Maisha na Huduma ya Yesu
Kielezi cha Zile Mina
LABDA Yesu angali nyumbani kwa Zakayo, ambako amesimama akiwa njiani kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake waamini kwamba wafikapo Yerusalemu, yeye atajulisha wazi ndiye Mesiya na kuanzisha Ufalme wake. Ili asahihishe wazo hili na kuonyesha kwamba Ufalme ungali mbali, Yesu atoa kielezi.
“Mtu mmoja, kabaila,” yeye asimulia, “alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.” Yesu ndiye huyo “kabaila,” na mbinguni ndiko “nchi ya mbali.” Awasilipo huko, Baba yake atampa mamlaka ya kifalme.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka, kabaila huyo aita watumwa kumi na kumpa kila mmoja wao fungu la fedha (mina ya fedha, NW], akisema: “Fanyeni biashara hata nitakapokuja.” Watumwa kumi hao katika utimizo wa kwanza wawakilisha wanafunzi wa mapema wa Yesu. Katika utumizi uliopanuliwa, wao ni picha ya wote wenye kutazamiwa kuwa pamoja naye katika Ufalme wa kimbingu.
Zile mina za fedha ni vipande vya pesa vilivyo na thamani kubwa, kila kimoja kikiwa ni mshahara wa miezi mitatu hivi kwa mkulima. Lakini mina hizo zawakilisha nini? Na watumwa hao wapaswa kufanya nazo biashara ya aina gani?
Mina hizo zawakilisha mali zenye thamani ambazo wanafunzi wapakwa mafuta kwa roho wangeweza kutumia ili watokeze warithi zaidi wa Ufalme wa kimbingu mpaka wakati wa kuja kwa Yesu akiwa Mfalme katika Ufalme ulioahidiwa. Baada ya yeye kufufuliwa na kuwatokea wanafunzi wake, aliwapa zile mina za ufananisho ili zitumiwe kufanya wanafunzi zaidi na kuongezea hivyo ile jamii ya Ufalme wa mbinguni.
“Lakini,” Yesu aendelea, “watu [raia NW] wa mji wake walimchukia [kabaila huyo], wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.” Raia hao ni Waisraeli, au Wayahudi, bila kuwahusisha ndani wanafunzi wake. Baada ya mwondoko wa Yesu kwenda mbinguni, Wayahudi hawa kwa kuwanyanyasa wanafunzi wake walijulisha kwamba hawakumtaka yeye awe mfaIme wao. Kwa njia hii walikuwa wanatenda kama raia waliotuma wale wajumbe [baraza la mabalozi, NW].
Wale watumwa kumi watumiaje mina zao? Yesu aeleza hivi: “Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano ya faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.”
Mtumwa yule mwenye mina kumi ni picha ya jamii moja, au kikundi kimoja, cha wanafunzi kuanzia Pentekoste 33 W.K. mpaka sasa, na jamii hiyo hutia ndani mitume pia. Wale waliojipatia mina tano wawakilisha pia kikundi kimoja katika kipindi kile kile, kikundi ambacho kinaongezea mali za mfalme wao duniani kulingana na fursa zao na uwezo mbalimbali. Vikundi vyote viwili vinahubiri habari njema kwa bidii, na tokeo ni kwamba watu wengi wenye mioyo ifaayo wapata kuwa Wakristo. Tisa wa watumwa hao walifanya biashara yenye mafanikio wakaongezea mali walizomiliki.
Lakini, Yesu aendelea kusema, “akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi [mina kumi, NW].”
Kupoteza mina ya ufananisho kwamaanisha kupoteza nafasi ya kuwa katika Ufalme wa kimbingu kwa mtumwa mwovu huyo. Ndiyo, yeye apoteza pendeleo la kutawala, kana kwamba ni juu ya majiji kumi au matano. Angalia, pia, kwamba mtumwa huyo hatangazwi kuwa mwovu kwa ubaya wowote afanyao, bali ni kwa kutofanya kazi aongezee utajiri wa ufalme wa bwana wake.
Wakati mina ya mtumwa mwovu ipewapo kwa mtumwa wa kwanza, ukinzani huu wafanywa: “Bwana, anayo mafungu kumi.” Hata hivyo, Yesu ajibu: “Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.” Luka 19:11-27; Mathayo 28:19, 20.
◆ Ni nini chafanya Yesu atoe kielezi chake juu ya zile mina?
◆ Yule kabaila ni nani, na nchi ile aendako ni nini?
◆ Wale raia ni akina nani, nao waonyeshaje chuki yao?
◆ Wale watumwa ni akina nani, na ni nini chenye kuwakilishwa na zile mina?
◆ Kwa nini mtumwa mmoja aitwa mwovu, na kupoteza mina yake kwamaanisha nini?