Maisha na Huduma ya Yesu
Mikano Katika Ua
BAADA ya kumwacha Yesu katika bustani ya Gethsemane na kukimbia kwa hofu pamoja na mitume wale wengine, Petro na Yohana wasimama katika kimbio lao. Labda wao wamfikia Yesu apelekwapo kwenye makao ya Anasi. Anasi aagizapo apelekwe kwa Kayafa, Kuhani wa Juu, Petro na Yohana wafuata wakiwa umbali wa kutosha, yaonekana wakiwa wametatizika kati ya kuhofia uhai wao wenyewe na hangaiko lao la kina kirefu juu ya yatakayopata Bwana-Mkubwa wao.
Awasilipo kwenye makao ya Kayafa yenye nafasi kubwa, Yohana aweza kuingia katika ua, kwa kuwa yeye ajulikana na kuhani wa juu. Hata hivyo, Petro aachwa akisimama nje ya mlango. Lakini muda si muda Yohana arudi na kusema na bawabu, kijakazi, na Petro aruhusiwa kuingia.
Kufikia sasa kuna baridi, na watumishi wa nyumba na maofisa wa kuhani wa juu wamewasha moto wa makaa. Petro ajiunga nao ili apate joto huku akingojea matokeo ya kesi ya Yesu. Huko, katika nuru ya ule moto mwangavu, bawabu aliyekuwa ameacha Petro aingie amtazama vizuri zaidi. “Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya”! apaaza sauti.
Akiudhika kwa kutambulishwa, Petro akana mbele yao wote kwamba hajapata kumjua Yesu. “Sijui wala sisikii unayoyasema wewe,” yeye asema.
Hapo basi, Petro aenda nje karibu na njia ya lango. Hapo, msichana mwingine amwona naye pia awaambia wale waliosimama karibu: “Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti.” Kwa mara nyingine, Petro akana, akiapa hivi: “Simjui mtu huyu”!
Petro abaki katika ua, akijaribu kutoonekana wazi kwa kadiri iwezekanavyo. Labda hapo agutushwa na kuwika kwa jogoo katika giza la asubuhi mapema. Kwa sasa, kesi ya Yesu yaendelea, yaonekana ikiendeshwa katika sehemu ya nyumba iliyo juu ya ua. Labda Petro na wengine wanaongojea chini waona kuja na kwenda kwa mashahidi mbalimbali waletwao ndani ili kushuhudia.
Karibu saa moja imepita tangu Petro alipotambulishwa mara ya mwisho kuwa mshirika wa Yesu. Sasa watu kadhaa kati ya wale wenye kusimama hapo wamjia na kusema: “Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako [lahaja yako, NW] wakutambulisha.” Mmoja wa kikundi hicho ni mtu wa ukoo wa Malko, ambaye Petro alikuwa amekata sikio lake. “Je! mimi simekuona wewe bustanini pamoja naye?” asema.
“Simjui mtu huyu[!]” Petro ashikilia sana kauli. Kwa uhakika, ajaribu kuwasadikisha kwamba wote wanakosea kwa kulaani na kuapa juu ya jambo hilo, maana yake, kujilaani mwenyewe ikiwa hasemi ukweli.
Mara Petro afanyapo mkano wa tatu huu, jogoo awika. Na wakati huo, Yesu, ambaye kwa wazi ametoka nje akaja kwenye roshani juu ya ua, ageuka na kumtazama. Mara hiyo, Petro akumbuka aliyosema Yesu saa chache tu mapema kidogo katika chumba cha juu: “Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.” Kwa kuvunjwa na uzito wa dhambi yake, Petro aenda nje na kulia machozi kwa uchungu.
Hilo lingewezaje kutukia? Baada ya kuwa na uhakika sana juu ya imara yake ya kiroho, ikawaje kwamba Petro aweze kukana Bwana-Mkubwa wake mara tatu kwa mfuatano wa haraka? Bila shaka hali zamshika Petro bila kutarajia. Ukwe-li unapotoshwa, na Yesu anaonyeshwa kuwa mhalifu mwovu. Lililo sawa lafanywa lionekane kuwa kosa, asiye na hatia kuwa mwenye hatia. Hivyo basi kwa sababu ya misongo ya ile pindi, Petro atetereshwa kukosa usawaziko. Kwa ghafula hisia yake ifaayo ya uaminifu-mshikamanifu yapinduka. Hofu ya binadamu yampiga kikumbo kumtia katika majonzi. Jambo hilo na lisije kamwe kutupata sisi! Mathayo 26:57, 58, 69-75; Marko 14:30, 53, 54, 66-72; Luka 22:54-62; Yohana 18:15-18, 25-27.
◆ Petro na Yohana wapataje mwingilio katika ua wa kuhani wa juu?
◆ Petro na Yohana wakiwa wangali katika ua, ni nini kinachoendelea katika nyumba?
◆ Jogoo awika mara ngapi, na Petro akana mara ngapi kutomjua Kristo?
◆ Yamaanisha nini kwamba Petro alaani na kuapa?
◆ Ni nini chasababisha Petro akane kwamba hamjui Yesu?