Maisha na Huduma ya Yesu
Muujiza wa Pili Katika Kana
WAKATI Yesu anaporudia eneo la nyumbani kwao baada ya shughuli ndefu ya kuhubiri katika Yudea, hafanyi hivyo ili kupumzika. Bali, anaanza huduma kubwa zaidi katika Galilaya, nchi aliyokulia. Lakini wanafunzi wake wanarudi nyumbani kwenye jamaa zao na shughuli zao za zamani badala ya kubaki pamoja naye.
Yesu anaanza kuhubiri ujumbe gani? Huu: “Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.” Nalo itikio linakuwa nini? Wagalilaya wanampokea Yesu. Yeye anaheshimiwa na wote. Lakini, haiwi hivyo hasa kwa sababu ya ujumbe wake, bali, ni kwa sababu wengi wao walikuwa kwenye Sikukuu ya Kupitwa katika Yerusalemu miezi kadha kabla ya hapo wakaona ishara za kustaajabisha alizozifanya.
Inaonekana kwamba Yesu anaanza huduma yake kuu ya Galilaya akiwa Kana. Utakumbuka kwamba kabla ya hapo aligeuza maji yakawa divai kwenye karamu ya arusi iliyofanywa huko, akiisha kurudi kutoka Yudea. Pindi hii ya pili mtoto wa afisa wa kiserikali wa Mfalme Herode Antipa ni mgonjwa sana. Anaposikia kwamba Yesu ametoka Yudea akaja Kana, afisa huyo anasafiri mwendo wote huo kutoka nyumbani kwake Kapernaumu akamtafute. Kwa kujawa na kihoro, anasihi hivi: ‘Tafadhali uje bila kukawia kabla mtoto wangu hajafa.’
Yesu naye asema: ‘Rudi nyumbani. Mwana wako ameponywa!’ Afisa wa Herode anaamini na kuanza ile safari ndefu ya kurudi nyumbani. Anapokuwa njiani wanamlaki watumishi wake, ambao wamefanya haraka kumwambia kwamba mambo ni mazuri—mwanaye amepona! ‘Alipata nafuu wakati gani?’ anauliza.
‘Jana saa saba ya mchana,’ wanajibu.
Afisa anatambua kwamba saa hiyo hiyo ndipo Yesu aliposema, ‘Mwana wako ameponywa!’ Baada ya hapo, mwanamume huyo na nyumba yake yote wanakuwa wanafunzi wa Kristo.
Hivyo Kana pakawa mahali palipopata upendeleo wa kufanyiwa miujiza miwili na Yesu kama ishara ya kwamba amerudi kutoka Yudea. Bila shaka, hiyo siyo tu miujiza aliyofanya kufikia wakati huo, lakini ina maana kubwa kwa sababu ilikuwa alama za kuonyesha amerudi Galilaya.
Sasa Yesu anaelekea nyumbani Nazareti. Anangojwa na mambo gani huko? Yohana 4:43-54; Marko 1:14, 15; Luka 4:14, 15.
◆ Yesu anaporudi Galilaya, ni jambo gani linalopata wanafunzi wake, na watu wanampokeaje?
◆ Yesu anafanya muujiza gani, nao unakuwa na matokeo gani juu ya wenye kuhusika?
◆ Hivyo Kana panakuwa ni mahali panapopendelewa na Yesu kwa njia gani?
[Picha ya ukurasa nzima katika ukurasa wa 8]