Maisha na Huduma ya Yesu
Bishano Lafoka
MAPEMA kidogo jioni, Yesu alifundisha somo zuri la utumishi wa unyenyekevu kwa kuosha miguu ya mitume wake. Baadaye, alianzisha Ukumbusho wa kifo chake kinachokaribia. Sasa, hasa kwa sababu ya kile ambacho kimetendeka sasa hivi, tukio la kushangaza latukia. Mitume wake wahusika katika bishano kali juu ya ni yupi kati yao aonekana kuwa mkubwa kabisa! Yaonekana kwamba hii ni sehemu ya ugomvi wenye kuendelea.
Kumbuka kwamba baada ya Yesu kugeuzwa sura mlimani, mitume walibishana juu ya nani miongoni mwao alikuwa mkubwa kabisa. Zaidi ya hilo, Yakobo na Yohana waliomba vyeo vya umashuhuri katika Ufalme, hiyo ikitokeza ushindani zaidi miongoni mwa mitume. Sasa, katika usiku wake wa mwisho wa kuwa pamoja nao, ni lazima Yesu awe ahuzunika kama nini kuwaona wakizozana tena! Yeye afanya nini?
Badala ya kuwagombeza mitume kwa mwenendo wao, kwa mara nyingine tena Yesu asababu pamoja nao kwa subira: “Wafalme wa mataifa hupiga ubwana juu yao, na wale walio na mamlaka juu yao huitwa Wafadhili. Ingawa hivyo, nyinyi hamtakuwa jinsi hiyo. . . . Kwa maana ni yupi aliye mkubwa zaidi, yule anayeegemea kwenye meza au yule anayehudumia? Je! si yule anayeegemea kwenye meza?” Halafu, akiwakumbusha juu ya kielelezo chake, asema hivi: “Lakini mimi niko kati yenu kama yule anayehudumia.”
Wajapokuwa na hali zao za kutokamilika, mitume wameshikamana na Yesu wakati wa majaribu yake. Kwa hiyo yeye asema: “Mimi nafanya agano pamoja nanyi, kama vile Baba yangu amefanya agano pamoja na mimi, kwa ajili ya ufalme.” Agano hili la kibinafsi kati ya Yesu na wafuasi wake waaminifu-washikamanifu huwaunga wao kwake ili washiriki umiliki wake wa kifalme. Ni hesabu ndogo tu ya 144,000 ambao mwishowe hutiwa ndani ya agano hili kwa ajili ya Ufalme.
Ingawa mitume wametokezewa tazamio hili zuri sana la kushiriki pamoja na Kristo katika utawala wa Ufalme, kwa sasa wao ni dhaifu kiroho. “Nyinyi nyote mtajikwaa kuhusiana na mimi usiku huu,” Yesu asema. Akimwambia Petro kwamba Yeye amesali kwa ajili yake, Yesu ahimiza hivi: “Mara ukiisha kurudi, waimarishe ndugu zako.”
“Watoto wadogo,” Yesu aeleza, “mimi niko pamoja nanyi kitambo kidogo zaidi. Nyinyi mtanitafuta mimi; na kama vile nilivyosema kwa Wayahudi, ‘Niendako nyinyi hamwezi kuja,’ nasema kwenu nyinyi pia kwa sasa. Mimi nawapa nyinyi amri mpya, kwamba mpendane; kama vile mimi nimewapenda nyinyi, ili kwamba nyinyi pia mpendane. Kwa hili wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwa nyinyi wenyewe.”
“Bwana, wewe unaenda wapi?” Petro auliza.
“Niendako huwezi wewe kunifuata sasa,” Yesu ajibu, “lakini utafuata baadaye.”
“Bwana, kwa nini mimi siwezi kukufuata wewe kwa sasa?” Petro ataka kujua. “Mimi nitaisalimisha amri nafsi yangu kwa ajili yako.”
“Je! wewe utaisalimisha amri nafsi yako kwa ajili yangu?” Yesu auliza. “Kwa kweli mimi nasema kwako wewe, Wewe leo, naam, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, hata wewe utanikana mimi mara tatu.”
“Hata ikinipasa mimi kufa pamoja na wewe,” Petro ateta, “kwa vyovyote mimi sitakukana.” Na ingawa mitume wale wengine wajiunga katika kusema hilo hilo, Petro ajisifu hivi: “Ingawa wengine wote wajikwae kuhusiana na wewe, mimi sitajikwaa kamwe!”
Akirejezea wakati ambao aliwatuma mitume nje kwenye safari ya kuhubiri Galilaya bila kibeti na kifuko cha chakula, Yesu auliza hivi: “Nyinyi hamkukosa kitu chochote, je! mlikosa?”
“La!” wao wajibu.
“Lakini sasa acheni yule mwenye kibeti akichukue, vivyo hivyo pia kifuko cha chakula,” yeye asema, “na acheni yule mwenye upanga auze vazi lake la nje anunue mmoja. Kwa maana mimi nasema kwa nyinyi kwamba hili ambalo limeandikwa ni lazima litimizwe katika mimi, yaani, ‘Na yeye alihesabiwa pamoja na wasiofuata sheria.’ Kwa maana lile ambalo lanihusu mimi linapata utendeko.”
Yesu anaelekeza kwenye wakati ambapo atatundikwa pamoja na watenda maovu, au wasiofuata sheria. Pia anaonyesha kwamba baada ya hapo wafuasi wake watakabili mnyanyaso mkali. “Bwana, tazama! panga mbili hizi,” wao wasema.
“Imetosha,” yeye ajibu. Kama tutakavyoona, kuwa kwao na panga hizo kutaruhusu Yesu karibuni afundishe somo jingine muhimu. Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Luka 22:24-38; Yohana 13:31-38; Ufunuo 14:1-3, NW.
◆ Kwa nini bishano la mitume linashangaza sana?
◆ Yesu ashughulikiaje bishano hilo?
◆ Ni nini kitimizwacho na agano ambalo Yesu afanya na wanafunzi wake?
◆ Yesu atoa amri gani mpya, nayo ni ya maana kadiri gani?
◆ Petro aonyeshaje uhakika gani wa kupita kiasi, na Yesu asema nini?
◆ Kwa nini maagizo ya Yesu juu ya kuchukua kibeti na kifuko cha chakula ni tofauti na yale aliyotoa mapema kidogo?