SOMO LA 92
Yesu Awatokea Wavuvi
Muda fulani baada ya Yesu kuwatokea mitume, Petro aliamua kwenda kuvua samaki katika Bahari ya Galilaya. Tomasi, Yakobo, Yohana, na wanafunzi wengine wakaenda pamoja naye. Walijaribu kuvua samaki usiku kucha lakini hawakuvua chochote.
Mapema asubuhi iliyofuata, waliona mwanamume akiwa amesimama ufuoni. Akawauliza hivi akiwa ufuoni: ‘Je, mmepata samaki wowote?’ Wakamwambia, “Hapana!” Mwanamume huyo akasema, “Utupeni wavu upande wa kuume wa mashua.” Walipofanya hivyo, wavu ukajaa samaki wengi sana hivi kwamba hawakuweza kuuvuta. Mara moja Yohana akatambua kwamba mwanamume huyo alikuwa Yesu na kusema: “Ni Bwana!” Papo hapo, Petro akajitumbukiza ndani ya maji na kuogelea hadi ufuoni. Wanafunzi wengine wakamfuata kwa mashua.
Walipofika ufuoni, wakaona mkate na samaki vikipikwa juu ya moto. Yesu akawaambia walete baadhi ya samaki waliowavua wawaongezee kwenye mlo wao. Kisha akawaambia hivi: “Njooni, mpate kiamsha-kinywa.”
Baada ya kula kiamsha kinywa, Yesu akamuuliza hivi Petro: ‘Je, unanipenda kuliko unavyopenda kuvua samaki?’ Petro akasema, “Ndiyo, Bwana, unajua ninakupenda.” Yesu akamwambia, ‘Basi walishe wana-kondoo wangu.’ Yesu akamwuliza tena: ‘Petro, unanipenda?’ Petro akasema, ‘Bwana, unajua ninakupenda.’ Yesu akamwambia, “Chunga kondoo wangu wadogo.” Yesu akauliza mara ya tatu. Petro akahuzunika sana. Akasema, “Bwana, wewe unajua mambo yote; unajua kwamba ninakupenda.” Yesu akasema, “Lisha kondoo wangu wadogo.” Kisha akamwambia Petro hivi: “Endelea kunifuata.”
“[Yesu] akawaambia: ‘Nifuateni, nami nitawafanya muwe wavuvi wa watu.’ Mara moja wakaziacha nyavu zao wakamfuata.”—Mathayo 4:19, 20