Sura 10
Ukristo—Je! Yesu Alikuwa Ndiye Njia ya Kuongoza kwa Mungu
Kufikia hapa, isipokuwa sura inayohusu Dini ya Kiyahudi, tumechunguza juu ya dini kubwa-kubwa ambazo kwa kadiri kubwa zategemea ngano. Sasa tutachunguza dini nyingine inayodai kuleta ainabinadamu karibu zaidi na Mungu—Ukristo. Ni nini msingi wa Ukristo—ngano au uhakika wa kihistoria?
1. (a) Ni kwa nini historia ya Jumuiya ya Wakristo husababisha wengine wawe na shaka kubwa juu ya Ukristo? (b) Ni tofauti gani tunayofanya kati ya Jumuiya ya Wakristo na Ukristo?
HISTORIA ya Jumuiya ya Wakristo,a pamoja na vita vyayo, mateso ya wazushi, krusedi (vita vitakatifu), na unafiki wa kidini, haikusaidia lengo la Ukristo. Waislamu wenye kufuata dini na wengine hutaja ufisadi wa adili na upotovu wa ulimwengu wa Magharibi, wa “Kikristo” kuwa msingi wa kukataa Ukristo. Kweli kweli, yaitwayo mataifa ya Kikristo yamepoteza mwongozo wayo wa kiadili na wamezamishwa na miamba ya ukosefu wa imani, pupa, na anasa.
2, 3. (a) Kuna tofauti gani kati ya mwenendo wa Wakristo wa mapema na ule wa watu wa Jumuiya ya Wakristo ya kisasa? (b) Ni baadhi ya maswali gani yatakayojibiwa?
2 Kwamba viwango vya Ukristo wa awali vilikuwa tofauti na tabia za leo za uendekezaji yathibitishwa na Profesa Elaine Pagels katika kitabu chake Adam, Eve and the Serpent, ambamo atoa taarifa hii: “Wakristo wengi wa karne nne za kwanza walijivunia kizuizi chao cha kingono; waliepuka kuwa na wake wengi na mara nyingi talaka pia, jambo ambalo pokeo la Kiyahudi liliruhusu; na walikataa katakata mazoea ya kingono ya nje ya ndoa ambayo kwa kawaida yalikubaliwa na wenzao wapagani, mazoea yaliyotia ndani umalaya na ngono ya watu wa jinsia moja.”
3 Kwa hiyo, yafaa kuuliza, Je! historia ya Jumuiya ya Wakristo na hali yao ya kiadili ya kisasa ni wonyesho wa kweli wa mafundisho ya Yesu Kristo? Yesu alikuwa mwanamume wa aina gani? Je! yeye alisaidia kuleta ainabinadamu karibu zaidi na Mungu? Je! yeye alikuwa Mesiya wa unabii wa Kiebrania? Hayo ni baadhi ya maswali tutakayofikiria katika sura hii.
Yesu—Sifa Zake Zilikuwa Zipi?
4. Katika uchunguzi wetu, tumeona tofauti gani iliyo wazi kati ya Ukristo na mizizi yao, na dini kubwa-kubwa za ulimwengu?
4 Katika sura zilizotangulia tumeona fungu lenye kutokeza ambalo ngano zimetimiza katika karibu dini zote kubwa-kubwa za ulimwengu. Hata hivyo, tulipogeukia vyanzo vya Dini ya Kiyahudi katika sura yetu iliyotangulia, hatukuanza na ngano bali na uhalisi wa kihistoria wa Abrahamu, wazazi wake wa mbele, na wazao wake. Kuhusu Ukristo na mwanzilishi wao, Yesu, twaanza vivyo hivyo, si kwa ngano, bali na mtu wa kihistoria.—Ona kisanduku, ukurasa 237.
5. (a) Ni sifa tatu zipi alizokuwa nazo Yesu zinazothibitisha kwamba alikuwa “mbegu” iliyoahidiwa ya Abrahamu? (b) Ni nani aliyeandika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo?
5 Mstari wa kwanza wa Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, ambayo kwa kawaida huitwa Agano Jipya (ona kisanduku, ukurasa 241), hutoa taarifa hii: “Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.” (Mathayo 1:1) Je! hilo ni dai la upuuzi linalotolewa na Mathayo, aliyekuwa hapo kwanza mtoza ushuru Myahudi na mwanafunzi wa karibu na mwandikaji-wasifu wa Yesu? La. Mistari ifuatayo 15 yataja mlango wa wazao wa Abrahamu kurudi mpaka Yakobo, ‘aliyemzaa Yusufu mumeye Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.’ Basi, kwa kweli Yesu alikuwa mzao wa Abrahamu, Yuda, na Daudi na kwa hiyo alikuwa na sifa tatu za “uzao [mbegu, NW]” uliotabiriwa wa Mwanzo 3:15 na wa Abrahamu.—Mwanzo 22:18; 49:10; 1 Mambo ya Nyakati 17:11.
6, 7. Ni kwa nini mahali alipozaliwa Yesu palikuwa na umaana?
6 Nyingine ya sifa za Mbegu ya Kimesiya ingekuwa ni mahali pake pa kuzaliwa. Yesu alizaliwa wapi? Mathayo atuambia kwamba Yesu ‘alizaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode.’ (Mathayo 2:1) Simulizi la Daktari Luka lathibitisha uhakika huo, anapotuambia juu ya baba-mlezi wa wakati ujao wa Yesu: “Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba.”—Luka 2:4, 5.
7 Kwa nini lilikuwa jambo la maana kwamba Yesu azaliwe katika Bethlehemu badala ya Nazareti au mji mwingine wowote? Kwa sababu ya unabii uliotolewa wakati wa karne ya nane K.W.K. na nabii Mika Mwebrania: “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” (Mika 5:2) Kwa hiyo, kwa mahali alipozaliwa, Yesu alikuwa na sifa nyingine ya kumtambulisha kuwa Mbegu aliyeahidiwa na Mesiya aliyeahidiwa.—Yohana 7:42.
8. Ni baadhi ya unabii gani aliotimiza Yesu?
8 Kwa kweli, Yesu alitimiza unabii mwingi zaidi kutoka Maandiko ya Kiebrania, hivyo akathibitisha kwamba yeye alikuwa na sifa zote za kuwa Mesiya aliyeahidiwa. Unaweza kuchunguza baadhi ya huo katika Biblia. (Ona kisanduku, ukurasa 245.)b Lakini sasa acheni tuchunguze kifupi ujumbe wa Yesu na huduma yake.
Maisha ya Yesu Yaelekeza Njia
9. (a) Yesu alianzaje huduma yake ya peupe? (b) Twajuaje kwamba Yesu alikuwa na kibali cha Mungu?
9 Simulizi la Biblia latuambia kwamba Yesu alilelewa akiwa kijana Myahudi wa kawaida wa wakati wake, akihudhuria sinagogi la mahali pao na hekalu katika Yerusalemu. (Luka 2:41-52) Alipofika umri wa miaka 30, yeye alianza huduma yake ya peupe. Kwanza alienda kwa binamu yake Yohana, aliyekuwa akibatiza Wayahudi katika wonyesho wa toba katika mto Yordani. Simulizi la Luka latuambia hivi: “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka [“roho takatifu ikashuka,” NW] juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”—Luka 3:21-23; Yohana 1:32-34.
10, 11. (a) Ni baadhi ya mambo gani yaliyojumlishwa katika njia za Yesu za kuhubiri na kufundisha? (b) Yesu alionyeshaje umaana wa jina la Baba yake?
10 Muda si muda, Yesu alianza huduma yake akiwa Mwana wa Mungu aliyepakwa mafuta. Alizunguka-zunguka Galilaya na Yudea akihubiri ujumbe wa Ufalme wa Mungu na kufanya miujiza, kama vile kuponya wagonjwa. Yeye hakukubali malipo yoyote wala hakutafuta utajiri wala kujikuza. Kwa kweli, yeye alisema kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko zilivyo katika kupokea. Yeye pia alifunza wanafunzi wake jinsi ya kuhubiri.—Mathayo 8:20; 10:7-13; Matendo 20:35.
11 Tunapochanganua ujumbe wa Yesu na njia alizotumia, twaona tofauti iliyo wazi kati ya mtindo wake na ule wa wahubiri wengi wa Jumuiya ya Wakristo. Yeye hakuvuta umati wa watu kwa kuchangamsha tu hisia-moyo zao wala kwa njia za kutisha juu ya moto wa mateso. Badala yake, Yesu alitumia njia rahisi ya kuonyesha sababu na mifano, au vielezo, kutokana na maisha ya kila siku ili kuvuta moyo na akili. Mahubiri ya Mlimani yake yanayojulikana sana ni kielelezo cha kutokeza cha mafundisho na njia zake. Inayotiwa ndani ya mahubiri hayo ni ile sala ya kielelezo ya Yesu, ambayo katika hiyo anatoa dokezo lililo wazi la mambo ya kutangulizwa na Ukristo kwa kuweka mahali pa kwanza kutakaswa kwa jina la Mungu. (Ona kisanduku, kurasa 258-9.)—Mathayo 5:1–7:29; 13:3-53; Luka 6:17-49.
12. (a) Yesu alidhihirishaje upendo katika mafundisho na vitendo vyake? (b) Ulimwengu ungekuwaje tofauti kama upendo wa Kikristo ungezoewa kikweli?
12 Katika kushughulika kwake na wafuasi wake na watu wote kwa ujumla, Yesu alidhihirisha upendo na huruma. (Marko 6:30-34) Alipokuwa akihubiri ujumbe wa Ufalme wa Mungu, yeye binafsi pia alizoea upendo na unyenyekevu. Kwa hiyo, katika saa za mwisho-mwisho za maisha yake, yeye angeweza kuwaambia wanafunzi wake: “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:34, 35) Kwa hiyo, maana halisi ya kuzoea Ukristo ni upendo wa kujidhabihu unaotegemea kanuni. (Mathayo 22:37-40) Kimatendo hiyo yamaanisha kwamba Mkristo apaswa kupenda hata maadui wake, ijapokuwa aweza kuchukia matendo yao maovu. (Luka 6:27-31) Fikiria hilo kidogo. Ulimwengu huu ungekuwa tofauti kama nini ikiwa kila mtu hasa angezoea namna hiyo ya upendo!—Warumi 12:17-21; 13:8-10.
13. (a) Kufundisha kwa Yesu kulikuwa tofauti kwa njia gani na kule kwa Confucius, Lao-tzu, na Buddha?
13 Hata hivyo, yale aliyofunza Yesu yalikuwa zaidi ya wema au falsafa, kama zilizofunzwa na Confucius na Lao-tzu. Kuongezea hayo, Yesu hakufundisha, kama Buddha, kwamba mtu aweza kujifanyia wokovu wake kupitia njia ya maarifa na mnurisho. Badala yake, yeye alitaja Mungu kuwa chanzo cha wokovu aliposema: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”—Yohana 3:16, 17.
14. Ni kwa nini Yesu angeweza kusema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima”?
14 Kwa kudhihirisha upendo wa Baba yake katika maneno na vitendo vyake, Yesu alivuta watu karibu na Mungu. Hiyo ni sababu moja kwa nini yeye angeweza kusema: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. . . . Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba [“nimo katika umoja na Baba,” NW], na Baba yu ndani yangu [“na Baba yumo katika umoja na mimi,” NW]? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. . . . Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.” (Yohana 14:6-28) Ndiyo, Yesu alikuwa “njia, na kweli, na uzima” kwa sababu yeye alikuwa akiwaongoza wale watu wa Kiyahudi warudi kwa Baba yake, Mungu wao wa kweli, Yehova. Kwa hiyo, kupitia kwa Yesu jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu kwa ghafula ilichochewa kwa sababu Mungu, katika upendo wake mkuu, alikuwa amemtuma Yesu duniani kuwa mmweko wa nuru na ukweli ili kuwaongoza watu kwa Baba.—Yohana 1:9-14; 6:44; 8:31, 32.
15. (a) Ni lazima tufanye nini ili tumpate Mungu? (b) Kuna uthibitisho gani hapa duniani wa upendo wa Mungu?
15 Kwa msingi wa huduma na kielelezo cha Yesu, misionari Paulo angeweza baadaye kuwaambia Wagiriki katika Athene hivi: “Naye [Mungu] alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu.” (Matendo 17:26-28) Ndiyo, Mungu aweza kupatikana ikiwa mtu ana nia ya kutia jitihada ya kumtafuta. (Mathayo 7:7, 8) Mungu amejifanya mwenyewe na upendo wake uwe dhahiri kwa maana ametayarisha dunia ambayo hutegemeza uhai mbalimbali unaoelekea kuwa hauna mwisho. Yeye hutoa yaliyo ya lazima kwa ainabinadamu yote, wawe ni waadilifu au wasio waadilifu. Pia amewapa ainabinadamu Neno lake lililoandikwa, Biblia, naye alimtuma Mwanae kuwa dhabihu ya ukombozi.c Zaidi ya hayo, Mungu ametoa msaada ambao watu wahitaji ili kuwasaidia wapate njia ya kumfikia Yeye.—Mathayo 5:43-45; Matendo 14:16, 17; Warumi 3:23-26.
16, 17. Ni lazima upendo wa kweli wa Kikristo udhihirishweje?
16 Bila shaka, upendo wa Kikristo lazima udhihirishwe si kwa maneno tu bali la maana zaidi kwa matendo. Kwa sababu hiyo mtume Paulo aliandika: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; haupungui neno wakati wo wote.”—1 Wakorintho 13:4-8.
17 Yesu pia alionyesha wazi jinsi lilivyo jambo la maana kutangaza Ufalme wa mbingu—utawala wa Mungu juu ya ainabinadamu wenye kujitiisha.—Mathayo 10:7; Marko 13:10.
Kila Mkristo ni Mweneza Evanjeli
18. (a) Ni nini kilichokaziwa katika Mahubiri ya Mlimani ya Yesu? (b) Kila Mkristo ana daraka gani? (c) Yesu aliwatayarishaje wanafunzi wake kwa ajili ya huduma yao, nao walipaswa kuhubiri ujumbe gani?
18 Katika Mahubiri ya Mlimani yake, Yesu alikazia kwa halaiki daraka lao la kumulika wengine kwa maneno na vitendo vyao. Yeye alisema: “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:14-16) Yesu alizoeza wanafunzi wake ili wajue jinsi ya kuhubiri na kufundisha wakati wa safari zao wakiwa wahudumu wenye kusafiri. Nao ujumbe wao ungekuwa nini? Ule ambao Yesu mwenyewe alihubiri, Ufalme wa Mungu, ambao ungetawala dunia katika uadilifu. Kama alivyoeleza Yesu katika pindi moja: “Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa.” (Luka 4:43; 8:1; 10:1-12) Pia yeye alitoa taarifa kwamba sehemu ya ishara ya kutambulisha siku za mwisho ingekuwa kwamba “habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.”—Mathayo 24:3-14.
19, 20. (a) Ni kwa nini Ukristo wa kweli umekuwa dini yenye kutenda, ya kuhubiri sikuzote? (b) Ni maswali gani ya msingi yanayohitaji majibu sasa?
19 Katika 33 W.K., kabla hajapaa mbinguni hatimaye, Yesu aliyefufuliwa aliwaagiza wanafunzi wake hivi: “Mimi nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Kwa hiyo nendeni mkafanye wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote, kuwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la roho takatifu, kuwafundisha kushika yote ambayo nimewaamuru nyinyi. Na tazama! mimi nipo pamoja na nyinyi siku zote mpaka umalizio wa mfumo wa mambo.” (Mathayo 28:18-20, NW) Hiyo ni sababu moja kwa nini Ukristo, tangu kuanzishwa kwao, ulikuwa dini yenye kutenda, ya kuongoa ambayo iliamsha hasira na wivu wa wafuasi wa dini za Kigiriki na Kiroma zilizokuwako siku hizo, ambazo msingi wazo ulikuwa ngano. Kuteswa kwa Paulo katika Efeso kulionyesha uhakika huo waziwazi.—Matendo 19:23-41.
20 Sasa maswali ni haya, Ujumbe wa Ufalme wa Mungu ulitoa nini kuhusu wafu? Kristo alihubiri tumaini gani kwa ajili ya wafu? Je! yeye alikuwa akizitolea “nafsi zisizoweza kufa” za waamini wake wokovu kutoka “moto wa mateso?” Au vipi?—Mathayo 4:17.
Tumaini la Uhai wa Milele
21, 22. (a) Yesu alilinganisha hali ya Lazaro mfu na nini, na kwa nini? (b) Martha alikuwa na tumaini gani kwa ajili ya ndugu yake aliyekufa?
21 Labda mwono-ndani ulio wazi zaidi katika tumaini ambalo Yesu alihubiri waweza kupatikana kutokana na aliyosema na kufanya wakati rafiki yake Lazaro alipokufa. Yesu alionaje kifo chake? Akifunga safari ya kwenda nyumbani kwa Lazaro, Yesu aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha.” (Yohana 11:11) Yesu alilinganisha hali ya kufa kwa Lazaro na usingizi. Katika usingizi mzito, hatuna fahamu juu ya lolote, jambo linalokubaliana na usemi wa Kiebrania kwenye Mhubiri 9:5: “Kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote.”
22 Ijapokuwa Lazaro alikuwa amekufa kwa siku nne, hatuoni lolote likisemwa na Yesu juu ya nafsi ya Lazaro ikiwa mbinguni, kwenye moto wa mateso, au purgatori (toharani)! Yesu alipowasili Bethania, naye Martha, dada yake Lazaro, akaja kumlaki, Yesu alimwambia, “Ndugu yako atafufuka.” Martha alijibuje? Je! yeye alisema tayari alikuwa mbinguni? Martha alijibu hivi: “Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.” Hilo laonyesha wazi kwamba tumaini la Kiyahudi wakati huo lilikuwa ni ufufuo, kurudi kwenye uhai hapa duniani.—Yohana 11:23, 24, 38, 39.
23. Yesu alifanya muujiza gani, na kukawa na tokeo gani kwa watazamaji?
23 Yesu alijibu: “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! unayasadiki hayo?” (Yohana 11:25, 26) Ili kuthibitisha jambo hilo, Yesu alienda kwenye pango ambamo Lazaro alikuwa amezikwa na kumwita atoke akiwa hai mbele ya macho ya dada zake, Mariamu na Martha, na majirani. Simulizi laendelea hivi: “Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini . . . Basi wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua.” (Yohana 11:45; 12:7) Wao walikuwa wamejionea muujiza huo, nao waliamini na kuthibitisha uhalisi wao. Wapinzani wa kidini wa Yesu lazima wawe waliamini tukio hilo, kwa maana maandishi yatuambia kwamba makuhani wakuu na Mafarisayo walitunga hila ya kumuua Yesu “maana mtu huyu afanya ishara nyingi.”—Yohana 11:30-53.
24. (a) Lazaro alikuwa amekuwa wapi kwa siku nne? (b) Biblia yasema nini juu ya hali ya kutoweza kufa?
24 Lazaro alikuwa ameenda wapi wakati wa siku nne alizokuwa mfu? Hakuna. Yeye alikuwa bila fahamu, amelala katika kaburi akingojea ufufuo. Yesu alimbariki kwa kumwinua kimuujiza kutoka kwa wafu. Lakini kulingana na simulizi la Yohana, Lazaro hakusema lolote juu ya kuwa alikuwa mbinguni, kwenye moto wa mateso, au purgatori wakati wa hizo siku nne. Kwa nini? Kwa sababu tu yeye hakuwa na nafsi isiyoweza kufa ambayo ingeweza kufunga safari ya kwenda sehemu kama hizo.d—Ayubu 36:14; Ezekieli 18:4.
25. (a) Biblia inaposema juu ya uzima wa milele, inarejezea kwenye nini? (b) Kuja kwa Ufalme wa Mungu ulioahidiwa kwategemea nini?
25 Kwa hiyo, Yesu alipozungumza juu ya uzima wa milele, alikuwa akirejezea maisha hayo ama katika mbingu akiwa mtawala-mwenzi wake wa kiroho aliyegeuzwa asiweze kufa katika Ufalme wake, au alikuwa akirejezea uzima wa milele akiwa binadamu juu ya dunia-paradiso chini ya utawala wa Ufalme huo.e (Luka 23:43, Zaire Swahili Bible; Yohana 17:3) Kulingana na ahadi ya Mungu, makao yake ya kitamathali pamoja na ainabinadamu tiifu duniani yataleta baraka tele duniani. Bila shaka, yote hayo yategemea kama Yesu alitumwa na kukubaliwa kweli kweli na Mungu.—Luka 22:28-30; Tito 1:1, 2; Ufunuo 21:1-4.
Kibali cha Mungu—Uhalisi, Si Ngano
26. Ni tukio gani la kutokeza lililotokea katika kuwapo kwa wanafunzi Petro, Yakobo, na Yohana?
26 Twajuaje kwamba Yesu alikuwa na kibali cha Mungu? Kwanza, Yesu alipobatizwa, sauti kutoka mbinguni ilisikiwa ikisema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye [“ambaye nimekubali,” NW]” (Mathayo 3:17) Baadaye, uthibitisho wa kibali hicho ulitolewa mbele ya mashahidi wengine. Wanafunzi Petro, Yakobo, na Yohana, ambao hapo awali walikuwa wavuvi kutoka Galilaya, waliambatana na Yesu kwenye mlima mrefu (yaelekea Mlima Hermoni, unaoinuka meta 2,814). Huko jambo lenye kutokeza lilitukia mbele ya macho yao: “[Yesu] akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. . . . Tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye [“ambaye nimekubali,” NW]; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.”—Mathayo 17:1-6; Luka 9:28-36.
27. (a) Kugeuka huko kwa sura kulikuwa na tokeo gani juu ya wanafunzi? (b) Twajuaje kwamba Yesu hakuwa ngano?
27 Uthibitisho uliosikika na kuonekana kutoka kwa Mungu ulitia nguvu nyingi imani ya Petro, kwa maana yeye aliandika hivi baadaye: “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu [Kigiriki: myʹthois, ngano], tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye [“ambaye mimi mwenyewe nimekubali,” NW]. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.” (2 Petro 1:16-18) Wanafunzi Wayahudi Petro, Yakobo, na Yohana kwa halisi waliona muujiza huo wa kubadilika sura kwa Yesu na wakasikia sauti ya kibali cha Mungu kutoka mbinguni. Imani yao ilitegemezwa juu ya uhalisi waliokuwa wameona na kusikia, wala si ngano wala juu ya “hadithi za Kiyahudi.” (Ona kisanduku, ukurasa 237.)—Mathayo 17:9; Tito 1:13, 14.f
Kifo cha Yesu na Muujiza Mwingine
28. Katika mwaka 33 W.K., Yesu alishtakiwaje kibandia?
28 Katika mwaka 33 W.K., Yesu alikamatwa na kujaribiwa na mamlaka za kidini za Kiyahudi, akishtakiwa kibandia juu ya kukufuru kwa kujiita mwenyewe Mwana wa Mungu. (Mathayo 26:3, 4, 59-67) Kwa kuwa ni wazi Wayahudi hao walipendeleaa mamlaka ya Kiroma imwue, walimpeleka kwa Pilato na tena wakamshtaki kibandia, wakati huu kuwa alikataza kulipa kodi kwa Kaisari na kusema kwamba yeye mwenyewe alikuwa mfalme.—Marko 12:14-17; Luka 23:1-11; Yohana 18:28-31.
29. Yesu alikufaje?
29 Baada ya Yesu kutoka kwa mtawala huyu mpaka huyu, liwali wa Kiroma Pontio Pilato, kwa kusisitiziwa na wafanya ghasia waliochochewa kidini, alichukua njia rahisi ya mkato akamhukumia Yesu kifo. Kwa sababu hiyo, Yesu akafa katika aibu juu ya mti, na mwili wake ukawekwa ndani ya kaburi. Lakini ndani ya muda wa siku tatu tukio fulani lilitokea ambalo liligeuza wanafunzi wa Yesu waliojaa masikitiko wakawa waamini wenye kushangilia na waeneza evanjeli wenye bidii.—Yohana 19:16-22; Wagalatia 3:13.
30. Viongozi wa kidini walichukua hatua gani ili kuzuia udanganyifu?
30 Viongozi wa kidini, wakiwa na shaka kwamba wafuasi wa Yesu wangetumia ujanja, walimwendea Pilato wakiwa na ombi: “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.” (Mathayo 27:62-66) Lilikuwa salama kadiri gani?
31. Kulitukia nini wakati wanawake waaminifu walipoenda kwenye kaburi la Yesu?
31 Katika siku ya tatu baada ya kifo cha Yesu, wanawake watatu walienda kwenye kaburi wakapake mafuta mwili huo kwa manukato. Walikuta nini? “Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza; wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno. Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu. Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulubiwa [“ambaye alitundikwa,” NW]; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.” (Marko 16:1-7; Luka 24:1-12) Ijapokuwa askari maalumu wa viongozi wa kidini, Yesu alikuwa amefufuliwa na Baba yake. Je! hiyo ni ngano au ni uhakika wa kihistoria?
32. Ni kwa sababu zipi imara Paulo aliamini kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa?
32 Miaka yapata 22 baada ya tukio hilo, Paulo, aliyekuwa hapo awali mtesaji wa Wakristo, aliandika na kueleza jinsi alivyokuja kuamini kwamba Kristo alikuwa amefufuliwa: “Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote.” (1 Wakorintho 15:3-7) Ndiyo, Paulo alikuwa na msingi wa mambo yenye uhakika wa kuhatarisha maisha yake kwa sababu ya Yesu aliyefufuliwa, nao ulitia ndani uthibitisho wa mashahidi waliojionea wapatao 500 ambao walimwona Yesu aliyefufuliwa akiwa mtu! (Warumi 1:1-4) Paulo alijua Yesu alikuwa amefufuliwa, naye alikuwa na sababu yenye nguvu hata zaidi ya kusema hivyo, kama anavyoendelea kueleza: “Na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.”—1 Wakorintho 15:8, 9; Matendo 9:1-19.
33. Ni kwa nini Wakristo wa kwanza walikuwa na nia ya kufia imani yao?
33 Wakristo wa mapema walikuwa tayari kufia imani katika nyanja za Kiroma. Kwa nini? Kwa sababu walijua kwamba imani yao ilitegemea uhalisi wa kihistoria, wala si ngano. Ulikuwa ni uhalisi kwamba Yesu alikuwa ndiye Kristo, au Mesiya, aliyeahidiwa katika unabii na kwamba alikuwa ametumwa duniani na Mungu, alikuwa amepata kibali cha Mungu, alikuwa amekufa juu ya mti akiwa Mwana wa Mungu aliyeshika ukamilifu, na alikuwa amefufuliwa kutoka kwa wafu.—1 Petro 1:3, 4.
34. Kulingana na mtume Paulo, ni kwa nini ufufuo wa Yesu ni wa lazima sana kwa imani ya Kikristo?
34 Twapendekeza kwamba usome sura yote hiyo ya 15 ya barua ya kwanza ya Paulo kwa Wakorintho ili uelewe aliyoamini Paulo juu ya ufufuo na kwa nini hilo ni jambo la lazima kwa imani ya Kikristo. Maana ya ujumbe wake yaelezwa katika maneno haya: “Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu [Adamu], kadhalika na kiyama [“ufufuo,” NW] ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. [“watafanywa hai,” NW].”—1 Wakorintho 15:20-22.
35. Ni baraka gani zinazoahidiwa na Mungu kwa ajili ya dunia na kwa ajili ya ainabinadamu? (Isaya 65:17-25)
35 Kwa hiyo kufufuliwa kwa Kristo Yesu kuna kusudi ambalo hatimaye litafaidi ainabinadamu yote.g Pia kulifungua njia kwa Yesu ili hatimaye atimize unabii wa Kimesiya uliosalia. Utawala wake wa uadilifu kutoka mbingu zisizoonekana lazima upesi uenee kwenye dunia iliyosafishwa. Halafu kutakuwako ambacho Biblia hueleza kuwa “mbingu mpya na nchi mpya” ambamo Mungu “atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”—Ufunuo 21:1-4.
Uasi-Imani na Mateso Yatazamiwa
36. Ni nini kilichotukia kwenye Pentekoste 33 W.K., na tokeo likawa nini?
36 Muda mfupi baada ya kifo na ufufuo wa Yesu, muujiza mwingine ulitokea uliotia nguvu na mwendo mahubiri ya Wakristo hao wa kwanza. Katika siku ya Pentekoste ya mwaka 33 W.K., Mungu alimimina kutoka mbinguni roho takatifu yake, au kani ya utendaji, juu ya Wakristo 120 waliokusanyika pamoja katika Yerusalemu. Tokeo likawa nini? “Na ndimi kana kwamba za moto zikaonekana kwao na zikajigawanya-gawanya, na mmoja ukaketi juu ya kila mmoja wao, nao wote wakajawa na roho takatifu na wakaanza kusema kwa lugha zilizo tofauti, kwa kadiri roho ilivyokuwa ikiwapa kutamka.” (Matendo 2:3, 4, NW) Wayahudi wenye kuzungumza lugha za kigeni waliokuwako Yerusalemu wakati huo walistaajabu kusikia Wayahudi hao wa Galilaya waliodhaniwa kuwa wasiojua mambo wakisema katika lugha za kigeni. Matokeo yakawa kwamba wengi wakaamini. Ujumbe wa Kikristo ulienea kama moto wa mwitu waamini hao wapya wa Kiyahudi waliporejea makwao.—Matendo 2:5-21.
37. Watawala fulani Waroma walichukua hatua gani kuelekea dini mpya ya Kikristo?
37 Lakini mawingu ya dhoruba yakakusanyika upesi. Waroma wakawa na wasiwasi juu ya dini hii mpya na iliyoelekea kuwa ya kiatheisti ambayo haikuwa na sanamu. Kuanzia na Maliki Nero, walileta mateso mabaya sana juu ya Wakristo katika karne tatu za kwanza za Wakati wa Kawaida wetu.h Wakristo wengi walihukumiwa kufa katika majumba ya michezo, ili kuridhisha uchu wa kikatili wa damu wa maliki na wafanya ghasia waliomiminika wapate kuona wafungwa wakitupwa penye hayawani-mwitu.
38. Ni hali gani iliyotabiriwa ambayo ingehangaisha kundi la Kikristo la mapema?
38 Kitu kingine chenye kuhangaisha katika siku hizo za mapema kilikuwa ni kile ambacho mitume walikuwa wametabiri. Kwa kielelezo, Petro alitoa taarifa hii: “Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.” (2 Petro 2:1-3) Uasi-imani! Huko kulikuwa ni kuondoka kwenye ibada ya kweli, kuridhiana na mitindo ya wakati huo ya ulimwengu wa Kiroma, uliojaa juu-chini falsafa na mawazo ya Kigiriki. Ulikujaje? Sura yetu ifuatayo itajibu hilo na maswali yanayohusiana nalo.—Matendo 20:30; 2 Timotheo 2:16-18; 2 Wathesalonike 2:3.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa kusema “Jumuiya ya Wakristo” twarejezea makao ya utendaji wa kifaraka yanayotawalwa na dini zinazodai kuwa za Kikristo. “Ukristo” hurejezea namna ya ibada ya awali na njia ya kumfikia Mungu aliyofunza Yesu Kristo.
b Ona pia Insight on the Scriptures, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1988, Buku 2, kurasa 385-9, chini ya “Messiah.”
c Fundisho la Biblia juu ya ukombozi na umaana wao litaelezwa wazi katika Sura 15.
d Usemi “nafsi isiyoweza kufa” hauonekani popote ndani ya Biblia. Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “-siyoweza kufa” na “kutokufa” huonekana mara tatu tu na hurejezea mwili mpya wa kiroho unaovaliwa au mtu kujipatia, wala si kitu kilicho ndani ya mtu. Hutumiwa kuhusu Kristo na Wakristo wapakwa-mafuta, wanaokuwa watawala wenzi pamoja naye katika Ufalme wake wa kimbingu.—1 Wakorintho 15:53, 54; 1 Timotheo 6:16; Warumi 8:17; Waefeso 3:6; Ufunuo 7:4; 14:1-5.
e Kwa mazungumzo ya kirefu zaidi ya utawala huo wa Ufalme, ona Sura 15.
f “Musa” na “Eliya” katika njozi hiyo walifananisha Sheria na Manabii iliyotimizwa katika Yesu. Kwa ajili ya ufafanuzi zaidi wa kubadilika kwa sura, ona Insight on the Scriptures, 1988, Buku 2, kurasa 1120-1.
g Kwa mazungumzo ya kirefu juu ya ufufuo wa Yesu, ona kitabu Biblia—Neno la Mungu au la Binadamu?, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1991, kurasa 78-86.
h Suetonio (karibu 69-140 W.K.), mwandika wasifu Mroma aliandika kwamba wakati wa utawala wa Nero, “adhabu . . . zilifikilizwa juu ya Wakristo, farakano lililodai imani mpya na yenye kuleta madhara.”
[Sanduku/Picture katika ukurasa wa 237]
Je! Yesu Alikuwa Ngano Tu?
“Je! hadithi ya maisha ya mwanzilishi wa Ukristo ni ubuni wa majonzi, wazio, na tumaini la kibinadamu—ngano inayolinganika na hekaya za Krishna, Osirisi, Attisi, Adonisi, Dionisio, na Mithrasi?” auliza mwanahistoria Will Durant. Ajibu kwamba katika karne ya kwanza, kukana kwamba Kristo hakupata kuishi “yaonekana hakukutokea kamwe hata kwa wapinzani wakali sana Wasio Wayahudi wa Ukristo uliokuwa umeanza juzijuzi.”—The Story of Civilization, Sehemu 3, “Kaisari na Kristo.”
Suetonio (c. 69-140 W.K.) mwanahistoria Mroma, katika historia yake The Twelve Caesars, alieleza hivi kuhusu maliki Klaudio: “Kwa sababu Wayahudi kule Roma walisababisha matata yenye kuendelea kwa kuchochewa na Krestasi [Kristo], aliwafukuza katika jiji hilo.” Hilo lilitukia yapata mwaka 52 W.K. (Linganisha Matendo 18:1, 2.) Angalia kwamba Suetonio haonyeshi shaka lolote juu ya kuishi kwa Kristo. Kwa msingi huo wa uhakika na ijapokuwa minyanyaso yenye kuhatarisha maisha, Wakristo wa mapema walikuwa wenye kutenda sana katika kutangaza imani yao. Haielekei hata kidogo kwamba wangalihatarisha maisha zao kwa msingi wa ngano. Kifo na ufufuo wa Yesu vilikuwa vimetukia katika wakati wa maisha yao, na baadhi yao walikuwa wamejionea matukio hayo.
Durant mwanahistoria akata shauri hili: “Kwamba wanaume wachache wa kikawaida wangeweza katika kizazi kimoja kubuni mtu mwenye nguvu na mwenye uvutano mwingi kadiri hiyo, elimu ya maadili ya hali ya juu kadiri hiyo na njozi yenye kuchochea kadiri hiyo ya udugu wa kibinadamu, ungekuwa muujiza wenye kustaajabisha mno zaidi ya wowote ulioandikwa katika Gospeli”
[Picha]
Yesu alihubiri na kufanya miujiza katika mkoa huu wa Kigalilaya wa Palestina ya kale
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 241]
Nani Aliandika Biblia?
Biblia ya Kikristo ina vitabu 39 vya Maandiko ya Kiebrania (ona kisanduku, ukurasa 220), vinavyoitwa na wengi Agano la Kale, na vitabu 27 vya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, mara nyingi vikiitwa Agano Jipya.i Hivyo, Biblia ni maktaba ndogo ya vitabu 66 vilivyoandikwa na wanaume wapatao 40 katika muda wa miaka 1,600 ya historia (kuanzia 1513 K.W.K. mpaka 98 W.K.).
Maandiko ya Kigiriki hutia ndani Gospeli nne, au masimulizi ya maisha ya Yesu na habari njema ambazo yeye alihubiri. Mbili kati ya hizo ziliandikwa na wafuasi wa karibu wa Kristo, Mathayo, mtoza ushuru, na Yohana, mvuvi. Zile nyingine mbili ziliandikwa na waamini wa mapema Marko na Luka, tabibu. (Wakolosai 4:14) Gospeli zinafuatwa na Matendo ya Mitume, simulizi la utendaji wa umisionari wa Ukristo wa mapema lililokusanywa na Luka. Halafu kuna barua 14 kutoka kwa mtume Paulo akiandikia Wakristo mmoja mmoja na makundi mbalimbali, zikifuatwa na barua kutoka kwa Yakobo, Petro, Yohana, na Yuda. Kitabu cha mwisho ni Ufunuo, kilichoandikwa na Yohana.
Kwamba watu wengi hivyo wa malezi yenye kutofautiana sana na wakiishi katika nyakati na katika tamaduni mbalimbali wangeweza kutokeza kitabu chenye upatano hivyo ni uthibitisho wenye nguvu sana kwamba Biblia si zao tu la akili ya kibinadamu bali imepuliziwa na Mungu. Biblia yenyewe yatoa taarifa hii: “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho.” Kwa hiyo, Maandiko yaliandikwa chini ya uongozi wa roho takatifu, au kani ya utendaji ya Mungu.—2 Timotheo 3:16, 17.
[Picha]
Mchoro huu wa Kiroma usio kamili unaotumia jina la Pontio Pilato katika Kilatini (mstari wa pili, “IVS PILATVS”) huthibitisha kwamba yeye alikuwa mtu mwenye uvutano mkubwa katika Palestina, kama inavyoeleza Biblia
[Maelezo ya Chini]
i Biblia ya Katoliki hutia ndani vitabu vya ziada vya Apocrypha na ambavyo havionwi kuwa vyenye kukubalika na Wayahudi na Waprotestanti.
[Sanduku katika ukurasa wa 245]
Mesiya Katika Unabii wa Biblia
Unabii Tukio Utimizo
Mwa. 49:10 Kazaliwa katika Mt. 1:2-16; Luka 3:23-33
kabila la Yuda
Mik. 5:2 Kazaliwa Bethlehemu Luka 2:4-11; Yn. 7:42
Isa. 7:14 Kazaliwa na bikira Mt. 1:18-23;
Hos. 11:1 Kaitwa kutoka Misri Mt. 2:15
Isa. 61:1, 2 Kapewa utume Luka 4:18-21
Isa. 53:4 Kachukua Mt. 8:16, 17
magonjwa yetu
Zab. 69:9 Mwenye bidii kwa ajili ya Mt. 21:12, 13;
nyumba ya Yehova Yn 2:13-17
Isa. 53:1 Hakuaminiwa Yn 12:37, 38;
Isa. 28:16; Kakataliwa lakini kawa Mt. 21:42, 45, 46;
Zab. 118:22, 23 jiwe kuu la pembeni Mdo 3:14; 4:11;
Zab. 41:9; Mtume mmoja Mt. 26:47-50;
Zab. 109:8 kamsaliti Yn 13:18, 26-30
Zek. 11:12 Kasalitiwa kwa ajili ya Mt. 26:15; 27:3-10;
vipande 30 vya fedha Mk 14:10, 11
Isa. 53:8 Kajaribiwa na kuhukumiwa Mt. 26:57-68;
Isa. 53:7 Kimya mbele ya Mt. 27:12-14;
Zab. 69:4 Kachukiwa bila sababu Luka 23:13-25;
Zab. 22:18 Kura kapigwa kwa ajili ya Mt. 27:35
mavazi yake Yn 19:23, 24
Isa. 53:12 Kahesabiwa pamoja na watenda dhambi Mt. 26:55, 56; 27:38;
Zab. 69:21 Kapewa siki na Mt. 27:34, 48;
Zab. 22:1 Kaachwa na Mungu Mt. 27:46; Mk 15:34
Zab. 34:20; Hakuna mifupa iliyovunjwa Yn 19:33, 36
Isa. 53:5; Kadungwa Mt. 27:49;
Isa. 53:5, 8, Kafa kifo cha kidhabihu Mt. 20:28;Yn 1:29;
Isa 53:11, 12 ili kuchukua Rum. 3:24; 4:25
dhambi
Isa. 53:9 Kazikwa pamoja na matajiri Mt. 27:57-60;
Yona 1:17; Ndani ya kaburi sehemu Mt. 12:39, 40; 16:21;
Yona 2:10 za siku tatu, Mt. 17:23; 27:64
halafu kafufuliwa
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 258, 259]
Yesu na Jina la Mungu
Alipokuwa akifunza wanafunzi wake jinsi ya kusali, Yesu alisema: “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”—Mathayo 6:9, 10.
Yesu alijua umaana mkubwa wa jina la Baba yake na akaukazia. Kwa hiyo, kwa maadui wake wa kidini, yeye alisema: “Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. . . . Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia.”—Yohana 5:43; 10:25; Marko 12:29, 30.
Katika sala kwa Baba yake, Yesu alisema: “Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”
Katika pindi ya baadaye, Yesu alisali: “Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”—Yohana 12:28; 17:6, 26.
Akiwa Myahudi, Yesu alipaswa kulizoelea jina la Baba yake, Yehova, au Yahwe, kwa maana yeye alijua andiko linalosema: “‘Nyinyi ni mashahidi wangu,’ ndio usemi wa Yehova, ‘hata mtumishi wangu ambaye mimi nimechagua, ili mpate kujua na kuwa na imani katika mimi, na kwamba mpate kufahamu ya kuwa mimi ndiye Yule Yule. Kabla yangu mimi kulikuwa hakuna Mungu aliyeumbika, na baada yangu mimi hakuna aliyeendelea kuwako. . . . Basi nyinyi ni mashahidi wangu,’ ndio usemi wa Yehova, ‘nami ni Mungu.’”—Isaya 43:10, 12, “NW.”
Kwa hiyo, Wayahudi wakiwa taifa walichaguliwa wawe mashahidi wa Yehova. Akiwa Myahudi, Yesu pia alikuwa shahidi wa Yehova.—Ufunuo 3:14.
Kwa wazi kufikia karne ya kwanza, Wayahudi walio wengi hawakuwa wakitamka tena jina la Mungu lililofunuliwa. Hata hivyo, kuna hati zinazothibitisha kwamba Wakristo wa mapema wenye kutumia tafsiri Septuagint ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania wangeweza kuona Tetragrammatoni ya Kiebrania iliyotumiwa katika maandishi ya Kigiriki. Kama ambavyo George Howard, profesa wa dini na Kiebrania alivyoeleza: “Wakati Septuagint ambayo kanisa la Agano Jipya lilitumia na kunukuu ilipokuwa na namna ya Kiebrania ya jina la kimungu, waandikaji wa Agano Jipya bila shaka waliingiza Tetragrammatoni katika manukuu yao. Lakini wakati namna ya Kiebrania ya jina hilo la kimungu ilipoondolewa [baadaye] kwa kupendelea namna za Kigiriki katika Septuagint, liliondolewa pia katika manukuu ya Agano Jipya ya Septuagint.”
Kwa hiyo, Profesa Howard atoa sababu kwamba Wakristo wa karne ya kwanza lazima wawe walielewa waziwazi maandishi kama vile Mathayo 22:44, ambapo Yesu alinukulia maadui wake Maandiko ya Kiebrania. Howard asema, “Kanisa la karne ya kwanza yaelekea lilisoma ‘YHWH akamwambia Bwana wangu’” badala ya tafsiri ya baadaye, “‘Bwana akamwambia Bwana wangu,’ . . . ambayo haieleweki kama vile isivyokuwa wazi.”—Zaburi 110:1.
Kwamba Yesu alitumia jina la kimungu yathibitishwa na shtaka la Kiyahudi karne nyingi baada ya kifo chake kwamba ikiwa alifanya miujiza, ni “kwa sababu alikuwa amejifanya bwana wa jina la ‘siri’ la Mungu.”—The Book of Jewish Knowledge.
Kwa hakika Yesu alijua jina la pekee la Mungu. Lijapokuwa pokeo la Kiyahudi la wakati huo, bila shaka Yesu angalitumia jina hilo. Yeye hakuruhusu mapokeo ya binadamu yatawale sheria ya Mungu.—Marko 7:9-13; Yohana 1:1-3, 18; Wakolosai 1:15, 16.
[Picha]
Kisehemu cha mafunjo (karne ya kwanza K.W.K.) kinachoonyesha jina la Mungu katika Kiebrania katika maandishi ya Kigiriki ya Septuagint
[Picha katika ukurasa wa 238]
Yesu alitumia mifano mingi katika kufundisha kwake—kupanda mbegu, kuvuna, kuvua samaki, kutafuta lulu moja, kundi la wanyama waliochanganyika, shamba la mizabibu, kati ya mingine (Mathayo 13:3-47; 25:32)
[Picha katika ukurasa wa 243]
Kwa nguvu za Mungu, Yesu alifanya miujiza mingi,kutia ndani kutuliza dhoruba
[Picha katika ukurasa wa 246]
Tetra-grammatoni, au konsonanti nne YHWH (Yehova)
[Picha katika ukurasa wa 251]
Simulizi la kuinuliwa kwa Lazaro kwenye uzima halitaji wala hatakudokeza kwamba yeye alikuwa na nafsi isiyoweza kufa
[Picha katika ukurasa wa 253]
Petro, Yakobo, na Yohana walijua kwamba kibali cha Mungukwa Yesu hakikuwa ngano tu—wao walisikia na wakaona hilo wakati wa kugeuka sura