Maisha na Huduma ya Yesu
Wanafunzi Wabishana Kifo cha Yesu Kikaribiapo
YESU na wanafunzi wake wako karibu na Mto Yordani, ambapo wanavuka kutoka wilaya ya Perea kuingia Yudea. Wengine wengi wanasafiri pamoja nao kwenda kwenye Sikukuu ya Kupitwa ya 33 W.K., ambayo iko umbali wa kama juma moja tu.
Yesu anatembea mbele ya wanafunzi, nao wanashangazwa na jinsi anavyopiga moyo konde kwa ujasiri. Kumbuka kwamba majuma machache mapema wakati Lazaro alipokufa na Yesu alikuwa anakaribia kutoka Perea kuingia Yudea, Tomaso aliwatia moyo wengine hivi: “Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” Kumbuka pia kwamba baada ya Yesu kumfufua Lazaro, Sanhedrini ilifanya mipango ya kumwua. Si ajabu kwamba hofu inawashika wanafunzi wanapoingia Yudea tena sasa.
Ili kuwatayarisha kwa yaliyo mbele, Yesu awachukua wale 12 faraghani na kuwaambia: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka.”
Hii ndiyo mara ya tatu katika miezi ya karibuni Yesu amewaambia wanafunzi wake juu ya kifo na ufufuo wake. Na ingawa wanamsikiliza, wao wanashindwa kufahamu. Labda ni kwa sababu wanaamini kurudishwa kwa ufalme wa Israeli duniani, nao wanatazamia kuona shangwe juu ya utukufu na heshima katika ufalme wa kidunia pamoja na Kristo.
Miongoni mwa wasafiri wanaokwenda kwa Sikukuu ya Kupitwa ni Salome, mama ya mitume Yakobo na Yohana. Yesu amewaita wanaume hawa “wana wa ngurumo,” bila shaka kwa sababu ya mwelekeo wao wa nia motomoto. Kwa muda fulani hawa wawili wameweka moyoni tamaa ya kutaka umashuhuri katika Ufalme wa Kristo, nao wamemjulisha mama yao tamaa zao. Sasa yeye anamkaribia Yesu kwa niaba yao, ainama mbele zake, na kuomba afanyiwe hisani fulani.
“Wataka nini?” Yesu auliza.
“Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.”
Aking’amua chanzo cha ombi hilo, Yesu awaambia Yakobo na Yohana: “Hamjui mnaloliomba. Je! mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?”
“Twaweza,” wakajibu. Hata ijapokuwa Yesu ametoka sasa tu kuwaambia kwamba anakabili mnyanyaso mkali na hatimaye kuuawa, yaelekea wao hawafahamu kwamba hilo ndilo analomaanisha kwa kusema “kikombe” ambacho karibu atakinywea.
Hata hivyo, Yesu awaambia: “Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.”
Baadaye wanafunzi wale wengine kumi wanapata kujua kile ambacho Yakobo na Yohana wameomba, nao wakasirika. Labda Yakobo na Yohana walitokeza sana katika mabishano ya mapema kati ya mitume kuhusu nani aliye mkubwa zaidi. Ombi lao la wakati huu laonyesha kwamba hawajatumia shauri ambalo Yesu alikuwa amewapa kuhusu jambo hilo. Jambo la kuhuzunisha ni kwamba, tamaa yao ya kuwa mashuhuri ingali yenye nguvu sana.
Kwa hiyo kushughulikia ugomvi huu ambao umetokea sasa hivi na uadui ambao umetokeza, Yesu awaita wale 12 pamoja. Akiwashauri kwa upendo, yeye asema: “Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu.”
Yesu ameweka kielelezo ambacho wapaswa kuiga, kama anavyoeleza: “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Si kwamba Yesu amewatumika tu kwa niaba ya wengine bali atafanya hivyo kwa kiwango cha kufia aina ya binadamu! Wanafunzi wanahitaji mwelekeo uo huo wa nia kama ya Kristo ya kutamani kutumika badala ya kutumikiwa na kuwa mdogo badala ya kuwa katika cheo cha umashuhuri. Mathayo 20:17-28; Marko 3:17; 9:33-37; 10:32-45; Luka 18:31-34; Yohana 11:16.
◆ Kwa nini hofu inawashika wanafunzi?
◆ Yesu anawatayarishaje wanafunzi wake kwa ajili ya yale yaliyo mbele?
◆ Ni ombi gani linalotolewa kwa Yesu, na wanafunzi wale wengine wanaathiriwaje?
◆ Yesu anashughulikaje na tatizo lililo miongoni mwa mitume wake?