Sura Zaweza Kuwa Zenye Kudanganya
“HUWEZI ukaamini sura,” akasema mtunga drama Richard Sheridan. Hilo ni kweli kuhusu miti na watu pia.
Siku moja katika mwisho-mwisho wa Machi mwaka wa 33 W.K., Yesu Kristo aliona mtini wakati yeye na wanafunzi wake walipokuwa wakitembea kutoka Bethania hadi Yerusalemu. Mti huo ulikuwa umejaa majani, lakini uchunguzi wa karibu zaidi ulifunua ya kwamba haukuwa na tunda hata moja. Kwa hiyo Yesu aliuambia hivi: “Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako.”—Marko 11:12-14.
Kwa nini Yesu aliulaani mti huo kwa kuwa, kama vile Marko aelezavyo, ulikuwa “si wakati wa tini”? (Marko 11:13) Mtini unapotoa majani, kwa kawaida huo hutoa pia tini za mapema. Halikuwa jambo la kawaida kwa mtini kuwa na majani wakati huo wa mwaka. Lakini kwa kuwa ulikuwa na majani, Yesu alitazamia ifaavyo kupata tini juu yao. (Ona picha iliyo juu.) Jambo la kwamba mti huo ulikuwa umetoa majani tu lilimaanisha kwamba usingekuwa wenye kuzaa matunda. Sura yao ilikuwa yenye kudanganya. Kwa kuwa miti ya matunda ilitozewa kodi, mti usiozaa matunda ulikuwa mzigo wa kiuchumi na ulihitaji kukatwa.
Yesu aliutumia mtini huo usiozaa matunda ili kuonyesha somo muhimu kuhusu imani. Siku iliyofuata, wanafunzi wake walishangaa kuona kwamba mti huo ulikuwa tayari umenyauka. Yesu alieleza hivi: “Mwaminini Mungu. . . . Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” (Marko 11:22-24) Zaidi ya kuonyesha uhitaji wa kusali katika imani, mtini huo ulionyauka ulionyesha waziwazi lile ambalo lingelipata taifa lenye kukosa imani.
Miezi kadhaa mapema zaidi Yesu alikuwa amelinganisha taifa la Kiyahudi na mtini ambao haukuwa umezaa matunda kwa miaka mitatu na ungekatwa ikiwa ungebaki bila kuzaa matunda. (Luka 13:6-9) Kwa kulaani ule mtini siku nne tu kabla ya kifo chake, Yesu alionyesha jinsi ambavyo taifa la Kiyahudi halikuwa limetokeza matunda yapatanayo na toba na hivyo lingepokea uharibifu. Ingawa taifa hilo—kama mtini—lilionekana kuwa lenye afya nzuri kijuujuu tu, uchunguzi wa karibu zaidi ulifunua ukosefu wa imani uliokuwa na upeo wao katika kumkatalia mbali Mesiya.—Luka 3:8, 9.
Katika mahubiri yake ya Mlimani, Yesu alionya dhidi ya “nabii wa uongo” akasema hivi: “Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.” (Mathayo 7:15-20) Maneno hayo ya Yesu na ule usimulizi wa mtini uliolaaniwa huonyesha waziwazi kwamba tunahitaji kujihadhari kiroho, kwani sura za kidini zaweza pia kuwa zenye kudanganya.