Maisha Katika Nyakati za Biblia—Mkulima
“[Yesu] akawaambia wanafunzi wake: ‘Ndiyo, mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Kwa hiyo, mwombeni Bwana wa mavuno awatume wafanyakazi katika mavuno yake.’”—MATHAYO 9:37, 38.
MARA nyingi Yesu alitumia mifano iliyohusu mbinu za kilimo na vifaa vya kilimo ili kufundisha mambo muhimu. (Mathayo 11:28-30; Marko 4:3-9; Luka 13:6-9) Kwa nini? Kwa sababu aliishi miongoni wa wakulima. Wengi waliomsikiliza walitumia njia za kilimo ambazo hazikuwa zimebadilika kwa karne nyingi. Walimwelewa alipozungumzia shughuli zao za kila siku. Yesu alifahamu njia yao ya maisha, nao walichochewa na mambo aliyofundisha.—Mathayo 7:28.
Tunaweza kuthamini hata zaidi mifano ambayo Yesu alitumia na pia masimulizi mengine ya Biblia ikiwa tutajua mambo fulani kumhusu mkulima aliyeishi katika karne ya kwanza, yaani, mimea aliyopanda, vifaa alivyotumia, na matatizo aliyokabili.
Wazia mkulima akifanya kazi mbalimbali. Soma maandiko yaliyoonyeshwa, na utafakari mambo utakayojifunza.
Wakati wa Kupanda
Huku akiyakinga macho yake kutokana na miale ya jua la asubuhi, mkulima anasimama mlangoni na kuvuta hewa yenye unyevunyevu. Mvua imelowesha udongo uliokuwa umekauka kwa sababu ya jua. Wakati wa kulima umefika. Anabeba mabegani jembe jepesi la kukokotwa lililotengenezwa kwa mbao na kuelekea kwenye shamba lake.
Mkulima anakusanya ng’ombe wake na kuwafunga nira pamoja, kisha anawachoma-choma kwa michokoo ili waanze kazi. Ncha ya jembe hilo iliyotengenezwa kwa chuma inachimba udongo wenye mawe-mawe. Jembe hilo halipindui udongo bali linapasua udongo na kuchimba mtaro usio na kina kirefu (1). Akiyumbayumba kushoto na kulia, mkulima anajitahidi kuhakikisha kwamba mtaro huo umenyooka. Haangalii nyuma kamwe, la sivyo jembe litaenda kombo. (Luka 9:62) Hapaswi kulima nje ya mpaka wa shamba lake na anahitaji kulitumia vizuri shamba hilo dogo.
Sasa kwa kuwa shamba lina mitaro, liko tayari kupandwa mbegu. Akiwa amebeba kwa mkono mmoja mfuko uliojaa shayiri, mkulima anazisambaza mbegu hizo zenye thamani kwa kuzirusha kushoto na kulia akitumia ule mkono mwingine (2). Kuna vijia ambavyo havijalimwa vinavyopita katika shamba hilo, hivyo anakuwa mwangalifu ili mbegu zianguke juu ya “udongo mzuri.”—Luka 8:5, 8.
Baada ya kupanda ni wakati wa kuvunja-vunja udongo. Mkulima anafunga matawi yenye miiba kwenye ng’ombe wake na kuyakokota matawi hayo ndani ya shamba lake. Makundi ya ndege yanatoa sauti kali na kudona-dona, yakiiba mbegu ambazo ziko karibu kufunikwa kwa udongo. Baadaye mkulima anatumia jembe dogo (3) kupiga-piga udongo na kuondoa magugu ambayo yanaweza kusonga mbegu zake kabla hazijakomaa.—Mathayo 13:7.
Wakati wa Kuvuna
Miezi inapita. Mvua inanyesha. Sasa masuke ya shayiri yaliyokomaa yanayumba-yumba katika jua, na kufanya mashamba yaonekane kuwa meupe.—Yohana 4:35.
Wakati wa kuvuna ni kipindi chenye shughuli nyingi kwa mkulima na familia yake. Mvunaji anashika mimea yenye nafaka kwa mkono wake wa kushoto na kuikata kwa mundu alioushika kwa mkono wake wa kuume (4). Wengine wanakusanya nafaka, na kuzifunga katika miganda (5), kisha wanaiweka juu ya punda au magari ya kukokotwa (6) ambayo yanapeleka nafaka hiyo kwenye uwanja wa kupuria ulio kijijini.
Jua ni kali katika anga la bluu lisilo na mawingu. Familia inapumzika kidogo chini ya kivuli cha mtini. Wanazungumza na kucheka huku wakila chakula chepesi kinachotia ndani mkate, nafaka iliyokaushwa, zeituni, tini zilizokaushwa, na zabibu kavu. Wanamalizia kwa kunywa maji yanayotiririka kutoka kwenye chemchemi.—Kumbukumbu la Torati 8:7.
Katika shamba lililo karibu, kuna watu wanaokusanya masalio ya nafaka (7). Wengine wao ni maskini na hawana mashamba.—Kumbukumbu la Torati 24:19-21.
Baadaye, katika uwanja wa kupuria ulio kijijini, mkulima anatandaza ile miganda ya nafaka mahali palipoinuka, penye udongo mgumu. Ng’ombe-dume wanakokota chombo kizito cha kupuria wakizunguka-zunguka (8). (Kumbukumbu la Torati 25:4) Ile miganda inakatwa-katwa na mawe yaliyochongoka na vipande vya chuma vilivyowekwa chini ya kile chombo kizito cha kupuria.
Mkulima anasubiri upepo wa jioni uanze. (Ruthu 3:2) Baada ya jua kutua anaingiza uma mrefu wenye ncha kali uliotengenezwa kwa mbao, au ‘sepetu ya kupepetea’ (9), chini ya miganda iliyopurwa na kuirusha juu hewani. (Mathayo 3:12) Nafaka nzito inaanguka sakafuni huku makapi yakipeperushwa na upepo. Anainua uma wake tena na tena mpaka anapomaliza kupepeta nafaka yote.
Jua linapochomoza, mke wa yule mkulima na binti zake wanaanza kuchekecha nafaka (10). Wanatikisa kichungi kilichojaa nafaka na changarawe. Shayiri inaanguka ndani ya vikapu, na wanatupa uchafu kando. Kumekuwa na mazao mengi. Wafanyakazi wanaweka nafaka ya ziada ndani ya mitungi mikubwa (11). Nafaka inayobaki itamwagwa ndani ya vyumba vya kuhifadhi nafaka.
Akiwa juu ya uwanja wa kupuria, mkulima ananyoosha mgongo na misuli yake iliyochoka, na kutazama mashamba yanayozunguka kijiji. Anaridhika anapotazama mashamba yenye rangi mbalimbali, yaliyobaki na vishina—jambo linaloonyesha kwamba imekuwa siku yenye kazi ngumu ya kuchosha. Anawatazama wafanyakazi wakitunza makomamanga, mitini, mashamba ya mizabibu, na mashamba ya mizeituni. Hapo karibu, anamwona jirani anayempungia mkono huku akilima shamba lake dogo. Katika shamba hilo, amepanda matango, dengu, maharagwe, njegere, na aina mbalimbali ya vitunguu. Mkulima anatua, anatazama mbinguni, na kutoa sala fupi inayotoka moyoni, akimshukuru Mungu kwa sababu ya zawadi nzuri anazowapa wanadamu.—Zaburi 65:9-11.
[Picha katika ukurasa wa 28-30]
(Ona nakala iliyochapishwa)