SURA YA 62
Somo Muhimu Kuhusu Unyenyekevu
MATHAYO 17:22–18:5 MARKO 9:30-37 LUKA 9:43-48
YESU ATABIRI TENA KUHUSU KIFO CHAKE
ALIPA KODI KWA SARAFU ILIYOTOKA KATIKA KINYWA CHA SAMAKI
NI NANI ATAKAYEKUWA MKUU KATIKA UFALME?
Baada ya kugeuka sura na kumponya mvulana mwenye roho mwovu huko Kaisaria Filipi, Yesu anaelekea Kapernaumu. Anasafiri kisiri akiwa na wanafunzi wake tu, ili umati ‘usijue.’ (Marko 9:30) Jambo hilo linampa nafasi zaidi ya kuwaandaa wanafunzi wake kwa ajili ya kifo chake na kazi ambayo watafanya baadaye. “Mwana wa binadamu atasalitiwa mikononi mwa watu,” anaeleza, “nao watamuua, na siku ya tatu atafufuliwa.”—Mathayo 17:22, 23.
Jambo hilo halipaswi kuwa jipya kwa wanafunzi wake. Hapo awali Yesu aliwaambia kwamba atauawa, ingawa Petro hakuamini kwamba jambo hilo litatokea. (Mathayo 16:21, 22) Pia mitume wake watatu waliona alipogeuka sura na walisikia mazungumzo kuhusu “kuondoka” kwa Yesu. (Luka 9:31) Sasa wafuasi wake ‘wanahuzunika sana’ kwa sababu ya mambo ambayo Yesu anasema, hata ingawa hawaelewi kikamili maana ya maneno yake. (Mathayo 17:23) Lakini wanaogopa kumuuliza zaidi kuhusu jambo hilo.
Baada ya muda wanafika Kapernaumu, kitovu cha kazi ya Yesu na mji wa nyumbani wa baadhi ya mitume. Wakiwa huko, watu wanaokusanya kodi ya hekalu wanamwendea Petro. Labda wakijaribu kumshtaki Yesu kwa kutolipa kodi, wanauliza: “Je, mwalimu wenu hulipa kodi [ya hekalu] ya drakma mbili?”—Mathayo 17:24.
Petro anajibu: “Ndiyo.” Anaporudi ndani ya nyumba, tayari Yesu anajua kilichotokea. Basi badala ya kusubiri Petro azungumzie jambo hilo, Yesu anauliza: “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru au kodi kutoka kwa nani? Kutoka kwa wana wao au kutoka kwa wageni?” Petro anajibu: “Kutoka kwa wageni.” Kisha Yesu anasema: “Basi, kwa kweli wana hawalipi kodi.”—Mathayo 17:25, 26.
Baba ya Yesu ndiye Mfalme wa ulimwengu mzima na Ndiye anayeabudiwa hekaluni. Kwa hiyo, kisheria Mwana wa Mungu hapaswi kulipa kodi ya hekalu. “Lakini ili tusiwakwaze,” Yesu anasema, “nenda baharini utupe ndoano na uchukue samaki wa kwanza atakayetokea, na utakapofungua kinywa chake, utapata sarafu ya fedha [stateri, au tetradrakma]. Ichukue uwape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”—Mathayo 17:27.
Baada ya muda, wanafunzi wanakusanyika, nao wanataka kumuuliza Yesu kuhusu ni nani atakayekuwa mkuu katika Ufalme. Wanaume haohao hivi karibuni waliogopa kumwuliza Yesu kuhusu kifo chake, lakini sasa hawaogopi kumuuliza kuhusu wakati wao ujao. Yesu anajua wanachofikiria. Walikuwa wakibishania jambo hilo wakiwa nyuma ya Yesu katika safari yao ya kurudi Kapernaumu. Basi anawauliza: “Mlikuwa mkibishania nini barabarani?” (Marko 9:33) Wakiwa wameaibika, wanafunzi wanakaa kimya kwa sababu walikuwa wanabishana kuhusu ni nani aliye mkuu kati yao. Mwishowe mitume wanamuuliza Yesu swali ambalo walikuwa wakizungumzia: “Kwa kweli ni nani aliye mkuu zaidi katika Ufalme wa mbinguni?”—Mathayo 18:1.
Inashangaza kwamba wanafunzi wanabishania jambo hilo hata baada ya kumwona na kumsikiliza Yesu kwa karibu miaka mitatu. Hata hivyo, wao si wakamilifu. Na wamelelewa katika mazingira ya kidini ambayo cheo na madaraka yanakaziwa sana. Isitoshe, hivi karibuni Petro alimsikia Yesu akiahidi kumpa “funguo” fulani za Ufalme. Je, hilo linamfanya ajihisi kuwa mkuu? Huenda Yakobo na Yohana wanahisi vivyo hivyo, kwa kuwa walimwona Yesu akigeuka sura.
Vyovyote vile, Yesu anachukua hatua ili kurekebisha mtazamo wao. Anamwita mtoto, anamsimamisha katikati yao na kuwaambia hivi wanafunzi: “Msipogeuka na kuwa kama watoto wadogo, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni. Kwa hiyo, yeyote atakayejinyenyekeza kama mtoto huyu mdogo ndiye mkuu zaidi katika Ufalme wa mbinguni; na yeyote anayempokea mtoto mdogo kama huyu kwa msingi wa jina langu ananipokea mimi pia.”—Mathayo 18:3-5.
Hiyo ni njia nzuri sana ya kufundisha! Yesu hawakasirikii wanafunzi wake na kuwaita wenye pupa au wanaojitakia makuu. Badala yake anatumia mfano ili kuwafundisha. Watoto wadogo hawajioni kamwe kuwa na cheo au mashuhuri. Basi Yesu anaonyesha kwamba wanafunzi wake wanahitaji kujiona hivyo. Kisha Yesu anamalizia somo hilo kwa wafuasi wake kwa kusema: “Anayejiendesha kama mdogo zaidi kati yenu nyote ndiye mkuu.”—Luka 9:48.