Kitabu Cha Biblia Namba 23—Isaya
Mwandikaji: Isaya
Mahali Kilipoandikiwa: Yerusalemu
Uandikaji ulikamilishwa: Baada ya 732 K.W.K
Wakati Uliohusishwa: c. 778-baada ya 732 K.W.K
1. Hali ilikuwa nini katika Mashariki ya Kati, na hasa katika Israeli na Yuda, katika karne ya nane K.W.K.?
KIVULI chenye kutisha cha mfalme Mwashuri mkatili kilining’inia sana juu ya milki nyinginezo na falme ndogo-ndogo za Mashariki ya Kati. Eneo lote lilikuwa limejaa maongezi ya njama na kufanya mseto (muungano) wa mataifa. (Isa. 8:9-13) Israeli yenye kuasi imani upande wa kaskazini karibuni ingeangukia hila hiyo ya kimataifa, huku wafalme wa Yuda upande wa kusini wakitawala wakiwa hatarini. (2 Fal., sura 15-21) Silaha mpya za pigano zilikuwa zasitawishwa na kutumiwa, kuongezea ogofyo la nyakati hizo. (2 Nya. 26:14, 15) Yeyote angetafuta wapi ulinzi na wokovu? Ingawa jina la Yehova lilikuwa kwenye midomo ya watu na makuhani katika ufalme mdogo wa Yuda, mioyo yao ilikuwa imegeukia mbali sana pande nyingine, kwanza kwa Ashuru na kisha chini kule Misri. (2 Fal. 16:7; 18:21) Imani katika nguvu za Yehova ilikuwa imefifia. Mahali ambapo haikuwa ibada ya sanamu ya moja kwa moja, ilikuwa imeenea njia ya kinafiki ya ibada, yenye kutegemea desturi wala si hofu ya kweli kwa Mungu.
2. (a) Ni nani aliyejibu wito wa kunena kwa ajili ya Yehova, na lini? (b) Ni nini lililo la maana kuhusu jina la nabii huyo?
2 Basi, ni nani angenena kwa ajili ya Yehova? Ni nani angejulisha rasmi nguvu zake za kuokoa? “Mimi hapa, nitume mimi,” likaja jibu lenye utayari. Mnenaji alikuwa Isaya, ambaye tayari alikuwa anatabiri kabla ya hilo. Ilikuwa katika mwaka ule ambao Mfalme Uzia mwenye ukoma alikufa, karibu 778 K.W.K. (Isa. 6:1, 8) Jina Isaya lamaanisha “Wokovu wa Yehova,” ambayo ndiyo maana ileile ya jina Yesu (“Yehova Ni Wokovu”), ingawa laandikwa kinyume. Tangu mwanzo hadi mwisho, unabii wa Isaya wakazia uhakika huu, kwamba Yehova ni wokovu.
3. (a) Ni nini kinachojulikana kuhusu Isaya? (b) Ni katika kipindi gani alichotabiri, na ni nani waliokuwa manabii wengine wa siku zake?
3 Isaya alikuwa mwana wa Amozi (isidhaniwe makosa kuwa ni Amosi, nabii mwingine kutoka Yuda). (1:1) Maandiko yako kimya kuhusu kuzaliwa na kifo chake, ingawa mapokeo ya Kiyahudi yasema alikatwa-katwa kwa msumeno na Mfalme Manase mwovu. (Linganisha Waebrania 11:37.) Maandishi yake yaonyesha kituo chake kikiwa Yerusalemu pamoja na mke wake aliye nabii wa kike na angalau wana wawili wenye majina ya kiunabii. (Isa. 7:3; 8:1, 3) Alitumika wakati wa angalau wafalme wanne wa Yuda: Uzia, Yothamu, Ahazi, na Hezekia; kwa wazi kuanzia karibu 778 K.W.K. (wakati Uzia alipokufa, au yawezekana mapema zaidi) na kuendelea angalau hadi baada ya 732 K.W.K. (mwaka wa 14 wa Hezekia), au muda usiopungua miaka 46. Bila shaka alikuwa pia ameandika unabii wake kufikia tarehe hii ya baadaye. (1:1; 6:1; 36:1) Manabii wengine wa siku yake walikuwa ni Mika katika Yuda na, kule kaskazini, Hosea na Odedi.—Mika 1:1; Hos. 1:1; 2 Nya. 28:6-9.
4. Ni nini kinachoonyesha kwamba Isaya alikuwa mwandikaji wa kitabu hicho?
4 Kwamba Yehova aliamuru Isaya aandike hukumu zake za kiunabii yathibitishwa na Isaya 30:8: “Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.” Marabi wa Kiyahudi wa kale walitambua Isaya kuwa mwandikaji na walijumuisha kitabu hicho kuwa kitabu cha kwanza cha manabii wakubwa (Isaya, Yeremia, na Ezekieli).
5. Ni nini kinachoshuhudia juu ya umoja wa kitabu cha Isaya?
5 Ingawa wengine wameelekeza kwenye badiliko la mtindo wa kitabu hicho kuanzia sura 40 na kuendelea kuwa yaonyesha ni mwandikaji tofauti, au “Isaya wa Pili,” badiliko la habari inayozungumzwa lapasa kutosha kuonyesha hiyo ndiyo sababu. Kuna uthibitisho mwingi kwamba Isaya aliandika kitabu chote chenye jina lake. Kwa kielelezo, umoja wa kitabu hicho waonyeshwa na usemi, “aliye Mtakatifu wa Israeli,” unaotokea mara 12 katika sura 1 hadi 39, na mara 13 katika sura 40 hadi 66, jumla ya mara 25; ambapo watokea mara 6 tu katika Maandiko ya Kiebrania mengineyo. Mtume Paulo pia ashuhudia umoja wa kitabu hiki kwa kunukuu kutoka sehemu zote za unabii na kumhesabia kitabu chote mwandikaji mmoja, Isaya.—Linganisha Warumi 10:16, 20; 15:12 pamoja na Isaya 53:1; 65:1; 11:1.
6. Hati-kunjo ya Isaya ya Bahari ya Chumvi inatoaje uthibitisho wenye kusadikisha (a) kwamba Biblia zetu leo zawakilisha maandishi yaliyopuliziwa na Mungu ya awali na (b) kwamba kitabu chote kiliandikwa na Isaya yule yule mmoja?
6 La kupendeza ni kwamba, kuanzia mwaka 1947, hati fulani za kale zilichomolewa kwenye giza la mapango yasiyo mbali kutoka Khirbet Qumran, karibu pwani ya kaskazini magharibi ya Bahari ya Chumvi. Hizo zilikuwa ni Makunjo ya Bahari ya Chumvi, ambayo yalitia ndani unabii wa Isaya. Yameandikwa kwa uzuri katika Kiebrania kilichohifadhiwa vizuri cha kabla ya Masora na yana umri wa miaka 2,000 hivi, tangu mwisho wa karne ya pili K.W.K. Kwa hiyo maandishi yayo yana umri wa miaka elfu moja hivi zaidi ya hati za kale zaidi zilizopo za maandishi ya Masora, ambayo juu yake tafsiri za kisasa za Maandiko ya Kiebrania zategemea. Kuna utofautiano mdogo-mdogo wa mwendelezo na tofauti fulani katika muundo wa sarufi (kanuni za lugha), lakini hayatofautiani kimafundisho na maandishi ya Masora. Hapa pana uthibitisho wenye kusadikisha kwamba Biblia yetu leo ina ujumbe ule wa awali wa Isaya uliopuliziwa na Mungu. Zaidi ya hayo, makunjo hayo ya kale yanakanusha madai ya wachambuzi ya kuwapo kwa “Isaya” wawili, kwa kuwa sura ya 40 yaanza kwenye mstari wa mwisho wa safu ya kuandikiwa yenye sura ya 39, sentensi ya kufungua ikikamilishwa katika safu ifuatayo. Kwa hiyo, kwa wazi mnakiliji hakuwa na habari ya badiliko lolote linalowaziwa la mwandikaji au mgawanyo wowote katika kitabu hiki kufikia hapa.a
7. Ni uthibitisho gani tele uliopo kuhusu uasilia wa Isaya?
7 Kuna uthibitisho wa kutosha wa uasilia wa kitabu cha Isaya. Mbali na Musa, hakuna nabii mwingine anayenukuliwa mara nyingi na waandikaji wa Biblia ya Kikristo. Pia kuna utele wa uthibitisho wa kihistoria na kiakiolojia unaotoa uthibitisho kuwa ni cha halisi, kama vile maandishi ya kihistoria ya wafalme Waashuri, kutia mche pembesita wa Senakeribu ambao juu yao yeye anatoa simulizi lake mwenyewe la mazingiwa ya Yerusalemu.b (Isa., sura 36, 37) Rundo la mabomoko ambalo wakati mmoja lilikuwa Babuloni bado latoa ushahidi wa utimizo wa Isaya 13:17-22.c Kulikuwako ushuhuda ulio hai kwa namna ya kila mmoja wa wale maelfu ya Wayahudi waliosafiri kurejea Babuloni, kwa kuwekwa huru na mfalme ambaye jina lake, Koreshi, lilikuwa limeandikwa na Isaya karibu miaka 200 mapema. Yawezekana kwamba Koreshi alionyeshwa maandishi hayo ya kiunabii baadaye, kwa maana, alipoweka huru baki la Kiyahudi, alinena juu ya kupewa utume na Yehova afanye hivyo.—Isa. 44:28; 45:1; Ezra 1:1-3.
8. Upulizio wa Mungu wathibitishwaje na utimizo wa unabii mbalimbali wa Kimesiya?
8 Wenye kutokeza katika kitabu cha Isaya ni unabii mbalimbali wa Kimesiya. Isaya ameitwa “nabii Mwevanjeli,” utabiri mwingi mbalimbali umetimizwa katika matukio ya maisha ya Yesu. Sura 53, kwa muda mrefu ikiwa “sura ya fumbo,” si kwa towashi Mwethiopia peke yake anayerejezewa katika Matendo sura ya 8 bali pia kwa watu wa Kiyahudi kwa ujumla, yatabiri kiwaziwazi alivyotendwa Yesu hivi kwamba ni kama simulizi la shahidi aliyejionea. Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo yanaandika juu ya utimizo mbalimbali wa kiunabii wa sura hii ya Isaya inayotokeza, kama ulinganishi mbalimbali ufuatao unavyoonyesha: mst. 1—Yohana 12:37, 38; mst. 2—Yohana 19:5-7; mst. 3—Marko 9:12; mst. 4—Mathayo 8:16, 17; mst. 5—1 Petro 2:24; mst. 6—1 Petro 2:25; mst. 7—Matendo 8:32, 35; mst. 8—Matendo 8:33; mst. 9—Mathayo 27:57-60; mst. 10—Waebrania 7:27; mst. 11—Warumi 5:18; mst. 12—Luka 22:37. Ni nani isipokuwa Mungu angeweza kuwa chanzo cha utabiri sahihi jinsi hiyo?
YALIYOMO KATIKA ISAYA
9. Yaliyomo katika Isaya yanajigawanyaje?
9 Sura sita za kwanza zatoa kikao cha Yuda na Yerusalemu na kusimulia hatia ya Yuda mbele ya Yehova na kupewa utume kwa Isaya. Sura za 7 hadi 12 zahusu hujuma (mashambulizi) zenye kutisha za adui na ahadi ya faraja na Mwana-Mfalme wa Amani aliyepewa utume na Yehova. Sura za 13 hadi 35 zina mfululizo wa matamko juu ya mataifa mengi na utabiri wa wokovu ambao ungetolewa na Yehova. Matukio ya kihistoria ya utawala wa Hezekia yasimuliwa katika sura za 36 hadi 39. Sura zinazosalia, 40 hadi 66, zina habari kuu ya kukombolewa kutoka Babuloni, kurejea kwa baki la Kiyahudi, na kurudishwa kwa Sayuni.
10. (a) Ni kwa nini Isaya anatoa wito kwa taifa linyooshe mambo? (b) Yeye atabiri nini kwa ajili ya sehemu ya mwisho ya siku?
10 Ujumbe wa Isaya “katika habari za Yuda na Yerusalemu” (1:1–6:13). Mwone amevaa magunia na sapatu akiwa amesimama Yerusalemu na kupaaza sauti hivi: Enyi watawala wa kiimla! Enyi watu! Sikilizeni! Taifa lenu limegonjeka tangu kichwa hadi kidole cha mguu, na mmechosha Yehova kwa mikono yenu yenye madoa ya damu iliyonyanyuliwa katika sala. Njoni, nyoosheni mambo pamoja naye, ili dhambi nyekundu zifanywe nyeupe kama theluji. Katika sehemu ya mwisho ya siku, mlima wa nyumba ya Yehova utainuliwa, na mataifa yote wataumiminikia kwa ajili ya maagizo. Hawatajifunza kupigana tena. Yehova atainuliwa juu na kutakaswa. Lakini kwa wakati huu Israeli na Yuda, ijapokuwa walipandwa mbegu nzuri ya zabibu, wanazaa zabibu za uvunjaji-sheria. Wanafanya wema kuwa ubaya na ubaya kuwa wema, kwa maana wao ni wenye hekima machoni pao wenyewe.
11. Isaya apokea utume wake kuambatana na njozi gani?
11 “Nalimwona Bwana [Yehova, NW] ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana,” asema Isaya. Pamoja na njozi hiyo waja utume wa Yehova: “Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia.” Kwa muda gani? “Hata miji itakapokuwa ukiwa.”—6:1, 9, 11.
12. (a) Isaya na wana wake watumiwaje kuwa ishara za kiunabii? (b) Ni ahadi gani yenye kutokeza inayotolewa katika Isaya sura ya 9?
12 Hujuma (mashambulizi) za adui zenye kutisha na ahadi ya faraja (7:1–12:6). Yehova atumia Isaya na wana wake kuwa ‘ishara na miujiza’ ili kuonyesha kwamba mseto (muungano) wa Shamu na Israeli wa kupigana na Yuda utashindwa lakini baada ya muda Yuda wataenda kwenye utekwa na kurudi baki tu. Mwanamwali atachukua mimba na kuzaa mwana. Ataitwa nani? Imanueli (maana yake, “Pamoja Nasi Ni Mungu”). Acha maadui waliofanya mseto kupigana na Yuda watambue hilo! “Jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande.” Kutakuwako nyakati zenye taabu, lakini ndipo nuru kubwa itang’aa juu ya watu wa Mungu. Kwa maana mtoto amezaliwa kwetu, “naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme [Mwana-Mfalme, NW] wa amani.”—7:14; 8:9, 18; 9:6.
13. (a) Ni tokeo gani linalongojea Mwashuri fidhuli? (b) Ni nini litakalokuwa tokeo la utawala wa ‘kitawi’ kutoka kwa Yese?
13 “Ole wake Ashuru,” Yehova apaaza sauti, “fimbo ya hasira yangu.” Baada ya kutumia fimbo hiyo juu ya “taifa lenye kukufuru,” Mungu atamkata Mwashuri fidhuli naye pia. Baadaye, ‘baki litarudi.’ (10:5, 6, 21) Ona sasa chipukizi, kitawi kutoka kisiki cha Yese (baba ya Daudi)! ‘Kitawi’ hicho kitatawala katika uadilifu, na kupitia kwake kutakuwako kuona shangwe kwa uumbaji wote, bila umizo wala uharibifu, “maana dunia itajawa na kumjua BWANA [Yehova, NW], kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (11:1, 9) Huyo akiwa ishara kwa ajili ya mataifa, barabara kuu yatoka Ashuru kwa ajili ya baki lenye kurejea. Kutakuwako shangwe kubwa katika kuchota maji kutoka chemchemi za wokovu na kufanyia Yehova wimbo.
14. Ni mshuko gani unaotabiriwa kwa ajili ya Babuloni?
14 Kutamka maangamizi ya Babuloni (13:1–14:27). Sasa Isaya atazama mbele ya siku za Mwashuri kwenye wakati wa kutia fora kwa Babuloni. Sikiliza! Mvumo wa watu wengi, ghasia ya falme, ya mataifa waliokusanyika pamoja! Yehova akusanya jeshi la pigano! Ni siku yenye giza kwa Babuloni. Nyuso zenye kustaajabu zachomeka, na mioyo yayeyuka. Wamedi wasio na huruma wataangusha Babuloni, “utukufu wa falme.” Utakuwa ukiwa usiokaliwa na makao ya viumbe wa mwitu “tangu kizazi hata kizazi.” (13:19, 20) Walio wafu katika Sheoli wagutushwa wampokee mfalme wa Babuloni. Funza wawa kitanda chake na mabuu kifuniko chake. Mshusho kama nini wa ‘nyota hii, mwana wa asubuhi’! (14:12) Yeye alitamani kukweza kiti chake cha enzi lakini amekuwa mzoga uliotupwa nje, wakati Yehova afagiapo Babuloni na ufagio wa uangamizi. Hakuna jina, hakuna baki, hakuna uzao, hakuna wajukuu, watakaobaki!
15. Ni kuhusu kuwekwa ukiwa gani kwa kimataifa anakotabiri Isaya?
15 Ukiwa wa kimataifa (14:28–23:18). Sasa Isaya aelekeza nyuma kwa Ufilisti kando ya Bahari ya Mediterrania na kisha Moabu, kusini mashariki mwa Bahari ya Chumvi. Aelekeza unabii wake kupita mpaka wa Israeli wa kaskazini hadi Dameski ya Shamu, ateremka sana kusini kuingia Ethiopia, na apanda na Naili hadi Misri, akiwa na hukumu za Mungu zenye kutokeza ukiwa njia yote hiyo. Aeleza juu ya mfalme Sargoni Mwashuri, mtangulizi wa Senakeribu, akipeleka amiri Tartani kukabiliana na mji wa Kifilisti wa Ashdodi, magharibi mwa Yerusalemu. Wakati huu Isaya aambiwa avue nguo na kwenda akiwa uchi na bila sapatu (viatu) kwa miaka mitatu. Kwa njia hiyo aonyesha kwa uwazi ubatili wa kutumaini Misri na Ethiopia, ambao, “matako yao wazi,” watapelekwa mateka na Mwashuri.—20:4.
16. Ni misiba gani inayoonwa ya Babuloni, Edomu na wenye fujo wa Yerusalemu, na pia ya Sidoni na Tiro?
16 Mlinzi juu ya mnara wake wa lindo aona anguko la Babuloni na miungu yake, naye aona upinzani wa kukabiliana na Edomu. Yehova mwenyewe asema na watu wa Yerusalemu wenye fujo ambao wasema, “tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.” ‘Mtakufa,’ asema Yehova. (22:13, 14) Merikebu za Tarshishi pia zitapiga yowe, na Sidoni itaaibishwa, kwa maana Yehova ametoa shauri juu ya Tiro, “kuwaaibisha watu [waheshimiwa, NW] wa duniani wote.”—23:9.
17. Ni hukumu na kurudishwa gani kunakotabiriwa kwa ajili ya Yuda?
17 Hukumu na wokovu wa Yehova (24:1–27:13). Lakini tazama sasa kwenye Yuda! Yehova anafanya bara kuwa tupu. Watu na kuhani, mtumwa na bwana, mnunuzi na mwuzaji—wote lazima waende, kwa maana wameepa sheria za Mungu na kuvunja agano la kudumu wakati usiojulikana. Lakini baada ya muda atageuza uangalifu wake kwa wafungwa na kuwakusanya. Yeye ni ngome na kimbilio. Atatayarisha karamu katika mlima wake na kumeza kifo milele, akipangusa machozi kutoka nyuso zote. “Huyu ndiye Mungu wetu” itasemwa. “Huyu ndiye BWANA [Yehova, NW].” (25:9) Yuda ina jiji lenye wokovu kwa kuwa na kuta. Amani yenye kuendelea ni ya wale wanaomtumaini Yehova, “Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele.” Lakini mwovu “hatajifunza haki.” (26:4, 10) Yehova atachinja wapinzani wake, lakini atarejesha Yakobo.
18, 19. (a) Ni ole na shangwe gani zenye kutofautiana zinazotangazwa rasmi kwa ajili ya Efraimu na Sayuni? (b) Yehova ataokoa na kuongoza watu wake katika nafasi zipi?
18 Ghadhabu na baraka za Mungu (28:1–35:10). Ole kwa walevi wa Efraimu, ambao “uzuri wa fahari” yao lazima ufifie! Lakini Yehova “atakuwa ni taji ya fahari, na kilemba cha uzuri” kwa baki la watu wake. (28:1, 5) Hata hivyo, wenye kujivuna wa Yerusalemu wanatazamia uwongo kuwa kimbilio, badala ya jiwe la msingi lililojaribiwa na lenye thamani katika Sayuni. Furiko la ghafula litawachukua wote. Manabii wa Yerusalemu wamelala, na kitabu cha Mungu kimetiwa muhuri wasikifungue. Midomo yakaribia, lakini mioyo iko mbali. Hata hivyo siku itakuja wakati viziwi watasikia maneno ya kitabu hiki. Vipofu wataona na wapole kushangilia.
19 Ole kwa wale washukao kwenda Misri kwa ajili ya kimbilio! Watu hawa wenye shingo ngumu wataka njozi za ubembelezi, zenye kudanganya. Watakatiliwa mbali, lakini Yehova atarejesha baki. Wao wataona Mfunzi Mkuu wao, nao watatapanya mifano yao, waiite “uchafu mtupu!” (30:22, NW) Yehova ndiye Mtetezi wa kweli wa Yerusalemu. Mfalme atatawala katika uadilifu, pamoja na wakuu wake. Ataleta amani, utulivu, na usalama hadi wakati usiojulikana. Hiana itasababisha wajumbe wa amani walie kwa uchungu wa moyo, lakini kwa watu wake mwenyewe Aliye Mwenye Fahari, Yehova, ndiye Hakimu, Mtoa-Sheria, na Mfalme, naye mwenyewe atawaokoa. Hakuna mkazi atakayesema wakati huo: “Mimi mgonjwa.”—33:24.
20. Ni ghadhabu gani itakayomwagikia mataifa, lakini ni baraka gani zinazongojea baki lililorudishwa?
20 Ghadhabu ya Yehova lazima imwagikie mataifa. Mizoga itavunda, na milima itayeyuka kwa damu. Edomu lazima ifanywe ukiwa. Lakini kwa ajili ya wakombolewa wa Yehova, uwanda wa jangwa utachanua, na “utukufu wa BWANA [Yehova, NW], ukuu wa Mungu wetu,” utatokea. (35:2) Vipofu, viziwi, na wasionena wataponywa, na Njia ya Utakatifu itafunguliwa wafidiwa wa Yehova warudipo Sayuni kwa shangwe.
21. Mwashuri atupa dhihaka gani kwa Yerusalemu?
21 Yehova afukuza Ashuru katika siku za Hezekia (36:1–39:8). Je! kitia-moyo cha Isaya cha kutegemea Yehova chatumika? Je! chaweza kustahimili jaribu? Katika mwaka wa 14 wa utawala wa Hezekia, Senakeribu wa Ashuru akata kama upanga kotekote Palestina na aelekeza baadhi ya vikosi vyake vijaribu kutisha Yerusalemu. Mnenaji wake mwenye kunena Kiebrania, Rabshake, atupa maswali ya dhihaka kwa watu waliojipanga kwenye kuta za mji huo: ‘Tumaini lenu ni nani? Misri? mwanzi uliopondeka! Yehova? Hakuna mungu anayeweza kuokoa kutoka mfalme wa Ashuru!’ (36:4, 6, 18, 20) Kwa kutii mfalme, watu hawatoi jibu.
22. Yehova ajibuje sala ya Hezekia, Naye atimizaje unabii wa Isaya?
22 Hezekia asali kwa Yehova kuomba wokovu kwa ajili ya jina Lake, na kupitia Isaya, Yehova ajibu kwamba Yeye atatia kulabu yake katika pua ya Mwashuri na kumwongoza kurudia njia aliyokuja nayo. Malaika mmoja apiga Waashuri 185,000 na kuwaua, na Senakeribu afanya mbiombio kurudi nyumbani, ambako wana wake mwenyewe wamwua baadaye katika hekalu lake la kipagani.
23. (a) Ni nini kinachofanya Hezekia atunge zaburi kwa Yehova? (b) Ni ukosefu gani wa busara anaofanya, hilo likitokeza unabii gani wa Isaya?
23 Hezekia awa mgonjwa mahututi. Hata hivyo, Yehova asababisha kimwujiza kivuli kilichotokezwa na jua kirudi nyuma, kuwa ishara kwamba Hezekia ataponywa, na miaka 15 yaongezwa kwenye maisha ya Hezekia. Katika kushukuru atunga zaburi ya kupendeza ya sifa kwa Yehova. Wakati mfalme wa Babuloni apelekapo wajumbe, akimpongeza kinafiki kwa ajili ya kupata kwake nafuu, kwa kukosa busara Hezekia awaonyesha hazina za kifalme. Kama tokeo, Isaya atabiri kwamba kila kitu katika nyumba ya Hezekia kitapelekwa Babuloni siku moja.
24. (a) Ni habari gani za utulizo ambazo Yehova anatangaza? (b) Je! miungu ya mataifa yaweza kulingana na Yehova kuhusiana na ukuu, naye atoa wito wa ushahidi gani?
24 Yehova atuliza mashahidi wake (40:1–44:28). Neno la kufunua la sura ya 40, ‘Tuliza’ yaeleza ile sehemu inayobaki ya Isaya. Sauti fulani katika jangwa yapaazwa hivi: ‘Itengenezeni njia ya BWANA [Yehova, NW]’ enyi watu! (40:1, 3) Kuna habari njema kwa ajili ya Sayuni. Yehova huchunga kundi lake, akibeba wana-kondoo wachanga katika kifua chake. Kutoka mbingu zilizo juu yeye hutazama chini kwenye duara ya dunia. Aweza kulinganishwa na nini katika ukuu? Yeye huwapa nguvu kamili na nishati yenye kutendesha wao waliochoka na kulegea wanaomtumaini. Yeye ajulisha rasmi kuwa ile mifano ya kuyeyushwa ya mataifa ni upepo na si halisi. Mchaguliwa wake atakuwa agano kwa ajili ya vikundi vya watu na nuru kwa mataifa ili kufungua macho yenye upofu. Yehova asema hivi kwa Yakobo, ‘mimi nimekupenda,’ na atoa wito kwa mashariki, magharibi, kaskazini, na kusini: ‘Usizuie, waleteni wana wangu na mabinti zangu.’ (43:4, 6) Mahakama ikiwa inakutana, aidai miungu ya mataifa itokeze mashahidi wathibitishe uungu wayo. Watu wa Israeli ni mashahidi wa Yehova, mtumishi wake, wakishuhudia kwamba yeye ni Mungu na Mwokoaji. Kwa Yeshuruni (“Aliye Mnyoofu,” Israeli) yeye aahidi roho yake na kisha aaibisha wafanyizaji wa mifano isiyoona chochote, isiyojua chochote. Yehova ndiye Mkombozi wa watu wake; Yerusalemu litakaliwa tena na hekalu lalo kujengwa upya.
25. Watu watakuja kujua nini kupitia hukumu za Yehova juu ya Babuloni na miungu bandia yake?
25 Kisasi juu ya Babuloni (45:1–48:22). Kwa ajili ya Israeli, Yehova ateua Koreshi akomeshe Babuloni. Watu watafanywa wajue kwamba Yehova pekee ndiye Mungu, Muumba wa mbingu, dunia, na mwanadamu juu yayo. Afanyia mzaha miungu ya Babuloni Beli na Nebo, kwa maana ni Yeye tu awezaye kueleza mwisho tangu mwanzo. Binti bikira wa Babuloni ataketi katika mavumbi, akiwa ameondoshwa kwenye kiti cha enzi na akiwa uchi, na umati wa washauri wake watateketezwa kama mabua makavu. Yehova awaambia waabudu sanamu wa Kiisraeli ‘wenye shingo ya chuma, na kipaji cha uso cha shaba’ kwamba wangeweza kuwa na amani, uadilifu, na fanaka kwa kumsikiliza, lakini ‘hapana amani kwa waovu.’—48:4, 22.
26. Sayuni litafarijiwaje?
26 Sayuni lafarijiwa (49:1–59:21). Akimtoa mtumishi wake kuwa nuru kwa mataifa, Yehova apaaza sauti kwa wale walio gizani: “Haya, tokeni.” (49:9) Sayuni litafarijiwa, na nyika yalo itakuwa kama Edeni, shamba la Yehova, lenye kufurika mshangilio, shangwe, shukrani, na sauti ya wimbo. Yehova atafanya mbingu ziteketee, dunia ichakae kama vazi, na wakaaji wayo wafe kama nzi hoi. Kwa hiyo kwa nini kuhofu suto la watu wanaokufa? Kikombe kichungu ambacho Yerusalemu limekunywa lazima sasa kiendee mataifa ambayo wamelikanyaga chini.
27. Ni habari njema gani linazotangaziwa Sayuni, na ni nini kinachotabiriwa kuhusu ‘mtumishi wa Yehova’?
27 ‘Amka, Ee Sayuni, jikung’ute mavumbi’ Ona mjumbe, akienda mbio juu ya milima akiwa na habari njema na kutoa wito kwa Sayuni, “Mungu wako anamiliki!” (52:1, 2, 7) Tokeni mahali palipo pachafu na kujitunza wenyewe safi, nyinyi mlio katika utumishi wa Yehova. Sasa nabii huyo aeleza ‘mtumishi wa Yehova.’ (53:11) Yeye ni mtu anayedharauliwa, anayeepukwa, mwenye kuchukua maumivu yetu na bado ahesabiwa kuwa amepigwa na Mungu. Alidungwa kwa ajili ya kosa letu, lakini alituponya sisi kwa majeraha yake. Kama kondoo aliyeletwa machinjoni, hakufanya jeuri yoyote na hakusema udanganyifu. Alitoa nafsi yake kuwa toleo la hatia ili kuchukua makosa ya watu wengi.
28. Ubarikiwa ujao wa Sayuni waelezwaje, na kwa kukamatana na agano gani?
28 Kama mwenyewe mume, Yehova aambia Sayuni lilie kwa shangwe kwa sababu ya kuzaa kwalo kujako. Ingawa lilipatwa na mteseko na kusukwa-sukwa na tufani, litakuwa jiji la misingi ya yakuti samawi, nguzo za akiki nyekundu, na malango ya almasi. Wana wake, waliofundishwa na Yehova, watashangilia amani tele, na hakuna silaha itakayofanyizwa juu yao itafanikiwa. “Haya, kila aonaye kiu,” apaaza sauti Yehova. Kama wakija, atafanya pamoja nao “agano la milele, naam, rehema za Daudi”; atatoa kiongozi na amiri kuwa shahidi wa vikundi vya kitaifa. (55:1-4) Mawazo ya Mungu ni ya juu sana kuliko ya binadamu, na neno lake litafaulu bila shaka. Matowashi wenye kushika sheria yake, hata wawe wa taifa gani, watapokea jina bora kuliko wana na mabinti. Nyumba ya Yehova itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya vikundi vyote vya watu.
29. Yehova awaambiaje waabudu sanamu, lakini anatoa uhakikisho gani kwa watu wake?
29 Akiwa Aliye Juu na Aliyekwezwa, ambaye jina lake ni takatifu, Yehova aeleza juu ya waabudu sanamu wenye kichaa cha ngono kwamba hawatashindana na Israeli hadi wakati usiojulikana. Kufunga kwao kwa kidini ni vifichio vya uovu. Mkono wa Yehova si mfupi mno usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito sana kuweza kusikia, lakini ‘maovu yenu ndiyo yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu,’ asema Isaya. (59:2) Ndiyo sababu wanatumainia nuru lakini wapapasa gizani. Kwa upande mwingine, roho ya Yehova juu ya watu wa agano lake takatifu yahakikisha kwamba neno lake litabaki katika kinywa chao kwa vizazi vyote vya wakati ujao, lisiondoleke.
30. Yehova anarembeshaje Sayuni, kama inavyotolewa kielezi na majina mapya gani?
30 Yehova arembesha Sayuni (60:1–64:12). “Ondoka [mwanamke, NW], uangaze; kwa kuwa . . . utukufu wa BWANA [Yehova, NW] umekuzukia.” Kinyume cha hilo, giza zito limeikumba dunia. (60:1, 2) Wakati huo Sayuni litainua macho yalo na kuangaza, na moyo walo utatetema uonapo mali za mataifa zikujia umati wenye kuinuka-inuka wa ngamia. Kama mawingu ya njiwa wanaoruka, watakusanyika kwalo. Wageni watajenga kuta zalo, wafalme watalihudumia, na malango yalo hayatafungwa kamwe. Mungu walo lazima awe uzuri walo, naye ataongeza kwa kasi mmoja kuwa elfu na mdogo kuwa taifa hodari. Mtumishi wa Mungu apaaza sauti kwamba roho ya Yehova iko juu yake, ikimpaka mafuta aeleze habari njema. Sayuni wapewa jina jipya, Upendezi Wangu Umo Ndani Yalo (Hefsiba), na bara lalo laitwa Uenyeji Kama Mke (Beula). (62:4, NW, kielezi-chini) Agizo latolewa barabara kuu ya kurudi kutoka Babuloni ifunikwe mchanga na ishara iinuliwe katika Sayuni.
31. Ni nani anayetoka Edomu, na watu wa Mungu wanatoa sala gani?
31 Kutoka Bozra katika Edomu aja mmoja aliyevaa mavazi ya wekundu wa damu. Katika kasirani yake amekanyagia chini watu katika hori ya divai, akisababisha watokwe na damu. Watu wa Yehova wahisi sana hali yao ya uchafu na watoa sala yenye kuchoma, wakisema, ‘Ee Yehova, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu. Usione hasira nyingi. Sisi sote tu watu wako.’—64:8, 9.
32. Tofauti na wale wanaomwacha Yehova, watu wa Yehova wenyewe waweza kushangilia nini?
32 “Mbingu mpya na dunia mpya!” (NW) (65:1–66:24). Watu ambao wamemwacha Yehova ili kufuatia miungu ya “Bahati Njema” na “Ajali” watakufa njaa na kutahayarika. (65:11, NW) Watumishi wa Mungu watashangilia katika wingi. Tazama! Yehova aumba mbingu mpya na dunia mpya. Furaha na shangwe vitapatikana Yerusalemu na katika watu walo kama nini! Nyumba zitajengwa na mashamba ya mizabibu kupandwa, naye mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha kama kitu kimoja. Hakutakuwako dhara wala uharibifu wowote.
33. Ni shangwe, utukufu, na udumifu gani unaotabiriwa kwa ajili ya wapendao Yerusalemu?
33 Mbingu ndizo kiti chake cha enzi na dunia ni kiti chake cha miguu, kwa hiyo watu waweza kumjengea Yehova nyumba gani? Taifa litazaliwa katika siku moja, na wapenda-Yerusalemu wote wanaalikwa washangilie wakati Yehova alipapo amani kama vile mto. Atakuja kama moto juu ya maadui wake—magari ya tufani ya upepo vikilipa kasirani yake juu ya mnofu wote usiotii, pamoja na ghadhabu kali na miali ya moto. Wajumbe wataenda miongoni mwa mataifa yote na kwenye visiwa vya mbali kueleza utukufu wake. Mbingu na dunia mpya zake zitakuwa za kudumu. Vivyo hivyo, wale wanaomtumikia na uzao wao wataendelea kusimama. Ni ama hilo au kifo cha milele.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
34. Ni nini baadhi ya vielezi vilivyo wazi vinavyoongeza nguvu kwenye ujumbe wa Isaya?
34 Kikiangaliwa katika pande zote, kitabu cha kiunabii cha Isaya ni zawadi yenye mafaa zaidi kutoka kwa Yehova. Kinaelimisha juu ya mawazo yaliyokwezwa ya Mungu. (Isa. 55:8-11) Wanenaji wa peupe wa kweli za Biblia wanaweza kutumia Isaya kikiwa nyumba ya hazina ya vielezi viliyo wazi ambavyo vinasadikisha hoja kwa nguvu sana kama ile ya mifano ya Yesu. Isaya atuvuta kwa nguvu kwa kuonyesha upumbavu wa binadamu anayetumia mti ule ule kwa ajili ya kuni na kwa ajili ya kutengeneza sanamu ya ibada. Atufanya tuhisi ukosefu wa starehe wa mtu ambaye yuko juu ya kitanda kilicho kifupi sana akiwa na kifuniko chembamba mno, na atufanya tusikie kulala usingizi mzito kwa manabii ambao ni kama mbwa wasiotoa kelele, wakiwa ni wavivu mno kuweza kubweka. Ikiwa sisi wenyewe, kama anavyotia moyo Isaya, ‘tunatafuta katika kitabu cha Yehova na kusoma kwa sauti,’ twaweza kuthamini ujumbe wenye nguvu uliomo katika Isaya kwa ajili ya siku hizi.—44:14-20; 28:20; 56:10-12; 34:16.
35. Isaya chakaziaje uangalifu kwenye Ufalme mikononi mwa Mesiya, na kwa yule mtangulizi, Yohana Mbatizaji?
35 Unabii huo unaelekeza fikira hasa kwenye Ufalme wa Mungu mikononi mwa Mesiya. Yehova mwenyewe ndiye Mfalme mkuu, na ndiye anayetuokoa. (33:22) Lakini vipi juu ya Mesiya mwenyewe? Tangazo rasmi la malaika kwa Mariamu kuhusu mtoto ambaye angezaliwa lilionyesha kwamba Isaya 9:6, 7 lingetimizwa katika kupokea kwake kiti cha enzi cha Daudi; “ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:32, 33) Mathayo 1:22, 23 yaonyesha kwamba kuzaliwa kwa Yesu na bikira kulikuwa ni utimizo wa Isaya 7:14 na yamtambulisha kuwa “Imanueli.” Miaka 30 hivi baadaye, Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri kwamba “ufalme wa mbinguni umekaribia.” Waandikaji wa Gospeli wote wanne hunukuu Isaya 40:3 ili kuonyesha kwamba Yohana huyu ndiye aliyekuwa ‘akilia nyikani.’ (Mt. 3:1-3; Mk. 1:2-4; Luka 3:3-6; Yn. 1:23) Kwenye ubatizo wake Yesu alikuwa Mesiya—Mpakwa Mafuta wa Yehova, kitawi au mzizi wa Yese—ili atawale mataifa. Juu yake yapaswa kuweka tumaini lao, kwa utimizo wa Isaya 11:1, 10.—Rum. 15:8, 12.
36. Ni utimizo gani wa unabii mbalimbali mwingi unaotambulisha waziwazi Mesiya aliye Mfalme?
36 Ona jinsi Isaya anavyoendelea kutambulisha Mesiya aliye Mfalme! Yesu alisoma utume wake kutoka hati-kunjo fulani ya Isaya ili kuonyesha kwamba alikuwa Mpakwa Mafuta wa Yehova, na kisha akaendelea “kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu” kama alivyosema, “kwa sababu hiyo nalitumwa.” (Luka 4:17-19, 43; Isa. 61:1, 2) Yale masimulizi manne ya Gospeli yamejawa na mambo mengi juu ya huduma ya kidunia ya Yesu na namna ya kifo chake kama ilivyotabiriwa katika Isaya sura ya 53. Ingawa walisikia habari njema za Ufalme na kuona kazi za ajabu za Yesu, Wayahudi hawakupata maana ya hayo kwa sababu ya mioyo yao isiyoamini, katika utimizo wa Isaya 6:9, 10; 29:13; na 53:1. (Mt. 13:14, 15; Yn. 12:38-40; Mdo. 28:24-27; Rum. 10:16; Mt. 15:7-9; Mk. 7:6, 7) Yesu alikuwa jiwe la kuwakwaza, lakini akawa jiwe la pembeni la msingi ambalo Yehova aliweka katika Sayuni na ambalo juu yalo Yeye hujenga nyumba yake ya kiroho katika utimizo wa Isaya 8:14 na 28:16.—Luka 20:17; Rum. 9:32, 33; 10:11; 1 Pet. 2:4-10.
37. Mitume wa Yesu walinukuu na kutumia Isaya jinsi gani?
37 Mitume wa Yesu Kristo waliendelea kutumia vizuri unabii wa Isaya, wakiutumia kwenye huduma. Kwa kielelezo, katika kuonyesha kwamba wahubiri wahitajiwa ili kujenga imani, Paulo alinukuu Isaya katika kusema: “Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!” (Rum. 10:15; Isa. 52:7; ona pia Warumi 10:11, 16, 20, 21.) Petro pia anukuu Isaya katika kuonyesha udumifu wa habari njema: “Maana, mwili wote ni kama majani, na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka; bali Neno la Bwana [Yehova, NW] hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu [kuwa habari njema, NW].”—1 Pet. 1:24, 25; Isa. 40:6-8.
38. Ni habari gani kuu ya Ufalme mtukufu inayosimuliwa katika Isaya, na kufuatiliwa baadaye na waandikaji wengine wa Biblia?
38 Isaya aonyesha kwa utukufu tumaini la Ufalme kwa ajili ya wakati ujao! Hilo ni “mbingu mpya na dunia mpya,” ambamo “mfalme atatawala kwa uadilifu wenyewe” na wakuu watatawala kwa ajili ya haki. Ni kisababishi kilichoje cha furaha na shangwe! (65:17, 18; 32:1, 2, NW) Kwa mara nyingine, Petro arudia ujumbe wa furaha wa Isaya: “Lakini kuna mbingu mpya na dunia mpya ambazo sisi twangojea kulingana na ahadi [ya Mungu], na katika hizi uadilifu utakaa.” (2 Pet. 3:13, NW) Habari hii kuu iliyo nzuri sana juu ya Ufalme yaja kwenye utukufu kamili katika sura za kumalizia za Ufunuo.—Isa. 66:22, 23; 25:8; Ufu. 21:1-5.
39. Isaya chaelekeza kwenye tumaini gani zuri ajabu?
39 Kwa hiyo, kitabu cha Isaya, kijapokuwa na laana kali zenye kuchoma maadui wa Yehova na wale wenye kudai kinafiki kuwa watumishi wake, chaelekeza kwa njia tukufu kwenye tumaini zuri ajabu la Ufalme wa Kimesiya ambao kwao jina kuu la Yehova litatakaswa. Chafanya mengi katika kueleza kweli za ajabu za Ufalme wa Yehova na kuchangamsha mioyo yetu katika tarajio lenye shangwe la “wokovu wake.”—Isa. 25:9; 40:28-31.
[Maelezo ya Chini]
a Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 324.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 957; Buku 2, kurasa 894-5.
c Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 1221-3.