SURA YA 32
Ni Mambo Gani Yaliyo Halali Siku ya Sabato?
MATHAYO 12:9-14 MARKO 3:1-6 LUKA 6:6-11
KUMPONYA MTU MKONO SIKU YA SABATO
Ni siku nyingine ya Sabato, Yesu anaenda kwenye sinagogi, huenda ni huko Galilaya. Humo anampata mtu aliyepooza mkono wa kulia. (Luka 6:6) Waandishi na Mafarisayo wanamtazama Yesu kwa makini. Kwa nini? Wanafunua nia yao wanapouliza: “Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?”—Mathayo 12:10.
Viongozi wa dini ya Kiyahudi wanaamini kwamba ni halali kuponya katika siku ya Sabato iwapo tu uhai umo hatarini. Kwa hiyo, siku ya Sabato si halali kutibu mfupa uliovunjika au kufunga kiungo kilichoteguka, kwa sababu hali hizo hazihatarishi uhai. Ni wazi kwamba Mafarisayo wanapomuuliza Yesu maswali si kwa sababu wanamhangaikia kikweli mtu huyu anayeteseka. Wanajaribu kupata sababu ya kumshutumu Yesu.
Hata hivyo, Yesu anajua maoni yao yaliyopotoka. Anatambua kwamba wana maoni yasiyo na usawaziko na yasiyopatana na maandiko kuhusu kuvunja amri ya kutofanya kazi siku ya Sabato. (Kutoka 20:8-10) Tayari amekabiliana na shutuma kama hizo zisizo na msingi kwa sababu ya kufanya mambo mema. Sasa Yesu anaanzisha makabiliano anapomwambia hivi mwanamume aliyepooza mkono: “Simama uje hapa katikati.”—Marko 3:3.
Yesu anawageukia waandishi na Mafarisayo na kuwaambia: “Ukiwa na kondoo mmoja, naye kondoo huyo atumbukie shimoni siku ya Sabato, je, kuna yeyote kati yenu ambaye hatamshika na kumtoa humo?” (Mathayo 12:11) Kondoo anaweza kuwaletea pesa, hivyo hawawezi kumwacha shimoni hadi siku inayofuata; anaweza kufia humo na kuwaletea hasara. Isitoshe, Maandiko yanasema: “Mwadilifu huwatunza wanyama anaowafuga.”—Methali 12:10.
Akionyesha jinsi mambo hayo yanavyohusiana, Yesu anaendelea kusema: “Kwa kweli, mwanadamu ni mwenye thamani sana kuliko kondoo! Basi ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” (Mathayo 12:12) Kwa hiyo, Yesu hatavunja Sabato ikiwa atamponya mtu huyo. Viongozi hao wa kidini wanashindwa kupinga hoja hizo zinazopatana na akili na zenye huruma. Wanakaa kimya tu.
Akiwa na hasira na huzuni kwa sababu ya maoni yao yenye makosa, Yesu anatazama huku na huku. Kisha anamwambia mtu huyo: “Nyoosha mkono wako.” (Mathayo 12:13) Yule mtu anapounyoosha mkono wake uliopooza, unapona. Mtu huyo anafurahi sana, lakini vipi kuhusu wale wanaojaribu kumtega Yesu?
Badala ya kufurahi kwamba yule mtu ameponywa mkono, Mafarisayo wanaenda nje na mara moja wanapanga njama “na wafuasi wa chama cha Herode ili wamuue Yesu.” (Marko 3:6) Inaelekea chama hiki cha kisiasa kinatia ndani washiriki wa kikundi cha kidini cha Masadukayo. Kwa kawaida, Masadukayo na Mafarisayo hawaelewani, lakini sasa wameungana kabisa ili kumpinga Yesu.