Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
Wafadhili ambao Yesu alizungumza kuwahusu katika usiku wa mwisho kabla ya kifo chake walikuwa nani, na kwa nini waliitwa hivyo?
Jioni ya mwisho kabla ya kifo chake, Yesu aliwashauri mitume wake wasijitafutie umashuhuri miongoni mwa waamini wenzao. Aliwaambia hivi: “Wafalme wa mataifa hupiga ubwana juu yao, na wale walio na mamlaka juu yao huitwa Wafadhili. Hata hivyo, ninyi hampaswi kuwa hivyo.”—Luka 22:25, 26.
Wafadhili ambao Yesu alizungumza kuwahusu walikuwa nani? Maandishi yaliyochongwa, sarafu, na vitabu vya kukunjwa, vinafunua kwamba ilikuwa desturi miongoni mwa Wagiriki na Waroma kuwaheshimu wanaume na watawala maarufu kwa kuwaita Euergetes, au Mfadhili. Wanaume hao walipewa cheo hicho kwa sababu walitimiza utumishi fulani ambao ulinufaisha sana umma.
Wafalme fulani pia walitambuliwa kwa cheo cha Mfadhili. Miongoni mwa wafalme hao ni mtawala wa Misri aliyeitwa Ptolemy III Euergetes (m. 247-222 K.W.K.) na Ptolemy VIII Euergetes II (m. 147-117 K.W.K.). Pia, mtawala Mroma Kaisari Yulio (48-44 K.W.K.) na Augusto (31 K.W.K.–14 W.K.) walijulikana kwa jina hilo la cheo, na vilevile Herode Mkuu, mfalme wa Yudea. Huenda Herode alipewa jina hilo la cheo alipoagiza ngano kwa ajili ya raia wake kulipokuwa na njaa kali na kuwapa nguo maskini.
Adolf Deissmann, msomi wa Biblia Mjerumani, anasema kwamba jina la cheo Mfadhili lilizoeleka sana miongoni mwa watu. Alisema hivi: “Bila hata kupoteza wakati, ilikuwa rahisi sana kulipata [jina hilo] likiwa limechongwa au kuandikwa zaidi ya mara mia moja.”
Hivyo basi, Yesu alimaanisha nini alipowaambia wanafunzi wake, “Ninyi hampaswi kuwa hivyo”? Je, Yesu alikuwa akimaanisha kwamba hawakupaswa kujishughulisha na masuala ya umma, yaani, hawakupaswa kuhangaikia hali za wanadamu wenzao kwa ujumla? Sivyo hata kidogo. Yesu alikuwa akirejezea nia iliyowafanya watu waonyeshe matendo hayo ya ukarimu.
Katika siku za Yesu, matajiri walifadhili maonyesho na michezo iliyofanywa kwenye viwanja vikubwa, walijenga mabustani na mahekalu, na kutegemeza shughuli nyingine kama hizo wakiwa na nia ya kujijengea jina. Hata hivyo, lengo lao kuu lilikuwa kujijengea sifa, umashuhuri, na kupata kura. Kitabu kimoja cha marejeo kinasema, “Ingawa kulikuwa na mifano ya Wafadhili walioonyesha ukarimu wa kweli, kwa kawaida ukarimu wa aina hiyo ulichochewa na tamaa ya kutaka kujinufaisha kisiasa.” Roho kama hiyo ya kujitakia makuu na kujitanguliza ndiyo ambayo Yesu aliwahimiza wafuasi wake waepuke.
Miaka kadhaa baadaye, mtume Paulo alikazia ukweli huo muhimu alipozungumza kuhusu kuwa na mtazamo unaofaa tunapotoa. Aliwaandikia hivi waamini wenzake huko Korintho: “Kila mmoja na afanye kama alivyoazimia moyoni mwake, si kwa kutopenda wala kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda mtoaji mchangamfu.”—2 Kor. 9:7.