Maisha na Huduma ya Yesu
Washindwa Kutega Yesu
YESU amekuwa akifundisha hekaluni, na ndiyo sasa tu amemaliza kuambia adui zake wa kidini vielezi vitatu ambavyo vyafichua uovu wao. Mafarisayo waingiwa na kasirani na kufanya shauri wamtege aseme jambo fulani ambalo wao waweza kulitumia kufanya akamatwe. Wao wakoroga hila na kutuma wanafunzi wao, pamoja na wafuasi wa chama cha Herode, kujaribu kumtega ajikwae.
“Mwalimu,” watu hao wasema, “twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?”
Yesu hapumbazwi na urairai huo. Yeye ang’amua kwamba akisema, ‘Hapana, si halali au si sawa kulipa kodi hii,’ atakuwa na hatia ya fitina dhidi ya Roma. Na bado, akisema, ‘Ndiyo, mwapaswa kulipa kodi hii,’ Wayahudi, ambao wadharau kutiishwa chini ya mamlaka ya Roma, watamchukia. Kwa hiyo yeye ajibu hivi: “Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha [sarafu, NW] ya kodi.”
Wamleteapo moja, auliza hivi: “Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?”
“Ni ya Kaisari,” wao wajibu.
“Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.”
Basi, watu hawa wasikiapo jibu hili la ustadi, wastaajabu sana. Nao waenda zao na kumwacha kabisa.
Waonapo kwamba Mafarisayo wameshindwa kupata jambo fulani dhidi ya Yesu, Masadukayo, wasemao hakuna ufufuo, wamfikia na kusema: “Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa watatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama [ufufuo, NW], atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye.”
Kwa kujibu Yesu asema hivi: “Je! hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.”
Hapo tena umati wa watu washangazwa sana na jibu la Yesu. Hata baadhi ya waandishi wakiri hivi: “Mwalimu, umesema vema.”
Mafarisayo waonapo kwamba Yesu amenyamazisha Masadukayo, wao wamjia wakiwa kikundi kimoja. Ili wamjaribu zaidi, mmoja wao auliza hivi: “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?”
Yesu ajibu hivi: “Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho [nafsi, NW] yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Kwa uhakika, Yesu aongezea hivi: “Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.”
“Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.”
Kwa kutambua kwamba mwandishi huyo amejibu kwa akili, Yesu amwambia: “Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu.”
Kwa siku tatu sasa—Jumapili, Jumatatu, na Jumanne—Yesu amekuwa akifundisha katika hekalu. Watu wamemsikiliza kwa furaha, hata hivyo viongozi wa kidini waliovurugiwa mipango yao wataka kumuua. Mathayo 22:15-40; Marko 12:13-34; Luka 20:20-40, NW.
◆ Mafarisayo wakoroga hila gani ili watege Yesu, na tokeo lingekuwa nini akitoa jibu la ndiyo au hapana?
◆ Yesu avurugaje pia majaribio ya Masadukayo ya kumtega?
◆ Ni jaribio gani zaidi ambalo Mafarisayo wafanya ili kutahini Yesu, na tokeo ni nini?
◆ Wakati wa huduma yake ya mwisho katika Yerusalemu, Yesu afundisha katika hekalu kwa siku ngapi, na tokeo ni nini?