Maisha na Huduma ya Yesu
Somo la Rehema
YESU huenda bado akawa katika Naini, ambako hivi majuzi alifufua mwana wa mjane, au labda yeye anatembelea mji fulani wa karibu. Farisayo mmoja jina lake Simoni anatamani amtazame kwa ukaribu mtu huyo anayefanya maajabu kama hayo. Kwa hiyo yeye anaalika Yesu akale chakula pamoja naye.
Akiiona pindi hiyo kuwa nafasi ya kuhudumia watu waliopo, Yesu anakubali mwaliko huo, kama vile yeye amekwisha kukubali mialiko kula pamoja na wakusanyaji kodi na watenda dhambi. Hata hivyo, anapoingia nyumba ya Simoni, Yesu hapokewi kwa uchangamfu kama ilivyo kawaida kuwapokea wageni.
Nyayo zilizovishwa sapatu zinapata joto na mavumbi kwa sababu ya kusafiri katika barabara zenye mavumbi za Galilaya, na ni kitendo kilicho desturi ya ukaribishaji kuosha nyayo za wageni kwa maji baridi. Lakini nyayo za Yesu hazioshwi anapofika. Wala yeye hapokei busu la kumkaribisha, ambalo ni kawaida ya mapokezi. Naye hapewi yale mafuta ya ukaribishaji yaliyo desturi kumpa mgeni kwa ajili ya nywele zake.
Wakati mlo unapoendelea, wageni wakiwa wangali wanaegemea meza, mwanamke mmoja asiyealikwa anaingia chumbani humo. Yeye anajulikana katika mji huo kuwa anaishi maisha ya ukosefu wa adili. Inaelekea yeye amesikia mafundisho ya Yesu, kutia na mwaliko wake wa kwamba ‘wote wale waliolemewa na mizigo waje kwake wapate burudisho.’ Na kwa kuvutwa sana moyoni na mambo ambayo ameona na kusikia, sasa mwanamke huyo amemtafuta Yesu.
Mwanamke huyo anakuja nyuma ya Yesu mezani na kupiga magoti kwenye nyayo zake. Huku machozi yake yakiangukia nyayo za Yesu, mwanamke huyo anayapangusa kwa nywele zake. Pia anachukua mafuta yenye manukato kutoka chupa yake. na anapobusu kwa wororo nyayo za Yesu, yeye anazimiminia mafuta yale. Simoni anatazama kwa kutokukubali jambo hilo. “Mtu huyu kama angekuwa nabii,” yeye anawaza, “angemtambua mwanamke huyo amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.”
Akifahamu kufikiri kwa Simoni, Yesu anasema: “Simoni, nina neno nitakalo kukuambia.”
“Mwalimu, nena,” yeye anajibu
“Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili,” Yesu anaanza. “Mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kulipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi?”
“Nadhani,” Simoni anasema, labda akiwa na maringo kidogo ya kutokujali ulizo lile kwa kuwa linaonekana ni kama halifai kisa kilichopo, “m yule ambaye alimsamehe nyingi.”
“Umeamua haki,” Yesu anajibu. Na ndipo akigeukia mwanamke yule, yeye anamwambia Simoni hivi: “Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyo amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyo tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyo amenipaka miguu yangu marhamu.”
Hivyo mwanamke huyo ametoa wonyesho wazi wa toba ya kutoka moyoni kwa ajili ya matendo yake ya kukosa adili wakati uliopita. Kwa hiyo Yesu anamalizia hivi: “Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.”
Yesu hatolei udhuru au haachilii tu kwa vyo vyote ukosefu wa adili. Bali, kisa hicho kinafunua ufahamu wake wenye huruma juu ya watu ambao wanafanya makosa maishani lakini ambao ndipo wanadhihirisha kwamba wanasikitikia makosa hayo na kwa hiyo wanamjia Kristo wapate kitulizo. Akimwandalia mwanamke huyo burudisho la kweli, Yesu anasema: “Umesamehewa dhambi zako. . . . Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.” Luka 7:36-50; Mathayo 11:28-30.
◆ Yesu anapokewaje na Simoni mkaribishaji wake?
◆ Ni nani anayetafuta Yesu, na kwa sababu gani?
◆ Yesu anaandaa mfano gani, naye anautumiaje?