Maria (Mama ya Yesu)
Maana: Mwanamke aliyechaguliwa na Mungu na kupendelewa sana ambaye alimzaa Yesu. Kuna Maria wengine watano wanaotajwa katika Biblia. Huyu alikuwa mzao wa Mfalme Daudi, wa kabila la Yuda, na binti ya Heli. Anapotajwa mara ya kwanza katika Maandiko, amechumbiwa na Yosefu, ambaye pia ni wa kabila la Yuda na mzao wa Daudi.
Tunaweza kujifunza nini kutokana na masimulizi ya Biblia kumhusu Maria?
(1) Kuwa na nia ya kusikiliza anayosema Mungu kupitia wajumbe wake hata ingawa tunayosikia huenda kwanza yakatusumbua au yakaonekana kuwa mambo yasiyowezekana.—Luka 1:26-37.
(2) Ujasiri wa kutenda kupatana na mapenzi ya Mungu ambayo amejifunza, na kumtumaini kabisa. (Ona Luka 1:38. Kama inavyoonyeshwa katika Kumbukumbu la Torati 22:23, 24, kungekuwa na matokeo mabaya ikiwa msichana Myahudi ambaye hajaolewa angepata mimba.)
(3) Nia ya Mungu kumtumia mtu bila kujali cheo chake maishani.—Linganisha Luka 2:22-24 na Mambo ya Walawi 12:1-8.
(4) Kutanguliza mambo ya kiroho. (Ona Luka 2:41; Matendo 1:14. Sheria haikuwataka wake Wayahudi wafunge safari ndefu pamoja na waume wao kwenda Yerusalemu wakati wa Pasaka kila mwaka, lakini Maria alifanya hivyo.)
(5) Kuthamini usafi wa kiadili.—Luka 1:34.
(6) Kuwa na bidii ya kufundisha watoto Neno la Mungu. (Hilo linaonekana kutokana na mambo ambayo Yesu alifanya akiwa na umri wa miaka 12. Ona Luka 2:42, 46-49.)
Je, kwa kweli Maria alikuwa bikira alipomzaa Yesu?
Luka 1:26-31 (BHN) husema kwamba “bikira” anayeitwa Maria ndiye ambaye malaika Gabrieli alimpelekea habari hizi: “Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu.” Ndipo, mstari wa 34 unasema hivi: “Maria akamjibu, Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira [“sijui mume,” UV; “silali na mwanamume,” NW]?” Mathayo 1:22-25 (UV) huongeza hivi: “Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.”
Je, jambo hilo linawezekana? Bila shaka halikuwa jambo lisilowezekana kwa Muumba, aliyeumba viungo vya uzazi vya wanadamu, kutungisha mimba yai katika tumbo la uzazi la Maria kwa njia isiyo ya asili. Kwa njia ya ajabu, Yehova alihamisha nguvu za uhai pamoja na utu wa Mwanawe mzaliwa wa kwanza wa mbinguni mpaka kwenye tumbo la uzazi la Maria. Nguvu za utendaji za Mungu mwenyewe, roho yake takatifu, zililinda ukuzi wa mtoto katika tumbo la Maria hivi kwamba mtoto huyo akazaliwa akiwa mwanadamu mkamilifu.—Luka 1:35; Yoh. 17:5.
Je, Maria alikuwa bikira sikuzote?
Mt. 13:53-56, UV: “Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze [Kigiriki, a·del·phoiʹ] si Yakobo, Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu [Kigiriki, a·del·phaiʹ] yake wote hawapo hapa petu?” (Kulingana na andiko hilo, je, ungekata shauri kwamba Yesu alikuwa mtoto pekee wa Maria au kwamba Maria alikuwa na wana wengine na pia mabinti?)
New Catholic Encyclopedia (1967, Buku la 9, uku. 337) inasema kuhusu maneno ya Kigiriki a·del·phoiʹ na a·del·phaiʹ, yaliyotumiwa katika Mathayo 13:55, 56, kwamba “kwa Wagiriki wa wakati wa Mweneza-Injili huyo, maneno hayo yalimaanisha ndugu na dada wa damu kamili, naye msomaji Mgiriki angeyaelewa vivyo hivyo. Kuelekea mwisho wa karne ya 4 (mwaka wa 380 hivi) Helvidius katika kitabu chake ambacho sasa kimepotea alikazia uhakika huo ili kuonyesha kwamba Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu ili kumfanya awe kielelezo kwa akina mama wenye familia kubwa. Mtakatifu Jerome, akichochewa na imani ya kimapokeo ya Kanisa kuhusu ubikira wa milele wa Maria, aliandika trakti ya kumpinga Helvidius (W.K. 383) iliyoeleza . . . mambo ambayo bado yanafuatwa na wasomi Wakatoliki.”
Marko 3:31-35, UV: “Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu, na umbu langu, na mama yangu.” (Hapa kuna tofauti iliyo wazi kati ya ndugu za asili za Yesu na ndugu zake wa kiroho, wanafunzi wake. Hakuna anayedai kwamba mtajo kuhusu mama ya Yesu unamaanisha mtu mwingine tofauti na mama yake. Je, ni jambo linalopatana na akili, kusema kwamba ndugu zake wa asili hawakuwa hivyo bali pengine walikuwa binamu zake? Ikiwa wanaotajwa ni watu wa ukoo, wala si ndugu, neno tofauti la Kigiriki [syg·ge·nonʹ] hutumiwa, kama vile katika Luka 21:16.)
Je, Maria alikuwa Mama ya Mungu?
Malaika aliyemwambia kuhusu mtoto huyo ambaye angezaliwa kimuujiza hakusema kwamba mwanawe angekuwa Mungu. Alisema hivi: “Utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu. . . . Hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”—Luka 1:31-35, UV; italiki zimeongezwa.
Ebr. 2:14, 17, UV: “Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye [Yesu] vivyo hivyo alishiriki yayo hayo . . . Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote.” (Lakini ikiwa yeye angalikuwa Mungu-mtu, je, yeye ‘angalifananishwa na ndugu zake katika mambo yote’?)
New Catholic Encyclopedia inasema hivi: “Maria ni mama ya Mungu kwelikweli ikiwa masharti mawili yanatimizwa: kwamba yeye kwelikweli ni mama ya Yesu na kwamba kwelikweli Yesu ni Mungu.” (1967, Buku la 10, uku. 21) Biblia inasema kwamba Maria alikuwa mama ya Yesu, lakini je, Yesu alikuwa Mungu? Katika karne ya nne, muda mrefu baada ya Biblia kumalizika kuandikwa, Kanisa lilitunga taarifa yake ya Utatu. (New Catholic Encyclopedia, 1967, Buku la 14, uku. 295; ona ukurasa wa 367, chini ya kichwa “Utatu.”) Wakati huo katika Imani ya Nisea, Kanisa lilisema kwamba Yesu Kristo ni “Mungu mwenyewe.” Baada ya hapo, katika Baraza la Efeso mwaka wa 431 W.K., Maria alitangazwa na Kanisa kuwa The·o·toʹkos, maana yake “Mzaa-Mungu” au “Mama ya Mungu.” Hata hivyo, neno hilo wala wazo hilo halipatikani katika maandishi ya tafsiri yoyote ya Biblia. (Ona ukurasa wa 430-434, chini ya kichwa “Yesu Kristo.”)
Je, Maria mwenyewe alikingiwa dhambi, wala hakurithi dhambi wakati mama yake alipomchukua mimba?
New Catholic Encyclopedia (1967, Buku la 7, uku. 378-381) inakiri hivi kuhusu chanzo cha imani hiyo: “ . . . [maneno] Mkingiwa Dhambi ya Asili hayafundishwi waziwazi katika Maandiko . . . Mababa wa kwanza wa Kanisa walimwona Maria kuwa mtakatifu lakini si asiye na dhambi kabisa . . . . Haiwezekani kutoa tarehe barabara wakati fundisho hilo liliposhikiliwa kuwa imani, lakini kufikia karne ya 8 au 9 inaonekana kwamba lilikuwa limekubaliwa kwa ujumla. . . . [Katika mwaka wa 1854 Papa Pius wa Tisa alifafanua fundisho hilo] ‘linalosema kwamba Bikira Maria alilindwa asipatwe na madoa yoyote ya dhambi ya asili wakati wa Kuchukuliwa Mimba kwake.’” Imani hiyo ilithibitishwa na Baraza la Pili la Vatikani (1962-1965).—The Documents of Vatican II (New York, 1966), kilichohaririwa na W. M. Abbott, S.J., uku. 88.
Biblia yenyewe inasema hivi: “Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja [Adamu] dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.” (Rom. 5:12, UV; italiki zimeongezwa.) Je, Maria pia anatiwa ndani? Biblia inasema kwamba kulingana na takwa la Sheria ya Musa, siku 40 baada ya kuzaliwa kwa Yesu, Maria alitoa toleo la dhambi kwa ajili ya kutakaswa uchafu hekaluni Yerusalemu. Yeye, pia, alikuwa amerithi dhambi na kutokamilika kutoka kwa Adamu.—Luka 2:22-24; Law. 12:1-8.
Je, Maria alipanda mbinguni akiwa na mwili wake wenye nyama?
Katika maelezo yake kuhusu tangazo lililofanywa na Papa Pius wa Kumi na Mbili mwaka wa 1950 lililofanya fundisho hilo kuwa kanuni rasmi ya imani ya Kikatoliki, kitabu New Catholic Encyclopedia (1967, Buku la 1, uku. 972) kinasema hivi: “Katika Biblia hakuna mtajo ulio wazi kuhusu Kuchukuliwa Mbinguni, hata hivyo Papa anasisitiza katika amri ya tangazo kwamba Maandiko ndiyo msingi wa ukweli huu.”
Biblia yenyewe inasema hivi: “Nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.” (1 Kor. 15:50, UV) Yesu alisema kwamba “Mungu ni roho.” Wakati wa kufufuliwa kwa Yesu yeye akawa tena roho, sasa akiwa “roho yenye kuhuisha.” Malaika ni roho. (Yoh. 4:24; 1 Kor. 15:45; Ebr. 1:13, 14, UV) Uko wapi msingi wa Kimaandiko wa kusema kwamba yeyote atapata uzima wa mbinguni akiwa katika mwili unaohitaji mazingira ya dunia ili kuuendeleza hai? (Ona ukurasa wa 320-323, chini ya “Ufufuo.”)
Je, inafaa kumpelekea Maria sala kama mwombezi?
Yesu Kristo alisema: “Ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni . . . ” Alisema pia: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. . . . Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya.”—Mt. 6:9; Yoh. 14:6, 14, UV; italiki zimeongezwa.
Je, sala kwa Baba kupitia Yesu Kristo zitapokewa kwa uelewaji mwingi na huruma kama vile zingepokewa ikiwa zingeelekezwa kupitia mtu fulani ambaye ameshiriki mambo yanayowapata wanawake? Biblia inatuambia hivi kumhusu Baba: “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.” Yeye ni “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli.” (Zab. 103:13, 14; Kut. 34:6, UV) Na imeandikwa hivi kumhusu Kristo: “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”—Ebr. 4:15, 16, UV.
Je, kusujudia sanamu za Maria kunapatana na Ukristo wa Biblia?
Zoea hilo liliungwa mkono waziwazi na Baraza la Pili la Vatikani (1962-1965). “Mkutano huu mtakatifu sana . . . unawashauri wana wote wa Kanisa kwamba madhehebu, hasa madhehebu ya liturjia, ya Bikira Maria, yaendelezwe kabisa. Unaamuru kwamba mazoea ya kumsujudia yathaminiwe kama ilivyopendekezwa na mamlaka ya kufundisha ya Kanisa ya karne nyingi, na kwamba amri zilizotolewa nyakati za zamani kuhusu kusujudiwa kwa sanamu za Yesu, Bikira Maria, na watakatifu, zifuatwe kwa uaminifu.”—The Documents of Vatican II, uku. 94, 95.
Ili kupata jibu la Biblia, ona “Sanamu,” ukurasa wa 260-264.
Je, Maria aliheshimiwa kwa njia ya pekee katika kutaniko la Kikristo la karne ya kwanza?
Mtume Petro hamtaji hata kidogo katika maandishi yake yaliyoongozwa na roho ya Mungu. Mtume Paulo hakutumia jina lake katika barua zake zilizoongozwa na roho ya Mungu bali alimtaja tu kuwa “mwanamke.”—Gal. 4:4.
Yesu mwenyewe aliweka mfano gani kuhusiana na mama yake?
Yoh. 2:3, 4, ZSB: “Wakati mvinyo ulipopunguka [kwenye karamu ya arusi huko Kana], mama yake Yesu akamwambia: Hawana mvinyo. Yesu akamwambia: Mwanamuke, nina nini nawe? Saa haijakuja bado.” (Yesu alipokuwa mtoto alimtii mama yake na baba yake mlezi. Lakini kwa kuwa sasa alikuwa mtu mzima, alikataa kwa fadhili lakini kwa uthabiti mwelekezo wa Maria. Mama yake alikubali sahihisho hilo kwa unyenyekevu.)
Luka 11:27, 28, UV: “Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika!” (Bila shaka huo ulikuwa wakati mzuri wa Yesu kumpa mama yake heshima ya pekee ikiwa jambo hilo lilifaa. Lakini yeye hakufanya hivyo.)
Zoea la kumsujudia Maria lilianzia wapi?
Andrew Greeley, kasisi Mkatoliki anasema hivi: “Maria ni mmoja wa mifano ya kidini yenye nguvu zaidi katika historia ya ulimwengu wa Magharibi . . . Mfano wa Maria unaunganisha Ukristo moja kwa moja na dini za kale za miungu-mama.”—The Making of the Popes 1978 (U.S.A., 1979), uku. 227.
Jambo la kupendeza ni mahali lilipothibitishiwa lile fundisho la kwamba Maria ndiye Mama ya Mungu. “Baraza la Efeso lilikusanyika katika kanisa la Theotokos mwaka wa 431. Haishangazi kwamba lile jina la cheo ‘Mzaa-Mungu’ halingekosa kukubaliwa, katika jiji lililojulikana sana kwa kuabudu Artemi, au Diana kama Waroma walivyomwita, ambapo ilisemekana kwamba sanamu yake ilianguka kutoka mbinguni, katika kivuli cha hekalu kubwa lililowekwa wakfu kwa Mama Mkuu tangu mwaka wa 330 K.W.K. na lililokuwa, kulingana na mapokeo, makao ya muda ya Maria.”—The Cult of the Mother-Goddess (New York, 1959), E. O. James, uku. 207.
Mtu Akisema—
‘Je, mnamwamini Bikira Maria?’
Unaweza kujibu hivi: ‘Maandiko Matakatifu yanasema waziwazi kwamba mama ya Yesu Kristo alikuwa bikira, nasi tunaamini hivyo. Mungu alikuwa Baba yake (Yesu). Mtoto aliyezaliwa alikuwa kweli Mwana wa Mungu, kama malaika alivyomwambia Maria. (Luka 1:35)’ Kisha unaweza kuongezea: ‘Lakini umewahi kujiuliza kwa nini ilikuwa muhimu kwamba Yesu azaliwe kwa njia hiyo? . . . Ni kwa njia hiyo tu fidia inayofaa ingeweza kutolewa, fidia ambayo ingefanya iwezekane kwetu kufunguliwa kutoka katika dhambi na kifo.—1 Tim. 2:5, 6; kisha unaweza kusoma pia Yoh. 3:16.’
Au unaweza kusema: ‘Ndiyo, tunamwamini. Tunaamini kila jambo ambalo Maandiko Matakatifu yanasema kumhusu, nayo yanasema waziwazi kwamba alikuwa bikira alipomzaa Yesu. Pia mambo mengine ambayo Maandiko yanatuambia kumhusu Maria na yale tunayoweza kujifunza kutoka kwake yananichangamsha moyo sana. (Tumia habari kwenye ukurasa wa 181.)’
‘Ninyi hammwamini Bikira Maria’
Unaweza kujibu hivi: ‘Nimetambua kwamba kuna watu ambao hawaamini kwamba yule aliyemzaa Mwana wa Mungu alikuwa bikira. Lakini sisi tunaamini alikuwa bikira. (Fungua kimoja cha vitabu vyetu kwenye sehemu inayozungumzia jambo hilo na umwonyeshe mwenye nyumba.)’ Kisha unaweza kuongezea: ‘Je, kuna jambo lolote zaidi linalohitajiwa ikiwa tunataka kupata wokovu? . . . Ona yale ambayo Yesu alimwambia Baba yake katika sala. (Yoh. 17:3)’