Wewe Unapigaje Mbio Katika Lile Shindano la Mbio la Kupata Uhai?
“Je! hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.”—1 WAKORINTHO 9:24.
1. Biblia huufananisha mwendo wetu wa Kristo na nini?
BIBLIA hufananisha utafutaji wetu wa uhai wa milele na shindano la mbio. Kuelekea mwisho wa uhai wake, mtume Paulo alisema hivi juu yake mwenyewe: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.” Aliwasihi Wakristo wenzake wafanya vivyo hivyo aliposema hivi: “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu.”—2 Timotheo 4:7; Waebrania 12:1.
2. Sisi huona mwanzo gani wenye kutia moyo katika lile shindano la mbio la kupata uhai?
2 Ulinganisho huo unafaa kwa sababu shindano la mbio huwa na mwanzo, mwendo uliowekwa, na mwisho, au lengo. Ndivyo ilivyo na taratibu ya maendeleo ya kiroho kuelekea uhai. Kama vile tumeona, kila mwaka mamia ya maelfu ya watu huanza vizuri katika lile shindano la mbio la kupata uhai. Kwa mfano, katika miaka mitano iliyopita, watu 1,336,429 wameanza rasmi katika shindano hilo la mbio kwa wakfu na ubatizo wa maji. Mwanzo wenye bidii jinsi hiyo ni wenye kutia moyo sana. Hata hivyo, jambo la maana zaidi ni kudumu katika shindano hilo la mbio mpaka mwisho unapofikiwa. Je! wewe unafanya hivyo?
Shindano la Mbio la Kupata Uhai
3, 4. (a) Paulo alionyeshaje umaana wa kudumu katika lile shindano la mbio? (b) Wengine wameshindwaje kulitii shauri la Paulo?
3 Ili kuukazia umaana wa kuendelea katika lile shindano la mbio, Paulo alihimiza hivi: “Je! hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo [zawadi, HNWW] ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.”—1 Wakorintho 9:24.
4 Ni kweli, katika michezo ya kale, ni mmoja tu aliyeweza kuipokea zawadi. Hata hivyo, katika lile shindano la mbio la kupata uhai, kila mtu aweza kupata zawadi. Jambo la maana ni kudumu mwendoni hadi mwisho! Kwa furaha, wengi wamepiga mbio kwa uaminifu mwendoni hadi mwisho wa uhai wao, kama mtume Paulo alivyofanya. Na mamilioni huendelea kupiga mbio. Hata hivyo, wengine wameshindwa kuendelea mbele au kufanya maendeleo hadi mwisho. Badala ya hivyo, waliruhusu mambo mengine yawazuie hivi kwamba waliliacha shindano hilo la mbio au wakakosa kustahili kwa njia fulani. (Wagalatia 5:7) Hilo lapasa litupe sisi sote sababu ya kuchunguza jinsi tunavyopiga mbio katika lile shindano la mbio la kupata uhai.
5. Je! Paulo alikuwa akilinganisha lile shindano la mbio la kupata uhai na shindano la michezo? Eleza.
5 Swali hili laweza kuulizwa: Paulo alimaanisha nini aliposema kwamba “apokeaye tuzo [zawadi, HNWW] ni mmoja”? Kama ilivyoonyeshwa mapema, yeye hakumaanisha kwamba miongoni mwa wale wote waliioanza katika lile shindano la mbio la kupata uhai, ni mmoja tu atakayepokea ile thawabu ya uhai wa milele. Kwa wazi isingekuwa hivyo, kwani tena na tena, alionyesha wazi kwamba ni mapenzi ya Mungu kwamba watu wa aina zote waokolewe. (Warumi 5:18; 1 Timotheo 2:3, 4; 4:10; Tito 2:11) La, yeye hakuwa akisema kwamba shindano la mbio la kupata uhai ni shindano ambalo katika hilo kila mshindani ajaribu kuwashinda wale wengine wote. Wakorintho walijua vema sana kwamba roho ya ushindani ya aina hiyo ilikuwako miongoni mwa wale washindani kwenye Michezo yao ya Kiisthmia, iliyosemwa kuwa maarufu zaidi ya Michezo ya Olimpiki wakati huo. Kwa hiyo, Paulo alimaanisha nini basi?
6. Muktadha hufunua nini kuhusu mazungumzo ya Paulo juu ya mpiga mbio na shindano la mbio?
6 Kwa kutaja kile kielelezo cha mpiga mbio, Paulo alikuwa akizungumzia hasa matarajio yake mwenyewe ya kupata wokovu. Katika mistari iliyotangulia, alieleza jinsi alivyofanya kazi kwa bidii na kujitahidi mwenyewe katika njia nyingi. (1 Wakorintho 9:19-22) Halafu, katika mstari 23, alisema hivi: “Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili [Habari Njema, HNWW] ili kuishiriki pamoja na wengine.” Alitambua kwamba wokovu wake haukuhakikishwa kwa sababu tu alikuwa amechaguliwa kuwa mtume au kwa sababu alikuwa ametumia miaka mingi akiwahubiri wengine. Ili kushiriki katika baraka za habari njema, ni lazima aendelee kufanya kila awezalo kwa ajili ya habari njema. Ni lazima apige mbio akiwa na nia kamili ya kushinda, akijitahidi mwenyewe kana kwamba alikuwa akipiga mbio katika shindano la mbio halisi katika Michezo ya Kiisthmia, ambapo “apokeaye tuzo [zawadi, HNWW] ni mmoja.”—1 Wakorintho 9:24a.
7. Ni nini kinachohitajiwa ili ‘kupiga mbio namna hiyo, ili kupata’?
7 Twaweza kujifunza mengi kutokana na hilo. Ingawa kila mtu anayejiunga mwenyewe katika shindano hilo la mbio ataka kushinda, ni wale tu wanaoazimia kikamili kushinda walio na tarajio lolote la kufanya hivyo. Kwa hiyo, hatupaswi kuridhika kwa sababu tu tumejiunga wenyewe katika shindano la mbio. Hatupaswi kuhisi kwamba kila jambo liko sawasawa kwa sababu tumo ‘katika kweli.’ Huenda tukawa na jina Mkristo, lakini je, tuna sifa za kuthibitisha kwamba sisi ni Wakristo? Kwa mfano, je, sisi hufanya mambo ambayo twajua Mkristo apaswa afanye—kuhudhuria mikutano ya Kikristo, kushiriki katika huduma ya shambani, na kadhalika. Ikiwa ndivyo, tunastahili pongezi, na tunapaswa kujitahidi kudumu katika mazoea hayo bora kabisa. Lakini, je, inawezekana kwamba twaweza kunufaika zaidi kutokana na yale tunayofanya? Kwa mfano, je, sisi sikuzote huwa tumejitayarisha ili kushiriki mikutanoni kwa kutoa maelezo? Je! sisi hujaribu kutumia yale tunayojifunza katika maisha yetu ya kibinafsi? Je! sisi hutoa uangalifu ili kufanyia maendeleo stadi zetu hivi kwamba tuweze kutoa ushahidi wa kikamili vijapokuwa vizuizi tunavyokabili shambani? Je! sisi tuko tayari kukubali ule mwito wa ushindani wa kurudia wale wenye kupendezwa na kuongoza mafunzo ya Biblia nyumbani? “Pigeni mbio namna hivyo, ili mpate,” akasihi Paulo.—1 Wakorintho 9:24b.
Zoea Kujidhibiti Katika Mambo Yote
8. Ni nini huenda ikawa kilimchochea Paulo awasihi Wakristo wenzake ‘wazoee kujidhibiti katika mambo yote’?
8 Maishani mwake, Paulo alikuwa amewaona wengi waliokuwa wamepunguza mwendo, kupeperuka, au kuliacha lile shindano la mbio la kupata uhai. (1 Timotheo 1:19, 20; Waebrania 2:1) Ndiyo sababu aliwakumbusha Wakristo wenzake tena na tena kwamba wamo katika shindano la bidii na lenye kuendelea. (Waefeso 6:12; 1 Timotheo 6:12) Alikiendeleza kile kielelezo cha mpiga mbio akasema: “Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia [huzoea kujidhibiti, NW] katika yote.” (1 Wakorintho 9:25a) Kwa kusema hivyo, Paulo alikuwa akitaja jambo ambalo Wakristo Wakorintho walifahamu sana, yaani, mazoezi magumu yaliyofanywa na washindani kwenye Michezo ya Kiisthmia.
9, 10. (a) Chanzo kimoja hufafanuaje washindani katika Michezo ya Kiisthmia? (b) Ni jambo gani lililo la maana zaidi kuhusu ufafanuzi huo
9 Ufuatao ni ufafanuzi dhahiri wa mshindani aliyekuwa akijizoeza:
“Kwa uradhi na bila lalamiko lolote ajitiisha mwenyewe kwa sheria na vizuizi vya mazoezi yake ya muda wa miezi kumi, ambavyo bila hivyo ni afadhali asishindane. . . . Aonea fahari magumu, na uchovu mbalimbali, na vizuizi vyake vidogo vidogo, na aliona kuwa jambo la kuonea fahari kuepuka kabisa jambo lolote ambalo huenda hata kidogo likapunguza nafasi yake ya kufanikiwa. Aona watu wengine wakitosheleza hamu yao ya chakula, wakipumzika huku akihema kwa ajili ya kujitahidi kimwili, wakijifurahisha katika mahali pa kuogea, wakionea shangwe uhai kwa anasa; lakini mara nyingi hawi na mawazo yenye kijicho, kwa sababu atamani sana ile zawadi, na mazoezi magumu ni ya lazima. Ajua kwamba nafasi zake za kushinda zitapotea akiulegeza ugumu wa nidhamu hiyo kwenye hatua yoyote au kwenye pindi yoyote.”—The Expositor’s Bible, Buku 5, ukurasa 674.
10 Jambo lenye kupendeza hasa ni ile habari kwamba yule aliye chini ya mazoezi “aliona kuwa jambo la kuonea fahari” kufuata taratibu hiyo ngumu ya kujinyima. Kwa kweli, yeye “mara nyingi hawi na mawazo yenye kijicho” juu ya raha na ustarehe ambao aona wengine wakionea shangwe. Je! twaweza kujifunza jambo fulani kutokana na hilo? Kwa kweli, ndiyo.
11. Ni lazima tujilinde na maoni gani yasiyofaa tunaposhiriki katika lile shindano la mbio la kupata uhai?
11 Kumbuka maneno ya Yesu kwamba “njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:13, 14) Unapojitahidi kusafiri kwenye ‘njia hiyo iliyosonga,’ je, wewe huonea kijicho ule uhuru na ile raha ambayo wale kwenye ile njia nyingine huonekana kuonea shangwe? Je! wewe unahisi kwamba unakosa kufurahia baadhi ya mambo ambayo wengine wanafanya, ambayo huenda yasionekane kuwa mabaya yenyewe? Ni rahisi kwetu kuhisi hivyo tukikosa kukumbuka ni kwa sababu gani tunafuata mwendo huo. “Basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika,” Paulo akasema.—1 Wakorintho 9:25b.
12. Ni kwa nini yaweza kusemwa kwamba ule utukufu na umaarufu ambao watu wametafuta ni kama ile taji iharibikayo iliyotolewa kwenye Michezo ya Kiisthmia?
12 Mshindi kwenye Michezo ya Kiisthmia alipokea shada la msunobari wa Kiisthmia au mmea mwingine kama huo, ambalo labda lilinyauka katika siku au majuma machache. Bila shaka, wanariadha hao hawakushindania shada hilo lililoweza kunyauka bali waliushandania utukufu, heshima, na umaarufu uliokuja nalo. Chanzo kimoja husimulia kwamba mshindi alipofika nyumbani, alikaribishwa kama shujaa aliyeshinda. Mara nyingi kuta za jiji zilivunjwa ili mwandamano wake uweze kupita, na sanamu za mawe zilichongwa kwa heshima yake. Hata hivyo, yajapokuwa mambo hayo yote, utukufu wake bado ulikuwa wenye kuharibika. Leo, ni watu wachache wajuao wale mashujaa walioshinda, na wengine kwa kweli hawajali. Wale wanaodhabihu wakati, nishati, afya, na hata furaha yao ya familia ili kupata nguvu, umaarufu, na utajiri wa ulimwengu, lakini hawajitajarishi kwa Mungu, watapata kwamba “taji” yao ya kufuatia mambo ya kimwili, kama uhai wao, inapitilia mbali tu.—Mathayo 6:19, 20; Luka 12:16-21.
13. Mwendo wa maisha wa mtu aliye katika lile shindano la mbio la kupata uhai hutofautianaje na ule wa mwanariadha?
13 Washindani katika mchezo wa riadha huenda wakawa na nia ya kukubali yale matakwa magumu ya kujizoeza, kama yale yaliyofafanuliwa juu, lakini kwa muda mfupi tu. Michezo inapoisha, wao hurudia njia ya maisha ya kawaida. Huenda wakajizoeza mara kwa mara ili kudumisha stadi zao, lakini hawafuati tena mwendo ule ule wa kujinyima vikali, angalau si mpaka shindano lingine liko karibu. Hali si hivyo kwa wale walio katika lile shindano la mbio la kupata uhai. Kwao ni lazima kujizoeza na kujinyima kuwe njia ya maisha.—1 Timotheo 6:6-8.
14, 15. Kwa nini ni lazima mshindani katika lile shindano la mbio la kupata uhai azoee kujidhibiti daima?
14 “Mtu ye yote akitaka kunifuata,” Yesu Kristo akaambia kusanyiko la wanafunzi na wengine, “na ajikane mwenyewe (au, “ni lazima ajiambie mwenyewe, ‘Hapana.’” tafsiri ya Charles B. Williams), ajitwike na msalaba [mti wake wa mateso, NW] anifuate [kwa kuendelea, NW].” (Marko 8:34) Tunapoukubali mwaliko huo, ni lazima tuwe tayari kufanya hivyo “kwa kuendelea,” si kwa sababu kuna ustahili wa pekee kwa kujinyima, bali kwa sababu ukosefu mmoja wa busara, kushindwa mara moja kuamua vema, huenda kukaharibu yote yaliyojengwa, hata kuhatarisha hali njema yetu ya milele. Maendelo ya kiroho kwa kawaida hufanya kwa mwendo wa polepole, lakini yaweza kubatilishwa kwa haraka jinsi gani ikiwa hatujihadhari daima!
15 Zaidi ya hayo, Paulo alisihi kwamba ni lazima tuzoee kujidhibiti “katika yote,” yaani, ni lazima tufanye hivyo daima katika sehemu zote za maisha. Hilo lafaa kwa sababu mwenye kujizoeza akijifurahisha kupita kiasi au akiishi bila maadili, yale maumivu yote ya kimwili na ule uchovu wote ambao amevumilia utakuwa wa faida gani? Vile vile katika shindano la mbio la kupata uhai, ni lazima tuzoee kujidhibiti katika mambo yote. Mtu huenda akajidhibiti mwenyewe katika mambo kama vile ulevi na uasherati, lakini thamani ya kufanya hivyo inapungua ikiwa ni mwenye kiburi na mwenye fitina. Au namna gani ikiwa yeye ni mstahimilivu na mwenye fadhili kuelekea wengine, lakini huficha dhambi fulani ya siri katika maisha yake ya faragha? Ili kujidhabiti kunufaishe kikamili, ni lazima kuzoewe “katika yote.”—Linganisha Yakobo 2:10, 11.
Piga Mbio “Si Kama Asitaye”
16. Kupiga mbio “si kama asitaye” kunamaanisha nini?
16 Akiona jitihada nyingi inayohitajiwa ili kufanikiwa katika lile shindano la mbio la kupata uhai, Paulo aliendelea kusema hivi: “Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa.” (1 Wakorintho 9:26) Lile neno “asitaye” lamaanisha kihalisi “-siyo waziwazi” (Kingdom Interlinear), “bila kutazamwa, bila kutiwa alama” (Lange’s Commentary) Kwa hiyo, kupiga mbio “si kama asitaye” humaanisha kwamba kwa yule atazamaye yapasa iwe wazi sana mahali ambapo mpiga mbio anaelekea. The Anchor Bible hulifasiri “si kwenye mwendo uliopindukapinduka.” Kama ungeona nyayo zinazozungukazunguka huku na huku ufukoni, zikigeuka mara kwa mara, na hata kwenda kinyume nyakati nyingine, usingefikiri hata kidogo kwamba mtu huyo alikuwa akipiga mbio, licha ya kwamba alikuwa akijua mahali alipokuwa akielekea. Lakini kama ungeona nyayo zinazofanyiza mstari mrefu ulionyoka, kila unyayo ukiwa mbele ya ule uliotangulia na zote zikiwa na umbali ule ule kati zao, ungekata maneno kwamba nyayo hizo ni za mtu ajuaye barabara mahali anapoelekea.
17. (a) Paulo alionyeshaje kwamba alikuwa akipiga mbio “si kama asitaye”? (b) Tunaweza kumwigaje Paulo kwa habari hiyo?
17 Uhai wa Paulo huonyesha kwa wazi kwamba alikuwa akipiga mbio “si kama asitaye.” Alikuwa na ushuhuda wa kutosha wa kuthibitisha kwamba alikuwa mhudumu Mkristo na mtume. Alikuwa na lengo moja tu, na alijitahidi mwenyewe sana maishani mwake mwote ili kulipata. Hakukengeushwa fikira kamwe na umaarufu, uweza, utajiri, au ustarehe, hata ingawa labda angaliweza kupata yoyote kati hayo. (Matendo 20:24; 1 Wakorintho 9:2; 2 Wakorintho 3:2, 3; Wafilipi 3:8, 13, 14) Utazamapo nyuma kwenye mwendo wako wa maisha, wewe waona njia ya aina gani? Mstari ulionyoka wenye mwelekeo wa waziwazi au njia inayozungukazunguka bila lengo? Je! kuna ushuhuda wa kwamba unashindana katika shindano la mbio la kupata uhai? Kumbuka, sisi tumo katika shindano hilo la mbio, si ili kujaribu kufanya jambo fulani tu bila uchangamfu wowote, bali kuufikia mwisho.
18. (a) ‘Kupiga hewa’ kungelinganishwa na nini kwa upande wetu? (b) Kwa nini huo ungekuwa mwendo wa hatari kufuata?
18 Akionyesha ulinganifu wa mchezo mwingine wa riadha, Paulo aliendelea kusema hivi: “Napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa.” (1 Wakorintho 9:26b) Katika shindano letu la kupata uhai, tuna maadui wengi, kutia na Shetani, ulimwengu, na kutokamilika kwetu wenyewe. Sawa na mwanabondia wa kale, ni lazima tuweze tuwazuie kwa ngumi zilizolengwa vizuri. Kwa furaha Yehova Mungu hutuzoeza na kutusaidia katika mapigano hayo. Yeye huandaa maagizo katika Neno lake, katika vichapo vyenye msingi wa Biblia, na kwenye mikutano ya Kikristo. Hata hivyo, tukisoma Biblia na vichapo na kwenda mikutanoni lakini hatuyatumii yale tunayojifunza, je, hatupotezi jitihada zetu, ‘tukipiga hewa’? Kufanya hivyo hutuweka katika hali ya hatari sana. Twafikiri kwamba tunapigana na hivyo twawa na hisia ya usalama isiyo ya kweli, lakini hatuwashindi maadui wetu. Ndiyo sababu mwanafunzi Yakobo alihimiza hivi: “Iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.” Kama vile ‘kupiga hewa’ hakutawazuia maadui wetu, ndivyo kuwa “wasikiaji tu” hakutahakikisha kwamba tunafanya mapenzi ya Mungu.—Yakobo 1:22; 1 Samweli 15:22; Mathayo 7:24, 25.
19. Tunaweza kuhakikishaje hatukataliwi?
19 Hatimaye, Paulo alituambia siri ya kufanikiwa kwake: “Nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” (1 Wakorintho 9:27) Sawa na Paulo, ni lazima sisi pia tuweze kudhibiti mnofu wetu usiokamilika badala ya kuuruhusu utudhibiti. Ni lazima tuondolee mbali mielekeo, hamu, na tamaa za kimnofu. (Warumi 8:5-8; Yakobo 1:14, 15) Kufanya hivyo kwaweza kuumiza, kwa kuwa neno lililotafsiriwa “nautesa” humaanisha kihalisi ‘kupiga chini ya jicho’ ( Kingdom Interlinear). Lakini, je, si bora zaidi kuwa kana kwamba umeumia jicho na kuishi kuliko kufuata tamaa za mnofu wenye dhambi na kufa?—Linganisha Mathayo 5:28, 29; 18:9; 1 Yohana 2:15-17.
20. Kwa nini ni jambo la hima wakati huu hasa kuchunguza jinsi tunavyopiga mbio katika lile shindano la mbio la kupata uhai?
20 Leo, tunaukaribia mwisho wa lile shindano la mbio. Wakati wa kutoa zawadi u karibu. Kwa Wakristo wapakwa-mafuta, zawadi ni ile “thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” (Wafilipi 3:14) Kwa wale wa ule umati mkubwa, zawadi ni uhai wa milele kwenye dunia-paradiso. Kukiwa na mengi tuwezayo kupoteza, acheni tuazimie, kama alivyoazimia Paulo, kwamba ‘tusiwe watu wa kukataliwa.’ Kila mmoja wetu na azingatie moyoni agizo hili: “Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.”—1 Wakorintho 9:24, 27.
Je! Unakumbuka?
◻ Kwa nini inafaa kulinganisha maisha ya Mkristo na shindano la mbio?
◻ Lile shindano la mbio la kupata uhai linatofautianaje na shindano la mbio halisi?
◻ Kwa nini tuzoee kujidhibiti daima na “katika yote”?
◻ Mtu hupigaje mbio “si kama asitaye”?
◻ Kwa nini ni jambo la hatari kuwa ‘ukipiga hewa’ tu?
[Picha katika ukurasa wa 16]
Shada la mshindi, pamoja na utukufu na heshima, ni lenye kufifia