NDOA YA NDUGU MKWE
Desturi ambayo mwanamume anamwoa mjane wa kaka yake asiye na mtoto ili kutokeza uzao utakaoendeleza jina la kaka yake. Kitenzi cha Kiebrania kinachomaanisha ‘kufunga ndoa ya ndugu mkwe’ ni ya·vamʹ, kinahusiana na neno la Kiebrania “ndugu mkwe” na “mjane wa kaka.”—Mwa 38:8; Kum 25:525:7.
Sheria inayohusiana na ndoa ya ndugu mkwe kwenye Kumbukumbu la Torati 25:5, 6 inasema hivi: “Ikiwa ndugu wanaishi pamoja na mmoja wao afe bila mwana, mke wa yule aliyekufa hapaswi kuolewa na mwanamume mwingine nje ya ukoo huo. Ndugu ya mume wake anapaswa kwenda kwake, amchukue awe mke wake, na kufunga naye ndoa ya ndugu mkwe. Mtoto wa kwanza atakayemzaa ataendeleza jina la ndugu yake aliyekufa, ili jina lake lisifutiliwe mbali kutoka Israeli.” Bila shaka, sheria hiyo ilifuatwa iwe ndugu ya aliyekufa alikuwa ameoa au la.
Yehova ndiye “ambaye kila familia mbinguni na duniani hupata jina kutoka kwake.” (Efe 3:15) Anajali kulindwa kwa jina la familia au ukoo. Kanuni hiyo ilifuatwa katika nyakati za wazee wa ukoo na baadaye ilikuwa sehemu ya agano la Sheria la Waisraeli. Mwanamke hakupaswa “kuolewa na mwanamume mwingine nje ya ukoo huo,” yaani, angeolewa na mtu wa ukoo huo tu. Ndugu mkwe alipomchukua, mwana wa kwanza kuzaliwa angeitwa jina la mwanamume aliyekufa na si la ndugu mkwe huyo. Hilo halimaanishi kwamba mwana huyo angeitwa jina lilelile la mwanamume aliyekufa, bali kwamba angeendeleza ukoo na urithi ulioachwa katika nyumba ya mwanamume aliyekufa.
Inaonekana maneno “ikiwa ndugu wanaishi pamoja” hayakumaanisha kwamba waliishi kwenye nyumba moja bali kwenye ujirani uleule. Hata hivyo, Mishna (Yevamot 2:1, 2) inasema kwamba haikumaanisha katika eneo lilelile bali wakati uleule. Bila shaka, kuishi mbali sana kungefanya iwe vigumu kwa mtu kutunza mali zake na urithi wa ndugu yake hadi wakati ambapo mrithi angekuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Mfano wa ndoa ya ndugu mkwe katika nyakati za wazee wa ukoo ni ule wa Yuda. Alimtafutia Eri mzaliwa wake wa kwanza mke aliyeitwa Tamari, na Eri alipomchukiza Yehova, Yehova alimuua. “Kwa hiyo, Yuda akamwambia Onani: ‘Lala na mke wa ndugu yako na ufunge naye ndoa ya ndugu mkwe, umpe ndugu yako mzao.’ Lakini Onani alijua kwamba mzao huyo hangehesabiwa kuwa wake. Kwa hiyo alipolala na mke wa ndugu yake, alimwaga shahawa zake ardhini ili asimpe ndugu yake mzao.” (Mwa 38:5-15) Kwa sababu Onani alikataa kutimiza wajibu wake kuhusiana na mpango wa ndoa ya ndugu mkwe, Yehova alimuua. Kisha, Yuda akamwambia Tamari asubiri mpaka Shela mwana wake wa tatu atakapokua, lakini Yuda hakumruhusu Shela amwoe Tamari.
Kwa wakati unaofaa, baada ya kifo cha mke wa Yuda, Tamari alifanya juu chini ili apate mrithi kutoka kwa baba mkwe wake. Alifanya hivyo kwa kujibadili, akajifunika uso kwa shela na kujifunika mabegani kwa mtandio, akaketi katika barabara ambayo alijua kwamba Yuda atapita. Yuda akamchukua akifikiri ni kahaba na akalala naye. Tamari alichukua baadhi ya vitu kutoka kwa Yuda kama rehani, na wakati ukweli ulipojulikana, Yuda hakumshutumu bali alisema kwamba Tamari ni mwadilifu kuliko yeye. Simulizi hilo linasema kwamba Yuda hakufanya ngono naye tena alipojua mwanamke huyo alikuwa ni Tamari. Hivyo, bila kujua Yuda alitokeza mrithi wa Eri kupitia binti mkwe wake.—Mwa 38.
Chini ya Sheria, ikiwa ndugu mkwe hakutaka kutimiza wajibu wake, mjane alipaswa kupeleka suala hilo kwa wazee wa jiji na kuwaeleza jambo hilo. Alipaswa kwenda mbele yao na kukiri kwamba hataki kumwoa mjane huyo. Ndipo mjane huyo angemvua kiatu chake na kumtemea mate usoni. Kisha, ‘jina la familia ya mwanamume huyo katika Israeli litakuwa “Familia ya mtu aliyevuliwa kiatu,”’ msemo uliofedhehesha nyumba yake.—Kum 25:7-10.
Huenda zoea hilo la kuchukua kiatu lilitokana na kile kilichofanywa pale ambapo mtu alitwaa ardhi, angefanya hivyo kwa kukanyaga udongo wa ardhi hiyo na kutangaza haki yake ya kumiliki kwa kusimama juu yake kwa viatu vyake. Kwa kuvua kiatu chake na kumkabidhi mtu mwingine, alitengua haki yake ya kumiliki mbele ya wanaume wazee waliokuwa mashahidi kwenye lango la jiji.—Ru 4:7.
Hilo linafafanuliwa zaidi kwenye kitabu cha Ruthu. Mwanamume Myahudi anayeitwa Elimeleki alikufa, na pia wanawe wawili, akamwacha Naomi, mke wake, pamoja na binti wakwe zake wawili wakiwa wajane. Kulikuwa na mwanamume ambaye Biblia inamwita “Fulani wa fulani” ambaye alikuwa ndugu wa karibu wa Elimeleki, huenda alikuwa kaka yake. Mwanamume huyo akiwa ndugu wa karibu zaidi, aliitwa go·ʼelʹ, au mkombozi. Mtu huyo alikataa kutimiza wajibu wake lakini alivua kiatu chake na kumpa Boazi, hivyo akamwachia Boazi, ndugu wa pili wa karibu, haki ya kukomboa. Kisha, Boazi akanunua ardhi ya Elimeleki na hivyo akamchukua Naomi, lakini kwa kuwa Naomi alikuwa amezeeka sana asiweze kupata mtoto, binti mkwe wake Ruthu aliyekuwa mjane ndiye aliyekuja kuwa mke wa Boazi ili azae mtoto kwa jina la Elimeleki. Obedi alipozaliwa, wanawake majirani walisema: “Naomi amezaa mwana,” wakimwona mtoto huyo kuwa mwana wa Elimeleki na Naomi. Boazi na Ruthu walifanya utumishi kwa Yehova, na jina alilopewa mwana wao lilimaanisha “Mtumishi; Mtu Anayetumikia.” Yehova alibariki mpango huo kwa kuwa Obedi alikuja kuwa babu ya Daudi, na hivyo akawa sehemu ya ukoo wa Yesu Kristo.— Ru 4.
Ni wazi kwamba haki ya ndoa ya ndugu mkwe ilienda kwa ndugu wa karibu zaidi kama inavyoonyeshwa na sheria inayohusu urithi wa mali, inayotaja, ndugu mkubwa, ndugu wengine kulingana na umri wao, kisha baba mkubwa, na kadhalika. (Hes 27:5-11) Ndoa ya ndugu mkwe inapotajwa kwenye andiko la Mathayo 22:23-28 na Luka 20:27-33, inaonekana kwamba wajibu wa kumwoa mjane wa mwanamume aliyekufa bila kuacha mtoto ungehama kutoka kwa ndugu mmoja hadi mwingine kwa kufuatana baada ya vifo vyao. Ni wazi kwamba ndugu mdogo asingeweza kumtangulia ndugu yake mkubwa, ambaye alikuwa na wajibu kwanza, isipokuwa ndugu huyo mkubwa akatae wajibu huo.