Zawadi Zilizofaa Mfalme
“Wanajimu kutoka sehemu za Mashariki . . . wakafungua hazina zao na kumtolea zawadi—dhahabu na ubani na manemane.”—Mathayo 2:1, 11.
UNGEPENDA kumpa zawadi gani mtu aliye muhimu sana kwako? Katika nyakati za Biblia baadhi ya vikolezo vilikuwa na thamani kama dhahabu—thamani kubwa sana iliyomfaa mfalme.a Hii ndiyo sababu vikolezo vyenye harufu nzuri vilikuwa miongoni mwa zawadi ambazo wanajimu walileta kwa “mfalme wa wayahudi.”—Mathayo 2:1, 2, 11.
Biblia inasema hivi pia kuhusu malkia wa Sheba alipofunga safari kumtembelea Mfalme Sulemani: “Ndipo akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, na mafuta ya zeri kwa wingi sana, na mawe ya thamani; na kulikuwa hakujapata kuwa na mafuta ya zeri kama yale ambayo malkia wa Sheba alimpa Mfalme Sulemani.”b (2 Mambo ya Nyakati 9:9) Pia wafalme walimpelekea Sulemani mafuta ya zeri ili kumtakia mema.—2 Mambo ya Nyakati 9:23, 24.
Kwa nini vikolezo hivyo na vitu vilivyotengenezwa kwa vikolezo hivyo, vilikuwa vyenye thamani na gharama kubwa sana katika nyakati za Biblia? Kwa sababu vilitumiwa katika urembo, dini, na mazishi. (Tazama sanduku “Matumizi ya Vikolezo Vyenye Harufu Nzuri Katika Nyakati za Biblia.”) Mbali na kwamba vikolezo hivyo vilihitajiwa sana, viliuzwa bei ghali kwa sababu ya gharama za usafirishaji na upatikanaji.
KUVUKA JANGWA LA ARABIA
Katika nyakati za Biblia, baadhi ya mimea ya vikolezo ilisitawi kwenye Bonde la Yordani. Hata hivyo, vikolezo vingine vililetwa kutoka nchi nyingine. Biblia imetaja vikolezo vya aina mbalimbali. Vikolezo vinavyotajwa vinatia ndani waridi, udi, mafuta ya zeri, mdalasini, ubani, na manemane. Zaidi ya hayo, kulikuwa na vikolezo vingine vya chakula kama vile bizari, mnanaa, na dili.
Vikolezo hivyo vilitoka wapi? Udi, kida, na mdalasini vilipatikana katika nchi za leo za China, India, na Sri Lanka. Vikolezo kama vile ubani na manemane vilitokana na miti na mimea ambayo ilisitawi katika maeneo ya jangwa kuanzia Arabia kusini hadi Somalia iliyo Afrika. Nardo, kilikuwa kikolezo cha pekee kilichotoka India katika maeneo ya Himalaya.
Ili kufika Israeli, vikolezo vingi vilisafirishwa kupitia Arabia. Kwa sababu hiyo, katika milenia ya kwanza na ya pili K.W.K., Arabia ilikuja kuwa “msambazaji mkuu wa bidhaa hizo kati ya Mashariki na Magharibi,” kikasema kitabu The Book of Spices. Miji ya kale, ngome, na vituo vya safari vilivyo katika eneo la Negev kusini mwa Israel vinaonyesha njia walizotumia wafanyabiashara wa vikolezo hivyo. Shirika la World Heritage Centre la UNESCO liliripoti kwamba makazi hayo “yalichangia faida kubwa ya biashara hiyo . . . kutoka Arabia kusini hadi Mediterania.”
“Kiwango kidogo kiliuzwa kwa bei ghali, na kwa kuwa watu wengi walivipenda sana, vikolezo vilitumiwa kufanya biashara.” —The Book of Spices
Kwa kawaida msafara uliobeba vikolezo hivyo vyenye harufu nzuri ulisafiri umbali wa kilometa 1,800 hivi ukipitia Arabia. (Ayubu 6:19) Biblia inataja msafara wa wafanyabiashara Waishmaeli waliokuwa wamebeba “ubani mweusi na zeri na gome lenye utomvu” kutoka Gileadi hadi Misri.” (Mwanzo 37:25) Wana wa Yakobo walimuuza ndugu yao Yosefu awe mtumwa kwa wafanyabiashara hao.
“SIRI YA BIASHARA ILIYOTUNZWA KULIKO ZOTE”
Wafanyabiashara wa Arabia ndio waliojulikana sana kwa kufanya biashara ya vikolezo kwa miaka mingi. Walikuwa wauzaji wakuu wa kida na mdalasini, vikolezo kutoka Asia. Ili kuzuia wafanyabiashara wa eneo la Mediterania wasianzishe uhusiano wa kibiashara na watu wa eneo la Mashariki, Waarabu walieneza hadithi za uwongo kuhusu hatari za kujihusisha na biashara hiyo. Kitabu The Book of Spices kinasema kwamba chanzo cha vikolezo hivyo “huenda ikawa ndiyo siri ya kibiashara iliyotunzwa kuliko zote.”
Waarabu walieneza hadithi gani? Herodoto mwanahistoria Mgiriki aliyeishi katika karne ya tano K.W.K., alieleza hadithi za ndege wanaotisha waliojenga viota kwenye gome la mdalasini juu ya jabali lisiloweza kufikika. Aliandika hivi: “Ili kupata vikolezo hivyo vyenye thamani, watu waliweka vipande vikubwa vya nyama chini ya jabali hilo. Kisha ndege wangebeba vipande hivyo vya nyama kwa pupa na kuvipeleka katika viota vyao ambavyo vililemewa na uzito na kuanguka chini. Kisha watu wangeyaokota haraka magome ya mdalasini na kuyauza kwa wafanyabiashara. Hadithi hizo zilienea kila mahali. Kitabu The Book of Spices kinasema hivi: “Madai ya hatari ya kupata kikolezo hicho yalifanya [mdalasini] kiuzwe kwa bei ghali.”
Mwishowe, siri ya Waarabu hao ilifichuliwa na wakapoteza umiliki wa biashara hiyo. Kufikia karne ya kwanza K.W.K., jiji la Aleksandria, Misri likawa bandari kubwa na kituo kikuu cha biashara ya vikolezo. Meli za Roma zilipitia bandari ya Misri kuelekea India kwa kuwa mabaharia walitumia pepo za msimu za Bahari ya Hindi. Matokeo ni kwamba vikolezo hivyo vyenye thamani vilianza kupatikana kwa wingi na kwa bei nafuu.
Leo, thamani ya vikolezo haiwezi kulingana na ile ya dhahabu. Wala hatuwezi kufikiri kwamba vikolezo ni zawadi inayomfaa mfalme. Hata hivyo, watu wengi ulimwenguni wanaendelea kutumia vikolezo ili kutengeneza manukato, dawa, na hata kuongeza ladha kwenye chakula. Kwa kweli, harufu yenye kuvutia imefanya vikolezo vipendwe sana leo kama tu ilivyokuwa maelfu ya miaka iliyopita.
a Katika Biblia, maneno “kikolezo” au “vikolezo” katika lugha ya awali yalirejelea hasa vitu vilivyotengenezwa kwa mimea yenye harufu nzuri wala si viungo vinavyowekwa katika chakula.
b “Mafuta ya zeri” yalirejelea mafuta yenye harufu nzuri au utomvu unaopatikana katika miti na mimea.