Maisha na Huduma ya Yesu
Ni Jambo Gani Lililo Halali Siku ya Sabato?
NI KATIKA Sabato nyingine Yesu anapotembelea sinagogi karibu na Bahari ya Galilaya. Aliyepo ni mwanamume mwenye mkono wa kuume uliopooza. Waandishi na Mafarisayo wanatazama kwa ukaribu waone kama Yesu atamponya. Mwishowe wanauliza: “Ni halali kuponya watu siku ya sabato? ”
Viongozi wa kidini Wayahudi wanaamini kwamba kuponya ni halali siku ya Sabato ikiwa tu uhai umo hatarini. Kwa mfano, wao wanafundisha kwamba siku ya Sabato si halali kuunganisha mfupa uliovunjika au kufunga mahali palipoteguka. Kwa hiyo waandishi na Mafarisayo wanamwuliza Yesu maulizo kwa jitihada ya kupata jambo la kumshtaki.
Lakini, Yesu anajua mawazo yao. Wakati ule ule, yeye anatambua kwamba wao wamechagua kufuata maoni ya kupita kiasi yasiyo ya kimaandiko juu ya mambo yaliyo uvunjaji wa takwa la siku ya Sabato linalokataza kazi. Hivyo Yesu anaandaa mambo ili kuwa na mkabiliano wa kutazamisha kwa kumwambia mwanamume yule mwenye mkono uliopooza: “Ondoka, simama katikati.”
Sasa, akiwageukia waandishi na Mafarisayo, Yesu anasema: “Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? ” Kwa kuwa kondoo anafananisha akiba ya pesa, wao hawangemwacha shimoni mpaka kesho yake, labda awe mgonjwa na kupoteza thamani yake. Zaidi ya hilo, Maandiko yanasema: “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake.”
Akitoa ulinganisho, Yesu anaendelea kusema; “Je! mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya Sabato.” Kwa kushindwa kukanusha hoja yenye akili na huruma ya kutoa sababu, viongozi wa kidini wananyamaza.
Kwa kukasirishwa na hali yao, na pia, kuhuzunika sana kwa sababu ya upumbavu wao wa moyo mgumu, Yesu anatazama uku na huku. Halafu anamwambia mwanamume yule: “Nyosha mkono wako.” Naye anaunyosha na mkono unaponywa.
Badala ya kufurahi kwamba mkono wa mwanamume huyo umerudishwa, Mafarisayo wanaenda nje na mara hiyo wanatunga hila pamoja na wafuasi wa chama cha Herodi ili kumwua Yesu. Chama hicho cha kisiasa kwa wazi ni kutia ndani na washiriki wa Masadukayo wa kidini. Kwa kawaida chama hicho cha kisiasa kinapingana na Mafarisayo waziwazi, lakini sehemu zote mbili zimeungana kwa uthabiti katika kumpinga Yesu. Mathayo 12:9-14; Marko 3:1-6; Luka 6:6-11; Mithali 12:10; Kutoka 20:8-10.
◆ Ni hali gani iliyokuwako hata kukatokea mkabiliano wa kutazamisha kati ya Yesu na viongozi wa kidini Wayahudi?
◆ Wayahudi waliamini nini juu ya kuponya siku ya Sabato?
◆ Yesu alitumia mfano gani kukanusha maoni yao yenye makosa?