Maisha na Huduma ya Yesu
Shauri la Wakati wa Kuachana
MLO wa ukumbusho umemalizika, lakini Yesu na mitume wake wangali katika chumba cha juu ghorofani. Ingawa punde si punde Yesu atakuwa hayupo, bado yeye ana mambo mengi ya kusema. “Msifadhaike mioyoni mwenu,” yeye awafariji. “Mnamwamini Mungu [jizoezeni imani katika Mungu, NW].” Lakini mengi zaidi yatakwa. “Niaminini na mimi,” yeye aongezea.
“Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi,” Yesu aendelea kusema hivyo. “Naenda kuwaandalia mahali . . . ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.” Mitume hawafahamu kwamba Yesu aongea juu ya kwenda zake mbinguni, kwa hiyo Tomaso auliza: “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?”
“Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima,” Yesu ajibu. Ndiyo, kukubali na kuiga mwendo wake wa maisha ndiyo njia pekee tu ambavyo mtu yeyote aweza kuingia katika nyumba ya kimbingu ya Baba kwa sababu, kama vile Yesu asemavyo: “Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”
“Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha,” Filipo atoa ombi hilo. Yaonekana Filipo ataka Yesu aandae udhihirisho wenye kuonekana kuhusu Mungu, kama ule uliotolewa nyakati za kale katika njozi kwa Musa, Eliya, na Isaya. Lakini, kwa kweli, mitume wana kitu fulani kilicho bora sana kuliko njozi za namna hiyo, kama vile Yesu aoneleavyo: “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba [pia, NW].”
Yesu aonyesha utu wa Baba yake kwa ukamilifu sana hivi kwamba kuishi pamoja naye na kumchungua ni kama kumwona Baba kikweli. Hata hivyo, Baba ni mkuu kuliko Mwana, kama vile Yesu akirivyo: “Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu.” Kwa kufaa Yesu ampa Baba yake wa kimbingu sifa yote kwa mafundisho yake.
Ni lazima iwe yawatia moyo sana mitume kumsikia Yesu sasa akiwaambia hivi: “Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya”! Yesu hamaanishi kwamba wafuasi wake watajizoeza nguvu za kimwujiza zilizo kubwa kuliko zile ambazo yeye alijizoeza. Sivyo, bali amaanisha kwamba wataendesha huduma kwa muda mrefu zaidi, katika eneo kubwa zaidi, na kwa watu wengi zaidi.
Yesu hatawaacha wanafunzi wake baada ya kuondoka kwake. “Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu,” yeye aahidi, “nitalifanya.” Zaidi ya hilo, asema hivi: “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli [roho ya kweli, NW].” Baadaye, akiisha kupaa mbinguni, Yesu amimina juu ya wanafunzi wake ile roho takatifu, msaidiaji huyu mwingine.
Kuondoka kwa Yesu ku karibu, kwa maana asema hivi: “Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena.” Yesu atakuwa kiumbe roho asiyeweza kuonwa na binadamu yeyote. Lakini Yesu awaahidi tena mitume wake waaminifu hivi: “Ninyi mnaniona . . . kwa sababu mimi ni hai, [na] ninyi nanyi mtakuwa hai.” Ndiyo, si kwamba tu Yesu atawatokea kwa umbo la kibinadamu baada ya ufufuo wake bali pia atawafufua wakati uwadiapo ili wawe pamoja naye kwenye uhai mbinguni wakiwa viumbe roho.
Sasa Yesu ataarifu ile kanuni sahili: “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
Hapo mtume Yuda, yule aitwaye pia Thadayo, akatiza hivi: “Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu?”
“Mtu [yeyote, NW] akinipenda,” Yesu ajibu, “atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda . . . Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu.” Tofauti na wafuasi wake watiifu, ulimwengu hupuuza mafundisho ya Kristo. Kwa hiyo yeye hajifunui kwao.
Wakati wa huduma yake ya kidunia, Yesu amefundisha mitume wake mambo mengi. Watayakumbukaje yote, hasa kwa kuwa akili zao zashindwa kushika mengi sana, hata kufikia sasa? La kufurahisha ni kwamba, Yesu aahidi hivi: “Huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu [roho takatifu, NW], ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”
Akiwafariji tena, Yesu asema hivi: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa . . . Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Kweli Yesu anaondoka, lakini aeleza hivi: “Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.”
Wakati wa Yesu unaobaki wa kuwa pamoja nao ni mfupi. “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena,” yeye asema, “kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu [hanidhibiti, NW].” Shetani Ibilisi, yeye aliyeweza kumwingia Yuda na kumdhibiti, ndiye mtawala wa ulimwengu. Lakini katika Yesu hamna udhaifu wowote wenye dhambi ambao Shetani aweza kutumia-tumia ili amgeuze asitumikie Mungu. Yohana 14:1-31; 13:27; Luka 22:3, 4; Kutoka 24:10; 1 Wafalme 19:9-13; Isaya 6:1-5, NW.
◼ Yesu anaenda wapi, na Tomaso apokea jibu gani kuhusu njia ya kwenda huko?
◼ Kwa ombi lake, yaonekana Filipo ataka Yesu aandae nini?
◼ Kwa nini mtu ambaye ameona Yesu ameona Baba pia?
◼ Ni jinsi gani wafuasi wa Yesu hufanya kazi kubwa kuliko zile alizofanya yeye?
◼ Ni katika maana gani Shetani hana kitu kwa Yesu?