Maisha na Huduma ya Yesu
Kula Mlo Mkuu Pamoja na Farisayo
BAADA ya Yesu kuwajibu wachambuzi wake wanaoswali chanzo cha nguvu zake kuponya mwanamume ambaye hangeweza kuongea, Farisayo mmoja anamwalika kula mlo mkuu. Kabla hawajala, Mafarisayo wanajitia katika ile desturi ya kunawa mikono yao mpaka kwenye kiko cha mkono. Wanafanya hivyo kabla na baada ya mlo na hata kati ya kula chakula hiki na hiki katika mlo mmoja. Ingawa pokeo hilo halivunji sheria iliyoandikwa ya Mungu, linaruka mipaka ya mambo ambayo Mungu anataka katika lile jambo la usafi wa kisherehe.
Inapokuwa kwamba Yesu hashiki pokeo hilo, mkaribishaji wake anashangaa. Hata ingawa huenda mshangao wake ukawa hauonyeshwi kwa maneno, Yesu anaugundua na kusema: “Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia?”
Hivyo Yesu anafichua unafiki wa Mafarisayo wanaonawa mikono yao kidesturi lakini hawaoshi mioyo yao isiwe na uovu. Yeye anashauri hivi: “Toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.” Utoaji wao unapasa kusukumwa na moyo wenye upendo, si na tamaa ya kushangaza wengine kwa kujifanya kwao kuwa wenye uadilifu.
“Ole wenu, Mafarisayo,” Yesu anaendelea, “kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.” Sheria ya Mungu kwa Israeli inataka kulipa zaka au sehemu ya kumi ya mazao yenye kutoka mashambani. Mnanaa na mchicha ni mimea midogo au vimea vifupi vinavyotumiwa katika kukolezea chakula. Mafarisayo wanafanya uangalifu wa kulipa kikumi cha hata vimea hivyo visivyo na maana kubwa, lakini Yesu anawashutumu wao kwa kupuuza lile takwa la maana zaidi la kuonyesha upendo, kujizoeza fadhili, na kuwa wenye kiasi.
Akizidi kuwashutumu, Yesu anasema: “Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo,” Kukosa kwao usafi hakuonekani wazi. Dini ya Mafarisayo ina ujionyesho wa kinje-nje lakini haina ustahiki wa ndani! Inategemea msingi wa unafiki.
Kwa kusikiliza shutumu hilo, mwana-sheria mmoja, mmoja wa wale wenye kisomo kingi katika Sheria ya Mungu, analalamika hivi: “Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi.”
Yesu anawachukua wastadi hawa wenye kujua Sheria kuwa wenye daraka la ulaumifu pia, akisema: “Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua.”
Mizigo ambayo Yesu anataja ni yale mapokeo yenye kupokezwa kwa mdomo, lakini wanasheria hawa hawakutaka kuinua hata kirekebi kimoja kidogo ili kufanya mambo yawe rahisi kidogo kwa watu. Yesu anafunua kwamba wao hata wanatoa idhini ya kuuawa kwa wanabii, na kwa hiyo yeye anaonya hivi: “Kwa kizazi hiki [itatakwa] damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.”
Ulimwengu wa aina ya binadamu wenye kukomboleka ulipata mwanzo wakati Adamu na Hawa walipopata uzaliwa wa watoto; hivyo, Abeli aliishi wakati wa “kupigwa msingi wa ulimwengu.” Baada ya uuaji wa kikorofi wa Zekaria, kanijeshi ya Kisiria iliteka nyara katika Yuda. Lakini Yesu anatabiri utekwaji nyara ulio mbaya zaidi wa kizazi chake mwenyewe kwa sababu ya uovu wacho ulio mkubwa zaidi. Utekwaji nyara huu unatukia karibu miaka 38 baadaye, katika 70 W.K.
Akiendelea na shutumu lake, Yesu anasema: “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.” Wastadi wanaojua ile Sheria wana wajibu wa lazima wa kuwaeleza watu Neno la Mungu, wakifungulia wazi maana yalo. Lakini wao hawafanyi hivyo na hata wananyang’anya watu ile fursa ya kuelewa.
Mafarisayo na wastadi wa kisheria wana kiruu juu ya Yesu kwa kuwafichua wazi. Anapoondoka kwenye nyumba hiyo, wao wanaanza kumpinga vikali na kumzingira kwa maswali. Wao wanajaribu kumtega aseme jambo fulani ambalo wanaweza kutumia wamfanye akamatwe. Luka 11:37-54; Kumbukumbu 14:22; Mika 6:8; 2 Nyakati 24:20-25.
◆ Kwa nini Yesu anashutumu Mafarisayo na wastadi wenye kujua ile Sheria?
◆ Ni mizigo gani ambayo wanasheria wanaweka juu ya watu?
◆ “Kupigwa msingi wa ulimwengu” kulitukia lini?