na uzaliwa wa Yesu. Mariamu alipopatwa kuwa mwenye mimba, mchumba wake, Yusufu, “aliazimu kumwacha kwa siri.” (1:19) Lakini angewezaje kufanya hivyo, kwa kuwa walikuwa wamefanya posa tu? Basi, kwa Wayahudi mwanamke aliyeposwa alikuwa na wajibu mbalimbali ulio sawa na wanawake walioolewa. Kama angefanya ngono na mtu fulani, angeweza kupigwa kwa mawe kama mwanamke mzinzi. (Kumbukumbu 22:23-29) Kwa hiyo, kwa sababu posa ilifunga mtu katika wajibu, Yusufu alipanga kutaliki Mariamu, ingawa hakuna sherehe yoyote iliyokuwa imewaungamanisha katika kifungo cha ndoa.
Sura za mapema za Gospeli ya Mathayo zina Mahubiri ya Mlimani aliyoyatoa Yesu. Humo, Kristo alionya kwamba mtu angekuwa na wajibu wa kuitolea hesabu “Mahakama Kuu Zaidi” kwa kutaja ndugu kwa “neno lisiloneneka la madharau.” (5:22, NW) Uneni huo ulikuwa ni kama mtu kumwita ndugu yake kuwa lijinga lenye kichwa maji tu.
Lakini “Mahakama Kuu Zaidi” ilikuwa nini? Ilikuwa Sanhedrini ya Yerusalemu yenye washiriki 71. Ni malezi gani yaliyohitajiwa ili kustahili kuwa mshiriki humo? Yasema hivi Cyclopedia ya McClintock na Strong: “Mwenye kuomba kuwa humo ilikuwa ni lazima awe bila lawama la kiadili wala la kimwili. Ilikuwa ni lazima awe ana umri wa makamo, mrefu, mwenye sura nzuri, tajiri, mwenye kisomo . . . Alitakwa kujua lugha kadhaa . . . Watu wazee sana, waongofu, matowashi, na Wanethini hawakufaa kwa sababu ya vikasoro-kasoro vyao; wala watakauchaguzi wasio na watoto hawangeweza kuchaguliwa, kwa sababu hawangeweza kuonyesha huruma katika mambo ya kinyumbani. . . ; wala wale wasioweza kuthibitisha kwamba walikuwa wazao halali wa kuhani, Mlawi, au Mwisraeli. . . . Mtakauchaguzi kuhusiana na ile Sanhedrini Kuu alitakwa, kwanza kabisa, awe alikuwa hakimu katika mji wa kwao; awe alihamia huko kutoka ile Sanhedrini Ndogo . . . , halafu tena awe alipanda cheo akafikia ile Sanhedrini Ndogo ya pili . . . kabla hajaweza kupokewa kuwa mshiriki wa ile yenye watu sabini na mmoja.”
Kwa hiyo Yesu alimaanisha kwamba “yeyote aambiaye ndugu yake neno lisiloneneka la madharau” achukua hatia yenye kulinganika na ile ya mtu aliyeshtakiwa na kuhukumiwa kifo na Mahakama Kuu Zaidi ya Kiyahudi. Hilo ni onyo lililoje la kutoharibu sifa ya ndugu zetu! Acheni tuutie lijamu ulimi wetu ili tusistahili kamwe kushutumiwa katika Mahakama ya Juu Zaidi, mbele za Yehova, “Hakimu wa dunia yote.”—Mwanzo 18:25, NW; Yakobo 3:2-12.
Yesu Mwalimu Mwenye Matokeo
Pia Gospeli hii inamwonyesha Yesu akiwa mwalimu awezaye kujibu maswali kwa ustadi. Kwa kielelezo, katika kujibu swali moja, yeye alieleza kwa nini wanafunzi wake hawakufunga. (9:14-17) Wao hawakuwa na sababu ya kufunga akiwa angali hai. Lakini kama alivyotabiri, walifunga na kuomboleza alipokufa kwa sababu hawakujua kwa nini kifo chake kiliruhusiwa. Hata hivyo, baada ya kupokea roho takatifu kwenye Pentekoste, waliangaziwa elimu na hawakufunga tena kwa majonzi.
Bado akishughulikia habari iyo hiyo, Yesu aliongezea kwamba hakuna mtu ambaye hupachika vazi la zamani kiraka cha nguo ambayo haijarudi kwa sababu imara ya nguo hiyo hufanya vazi liraruke hata zaidi. Pia alisema kwamba divai mpya haitiwi ndani ya viriba vya zamani. Kiriba, au chupa-ngozi, kilikuwa ni ngozi ya mnyama iliyotiwa dawa ili ikauke na ikashonwa karibu kila mahali isipokuwa nafasi wazi ya mguuni. Divai mpya yenye kuchacha hufanyiza kaboni dayoksaidi yenye kutokeza mkazo wa kutosha kupasua viriba vya zamani, vilivyokauka. Kwa ulinganisho, ukweli alioufundisha Kristo ulikuwa na nguvu nyingi mno kwa dini ya Kiyahudi iliyokuwa ya zamani, isiyopindikana. Zaidi ya hilo, yeye hakuwa akijaribu kupachika viraka katika mfumo wowote wa kidini uliochakaa wala kuudumisha pamoja na desturi zao za kufunga na desturi nyinginezo. Bali, Mungu alitumia Yesu kuanzisha mfumo mpya wa ibada. Basi, kwa uhakika haitupasi kufanya jambo lolote la kuunga mkono harakati zozote za kuchanganya imani mbalimbali wala kuidumisha dini bandia.
Tii Shauri Kutoka kwa Mwana wa Mungu
Kulingana na usimulizi wa Mathayo wa kugeuka sura, Mungu alimwita Yesu kuwa ni Mwana Wake mkubaliwa na akasema kwamba inatupasa tumsikilize. (17:5) Kwa hiyo yatupasa tutii shauri lote la Kristo, kama vile onyo lake kwamba ingekuwa afadhali yeyote anayekwaza mtu mwenye kumwamini azamishwe baharini akiwa amefungiliwa shingoni jiwe la kusagia. (18:6) Hili lilikuwa jiwe la aina gani? Si jiwe dogo, kwa maana Yesu alimaanisha jiwe la kusagia la upande wa juu, lenye mviringo wa meta 1.2 hadi 1.5. Kuligeuza likiwa juu ya jiwe kubwa la upande wa chini kulihitaji utumizi wa nguvu za mnyama. Hakuna mtu ambaye angeweza kuokoka baharini akiwa amefungiliwa shingoni uzito mkubwa hivyo. Basi, Yesu alikuwa akitushauri tuepuke hatia ya kukwaza yeyote wa wafuasi wake. Akiwa na kusudio la jinsi iyo hiyo, mtume Paulo aliandika hivi: “Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lo lote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa.”—Warumi 14:21.
Mwana wa Mungu alitoa shauri lisilo la moja kwa moja alipotangaza ole juu ya waandishi na Mafarisayo na kusema kwamba walifanana na makaburi yaliyopakwa chokaa. (23:27, 28) Ilikuwa desturi kuosha makaburi na maziara ili watu wasiyaguse kiaksidenti wakawa wasio safi. Kwa kugusia zoea hili, Yesu alionyesha kwamba waandishi na Mafarisayo walionekana waadilifu njenje lakini ‘walijaa unafiki na maasi.” Kutii shauri hili lenye kudokezwa hapo kutatusababisha tuepuke kabisa mambo ya kombokombo na tutende ‘kwa imani isiyo na unafiki.’— 1 Timotheo 1:5; Mithali 3:32; 2 Timotheo 1:5.
Kielelezo Chetu Mshika Ukamilifu
Baada ya kuandika unabii wa Yesu juu ya ‘ishara ya kuwapo kwake,’ Mathayo anaeleza juu ya kusalitiwa kwa Kristo, kukamatwa, kujaribiwa, kuuawa, na kufufuliwa kwake. Akiwa juu ya mti, Yesu alikataa kunywa divai iliyochanganywa na nyongo, kitu chenye nguvu kama dawa ya kufisha ganzi. (27:34) Ilikuwa desturi ya wanawake kuwapa wahalifu divai ya jinsi hiyo ili kufisha maumivu ya kutundikwa mtini. Marko 15:23 inasema kwamba divai hiyo ‘ilitiwa mane-mane,’ ambayo ingeiongezea ladha nzuri. Yaonekana kwamba vyote viwili, nyongo na manemane, vilikuwa katika divai ambayo Kristo aliikataa. Alipokuwa akifikia upeo wa mwendo wake wa kidunia, yeye hakutaka kutiliwa dawa za kulevya wala kuzubaishwa akili. Yesu alitamani kujiweza hisia zake ili awe mwaminifu mpaka kifo. Kama huyo Kielelezo chetu, sikuzote sisi na tuhangaikie kushika ukamilifu wetu kwa Yehova Mungu.—Zaburi 26:1, 11.