SURA YA 126
Akanwa Nyumbani kwa Kayafa
MATHAYO 26:69-75 MARKO 14:66-72 LUKA 22:54-62 YOHANA 18:15-18, 25-27
PETRO AMKANA YESU
Yesu anapokamatwa katika bustani ya Gethsemane, mitume wanamwacha na kukimbia kwa woga. Hata hivyo, wawili kati yao wanaacha kukimbia. Nao ni Petro “na mwanafunzi mwingine,” labda ni mtume Yohana. (Yohana 18:15; 19:35; 21:24) Wanaweza kumfikia Yesu atakapopelekwa nyumbani kwa Anasi. Anasi anapoagiza Yesu apelekwe kwa Kuhani Mkuu Kayafa, Petro na Yohana wanafuata kwa mbali. Huenda wanahangaika kwa sababu wanahofia uhai wao wenyewe na kile kitakachompata Bwana wao.
Yohana anafahamiana na kuhani mkuu, kwa hiyo anaingia katika ua wa nyumba ya Kayafa. Petro anabaki mlangoni hadi Yohana anaporudi kuzungumza na kijakazi anayelinda mlango. Kisha Petro anaruhusiwa kuingia.
Usiku huo kuna baridi, kwa hiyo wale walio ndani ya ua wamewasha moto wa makaa. Petro anakaa pamoja nao ili aote moto anaposubiri ‘kuona’ matokeo ya kesi ya Yesu. (Mathayo 26:58) Sasa kwa sababu ya mwangaza wa moto, yule mlinzi wa mlango aliyemruhusu Petro aingie anamwona vizuri. “Wewe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu, sivyo?” anauliza. (Yohana 18:17) Si msichana huyo peke yake anayemtambua Petro na kudai kwamba alikuwa pamoja na Yesu.—Mathayo 26:69, 71-73; Marko 14:70.
Jambo hilo linamshtua Petro. Anajaribu kujificha, hata anaondoka na kwenda mlangoni. Basi Petro anakana kwamba alikuwa pamoja na Yesu, pindi fulani anasema: “Simjui wala sielewi unachosema.” (Marko 14:67, 68) Pia anaanza “kulaani na kuapa,” akimaanisha kwamba yuko tayari kuapa kwamba anasema ukweli na kuadhibiwa ikiwa anadanganya.—Mathayo 26:74.
Wakati huohuo, kesi ya Yesu inaendelea, labda katika sehemu fulani ya nyumba ya Kayafa iliyo juu ya ua. Petro na wengine wanaosubiri chini wanaweza kuwaona mashahidi mbalimbali wakiingia na kutoka ili kutoa ushahidi.
Petro anapomkana Yesu, matamshi yake ya Kigalilaya yanaonyesha kwamba anadanganya. Isitoshe, mtu fulani katika kikundi hicho ni mtu wa ukoo wa Malko, ambaye alikatwa sikio na Petro. Basi anamuuliza hivi Petro: “Nilikuona katika bustani pamoja naye, sivyo?” Petro anapokana mara hii ya tatu, jogoo anawika, kama ilivyotabiriwa.—Yohana 13:38; 18:26, 27.
Wakati huo, huenda Yesu yuko ghorofani akitazama uani. Bwana anageuka na kumtazama Petro moja kwa moja, jambo ambalo lazima linamuumiza sana Petro. Anakumbuka jambo ambalo Yesu alisema saa chache tu awali walipokuwa katika chumba cha juu. Wazia jinsi Petro anavyohisi anapotambua kile alichofanya! Petro anaenda nje na kuanza kulia kwa uchungu.—Luka 22:61, 62.
Jambo hilo linawezekanaje? Petro ambaye alikuwa na uhakika kwamba ni mshikamanifu na yuko imara kiroho, angewezaje kumkana Bwana wake? Watu wanapotosha ukweli, na Yesu anahukumiwa kuwa mhalifu mbaya. Ingawa Petro angemtetea mtu huyo asiye na hatia, alimkana Yule aliye na “maneno ya uzima wa milele.”—Yohana 6:68.
Jambo hilo la kuhuzunisha lililompata Petro linaonyesha kwamba hata mtu mwenye imani na aliyejitoa kabisa anaweza kuanguka ikiwa hajajitayarisha vizuri kwa ajili ya majaribu au vishawishi visivyotarajiwa. Mambo yote yaliyompata Petro yanapaswa kuwa onyo kwa watumishi wote wa Mungu!