Iweni Watendaji wa Neno, Si Wasikiaji Tu
“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”—MATHAYO 7:21.
1. Wafuasi wa Yesu wapaswa kuendelea kufanya nini?
ENDELEENI kuomba. Endeleeni kutafuta. Endeleeni kubisha hodi. Dumuni katika kusali, kujifunza, na kufanya semi za Yesu zilizorekodiwa katika yale Mahubiri juu ya Mlima. Yesu aambia wafuasi wake wao ndio chumvi ya dunia, wakiwa na ujumbe wenye kuhifadhi uliokolezwa chumvi ambao ni lazima wasiuruhusu uwe chapwa, upoteze ladha yao au nguvu yao ya kuhifadhi. Wao ndio nuru ya ulimwengu, wakifanya mrudisho wa nuru itokayo kwa Kristo Yesu na Yehova Mungu si kwa yale wasemayo tu bali pia kwa yale wafanyayo. Kazi zao njema zaangaza sana kama maneno yao yenye kunurisha—na huenda hata yakasema kwa sauti kubwa zaidi katika ulimwengu uliozoea unafiki wa Kifarisayo wa viongozi wa kidini na wa kisiasa pia, ambao husema mengi na kufanya machache.—Mathayo 5:13-16.
2. Yakobo atoa onyo gani, lakini ni msimamo gani wa kujistarehesha ambao watu fulani huchukua kimakosa?
2 Yakobo aonya kwa upole hivi: “Iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.” (Yakobo 1:22) Wengi hujidanganya kwa fundisho la kwamba ‘ukiisha kuokolewa umeokolewa sikuzote,’ kana kwamba sasa wao waweza kustaafu na kungojea thawabu fulani isemwayo kuwa ya kimbingu. Hilo ni fundisho bandia na tumaini tupu. “Mwenye kuvumilia hata mwisho,” akasema Yesu, “ndiye atakayeokoka.” (Mathayo 24:13) Ili upate uhai wa milele, ni lazima “uwe mwaminifu hata kufa.”—Ufunuo 2:10; Waebrania 6:4-6; 10:26, 27.
3. Ni agizo gani juu ya kuhukumu ambalo Yesu atoa halafu katika yale Mahubiri juu ya Mlima?
3 Kadiri Yesu alivyoendelea na Mahubiri yake juu ya Mlima, semi zaidi ziliongezeka ambazo ni lazima Wakristo wajitahidi kufuata. Hapa pana mmoja uonekanao kuwa sahili, lakini washutumu moja la maelekeo yaliyo magumu kabisa kuondolea mbali: “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”—Mathayo 7:1-5.
4. Ni agizo gani zaidi ambalo usimulizi wa Luka watoa, na utumizi walo hutokeza nini?
4 Katika usimulizi wa Luka wa yale Mahubiri juu ya Mlima, Yesu aliambia wasikiaji wake wasitafute makosa kwa wengine. Bali, waendelee ‘kuachilia,’ yaani, kusamehe mapungukio ya binadamu mwenzao. Hiyo ingesababisha wengine waitikie hivyo hivyo, kama alivyosema Yesu: “Wapeni watu vitu [zoeeni kutoa, NW], nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”—Luka 6:37, 38.
5. Kwa nini ni rahisi zaidi kuona dosari katika wengine kuliko zile zilizo katika sisi wenyewe?
5 Wakati wa karne ya kwanza W.K., kwa sababu ya mapokeo ya mdomo, Mafarisayo kwa ujumla walielekea kuhukumu wengine vikali. Wowote wa wasikilizaji wa Yesu waliokuwa katika zoea la kufanya hivyo walipaswa kulikomesha. Ni rahisi zaidi kuona kibanzi katika macho ya wengine kuliko maboriti yaliyo katika macho yetu wenyewe—tena kufanya hivyo kwatuongezea uhakika ili tujione! Kama alivyosema mwanamume mmoja, “Mimi napenda kuchambua wengine kwa sababu hiyo hunifanya nihisi vizuri sana!” Tabia ya kuchambua-chambua wengine huenda ikatupa sisi hisia za wema zionekanazo ni kama zasawazisha makosa yetu wenyewe tutakayo kuyaficha. Lakini ikiwa sahihisho ni la lazima, lapasa kutolewa kwa roho ya upole. Mwenye kutoa sahihisho apaswa kukumbuka wakati wote mapungukio yake mwenyewe.—Wagalatia 6:1.
Kabla ya Kuhukumu, Jaribu Kuelewa
6. Iwapo lazima, hukumu zetu zapasa kuwa juu ya msingi gani, na twapaswa kutafuta msaada gani ili tusiwe wachambuzi kupita kiasi?
6 Yesu hakuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. Hukumu zozote alizofanya hazikuwa zake bali msingi wazo ulikuwa maneno ambayo Mungu alimpa ayaseme. (Yohana 12:47-50) Hukumu zozote tufanyazo zapaswa pia kupatana na Neno la Yehova. Ni lazima tulikanyage-kanyage lile elekeo la kibinadamu la kuhukumu-hukumu. Katika kufanya hilo, twapaswa kusali kwa udumifu ili tupate msaada wa Yehova: “Endeleeni kuomba, nanyi mtapewa; endeleeni kutafuta, nanyi mtapata; endeleeni kubisha, nanyi mtafunguliwa. Kwa maana kila mmoja anayeomba hupokea, na kila mmoja anayetafuta hupata, na kila mmoja anayebisha atafunguliwa.” (Mathayo 7:7, 8, NW) Hata Yesu alisema: “Siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki [uadilifu, NW], kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.”—Yohana 5:30.
7. Ni tabia gani tupaswayo kusitawisha itakayotusaidia kutumia ile Kanuni ya Kidhahabu?
7 Twapaswa kusitawisha tabia, si ya kuhukumu watu, bali ya kujaribu kuwaelewa kwa kujitia katika hali yao—si jambo rahisi kufanya lakini ni la lazima ikiwa tutakaa kulingana na ile Kanuni ya Kidhahabu, ambayo Yesu aliipigia mbiu halafu: “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.” (Mathayo 7:12) Kwa hiyo ni lazima wafuasi wa Yesu wawe na hisia za kuelewa haraka na kufahamu hali ya wengine ya kiakili, ya kihisia-moyo, na ya kiroho. Ni lazima wawe wafahamivu na kuelewa mahitaji ya wengine na kuchukua upendezi wa kibinafsi katika kuwasaidia. (Wafilipi 2:2-4) Miaka kadhaa baadaye Paulo aliandika hivi: “Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.”—Wagalatia 5:14.
8. Yesu alizungumzia barabara gani mbili, na kwa nini moja yazo huchaguliwa na watu walio wengi?
8 “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba,” akasema Yesu halafu, “maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:13, 14) Wengi katika siku hizo waliichagua barabara iendayo kwenye uharibifu na wengi wangali wakifanya hivyo. Ile njia pana huruhusu watu wafikiri kama watakavyo na waishi kama iwapendezavyo: bila amri, bila wajibu, ila mtindo-maisha wa kilegevu tu, kila kitu ni mswaki. Kwao hakuna jambo hili la “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba”!—Luka 13:24.
9. Ni nini ambacho chahitajiwa ili kutembea katika ile barabara nyembamba, na Yesu awapa onyo gani wale wanaoitembea?
9 Lakini mlango mwembamba ndio hufunguka kwenye ile barabara ya uhai wa milele. Ni mwendo utakao kujidhibiti. Huenda ukahusisha nidhamu itakayopekua matilaba (madhumuni) zako na kutahini umadhubuti wa wakfu wako. Minyanyaso ijapo, barabara huparuzika ikataka uvumilivu. Yesu awaonya wale watembeao katika barabara hii: “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.” (Mathayo 7:15) Elezo hilo lililingana na Mafarisayo kikamilifu. (Mathayo 23:27, 28) Wao ‘walijiketisha juu ya kiti cha Musa,’ wakidai kumsemea Mungu hali wakifuata mapokeo ya wanadamu.—Mathayo 23:2, NW.
Jinsi Mafarisayo
‘Walivyoufunga Ufalme’
10. Ni kwa njia gani hususa waandishi na Mafarisayo walitafuta ‘kuwafungia watu ufalme’?
10 Zaidi ya hilo, makasisi Wayahudi walitafuta kuwawekea pingamizi wale wenye kutafuta kuingia kupitia lile lango jembamba. “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.” (Mathayo 23:13) Mbinu ya Mafarisayo ilikuwa kama vile Yesu alivyoonya. Walikuwa ‘wakitupa nje jina la wanafunzi wake kuwa ovu kwa ajili ya Mwana wa binadamu.’ (Luka 6:22, NW) Kwa sababu yule mwanamume aliyezaliwa akiwa kipofu na kuponywa na Kristo aliamini kwamba Yesu ndiye Mesiya, wao walimwondosha katika sinagogi. Wazazi wake hawakutaka kujibu maswali yoyote kwa sababu walihofu kuondoshwa katika sinagogi. Kwa sababu iyo hiyo, wengine waliomwamini Yesu kuwa ndiye Mesiya walisita kukiri hivyo peupe.—Yohana 9:22, 34; 12:42; 16:2.
11. Makasisi wa Jumuiya ya Wakristo huzaa matunda gani ya utambulishi?
11 “Mtawatambua kwa matunda yao,” Yesu akasema. “Kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.” (Mathayo 7:16-20) Kanuni ile ile yatumika leo. Wengi wa makasisi wa Jumuiya ya Wakristo husema jambo moja na kufanya jingine. Ingawa wanadai kufundisha Biblia, wao hukubali makufuru kama Utatu na helo yenye moto. Wengine hukana ukombozi, hufundisha mageuzi badala ya uumbaji, na huhubiri saikolojia ipendwayo na wengi ili ku-tekenya masikio. Kama Mafarisayo, wengi wa makasisi wa leo ni wapenda pesa, wakiyanyoa makundi yao ya kondoo mamilioni ya dola. (Luka 16:14) Wote hupaaza sauti, “Bwana, Bwana,” lakini jibu la Yesu kwao ni hili: “Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”—Mathayo 7:21-23.
12. Kwa nini watu fulani ambao wakati mmoja walitembea katika ile njia nyembamba walikoma kufanya hivyo, na tokeo likiwa nini?
12 Leo, watu fulani ambao wakati mmoja walitembea katika ile njia nyembamba wamekoma kufanya hivyo. Wao wasema wampenda Yehova, lakini hawatii amri yake kuhubiri. Wao wasema wampenda Yesu, lakini hawalishi kondoo zake. (Mathayo 24:14; 28:19, 20; Yohana 21:15-17; 1 Yohana 5:3) Hawataki kufungwa nira pamoja na wale watembeao katika hatua za Yesu. Waliiona ile barabara yenye kufinyika kuwa imefinyika mno. Walichoka kufanya mazuri, hivyo basi “walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi.” (1 Yohana 2:19) Walirudi gizani, nalo “si giza hilo!” (Mathayo 6:23) Walipuuza usihi wa Yohana: “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli.”—1 Yohana 3:18.
13, 14. Yesu alitoa kielezi gani juu ya kutumia semi zake katika maisha zetu, na kwa nini kiliwafaa sana wale waliokuwa katika Palestina?
13 Yesu alimalizia Mahubiri yake juu ya Mlima kwa kielezi cha kutazamisha: “Kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.”—Mathayo 7:24, 25.
14 Katika Palestina mvua zilizo nzito zingeweza kutiririsha maji mbio-mbio kwenye mabonde makavu ya mabubujiko na kuyafanya mafuriko maharibifu ya ghafula. Ikiwa nyumba zingebaki zimesimama, zilihitaji kuwa na misingi juu ya mwamba thabiti. Usimulizi wa Luka waonyesha kwamba yule mtu ‘alichimba sana, na kuweka msingi juu ya mwamba.” (Luka 6:48) Ilikuwa kazi ngumu, lakini ikawa na malipo dhoruba ilipokuja. Hivyo basi kujenga sifa za Kikristo juu ya semi za Yesu kutathawabisha wakati furiko la ghafula la taabu kubwa likumbapo.
15. Tokeo litakuwa nini kwa wale wafuatao mapokeo ya wanadamu badala ya kutii semi za Yesu?
15 Nyumba ile nyingine ilijengwa juu ya mchanga: “Kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.” Ndivyo itakavyokuwa kwa wale wasemao “Bwana, Bwana” lakini hawafanyi kulingana na semi za Yesu.—Mathayo 7:26, 27.
“Si kama Waandishi Wao”
16. Tokeo lilikuwa nini juu ya wale walioyasikia Mahubiri juu ya Mlima?
16 Tokeo la yale Mahubiri juu ya Mlima lilikuwa nini? “Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.” (Mathayo 7:28, 29) Walichochewa kwenye vina vyao na mmoja aliyesema kwa mamlaka wasiyopata kuihisi kabla ya hapo.
17. Waandishi walilazimika kufanya nini ili watie uhalali katika fundisho lao, nao walidai nini juu ya wahenga wafu walionukuliwa?
17 Hakuna mwandishi yeyote aliyepata kusema kwa mamlaka yake mwenyewe, kama vile rekodi hii ya kihistoria ionyeshavyo: “Waandishi waliazima ustahili wa fundisho lao kutokana na mapokeo, na mababa wa mapokeo hayo: na hakuna mahubiri ya mwandishi yeyote yaliyokuwa na mamlaka au thamani yoyote, bila [kudondoa] . . . Marabini wana pokeo moja, au . . . Watu wenye hekima husema; au mhenga fulani wa kimapokeo wa jinsi hiyo. Hillel Mkubwa alifundisha kikweli, na kama vile pokeo lilivyohusu jambo fulani; ‘Lakini, ingawa alihutubu juu ya jambo hilo mchana kutwa, . . . wao hawakupokea fundisho lake, mpaka hatimaye aliposema, Hivyo ndivyo mimi nilivyosikia kutoka kwa Shemaia na Abtalioni [wenye mamlaka waliomtangulia Hillel].’” (A Commentary on the New Testament From the Talmud and Hebraica, cha John Lightfoot) Mafarisayo hata walidai hivi juu ya wahenga wenye hekima waliokufa zamani: “Midomo ya waadilifu, wakati mtu fulani adondoapo fundisho la sheria kwa kutumia majina yao—midomo yao hunong’ona pamoja nao kaburini.”—Torah—From Scroll to Symbol in Formative Judaism.
18. (a) Kulikuwa na tofauti gani kati ya fundisho la waandishi na lile la Yesu? (b) Fundisho la Yesu lilikuwa la kutokeza sana katika njia zipi?
18 Waandishi walinukuu watu wafu kuwa mamlaka zao; Yesu alisema kwa mamlaka kutokana na Mungu aliye hai. (Yohana 12:49, 50; 14:10) Marabi walichota maji yaliyochacha kutoka kwenye hodhi zilizofungiwa; Yesu alitokeza chemchemi za maji baridi kwa upya yaliyozima kiu ya ndani. Yeye alisali na kufikiri usiku wote, na aliposema, aligusa watu kwa vina wasivyopata kujua kabla ya hapo. Alisema kwa nguvu ambayo wangeweza kuhisi, mamlaka ambayo hata waandishi, Mafarisayo, na Masadukayo hatimaye walihofu kushindana nayo. (Mathayo 22:46; Marko 12:34; Luka 20:40) Alikuwa hajapata kamwe binadamu mwingine kusema kama hivi! Kwenye umalizio wa mahubiri, umati wa watu uliachwa umeduwaa!
19. Njia fulani za kufundisha zitumiwazo na Mashahidi wa Yehova leo zafananaje na zile zilizotumiwa na Yesu katika Mahubiri juu ya Mlima?
19 Namna gani leo? Wakiwa ni wahudumu wa nyumba kwa nyumba, Mashahidi wa Yehova hutumia njia kama hizo. Mwenye nyumba akuambia hivi: “Kanisa langu husema dunia itateketezwa.” Wewe wajibu hivi: “Biblia yako mwenyewe husomeka hivi kwenye Mhubiri 1:4: ‘Dunia hudumu daima.’ Yule mtu ashangaa. “Ala, mimi hata sikujua hilo limo katika Biblia yangu!” Mwingine asema hivi: “Sikuzote mimi nimesikia kwamba watenda dhambi watachomwa katika moto wa helo.” “Lakini Biblia yako mwenyewe yasema hivi kwenye Warumi 6:23: ‘Mshahara wa dhambi ni mauti.’” Au kuhusu Utatu: “Mhubiri wangu husema kwamba Yesu na Baba yake wako sawa.” “Lakini kwenye Yohana 14:28 Biblia yako humnukuu Yesu akisema hivi: ‘Baba ni mkuu kuliko mimi.’” Mtu mwingine asema kwako hivi: “Mimi nimesikia ikisemwa kwamba Ufalme wa Mungu umo ndani yako.” Jibu lako: “Kwenye Danieli 2:44 Biblia yako husema hivi: ‘Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa . . . ; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele.’ Huo ungewezaje kuwa ndani yako?”
20. (a) Kuna utofautiano gani kati ya njia ya kufundisha ya Mashahidi na ile ya makasisi wa Jumuiya ya Wakristo? (b) Sasa ni wakati wa nini?
20 Yesu alisema kwa mamlaka kutoka kwa Mungu. Mashahidi wa Yehova husema kwa mamlaka ya Neno la Mungu. Makasisi wa Jumuiya ya Wakristo huongea mapokeo ya kidini ambayo yamechafuzwa na mafundisho yaliyopokezwa kutoka Babuloni na Misri. Watu wenye moyo mweupe wasikiapo imani zao zikikanushwa na Biblia, wao huduwaa na kupaaza sauti hivi: ‘Sikujua kamwe hilo limo katika Biblia yangu!’ Lakini limo. Sasa ndio wakati wa wote wajuao uhitaji wao wa kiroho kutii semi za Yesu katika yale Mahubiri juu ya Mlima na hivyo wajenge juu ya msingi wa mwamba uwezao kudumu.
Maswali ya Kupitia
◻ Badala ya kukata hukumu, twapaswa kujaribu kufanya nini, na kwa nini?
◻ Wengi sana leo huichaguaje ile njia pana?
◻ Kwa nini njia ya Yesu ya kufundisha ilitofautiana sana na ile ya waandishi?
◻ Tokeo la Mahubiri juu ya Mlima lilikuwa nini juu ya wasikiaji?