Kitabu Cha Biblia Namba 43—Yohana
Mwandikaji: Mtume Yohana
Mahali Kilipoandikiwa: Efeso au karibu
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 98 W.K.
Wakati Uliohusishwa: Baada ya dibaji, 29–33 W.K.
1. Maandiko yaonyesha nini juu ya ukaribiano wa ushirika wa Yohana na Yesu?
MAANDISHI ya Gospeli (Injili) za Mathayo, Marko, na Luka yalikuwa yamezunguka kwa miaka zaidi ya 30 nayo yalikuwa yamekuja kuonwa na Wakristo wa karne ya kwanza kuwa hazina iliyo kazi za wanaume waliopuliziwa na Mungu na roho takatifu. Sasa, kumalizika kwa karne kukikaribia na hesabu ya wale waliokuwa wamekuwa na Yesu ikipungua, yawezekana swali hili liliulizwa, Je! kungali kulikuwa jambo la kusimuliwa? Je! bado kulikuwa mtu fulani ambaye angeweza, kutoka kwa kumbukumbu za kibinafsi, kujazia mambo yenye thamani ya huduma ya Yesu? Ndiyo. Yohana mzee-mzee alikuwa amebarikiwa kibinafsi kwa ushirika wake na Yesu. Ni wazi yeye alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza wa Yohana Mbatizaji kujulishwa kwa Mwana-Kondoo wa Mungu na mmoja wa wale wanne wa kwanza kualikwa na Bwana wajiunge naye wakati wote katika huduma. (Yn. 1:35-39; Mk. 1:16-20) Yeye aliendelea katika ushirika wa karibu na Yesu katika huduma yake yote, naye alikuwa mwanafunzi “ambaye Yesu alimpenda” aliyeegemea mbele ya kifua cha Yesu katika Kupitwa ya mwisho. (Yn. 13:23; Mt. 17:1; Mk. 5:37; 14:33) Yeye alikuwako kwenye lile tukio lenye kuvunja moyo la uuaji, ambapo Yesu alimkabidhi uangalizi wa mama Yake wa kimwili, na ndiye aliyekimbia haraka zaidi ya Petro walipotimua mbio kwenda kwenye kaburi wakapeleleze ripoti ya kwamba Yesu alikuwa ameinuka.—Yn. 19:26, 27; 20:2-4.
2. Yohana alitayarishwaje na kutiwa nguvu ili aandike Gospeli yake, na kwa kusudi gani?
2 Akiwa amekomazwa na miaka karibu 70 katika huduma yenye kitendo na kwa kuimarishwa na njozi na matafakario yake ya kufungwa gerezani kwenye upweke kwa hivi karibuni kwenye kisiwa cha Patmo, Yohana alikuwa ametayarishwa vizuri kuandika mambo ambayo alikuwa ameyaweka kuwa hazina moyoni mwake kwa muda mrefu. Roho takatifu sasa ilitia nguvu akili yake ikumbuke na kuandika nyingi za semi zile zenye thamani, zenye kutoa uhai ili kila mmoja mwenye kusoma ‘aamini kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini awe na uzima kwa jina lake.’—20:31.
3, 4. Ni nini uthibitisho wa nje na wa ndani wa (a) kukubalika kwa Gospeli hii, na (b) Uandikaji wa Yohana?
3 Wakristo wa mapema katika karne ya pili walikubali Yohana kuwa mwandikaji wa simulizi hili na pia waliyachukua maandishi haya kuwa sehemu isiyotiliwa shaka ya vitabu vinavyokubaliwa vya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu. Clement wa Aleksandria, Irenaeus, Tertullian, na Origen, wote ambao walikuwa wa mwisho-mwisho wa karne ya pili na mapema karne ya tatu, washuhudia uandikaji wa Yohana. Zaidi ya hayo, uthibitisho mwingi wa ndani kwamba Yohana alikuwa ndiye mwandikaji wapatikana katika kitabu chenyewe. Kwa wazi mwandikaji alikuwa Myahudi na alizoeana sana na desturi za Kiyahudi na bara lao. (2:6; 4:5; 5:2; 10:22, 23) Ile hali ya kindani yenyewe ya simulizi hilo yaonyesha kwamba yeye hakuwa mtume tu bali mmoja wa wale watatu wa karibu zaidi—Petro, Yakobo, na Yohana—walioambatana na Yesu kwenye pindi za pekee. (Mt. 17:1; Mk. 5:37; 14:33) Kati ya hao, Yakobo (mwana wa Zebedayo) hawezi kuwa ndiye kwa sababu yeye aliuawa na Herode Agripa 1 kwa ajili ya imani yake karibu 44 W.K., muda mrefu kabla ya kitabu hiki kuandikwa. (Mdo. 12:2) Petro hawezi kuwa ndiye kwa sababu atajwa akiandamana na mwandikaji katika Yohana 21:20-24.
4 Katika mistari hii ya kumalizia, mwandikaji arejezewa kuwa mwanafunzi “aliyependwa na Yesu,” uneni huo na mwingine kama huo watumiwa mara kadhaa katika maandishi haya, ingawa jina la mtume Yohana halitajwi kamwe. Hapa Yesu anukuliwa kuwa akisema juu yake: “Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?” (Yn. 21:20, 22) Hilo laonyesha kwamba mwanafunzi anayerejezewa angeliishi muda mrefu kuliko Petro na wale mitume wengine. Yote haya yamfaa mtume Yohana. Yapendeza kwamba Yohana, baada ya kupewa njozi ya Ufunuo ya kuja kwa Yesu, amalizia unabii huo wenye kutokeza kwa maneno haya: “Amina; na uje, Bwana Yesu.”—Ufu. 22:20.
5. Yaaminiwa Yohana aliandika Gospeli yake lini?
5 Ingawa maandishi ya Yohana yenyewe hayatoi habari kamili juu ya jambo hilo, kwa ujumla huaminiwa kwamba Yohana aliandika Gospeli yake baada ya kurejea kwake kutoka uhamisho katika kisiwa cha Patmo. (Ufu. 1:9) Maliki Mrumi Nerva, 96-98 W.K., aliita tena wengi waliokuwa wamehamishwa mwishoni mwa utawala wa mtangulizi wake, Domitian. Baada ya kuandika Gospeli yake, karibu 98 W.K., yaaminiwa Yohana alikufa kwa amani kule Efeso katika mwaka wa tatu wa Maliki Trajan, 100 W.K.
6. Ni uthibitisho gani unaoonyesha kwamba Gospeli ya Yohana iliandikiwa nje ya Palestina, katika Efeso au karibu hapo?
6 Juu ya Efeso au ujirani walo kuwa mahali pa uandikiaji, mwanahistoria Eusebio (c. 260-342 W.K.) anakili Irenaeus akisema: “Yohana, mwanafunzi wa Bwana, ambaye hata alikuwa amepumzika juu ya kifua chake, mwenyewe pia alitoa gospeli hii, alipokuwa akiishi kule Efeso katika Asia.”a Kwamba kitabu hicho kiliandikwa nje ya Palestina yaungwa mkono na marejezo yacho mengi juu ya wapinzani wa Yesu kwa namna ya ujumla, “Wayahudi,” badala ya “Mafarisayo,” “makuhani wakuu,” na kadhalika. (Yn. 1:19; 12:9) Pia, Bahari ya Galilaya yaelezwa kwa jina yalo ya Kirumi, Bahari ya Tiberia. (6:1; 21:1) Kwa ajili ya wasio Wayahudi, Yohana atoa maelezo yenye msaada ya miadhimisho ya Kiyahudi. (6:4; 7:2; 11:55) Mahali pa uhamisho wake, Patmo, palikuwa karibu na Efeso, na kuzoeana kwake na Efeso, na pia makundi mengine ya Asia Ndogo, kwaonyeshwa na Ufunuo sura za 2 na 3.
7. Papyrus Rylands 457 ina umaana gani?
7 Yenye kuthibitisha uasilia wa Gospeli ya Yohana ni mavumbuzi ya hati zenye maana ya karne ya 20. Moja yazo ni kipande cha Gospeli ya Yohana kilichopatikana Misri, kinachojulikana sasa kuwa Papyrus Rylands 457 (P52), chenye Yohana 18:31-33, 37, 38, na kilichohifadhiwa katika Maktaba ya John Rylands, Manchester, Uingereza.b Kuhusu kuthibitisha kwacho juu ya ukale wa uandikaji wa Yohana mwishoni mwa karne ya kwanza, Sir Frederic Kenyon aliyeaga alisema hivi katika kitabu chake The Bible and Modern Scholarship, 1949, ukurasa 21: “Kijapokuwa kidogo hivyo, chatosha kutoa uthibitisho kwamba hati ya Gospeli hii ilikuwa ikizunguka, yawezekana katika mkoa wa Misri kilikopatikana, karibu na kipindi A.D. 130-150. Hata kuruhusu wakati mchache zaidi wa mzunguko wa kazi hiyo toka mahali payo pa asilia, hilo lingerudisha tarehe ya mtungo huo karibu sana na tarehe ya kale katika miaka kumi ya mwisho ya karne ya kwanza hivi kwamba hakuna tena sababu yoyote ya kutilia shaka ukweli wa mapokeo hayo.”
8. (a) Ni nini chenye kutokeza juu ya utangulizi wa Gospeli ya Yohana? (b) Inathibitishaje kwamba huduma ya Yesu ilikuwa na urefu wa miaka mitatu na nusu?
8 Gospeli ya Yohana yatokeza kwa ajili ya utangulizi wayo, unaofunua Neno, ambaye “alikuwa mwanzoni pamoja na Mungu,” kuwa Yeye ambaye kupitia kwake vitu vyote vilikuja kuwapo. (1:2, NW) Baada ya kujulisha uhusiano wenye thamani kati ya Baba na Mwana, Yohana aingilia uonyeshaji wa ustadi wa kazi na hotuba za Yesu, hasa kwa maoni ya upendo wa karibu sana unaofungamanisha katika umoja kila kitu katika mpango mkuu wa Mungu. Simulizi hili la uhai wa Yesu duniani lahusu kipindi cha 29-33 W.K., na lafanya uangalifu kutaja Kupitwa nne ambazo Yesu alihudhuria wakati wa huduma yake, hivyo kutoa moja ya vithibitisho vya kwamba huduma yake ilikuwa ya urefu wa miaka mitatu na nusu. Tatu kati ya Kupitwa hizo zatajwa hivyo. (2:13; 6:4; 12:1; 13:1) Moja yarejezewa kuwa “sikukuu ya Wayahudi,” lakini muktadha (habari inayozunguka) waiweka muda mfupi baada ya Yesu kusema “bado miezi minne, ndipo yaja mavuno,” hivyo kuonyesha mwadhimisho huo ni Kupitwa, iliyokuja karibu na mwanzo wa mavuno.—4:35; 5:1.c
9. Ni nini kinachoonyesha Gospeli ya Yohana ni ujazio, na hata hivyo je! inajazia habari zote za huduma ya Yesu?
9 Habari njema “kulingana na Yohana” kwa sehemu kubwa ni ujazio; asilimia 92 ni habari mpya isiyokuwamo katika zile Gospeli tatu nyingine. Hata hivyo, Yohana amalizia kwa maneno haya: “Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.”—21:25.
YALIYOMO KATIKA YOHANA
10. Yohana asema nini juu ya “Neno”?
10 Dibaji: Kujulisha yule “Neno” (1:1-18). Kwa maneno rahisi yenye kupendeza, Yohana aeleza kwamba hapo mwanzo “Neno alikuwako kwa [pamoja na, NW] Mungu,” kwamba uhai wenyewe ulikuwa kupitia kwake, kwamba yeye alikuja kuwa “nuru ya watu,” na kwamba Yohana (Mbatizaji) alitoa ushahidi juu yake. (1:1, 4) Nuru alikuwa katika ulimwengu, lakini ulimwengu haukumjua. Wale waliompokea wakawa watoto wa Mungu, waliozaliwa kutoka kwa Mungu. Sawa na ambavyo Sheria ilitolewa kupitia Musa, ndivyo “neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.”—1:17.
11. Yohana Mbatizaji atambulisha Yesu kuwa nini, nao wanafunzi wa Yohana wamkubali Yesu kuwa nani?
11 Kumtokeza “Mwana-kondoo wa Mungu” kwa watu (1:19-51). Yohana Mbatizaji aungama yeye siye Kristo bali asema kwamba kuna mmoja anayekuja nyuma yake, na gidamu (kamba) ya kiatu chake hastahili kuilegeza. Siku ifuatayo, Yesu akija aliko, Yohana amtambulisha kuwa “Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” (1:27, 29) Kisha, atanguliza wawili wa wanafunzi wake kwa Yesu, na mmoja wao, Andrea, aleta ndugu yake Petro kwa Yesu. Filipo na Nathanaeli pia wamkubali Yesu kuwa ‘Mwana wa Mungu, Mfalme wa Israeli.’—1:49.
12. (a) Mwujiza wa kwanza wa Yesu ni upi? (b) Yeye afanya nini akiwa kule Yerusalemu kwa ajili ya Kupitwa ya kwanza wakati wa huduma yake?
12 Miujiza ya Yesu yathibitisha kuwa yeye ndiye “Mtakatifu wa Mungu” (2:1–6:71). Yesu afanya mwujiza wake wa kwanza katika Kana ya Galilaya, akigeuza maji kuwa divai bora zaidi katika karamu ya arusi. Huo ndio ‘mwanzo wa ishara zake, nao wanafunzi wake wamwamini.’ (2:11) Yesu akwea kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Kupitwa. Akutapo wachuuzi na wabadilisha-pesa katika hekalu, achukua mjeledi na kuwafukuza kwa juhudi nyingi hivi kwamba wanafunzi wake watambua utimizo wa unabii huu: “Wivu wa nyumba yako utanila.” (Yn. 2:17; Zab. 69:9) Yeye atabiri kwamba hekalu la mwili wake mwenyewe litabomolewa na kuinuliwa tena katika siku tatu.
13. (a) Yesu aonyesha nini kuwa cha lazima ili kupata uhai? (b) Yohana Mbatizaji anenaje juu yake mwenyewe kuhusiana na Yesu?
13 Nikodemo mwenye hofu amjia Yesu usiku. Aungama kwamba Yesu amepelekwa na Mungu, na Yesu amwambia kwamba ni lazima mtu azaliwe kutoka kwa maji na roho ili auingie Ufalme wa Mungu. Kuamini Mwana wa Adamu kutoka mbinguni ni kwa lazima kwa ajili ya uhai. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yn. 3:16) Nuru ambayo imekuja ulimwenguni yapingana na giza, “bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru,” amalizia Yesu. Kisha Yohana Mbatizaji ajua juu ya utendaji wa Yesu katika Yudea na kujulisha rasmi kwamba ingawa yeye mwenyewe siye Kristo, “lakini rafiki yake bwana arusi . . . aifurahia sana sauti yake bwana arusi.” (3:21, 29) Sasa lazima Yesu aongezeke, na Yohana kupungua.
14. Yesu aeleza nini mwanamke Msamaria kule Sikari, na tokeo la kuhubiri kwake huko ni nini?
14 Yesu afunga tena safari ya kwenda Galilaya. Akiwa njiani, amejaa vumbi na ‘kuchoka kwa safari yake,’ aketi ili apumzike kwenye chemchemi ya Yakobo katika Sikari, huku wanafunzi wake wakiwa wameenda zao kununua chakula katika jiji. (4:6) Ni mchana-kati, saa sita. Mwanamke mmoja Msamaria akaribia ili ateke maji, na Yesu aomba kinywaji. Kisha, ajapokuwa amechoka, aanza kunena naye juu ya “maji” ya kweli kweli yanayoburudisha kikweli, yakitoa uhai wa milele kwa wale wanaoabudu Mungu “katika roho na kweli.” Wanafunzi warejea na kumsihi ale, naye ajulisha rasmi hivi: “Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.” Atumia siku mbili zaidi katika eneo hilo, hivi kwamba Wasamaria wengi waja kuamini kwamba “hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.” (4:24, 34, 42) Afikapo Kana ya Galilaya, Yesu aponya mwana wa mkuu bila ya hata kwenda karibu na kitanda chake.
15. Ni mashtaka gani yanayoletwa juu ya Yesu katika Yerusalemu, lakini yeye awajibuje wachambuzi wake?
15 Yesu aenda tena Yerusalemu kwa ajili ya mwadhimisho wa Wayahudi. Aponya mwanamume mgonjwa siku ya Sabato, na hilo latokeza uchambuzi mwingi. Yesu ajitetea hivi: “Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi.” (5:17) Viongozi Wayahudi sasa wadai kwamba Yesu ameongeza kufuru, lile la kujifanya alingana na Mungu, kwenye uhalifu wa kuvunja Sabato. Yesu ajibu kwamba Mwana hawezi kufanya jambo hata moja la kujitanguliza bali ategemea kabisa Baba. Atoa taarifa hii ya ajabu kwamba “wote waliomo makaburini [ya ukumbusho, NW] watasikia sauti yake. Nao watatoka” kwa ufufuo. Lakini kwa wasikilizaji wake wasio na imani, Yesu asema: “Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?”—5:28, 29, 44.
16. (a) Yesu afundisha nini kuhusu chakula na uhai? (b) Petro aelezaje usadikisho wa mitume?
16 Yesu alishapo kimwujiza wanaume 5,000 kwa boflo (mikate) tano na samaki wawili wadogo, umati wafikiria kumkamata na kumfanya mfalme, lakini yeye aenda zake kwenye mlima. Baadaye, awakaripia kwa kufuatia “chakula chenye kuharibika.” Badala yake, wapaswa kufanyia kazi “chakula kidumucho hata uzima wa milele.” Ataja kwamba kuzoea imani katika yeye akiwa Mwana ni kushiriki mkate wa uhai, naye aongeza hivi: “Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.” Wengi wa wanafunzi wake wachukizwa na hilo na kumwacha. Yesu awauliza wale 12: “Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka?” na Petro ajibu: “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.” (6:27, 53, 67-69) Hata hivyo, Yesu, akijua kwamba Yuda atamsaliti, asema kwamba mmoja wao ni mchongezi.
17. Fundisho la Yesu katika hekalu kwenye Mwadhimisho wa Vibanda lawa na tokeo gani?
17 “Nuru” yapingana na giza (7:1–12:50). Yesu akwea kisiri mpaka Yerusalemu na kujitokeza Mwadhimisho wa Vibanda ukiwa umeendelea nusu ya wakati wake, akifundisha waziwazi katika hekalu. Watu wabishana juu ya kama yeye ndiye Kristo kweli kweli. Yesu awaambia: “Sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, . . . naye ndiye aliyenituma.” Katika pindi nyingine apaaza sauti hivi kwa umati: “Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.” Maofisa wanaotumwa wakamkamate Yesu warudi mikono mitupu na kuripoti kwa makuhani hivi: “Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena.” Wakiwa wamefoka kwa hasira, Mafarisayo wajibu kwamba hakuna yeyote wa watawala ameamini, wala hakuna nabii atakayeinuliwa kutoka Galilaya.—7:28, 29, 37, 46.
18. Wayahudi waleta upinzani gani juu ya Yesu, naye ajibuje?
18 Katika uneni mwingine, Yesu asema: “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu.” Kuhusu mashtaka yenye nia mbaya kwamba yeye ni shahidi bandia, kwamba amezaliwa nje ya ndoa, na kwamba yeye ni Msamaria na mtu aliyepagawa na roho waovu, Yesu ajibu hivi kwa mkazo: “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu.” Ajulishapo rasmi, “Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko,” Wayahudi wafanya jaribio jingine linaloshindwa la kumwua. (8:12, 54, 58) Wakiwa wameshindwa, baadaye wauliza maswali mwanamume ambaye amerudishiwa kuona kwake kimwujiza na Yesu, nao wamtupa nje mtu huyo.
19. (a) Yesu anenaje juu ya uhusiano wake na Baba yake na uangalizi wake wa kondoo zake? (b) Yeye ajibuje Wayahudi wanapomtisha?
19 Kwa mara nyingine Yesu anena na Wayahudi, wakati huu kuhusu yule mchungaji mwema, anayeita kondoo zake kwa jina na anayetoa nafsi yake kwa ajili ya kondoo ‘ili wawe na uhai tele.’ Yeye asema: “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.” (10:10, 16) Awaambia Wayahudi kwamba hakuna anayeweza kunyakua kondoo kutoka mkono wa Baba yake, naye asema kwamba yeye na Baba yake wana umoja. Kwa mara nyingine watafuta kumpiga kwa mawe afe. Katika kujibu shtaka lao la kufuru, awakumbusha kwamba katika kitabu cha Zaburi, watu fulani hodari wa dunia warejezewa kuwa “miungu,” ambapo yeye amejirejezea kuwa Mwana wa Mungu. (Zab. 82:6) Yeye awahimiza angalau waamini kazi zake.—Yn. 10:34.
20. (a) Kisha Yesu afanya mwujiza gani wenye kutokeza? (b) Hilo laongoza kwenye nini?
20 Kutoka Bethania karibu na Yerusalemu zaja habari kwamba Lazaro, ndugu ya Mariamu na Martha, ameugua. Yesu afikapo huko, Lazaro amekufa na tayari amekuwa ndani ya kaburi siku nne. Yesu afanya mwujiza mkubwa wa kumwita Lazaro kwenye uhai tena, akisababisha wengi watie imani katika Yesu. Hilo lachochea mkutano wa pekee wa Sanhedrini, ambako kuhani wa juu, Kayafa, alazimika kutabiri kwamba Yesu aelekea kufa kwa ajili ya taifa hilo. Makuhani wakuu na Mafarisayo wanapofanya shauri la kumwua, Yesu ajiondoa hadharani kwa muda.
21. (a) Watu na Mafarisayo waitikiaje mwingio wa Yesu katika Yerusalemu? (b) Ni kielezi gani anachotoa Yesu kuhusu kifo chake na kusudi lacho, naye ahimiza nini wasikiaji wake?
21 Siku sita kabla ya Kupitwa, Yesu aja tena Bethania akiwa njiani kwenda Yerusalemu, naye aburudishwa na watu wa nyumba ya Lazaro. Kisha, siku inayofuata baada ya Sabato, Nisani 9, akiwa ameketi juu ya punda mchanga, aingia Yerusalemu kwa vigelegele vya umati mkubwa; na Mafarisayo waambiana: “Mwaona kwamba hamfai neno lo lote; tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake.” Kwa kielezi cha punje ya ngano, Yesu aonyesha kwamba ni lazima apandwe katika kifo kusudi matunda yazaliwe kwa ajili ya uhai wa milele. Atoa wito kwa Baba yake atukuze jina Lake, na sauti yasikiwa kutoka mbinguni: “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” Yesu awahimiza wasikiaji wake waepuke giza na kutembea katika nuru, ndiyo, wawe “wana wa nuru.” Nguvu za giza zinapomkaribia, asihi hadharani kwa nguvu kuwa watu watie imani katika yeye ‘akiwa nuru iliyokuja ulimwenguni.’—12:19, 28, 36, 46.
22. Ni kigezo gani anachotoa Yesu kwenye mlo wa Kupitwa, na ni amri gani mpya anayotoa?
22 Maneno ya Yesu ya kuaga mitume waaminifu (13:1–16:33). Chakula cha jioni cha Sikukuu-Kupitwa pamoja na wale 12 kikiwa chaendelea, Yesu ainuka na, avua mavazi yake ya nje, atwaa taulo (kitambaa) na karai (bakuli) ya miguu na kuanza kuosha miguu ya wanafunzi wake. Petro apinga, lakini Yesu amwambia lazima yeye pia aoshwe miguu. Yesu aonya kwa upole wanafunzi wake wafuate kigezo chake cha unyenyekevu, kwa maana “mtumwa si mkuu kuliko bwana wake.” Anena juu ya msaliti na kisha amfukuza Yuda. Baada ya Yuda kwenda nje, Yesu aanza kunena kwa kuwafunulia ya moyoni wale wengine. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”—13:16, 34, 35.
23. Ili kuwa kitulizo, Yesu azungumza juu ya tumaini gani na msaidizi gani aliyeahidiwa?
23 Yesu anena maneno ya ajabu ya kufariji wafuasi wake katika saa hii ya hatari. Ni lazima wazoee imani katika Mungu na pia katika yeye. Katika nyumba ya Baba yake, kuna makao mengi, naye atakuja tena na kuwapokea nyumbani kwake. “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima,” asema Yesu. “Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Kwa kufariji aeleza wafuasi wake kwamba kwa kuzoea imani, watafanya kazi kubwa zaidi yake na kwamba atatoa chochote wanachoomba katika jina lake, ili kwamba Baba yake atukuzwe. Yeye awaahidi msaidizi mwingine, “roho wa [ya, NW] kweli,” itakayowafundisha mambo yote na kurudisha akilini mwao yote ambayo amewaambia. Wapaswa kuona shangwe kwamba yeye aenda zake kwa Baba yake, kwa maana, asema Yesu, “Baba ni mkuu kuliko mimi.”—14:6, 17, 28.
24. Yesu azungumzaje juu ya uhusiano wa mitume na yeye mwenyewe na Baba, na baraka zikiwa nini kwao?
24 Yesu anena juu yake mwenyewe kuwa ndiye mzabibu wa kweli na Baba yake kuwa ndiye mpandaji wa huo. Yeye awahimiza wabaki katika umoja naye, akisema: “Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.” (15:8) Nayo shangwe yao yaweza kujaa jinsi gani? Kwa kupendana sawa na alivyokuwa amewapenda. Yeye awaita marafiki. Jinsi huo ulivyo uhusiano wenye thamani! Ulimwengu utawachukia sawa na ulivyokuwa umemchukia, nao utawanyanyasa, lakini Yesu atatuma msaidizi ili kutoa ushahidi juu yake na kuwaongoza wanafunzi wake kwenye ukweli wote. Mahali pa huzuni yao ya wakati huu patachukuliwa na shangwe awaonapo tena, na hakuna atakayetwaa shangwe yao kutoka kwao. Maneno yake ni yenye kutuliza: “Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba.” Ndiyo, watatawanywa, lakini, Yesu asema hivi, “hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”—16:27, 33.
25. (a) Yesu akiri nini katika sala kwa Baba yake? (b) Yeye aomba nini kuhusu yeye mwenyewe, wanafunzi wake, na wale ambao watazoea imani kupitia neno lao?
25 Sala ya Yesu kwa ajili ya wanafunzi wake (17:1-26). Katika sala Yesu akiri hivi kwa Baba yake: “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.” Akiwa amekwisha maliza kazi aliyogawiwa duniani, Yesu sasa aomba atukuzwe kando ya Baba yake kwa utukufu ule aliokuwa nao kabla ya ulimwengu kuwapo. Amedhihirisha jina la Baba kwa wanafunzi wake na aomba Baba awalinde wao ‘kwa jina lake.’ Aomba Baba, si kwamba awatoe ulimwenguni, bali awatunze kutokana na yule mwovu na kuwatakasa kupitia neno Lake la ukweli. Yesu apanua sala yake itie ndani wale wote ambao bado watazoea imani kupitia kusikia neno la wanafunzi hawa, “wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” Aomba pia hao waweze kushiriki pamoja naye katika utukufu wake wa kimbingu, kwa maana yeye amejulisha jina la Baba kwao, ili kwamba upendo Wake ukae ndani yao.—17:3, 11, 21.
26. Simulizi hilo lasema nini kuhusu kukamatwa na kujaribiwa kwa Yesu?
26 Kristo ajaribiwa na kutundikwa (18:1–19:42). Yesu na wanafunzi wake sasa waenda kwenye bustani moja ng’ambo ya Bonde Kidroni. Hapa ndipo Yuda ajitokeza akiwa na kikosi cha askari na kumsaliti Yesu, ambaye kwa upole anyenyekea. Hata hivyo, Petro amkinga kwa upanga naye akaripiwa hivi: “Je! kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” (18:11) Kisha Yesu apelekwa amefungwa kwa Anasi, baba-mkwe wa Kayafa, kuhani wa juu. Yohana na Petro wawaandamia karibu, na Yohana awawezesha waingie kwenye ua wa kuhani wa juu, ambapo mara tatu Petro akana hajui Kristo. Yesu aulizwa maswali kwanza na Anasi na kisha aletwa mbele ya Kayafa. Baadaye, Yesu aletwa mbele ya Pilato, liwali Mrumi, huku Wayahudi wakifanya ghasia apewe hukumu ya kifo.
27. (a) Ni maswali gani kuhusu ufalme na mamlaka yatokezwa na Pilato, na Yesu aelezaje? (b) Wayahudi wachukua msimamo gani juu ya ufalme?
27 Kwa swali la Pilato, “Wewe u Mfalme?” Yesu ajibu: “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli.” (18:37) Kwa kukosa kuona uthibitisho wowote halisi juu ya Yesu, Pilato ataka kumwachilia, kwa kuwa ilikuwa desturi kuweka huru mfungwa fulani wakati wa Kupitwa, lakini Wayahudi watoa wito kwa ajili ya Baraba badala yake. Pilato aamuru Yesu apigwe mijeledi, na tena ajaribu kumwachilia, lakini Wayahudi wapaaza sauti hivi: “Msulubishe [Mtundike, NW]! Msulubishe [Mtundike, NW]! . . . kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.” Pilato amwambiapo Yesu ana mamlaka ya kumtundika, Yesu ajibu: “Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu.” Kwa mara nyingine Wayahudi wapaaza sauti hivi: “Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe [Mtundike, NW]! . . . Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.” Kisha, Pilato amkabidhi akatundikwe.—19:6, 7, 11, 15.
28. Ni nini kinachotukia Golgotha, na ni unabii gani mbalimbali unaotimizwa huko?
28 Yesu apelekwa “mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha,” na atundikwa katikati ya wengine wawili. Juu yake Pilato afungilia taji “YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI,” iliyoandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki, ili wote waone na kuelewa. (19:17, 19) Yesu akabidhi mama yake kwenye uangalizi wa Yohana na, baada ya kupokea siki kidogo, atamka hivi: “Imekwisha!” Kisha ainamisha kichwa chake na kukata roho. (19:30) Katika utimizo wa unabii mbalimbali, kikosi cha ufishaji chapigia kura mavazi yake, chaepuka kuvunja miguu yake, na chadunga ubavu wake kwa mkuki. (Yn. 19:24, 32-37; Zab. 22:18; 34:20; 22:17; Zek. 12:10) Baadaye, Yusufu wa Arimathaya na Nikodemo watayarisha mwili wake kwa ajili ya maziko na kuuweka ndani ya kaburi la ukumbusho jipya lililoko karibu.
29. (a) Ni mionekano gani anayofanya Yesu aliyefufuliwa kwa wanafunzi wake? (b) Ni mambo gani anayojulisha Yesu katika maelezo yake ya mwisho kwa Petro?
29 Mionekano ya Kristo aliyefufuliwa (20:1–21:25). Uthibitisho mwingi wa Yohana juu ya Kristo wamalizikia kwa furaha ya ufufuo. Mariamu Magdalene akuta kaburi likiwa tupu, na Petro na mwanafunzi mwingine (Yohana) watimua mbio huko lakini waona vitambaa vya sanda na kitambaa cha kichwa ndivyo vimebaki tu. Mariamu, ambaye amebaki karibu na kaburi, anena na malaika wawili na hatimaye, na mtunza bustani, kama anavyofikiri. Ajibupo, “Mariamu!” mara moja amtambua kuwa Yesu. Kisha, Yesu ajidhihirisha kwa wanafunzi wake nyuma ya milango iliyofungwa, naye awaambia juu ya uwezo watakaopokea kupitia roho takatifu. Baadaye, Tomaso, ambaye hakuwapo, akataa kuamini, lakini siku nane baadaye Yesu atokea tena na kumthibitishia, kisha Tomaso asema hivi kwa mshangao: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (20:16, 28) Siku kadhaa baadaye Yesu tena akutana na wanafunzi wake, kwenye Bahari ya Tiberia; afanya wavue samaki kimwujiza na kisha ala kiamsha-kinywa pamoja nao. Mara tatu auliza Petro kama ampenda. Petro asisitizapo kwamba ampenda, Yesu asema waziwazi: “Lisha wana-kondoo wangu,” “Chunga kondoo zangu,” “Lisha kondoo zangu.” Kisha atabiri ni kwa kifo cha aina gani Petro atatukuza Mungu. Petro auliza juu ya Yohana, na Yesu asema: “Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?”—21:15-17, 22.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
30. Yohana atiaje mkazo wa pekee kwa sifa ya upendo?
30 Kwa njia ya moja kwa moja kwa nguvu na kwa maono ya moyoni yenye kusadikisha, udhihirisho wenye kuchangamsha moyo wa yule Neno, ambaye alikuja kuwa Kristo, habari njema “kulingana na Yohana” yatupa maoni ya karibu ya huyu Mwana wa Mungu mpakwa mafuta katika neno na kitendo. Ingawa mtindo na msamiati wa Yohana ni rahisi, ikimtia alama kuwa ‘asiye na elimu na asiye na maarifa [wa kawaida, NW],’ uneni wake una nguvu kubwa. (Mdo. 4:13) Gospeli yake yafikia upeo kwa kujulisha upendo wa kindani sana kati ya Baba na Mwana, na pia uhusiano uliobarikiwa, wenye upendo unaopatikana kwa kuwa katika umoja nao. Yohana atumia maneno “upendo” na “-penda” mara nyingi zaidi ya Gospeli zile nyingine tatu zikiunganishwa.
31. Ni uhusiano gani unaokaziwa katika Gospeli yote ya Yohana, nao wafikiaje upeo wa wonyesho wayo?
31 Hapo mwanzo jinsi kulivyokuwako uhusiano mtukufu kati ya Neno na Mungu aliye Baba! Kwa hisani ya Mungu “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Yn. 1:14) Kisha, katika simulizi lote la Yohana, Yesu akazia uhusiano wake kuwa wa unyenyekeo katika utii usio na shaka kwa mapenzi ya Baba. (4:34; 5:19, 30; 7:16; 10:29, 30; 11:41, 42; 12:27, 49, 50; 14:10) Uneni wake wa huu uhusiano wa kindani wafikia upeo wao mtukufu katika sala yenye kugusa moyo iliyoandikwa katika Yohana sura ya 17, ambapo Yesu aripoti kwa Baba yake kwamba amemaliza kazi ambayo Yeye alimpa afanye duniani na kuongezea hivi: “Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.”—17:5.
32. Ni kwa uneni gani Yesu aonyesha uhusiano wake mwenyewe na wanafunzi wake na kwamba yeye ndiye kipitio pekee ambacho kwacho baraka za uhai zawajia ainabinadamu?
32 Vipi juu ya uhusiano wa Yesu na wanafunzi wake? Fungu la Yesu akiwa kipitio pekee ambacho kwacho baraka za Mungu zawafikia wao na ainabinadamu wote laendelea kutangulizwa. (14:13, 14; 15:16; 16:23, 24) Yeye arejezewa kuwa “Mwana-kondoo wa Mungu,” “chakula cha uzima,” “nuru ya ulimwengu,” “mchungaji mwema,” “ufufuo, na uzima,” “njia, na kweli, na uzima,” na “mzabibu wa kweli.” (1:29; 6:35; 8:12; 10:11; 11:25; 14:6; 15:1) Ni chini ya kielezi hiki cha “mzabibu wa kweli” kwamba Yesu ajulisha umoja wa ajabu uliopo si kati ya wafuasi wake wa kweli naye mwenyewe, bali pia pamoja na Baba. Kwa kuzaa matunda mengi, wao watatukuza Baba yake. “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu,” ashauri Yesu.—15:9.
33. Ni kusudi gani la huduma yake analoonyesha Yesu katika sala?
33 Kisha jinsi anavyosali kwa bidii kwa Yehova kwamba wapendwa wote hao, na ‘wanaomwamini kwa sababu ya neno lao,’ wawe na umoja na Baba yake na yeye mwenyewe, wakitakaswa kwa neno la ukweli! Hakika, kusudi lote la huduma ya Yesu laelezwa kiajabu katika maneno ya mwisho ya sala yake kwa Baba yake: “Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ile pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.”—17:20, 26.
34. Ni ushauri gani wenye mafaa aliotoa Yesu juu ya jinsi ya kuushinda ulimwengu?
34 Ingawa Yesu alikuwa akiwaacha wanafunzi wake katika ulimwengu, yeye hakuwa akiwaacha bila ya msaidizi, “roho wa [ya, NW] kweli.” Zaidi ya hayo, yeye aliwapa ushauri wa wakati unaofaa juu ya uhusiano wao na ulimwengu, akiwaonyesha jinsi ya kushinda wakiwa “wana wa nuru.” (14:16, 17; 3:19-21; 12:36) “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli,” akasema Yesu, “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Kinyume cha hilo, yeye aliwaambia hivi wana wa giza: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. . . . Hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake.” Basi, na tuazimie sikuzote kusimama imara katika kweli, ndiyo, ‘kuabudu Baba katika roho na kweli,’ na kupata nguvu kutokana na maneno haya ya Yesu: “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”—8:31, 32, 44; 4:23; 16:33.
35. (a) Ni ushuhuda gani anaotoa Yesu kuhusu Ufalme wa Mungu? (b) Ni kwa nini Gospeli ya Yohana yatoa sababu ya kuwa na furaha na shukrani?
35 Pia, yote hayo yana uhusiano na Ufalme wa Mungu. Yesu alishuhudia hivi alipokuwa katika hukumu: “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungalikuwa sehemu ya ulimwengu huu, wahudumu wangu wangalikuwa wamepiga vita kwamba nisitolewe nipewe kwa Wayahudi. Lakini, kama ilivyo, ufalme wangu si wa kutoka chanzo hiki.” Kisha, katika kujibu swali la Pilato, yeye alisema: “Wewe mwenyewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa ajili ya hili mimi nimezaliwa, na kwa ajili ya hili mimi nimekuja katika ulimwengu, kwamba nipaswe kutoa ushuhuda kwa ile kweli. Kila mtu ambaye yu upande wa ile kweli husikiliza sauti yangu.” (18:36, 37, NW) Kweli kweli wana furaha wale wanaosikiliza na ‘wanaozaliwa mara ya pili’ ili ‘waingie katika ufalme wa Mungu’ katika umoja na Mfalme. Wenye furaha ni “kondoo wengine” wanaosikiliza sauti ya Mfalme-Mchungaji huyu na kupata uhai. Hakika, kuna sababu ya kushukuru kwa ajili ya kutolewa kwa Gospeli ya Yohana, kwa maana iliandikwa “ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.”—3:3, 5; 10:16; 20:31.
[Maelezo ya Chini]
a The Ecclesiastical History, Eusebio, 5, VIII, 4.
b Insight on the Scriptures, Buku 1, ukurasa 323.
c Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 57-8.