Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Je! Zakaria, baba ya Yohana Mbatizaji, alifanywa kuwa kiziwi na bubu, kama Luka 1:62 huonekana ikionyesha?
Baadhi ya watu wamefikia mkataa wa kwamba Zakaria alipata kuwa kiziwi pia. Twasoma hivi katika masimulizi ya Biblia: “Wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema, La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana.”—Luka 1:59-63.
Ingawa hivyo, hamna lolote katika masimulizi hayo ambalo husema hususa kwamba Zakaria hakuweza kusikia kwa kipindi cha wakati.
Mapema malaika Gabrieli alikuwa ametangaza kwa Zakaria kuzaliwa kulikokuwa kukija kwa mwana ambaye angeitwa Yohana. Zakaria aliyezeeka aliliona hilo kuwa jambo gumu kuamini. Malaika huyo akajibu: “Tazama! utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.” (Luka 1:13, 18-20) Malaika huyo alisema kwamba usemi wa Zakaria, si usikizi wake, ungeathiriwa.
Masimulizi hayo huzidi kusema: “Alipotoka [hekaluni] hali hawezi kusema nao [watu waliokuwa wakingoja], walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu.” (Luka 1:22) Neno la Kigiriki ambalo hapa latafsiriwa “bubu” huwasilisha wazo la kutoweza, katika usemi, usikizi, au hali zote mbili. (Luka 7:22) Namna gani Zakaria? Basi, fikiria lililotukia alipoponywa. “Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu.” (Luka 1:64) Kwa kupatana na akili hilo laongoza kwenye maoni ya kwamba ni uwezo wa kusema tu wa Zakaria uliokuwa umeathiriwa.
Kwa nini, basi wengine wakamwuliza Zakaria ‘kwa kumwashiria atakavyo kumwita [mtoto]’? Baadhi ya watafsiri hata hutafsiri hilo “kwa lugha ya ishara“ au “kwa kutumia lugha ya ishara.”
Mara nyingi, Zakaria, ambaye alikuwa bubu tangu tangazo la malaika, alilazimika kutumia ishara, namna fulani ya lugha ya ishara, ili kujieleza. Kwa mfano, yeye “aliendelea kuwaashiria” waliokuwa hekaluni. (Luka 1:21, 22) Baadaye, wakati walipoomba kibao, lazima awe alitumia ishara. (Luka 1:63) Kwa hiyo, yawezekana kwamba wale waliokuwa karibu naye wakati wake wa kuwa bubu walielekea kutumia ishara pia.
Walakini, kuna yale yanayoelekea zaidi kuwa maelezo ya ishara zilizotajwa kwenye Luka 1:62. Elisabeti alikuwa ndipo tu amejieleza kuhusu jina la mwana wake. Hivyo, bila kumpinga, huenda wakawa tu walichukua hatua ifaayo iliyofuata ya kupata uamuzi wa mume wake. Wangeweza kufanya hivyo kwa ishara ya kichwa. Uhakika wa kwamba hawakuandikia Zakaria swali lao alisome waweza hata kuwa ushuhuda kwamba yeye alisikia maneno ya mke wake. Hivyo, ishara ya kichwa tu, au nyingine kama hiyo ikitolewa kwake ingekuwa na maana ya, ‘Basi, sisi sote (kutia wewe, Zakaria) tumesikia pendekezo lake, lakini uamuzi wako wa mwisho juu ya jina la mtoto ni nini?’
Na mara baada ya hapo mwujiza mwingine ukafanyika, hali iliyo kinyume. “Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena.” (Luka 1:64) Haikuhitajiwa kutaja usikizi wake ikiwa huo haukuwa umeathiriwa.