Maisha na Huduma ya Yesu
Shauri Zaidi Wakati wa Kuachana
YESU na mitume wamejiandaa kuondoka kwenye chumba cha juu. “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa,” yeye aendelea kusema. Halafu atoa onyo hili zito: “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.”
Kwa wazi mitume wafadhaishwa kwa kina kirefu na onyo hili. Ingawa mapema kidogo Yesu alikuwa amesema kwamba ulimwengu ungewachukia, hakuwa amesema kwamba wangeuawa. “Sikuwaambia hayo tangu mwanzo,” Yesu aeleza, “kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.” Hata hivyo, ni vizuri kama nini kutangulia kuwazatiti kwa habari hiyo kabla hajaondoka!
“Lakini sasa,” Yesu aendelea kusema, “naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?” Mapema kidogo jioni hiyo, walikuwa wameuliza anaenda wapi, lakini sasa wametikiswa sana na lile ambalo amewaambia hivi kwamba washindwa kuuliza zaidi juu ya jambo hilo. Kama asemavyo Yesu: “Kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.” Mitume wana kihoro si kwa sababu tu wamejifunza kwamba watapatwa na mnyanyaso mbaya sana na kuuawa bali pia kwa sababu Bwana-Mkubwa wao anawaacha.
Hivyo basi Yesu aeleza: “Yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” Yesu aweza kuwa mahali pamoja tu kwa wakati mmoja, lakini awapo mbinguni, aweza kupeleka msaidizi, roho takatifu ya Mungu, kwa wafuasi wake popote walipo duniani. Hivyo basi kuondoka kwa Yesu kutakuwa na manufaa.
Yesu asema roho takatifu ‘itahakikishia ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.’ Dhambi ya ulimwengu, kushindwa kwao kujizoeza imani katika Mwana wa Mungu, itafichuliwa. Kwa kuongezea, ithibati yenye kusadikisha juu ya uadilifu wa Yesu itaonyeshwa kwa kupaa kwake kwenda kwa Baba. Na kushindwa kwa Shetani na ulimwengu wake mwovu kuvunja ukamilifu-maadili wa Yesu ni uthibitisho wenye kusadikisha kwamba mtawala wa ulimwengu amehukumiwa vikali.
“Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia,” Yesu aendelea kusema, “lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.” Kwa hiyo Yesu aahidi kwamba wakati amiminapo roho takatifu, ambayo ni kani ya utendaji ya Mungu, itawaongoza katika uelewevu wa mambo hayo kwa kulingana na uwezo wao wa kushika mambo.
Mitume washindwa kuelewa hususa kwamba Yesu atakufa halafu awatokee baada ya yeye kufufuliwa. Kwa hiyo wao waulizana hivi: “Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba?”
Yesu ang’amua kwamba wao wataka kumwuliza swali, kwa hiyo aeleza hivi: “Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.” Alasiri ifuatayo, wakati Yesu auawa, viongozi wa kidini walio walimwengu washangilia, lakini wanafunzi wana kihoro. Hata hivyo, kihoro chao chabadilika kuwa shangwe Yesu afufuliwapo! Na shangwe yao yae-ndelea awatiapo nguvu kwenye Pentekoste ili wawe mashahidi wake kwa kumimina roho takatifu ya Mungu juu yao!
Akilinganisha hali ya mitume na ile ya mwanamke wakati wa maumivu ya kuzaa, Yesu asema: “Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika.” Lakini kama vile yeye hakumbuki tena dhiki yake mtoto wake akiisha kuzaliwa, Yesu asema: “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena [nifufuliwapo]; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye.”
Kufikia wakati huu, mitume hawajapata kamwe kuomba mambo kwa jina la Yesu. Lakini sasa yeye asema: “Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. . . . Kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba [nilitoka nikiwa mwakilishi wa Baba, NW]. Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.”
Maneno ya Yesu ni kitia-moyo kikubwa kwa mitume. “Kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu,” wao wasema.
“Je! mnasadiki sasa?” Yesu auliza. “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu.” Ingawa huenda hilo likaonekana kama jambo lisiloaminika, latukia kabla ya usiku kwisha!
“Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu [kwa njia ya mimi, NW],” Yesu amalizia. “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yesu alishinda ulimwengu kwa kutimiza mapenzi ya Mungu kwa uaminifu japo kila jambo ambalo Shetani na ulimwengu wake walijaribu kufanya ili wavunje ukamilifu wa Yesu. Yohana 16:1-33; 13:36.
◼ Ni onyo gani la Yesu ambalo lafadhaisha mitume wake?
◼ Kwa nini mitume wameshindwa kumwuliza Yesu swali juu ya anakoenda?
◼ Ni jambo gani hususa ambalo mitume washindwa kuelewa?
◼ Yesu atoaje kielezi cha kwamba hali ya mitume itabadilika iache kuwa ya kihoro iwe ya shangwe?
◼ Yesu asema mitume watafanya nini karibuni?
◼ Yesu ashindaje ulimwengu?