Kutumika Tukiwa Wavuvi wa Watu
“Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu [wakiwa hai, “NW”].”—LUKA 5:10.
1, 2. (a) Uvuvi umekuwa na sehemu gani katika historia ya ainabinadamu? (b) Ni aina gani ya uvuvi iliyoanzishwa karibu miaka 2,000 iliyopita?
KWA maelfu ya miaka, ainabinadamu imevua samaki kwa ajili ya chakula katika bahari, maziwa, na mito ya dunia. Katika Misri ya kale, samaki kutoka Naili walikuwa sehemu ya maana ya vyakula. Maji ya Naili yalipogeuzwa kuwa damu katika siku za Musa, Wamisri walitaabika si kwa sababu tu ya upungufu wa maji uliotokea bali pia kwa sababu samaki walikufa, ikaathiri ugavi wao wa chakula. Baadaye, kwenye Sinai, Yehova alipowapa Israeli Sheria, aliwaambia kwamba samaki fulani wangeweza kuliwa lakini kwamba wengine walikuwa si safi, wasiliwe. Hiyo ilionyesha kwamba Waisraeli wangekula samaki wafikapo Bara Lililoahidiwa, hivyo baadhi yao wangekuwa wavuvi.—Kutoka 7:20, 21; Mambo ya Walawi 11:9-12.
2 Lakini, karibu miaka 2,000 iliyopita, aina nyingine ya uvuvi ilianzishwa kwa ainabinadamu. Huo ulikuwa aina ya uvuvi wa kiroho ambao ungefaidi si wavuvi tu bali pia samaki! Aina hii ya uvuvi ingali inazoewa leo, ukiwa na manufaa kubwa kwa mamilioni ulimwenguni pote.
‘Kuvua Watu Wakiwa Hai’
3, 4. Ni wavuvi gani wawili walioonyesha kupendezwa sana na Yesu Kristo?
3 Katika mwaka 29 W.K., Yesu, Yule ambaye angeanzisha namna hii mpya ya uvuvi, alibatizwa katika mto Yordani na Yohana Mbatizaji. Majuma machache baadaye, Yohana aliwaelekeza wawili wa wanafunzi wake kwa Yesu na kusema: “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!” Mmoja wa wanafunzi hao, ambaye jina lake ni Andrea, upesi akamwambia ndugu yake Simoni Petro: “Tumemwona Masihi”! Kwa kupendeza, wote wawili Andrea na Simoni walikuwa wavuvi.—Yohana 1:35, 36, 40, 41; Mathayo 4:18.
4 Muda fulani baadaye, Yesu alikuwa akihubiria makutano kando ya Bahari ya Galilaya, si mbali na walikoishi Petro na Andrea. Yeye alikuwa anawaambia watu: “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mathayo 4:13, 17) Twaweza kuwazia kwamba Petro na Andrea walikuwa na hamu ya kusikia ujumbe wake. Hata hivyo, yaelekea hawakujua kwamba Yesu angesema jambo fulani kwao ambalo lingegeuza maisha zao milele. Zaidi ya hilo, yale ambayo Yesu angesema na kufanya wao wakiwapo yana maana kubwa kwetu sisi sote leo.
5. Mvuvi Petro aliwezaje kumhudumia Yesu?
5 Tunasoma: “Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao.” (Luka 5:1, 2) Huko nyuma, wale ambao kazi yao ya maisha ilikuwa kuvua mara nyingi walifanya kazi usiku, na wanaume hawa walikuwa wakiosha nyavu zao baada ya kuvua usiku. Yesu aliamua kutumia kimojawapo vyombo vyao ili kuhu-biria makutano kwa mafanikio zaidi. “Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.”—Luka 5:3.
6, 7. Ni muujiza gani unaohusu uvuvi ambao Yesu alifanya, ukiongoza kwenye maneno gani kuhusu uvuvi?
6 Angalia kwamba Yesu alikuwa akifikiria jambo zaidi ya kufundisha makutano: “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.” Kumbuka, tayari wavuvi hao walikuwa wamekuwa wakifanya kazi usiku kucha. Bila kushangaza, Petro ajibu: “Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Ni nini kilichotukia walipofanya hivyo? “Walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.”—Luka 5:4-7.
7 Yesu alikuwa amefanya muujiza. Sehemu hiyo ya bahari ilikuwa bila matokeo usiku kucha; sasa ilikuwa imejaa samaki. Muujiza huo ulikuwa na matokeo yenye nguvu kwa Petro. “Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. Maana alishikwa na mshangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni.” Yesu alimtuliza Petro halafu akasema maneno ambayo yangebadilisha maisha ya Petro. “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu [wakiwa hai, NW].”—Luka 5:8-10.
Wavuvi wa Watu
8. Wavuvi wanne ambao kazi yao ya maisha ilikuwa ni kuvua waliitikiaje mwaliko wa ‘kuvua watu wakiwa hai’?
8 Hivyo Yesu alilinganisha watu na samaki, naye akaalika mvuvi huyo mnyenyekevu aache biashara yake ya kimwili kwa ajili ya namna tukufu zaidi ya uvuvi—kuvua watu wakiwa hai. Petro, na ndugu yake Andrea, walikubali mwaliko huo. “Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.” (Mathayo 4:18-20) Halafu Yesu aliwaita Yakobo na Yohana, waliokuwa katika chombo chao, wakitengeneza nyavu zao. Aliwaalika hao pia wapate kuwa wavuvi wa watu. Waliitikiaje? “Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.” (Mathayo 4:21, 22) Yesu alionyesha ustadi akiwa mvuvi wa nafsi. Katika pindi hiyo, yeye alivua watu wanne wakiwa hai.
9, 10. Petro na wenzake walionyesha imani ya aina gani, nao walizoezwaje katika uvuvi wa kiroho?
9 Mvuvi ambaye kazi yake ni kuvua samaki hupata riziki kwa kuuza kile anachovua, lakini mvuvi wa kiroho hawezi kufanya hivyo. Kwa hiyo, wanafunzi hao walionyesha imani kubwa walipoacha yote na kumfuata Yesu. Hata hivyo, hawakuwa na shaka yoyote kwamba uvuvi wao wa kiroho ungefanikiwa. Yesu alikuwa ameweza kufanya maji yasiyotoa kitu yajawe na samaki halisi. Vivyo hivyo, waliposhusha nyavu zao ndani ya maji ya taifa la Israeli, wanafunzi wangeweza kuwa na uhakika kwamba, kwa msaada wa Mungu, wangeweza kuvua watu wakiwa hai. Kazi ya uvuvi wa kiroho iliyoanza wakati huo huendelea, na Yehova bado hutoa mavuno mengi.
10 Kwa zaidi ya miaka miwili, wanafunzi hao walizoezwa na Yesu kuvua watu. Pindi kwa pindi, yeye aliwapa maagizo ya uangalifu na kuwatuma mbele yake wakahubiri. (Mathayo 10:1-7; Luka 10:1-11) Yesu aliposalitiwa na kuuawa, wanafunzi hao waliduwaa. Lakini je! kifo cha Yesu kilimaanisha hakuna kuvua watu tena? Matukio yalitoa jibu upesi.
Kuvua Katika Bahari ya Ainabinadamu
11, 12. Baada ya ufufuo wake, Yesu alifanya muujiza gani uliohusiana na uvuvi?
11 Muda mfupi baada ya kifo cha Yesu nje ya Yerusalemu na ufufuo wake, wanafunzi walirudi Galilaya. Katika pindi moja, saba kati yao walikuwa pamoja karibu na Bahari ya Galilaya. Petro alisema anaenda kuvua samaki, na wale wengine wakajiunga naye. Kama kawaida, walivua usiku. Kwa kweli, walishusha nyavu zao ndani ya bahari usiku kucha wasivue chochote. Ndipo, kwenye mapambazuko, umbo fulani lililoonekana limesimama ufuoni likawaita wakiwa kwenye maji na kusema: “Wanangu, mna kitoweo?” Wanafunzi wakarudisha jibu: “La”! Kwa hiyo, yule aliyekuwa amesimama ufuoni akawaambia: “Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki.”—Yohana 21:5, 6.
12 Ni tukio lenye kushangaza kama nini! Inaelekea kwamba wanafunzi walikumbuka ule muujiza wa mapema kidogo kuhusiana na uvuvi, na angalau mmoja kati yao alitambua umbo hilo lililokuwa ufuoni lilikuwa nani. “Yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili.”—Yohana 21:7, 8.
13. Baada ya Yesu kupaa mbinguni, ni programu gani ya uvuvi wa kimataifa iliyoanza?
13 Muujiza huo ulionyesha nini? Kwamba kazi ya kuvua watu haikuwa imekwisha. Uhakika huo ulikaziwa wakati Yesu alipomwambia Petro mara tatu—na kupitia yeye wanafunzi wote—alishe kondoo za Yesu. (Yohana 21:15-17) Naam, programu ya kulisha kiroho ilikuwa mbele. Kabla ya kifo chake, alikuwa ametabiri hivi: “Habari njema hizi za ufalme zitahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa kwa ajili ya ushahidi kwa mataifa yote.” (Mathayo 24:14, NW) Sasa ulikuwa ndio wakati wa utimizo wa karne ya kwanza wa unabii huo kuanza. Wanafunzi wake walikuwa wanakaribia kutupa nyavu zao ndani ya bahari ya ainabinadamu, na nyavu hizo hazingetoka zikiwa tupu.—Mathayo 28:19, 20.
14. Uvuvi wa wafuasi wa Yesu ulibarikiwaje katika miaka ya kabla ya uharibifu wa Yerusalemu?
14 Kabla ya kupaa kwake hadi kiti cha Babaye mbinguni, Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu [roho takatifu, NW]; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” (Matendo 1:8) Wakati roho takatifu ilipomiminwa juu ya wanafunzi wakati wa Pentekoste 33 W.K., ile kazi kubwa ya kimataifa ya kuvua kiroho ikaanza. Katika siku ya Pentekoste peke yake, nafsi elfu tatu zilivuliwa zikiwa hai, na upesi baada ya hapo, “hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano.” (Matendo 2:41; 4:4) Ongezeko hilo likaendelea. Maandishi hutuambia: “Walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake.” (Matendo 5:14) Upesi, Wasamaria wakaitikia habari njema, na muda mfupi baada ya hapo wakafuata wasio Wayahudi wasiotahiriwa. (Matendo 8:4-8; 10:24, 44-48) Miaka 27 hivi baada ya Pentekoste, mtume Paulo aliandikia Wakristo Wakolosai kwamba habari njema zilikuwa ‘zimehubiriwa katika uumbaji wote ulio chini ya mbingu.’ (Wakolosai 1:23, NW). Kwa wazi, wanafunzi wa Yesu walikuwa wamevua katika sehemu ya mbali kutoka kwa maji ya Galilaya. Walikuwa wametupa nyavu zao miongoni mwa Wayahudi waliosambaa katika Milki ya Roma, kutia na kwenye bahari zilizoonekana kana kwamba hazingetoa kitu za watu wasio Wayahudi. Na nyavu zao zikatoka zikiwa zimejaa. Kwa mahitaji ya Wakristo wa karne ya kwanza, unabii wa Yesu kwenye Mathayo 24:14 ulitimizwa kabla ya Yerusalemu kuharibiwa katika 70 W.K.
Kuvua Watu Katika “Siku ya Bwana”
15. Katika kitabu cha Ufunuo, ni kazi gani zaidi ya uvuvi iliyotolewa unabii, nayo ingetekelezwa lini?
15 Lakini, mambo zaidi yalikuwa mbele. Karibu na mwisho wa karne ya kwanza, Yehova alimjalia mtume wa mwisho aliyekuwa akiishi, Yohana, apate ufunuo wa mambo yaliyopasa kutukia wakati wa “siku ya Bwana.” (Ufunuo 1:1, 10) Sehemu moja yenye kutokeza ilipasa iwe kuhubiriwa kwa habari njema ulimwenguni pote. Twasoma hivi: “Nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa.” (Ufunuo 14:6) Chini ya mwelekezo wa kimalaika, watumishi wa Mungu wangehubiri habari njema kihalisi katika dunia yote inayokaliwa, si kotekote tu katika Milki ya Roma. Kazi ya ulimwenguni pote ya kuvua nafsi ilipaswa ianze, na katika siku yetu tumeona utimizo wa njozi hiyo.
16, 17. Kazi ya uvuvi ya siku za baadaye ilianza lini, na Yehova ameibarikije?
16 Uvuvi umekuwaje wakati wa karne hii ya 20? Mwanzoni, wavuvi walikuwa wachache. Baada ya Vita ya Ulimwengu 1 kumalizika, walikuwako wapata wahubiri watendaji wa habari njema elfu nne, wanaume na wanawake wenye bidii ambao kwa sehemu kubwa walikuwa wa wale wapakwa-mafuta. Walitupa nyavu zao popote Yehova alipofungua njia, na nafsi nyingi zilivuliwa zikiwa hai. Kufuatia vita ya ulimwengu ya pili, Yehova alifungua maji mapya ya kuvulia. Wamishonari waliokuwa wamehudhuria Watchtower Bible School of Gilead waliongoza kazi katika mabara mengi. Nchi kama vile Japani, Italia, na Hispania, ambazo huenda mwanzoni zilionekana kuwa tupu, hatimaye zilitoa mavuno mengi ya nafsi. Hivi karibuni tumejulishwa pia kuhusu jinsi kazi ya uvuvi imefanikiwa katika Ulaya ya Mashariki.
17 Leo, katika nchi nyingi nyavu zakaribia kukatika. Mavuno makubwa ya nafsi yamefanya iwe lazima kupanga makundi na mizunguko mipya. Ili kuweza kutumikia hayo, Majumba ya Ufalme mapya na Majumba ya Kusanyiko yanajengwa wakati wote. Wazee na watumishi wa huduma zaidi wanahitajiwa kutunza ongezeko hilo. Kazi kubwa ilianzishwa na wale waaminifu huko nyuma katika 1919. Kwa njia halisi, Isaya 60:22 limetimizwa. ‘Mdogo amekuwa elfu,’ kwa kuwa wale wavuvi elfu nne wamepata kuwa zaidi ya milioni nne leo. Na mwisho bado.
18. Sisi tunaweza kuigaje mfano bora wa wale wavuvi wa kiroho wa karne ya kwanza?
18 Yote hayo yamaanisha nini kwa watu mmoja mmoja? Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana walipoalikwa wawe wavuvi wa watu, andiko husema, ‘Waliacha vyote wakamfuata.’ (Luka 5:11) Ni kielelezo chema kama nini cha imani na ujitoaji! Je! sisi twaweza kusitawisha roho iyo hiyo ya kujidhabihu, utayari uo huo wa kutumikia Yehova hata gharama iweje? Mamilioni wamejibu kwamba waweza. Katika karne ya kwanza, wanafunzi walivua watu popote Yehova aliporuhusu. Iwe ni miongoni mwa Wayahudi au wasio Wayahudi, walivua bila kusita. Acheni sisi tuhubirie kila mmoja bila kujizuia au kubagua.
19. Tunapaswa tufanye nini ikiwa maji tunayovulia hayaonekani kuwa na mazao?
19 Ingawa hivyo, namna gani kama eneo lenu kwa sasa laonekana kutokuwa na mazao? Usivunjike moyo. Kumbuka, Yesu alijaza nyavu za wanafunzi baada ya wao kuwa wamevua usiku kucha bila matokeo. Yaweza kuwa vivyo hivyo kwa njia ya kiroho. Kwa mfano, katika Ailandi, Mashahidi waaminifu walifanya kazi ngumu kwa miaka mingi kukiwa na matokeo kidogo sana. Hata hivyo, hivi karibuni hiyo imebadilika. Kitabu-mwaka cha Mashahidi wa Yehova cha 1991 charipoti kwamba kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1990, Ailandi ilikuwa imefurahia vilele 29 mfululizo! Labda eneo lenu litazaa siku moja jinsi iyo hiyo. Maadamu Yehova aruhusu, endelea kuvua!
20. Tunapaswa kuwavua watu wakati gani?
20 Katika Israeli, wavuvi walienda kuvua usiku, wakati kila mtu mwingineye yote alikuwa akipata joto na kustarehe kitandani. Walitoka nje, si wakati ilipowafaa, bali wakati ule wangeweza kuvua samaki wengi zaidi. Sisi pia twapaswa kuchunguza eneo letu ili twende kuvua, wakati ambao, kwa kweli, watu walio wengi wamo nyumbani na wangeitikia. Huenda hiyo ikawa wakati wa jioni, wakati wa mwisho wa juma, au wakati mwingineo. Hata iwe wakati gani, acheni sisi tufanye yote tuwezayo kuwapata watu wenye mioyo inayofaa.
21. Tunapaswa tukumbuke nini ikiwa eneo letu linafanyiwa kazi mara nyingi?
21 Namna gani ikiwa eneo letu linafanyiwa kazi mara nyingi? Katika ulimwengu wavuvi ambao uvuvi ndiyo kazi yao ya maisha mara nyingi hulalamika kwamba maeneo yao ya kuvua yamevuliwa mno. Je! maeneo yetu ya kuvua yaweza kuwa yamevuliwa mno? Sivyo hata kidogo! Maeneo mengi huzaa ongezeko hata wakati yameenezwa mara nyingi. Baadhi yayo huzaa vizuri zaidi kwa sababu ya kuwa yamefanyiwa kazi sana. Hata hivyo, wakati makao yanapotembelewa mara nyingi, hakikisha zaidi kwamba wote wasiokuwa nyumbani wanaandikwa na kutembelewa baadaye. Jifunze vichwa vya mazungumzo tofauti-tofauti. Kumbuka kwamba mtu mwingine atatembea tena karibuni, kwa hiyo usikae sana unapokaribishwa au ukasirishe wenye nyumba bila kujua. Na usitawishe stadi zako katika kazi ya barabarani na ya ushuhuda wa vivi hivi. Shusha nyavu zako za kiroho katika kila pindi na kwa njia yoyote iwezekanayo.
22. Ni pendeleo gani kuu tunalofurahia wakati huu?
22 Kumbuka, katika uvuvi huu wote wawili wavuvi na samaki hunufaika. Ikiwa wale tunaovua wanastahimili, wanaweza kuishi milele. Paulo alimtia moyo Timotheo hivi: “Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.” (1 Timotheo 4:16) Alikuwa ni Yesu ambaye mwanzoni alizoeza wanafunzi wake katika uvuvi wa kiroho, na kazi hiyo bado inafanywa chini ya mwelekezo wake. (Linganisha Ufunuo 14:14-16.) Jinsi tulivyo na pendeleo kuu kufanya kazi chini yake ili kuikamilisha kazi hiyo! Acheni tuendelee kushusha nyavu zetu maadamu Yehova anaruhusu. Ni kazi gani ingeweza kuwa kuu zaidi ya ile ya kuvua nafsi zikiwa hai?
Je! Wakumbaka?
◻ Yesu aliwazoeza wafuasi wake kufanya kazi gani?
◻ Yesu alionyeshaje kwamba kazi ya uvuvi wa kiroho haikukomeshwa na kifo chake?
◻ Yehova alibarikije kazi ya uvuvi wa kiroho katika karne ya kwanza?
◻ Ni mavuno gani makubwa ya samaki ambayo yamevuliwa wakati wa “siku ya Bwana”?
◻ Sisi tukiwa watu mmoja mmoja tunaweza kuwaje wenye mafanikio hata zaidi tukiwa wavuvi wa watu?
[Picha katika ukurasa wa 15]
Baada ya Yesu kufufuliwa, mitume wake walieneza kazi ya kimungu ya kuvua watu