Maisha na Huduma ya Yesu
Huruma kwa Wanaosumbuka
BAADA ya kuwalaumu waziwazi Mafarisayo kwa mapokeo yao ya kujitumikia wenyewe, Yesu anaondoka akiwa na wanafunzi wake. Muda mfupi baadaye, huenda ukakumbuka, jaribio lake la kuondoka akiwa pamoja nao ili wakapumzike kidogo lilivurugwa wakati umati ulipowapata. Sasa, akiwa na wanafunzi wake, yeye anaondoka na kuelekea pande za Tiro na Sidoni, ambazo ni maili nyingi kaskazini. Yaelekea kwamba hii peke yayo ndiyo safari anayofanya Yesu akiwa pamoja na wanafunzi wake kuvuka mipaka ya Israeli.
Baada ya kupata nyumba ambamo wangekaa, Yesu anawajulisha kwamba hataki ye yote ajue walipo. Hata hivyo, hata katika eneo hili lisilo la Waisraeli, yeye hawezi kuepuka kutambuliwa. Mwanamke Mgiriki ambaye alizaliwa hapa Foinike katika Shamu, anampata na kuanza kumsihi: “Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.” Hata hivyo, Yesu hasemi lo lote kwa kumjibu.
Hatimaye, wanafunzi wake wanamwambia Yesu: “Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.”
Akieleza sababu ya kumpuuza, Yesu anasema: “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.”
Hata hivyo, mwanamke huyo hatamaushwi. Yeye anamkaribia Yesu, anasujudu mbele zake, na kusihi, “Bwana, unisaidie!”
Lazima moyo wa Yesu uwe unasukumwa na ombi hilo la kujikaza la mwanamke huyo kama nini! Hata hivyo, yeye tena anaelekeza kwenye daraka lake la kwanza, kuwahudumia watu wa Mungu wa Israeli. Wakati ule ule, yaonekana waziwazi kutahini imani ya mwanamke huyo, yeye anatumia oni la ubaguzi la Wayahudi kwa wale wa mataifa mengine, akitoa hoja hivi: “Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa [wadogo].”
Kwa sauti yake ya huruma na wonyesho wa sura yake, kwa kweli Yesu anafunua hisia nyororo zake kuwaelekea wasio Wayahudi. Hata yeye anapunguza ulinganifu kwenye ubaguzi wa Mataifa kuwa mbwa kwa kuwarejezea kuwa kama “mbwa [wadogo],” au tutoto twa mbwa. Badala ya kukasirika, mwanamke huyo anaendeleza rejezo la Yesu kwa ubaguzi wa Kiyahudi na anasema maneno haya kwa unyenyekevu: “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukao mezani pa bwana zao.”
“Mama, imani yako ni kubwa,” akajibu Yesu. “Na iwe kwako kama utakavyo.” Na inatukia hivyo! Mwanamke huyo anaporudi nyumbani kwake, anampata binti yake akiwa kitandani, amepona kabisa.
Kutoka pwani mwa Sidoni, Yesu na wanafunzi wake wanaenda kupitia nchini kuelekea chemchemi ya Mto Yordani. Yaonekana wanavuka Yordani kwa miguu mahali fulani juu ya Bahari ya Galilaya na kuingia upande wa Dekapoli, mashariki mwa bahari. Huko wanapanda mlima, lakini umati unawapata na kumletea Yesu vilema, viwete, vipofu, na mabubu, na wengine wengi ambao ni wagonjwa au wamelemaa. Wanawaweka miguuni pa Yesu, naye anawaponya. Watu wanastaajabu wanapowaona mabubu wakiongea, vilema wakitembea, na vipofu wakiona, nao wanamsifu Mungu wa Israeli.
Mwanamume mmoja ambaye ni kiziwi na hawezi hata kuongea anaelekezewa fikira kwa njia ya pekee na Yesu. Mara nyingi viziwi wanafadhaika kwa urahisi, hasa katika umati. Huenda Yesu aliona wasiwasi wa mwanamume huyu hasa. Kwa hivyo Yesu kwa huruma anamchukua kutoka kwa umati na kumweka faraghani. Akiwa peke yake, Yesu aonyesha kile ambacho atamfanyia. Anaviweka vidole vyake masikioni mwa mwanamume huyo na, baada ya kutema mate, anaugusa ulimi wake. Kisha, akitazama kuelekea mbingu, Yesu augua sana na kusema: “Funguka.” Mara, uwezo wa kusikia wa mwanamume huyo unarudishwa, naye anaweza kuongea kwa njia ya kawaida.
Yesu akiisha kutenda maponyo hayo yote, umati unaitikia kwa kuthamini: “Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, mabubu waseme.” Mathayo 15:21-31; Marko 7:24-37.
◻ Kwa sababu gani Yesu hamponyi mtoto wa mwanamke Mgiriki mara moja?
◻ Baadaye, Yesu anawapeleka wapi wanafunzi wake?
◻ Kwa huruma Yesu anamtendeaje mwanamume kiziwi ambaye hawezi hata kuongea?