Johari Kutoka Gospeli ya Yohana
ROHO ya Yehova ilivuvia mtume mzee Yohana kuandika usimulizi wa kuvutia juu ya maisha na huduma ya Yesu Kristo. Gospeli hii iliandikwa katika au karibu na Efeso yapata 98 W.K. Lakini usimulizi huo una hali gani? Ni nini baadhi ya johari zilizomo?
Sana-Sana Ni ya Kinyongeza
Yohana alikuwa mteuzi, naye hakurudia mengi ambayo Mathayo, Marko, na Luka waliandika. Kwa kweli, usimulizi wake wa kushuhudia kwa macho yake mwenyewe ni wa kinyongeza sana-sana katika maana ya kwamba zaidi ya asilimia 90 ya huo huzungumzia mambo yasiyotajwa katika Gospeli zile nyingine. Mathalani, yeye peke yake ndiye hutuambia juu ya kuwako kwa Yesu kabla hajawa mwanadamu na kwamba “Neno akawa mnofu.” (1:1-14, NW) Ingawa waandikaji wale wengine wa Gospeli husema kwamba Yesu alisafisha hekalu mwishoni mwa huduma yake, Yohana husema kwamba Kristo alifanya hivyo mwanzoni mwayo pia. (2:13-17) Mtume huyo mzee ndiye peke yake hutuambia juu ya miujiza fulani iliyofanywa na Yesu, kama vile kubadili maji yawe divai, kuinua Lazaro mfu, na vuo la kimuujiza la samaki baada ya ufufuo Wake.—2:1-11; 11:38-44; 21:4-14.
Waandikaji wote wa Gospeli husimulia jinsi Yesu alivyoanzisha Ukumbusho wa kifo chake, lakini ni Yohana peke yake ambaye huonyesha kwamba Kristo aliwapa mitume somo la unyenyekevu kwa kuosha miguu yao usiku huo. Tena, Yohana peke yake ndiye huzitia katika maandishi hotuba za moyo kwa moyo ambayo Yesu alitoa na sala aliyotoa kwa ajili yao wakati huo.—13:1–17:26.
Katika Gospeli hii, jina Yohana larejezea yule Mbatizaji, huku mwandikaji akijiita mwenyewe ‘mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda.’ (13:23) Kwa uhakika mtume huyo alimpenda Yesu, na upendo wetu wenyewe kwa Kristo waongezeka wakati Yohana amwonyeshapo kuwa yule Neno, mkate wa uhai, nuru ya ulimwengu, Mchungaji Mwema, ile njia, ile kweli, na ule uhai. (1:1-3, 14; 6:35; 8:12; 10:11; 14:6) Hilo latimiza kusudi lililotaarifiwa na Yohana: “Hizi (habari) zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.”—20:31.
Unyenyekevu na Shangwe
Gospeli ya Yohana hutoa utangulizi kujulisha Yesu kuwa Neno na Mwana-Kondoo mwenye kufanya upatanisho wa dhambi na hutaja miujiza inayothibitisha Yeye kuwa “Mtakatifu wa Mungu.” (1:1–9:41) Miongoni mwa mambo mengine, usimulizi huo wakazia unyenyekevu na shangwe ya Yohana Mbatizaji. Yeye alikuwa mtangulizi wa Kristo lakini alisema: “Mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu (makubazi, NW) chake.” (1:27) Makubazi yalifungwa kwa kanda za ngozi, au gidamu. Mtumwa angeweza kufungua gidamu za makubazi ya mtu mwingine na kumchukulia, kwa maana huo ulikuwa wajibu wa mtumishi wa kinyumbani. Hivyo Yohana Mbatizaji alionyesha unyenyekevu na ung’amuzi wa ukosefu wake wa umaana kwa kulinganishwa na Bwana-mkubwa wake. Ni somo zuri hilo, kwa maana wanyenyekevu peke yao ndio hufaa kutumikia Yehova na Mfalme wake wa Kimesiya!—Zaburi 138:6; Mithali 21:4.
Badala ya kumwonea Yesu uchungu kwa kiburi, Yohana Mbatizaji alisema hivi: “Rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia.” (3:29, 30) Akiwa mwakilishi wa bwana arusi, rafiki ya bwana arusi alifanya makubaliano ya ndoa, nyakati fulani akipanga posa na upelekaji wa zawadi kwa bibi arusi na malipo ya bibi arusi kwa baba yake. Naibu huyu alikuwa na sababu ya kuterema wakati wajibu wake ulipotimizwa. Vivyo hivyo, Yohana alishangilia kumleta Yesu pamoja na washiriki wa kwanza wa bibi arusi Wake. (Ufunuo 21:2, 9) Kwa kuwa huduma za rafiki ya bwana arusi zilikuwa za muda mfupi tu, ndivyo kazi ya Yohana ilivyomalizika upesi. Yeye alifuliza kupungua, huku Yesu akiendelea kuongezeka.—Yohana 3:30.
Hali ya Yesu ya Kujali Watu
Kwenye kisima karibu na jiji la Sikari, Yesu aliambia mwanamke Msamaria juu ya maji ya ufananisho ambayo hutoa uhai wa milele. Wanafunzi wake walipowasili, “wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke.” (4:27) Kwa nini waitikie hivyo? Ni kwamba, Wayahudi walidharau Wasamaria na hawakufanya shughuli nao. (4:9; 8:48) Pia halikuwa jambo la kawaida mwalimu wa Kiyahudi kuongea na mwanamke peupe. Lakini hali ya Yesu ya kujali watu kwa huruma ilimsukuma atoe ushahidi huu, na kwa sababu ya huo, wakaaji wa jiji “wakaanza kumjia.”—4:28-30, NW.
Hali ya kujali watu ilisukuma Yesu aseme hivi: “Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.” (7:37) Kwa wazi, yeye alidokeza hivyo juu ya desturi iliyoongezwa kwenye ile Sikukuu ya Vibanda ya siku nane. Kila asubuhi kwa siku saba, kuhani alichota maji kutoka kidimbwi cha Siloamu na kuyamimina kwenye madhabahu ya hekalu. Miongoni mwa mambo mengine, jambo hili lilisemwa kuwakilisha kumiminwa kwa roho. Kuanzia Pentekoste 33 W.K., roho ya Mungu ilishurutisha wafuasi wa Yesu kupelekea watu duniani pote maji yanayotoa uhai. Ni kutoka kwa Yehova tu, aliye “chemchemi ya maji ya uzima,” kupitia Kristo kwamba mtu yeyote aweza kupokea uhai wa milele.—Yeremia 2:13; Isaya 12:3; Yohana 17:3.
Mchungaji Mwema Ajali!
Hali ya Yesu ya kujali watu yaonekana wazi katika sehemu anayotimiza akiwa Mchungaji Mwema mwenye kujali wafuasi wake walio kama kondoo. Hata kifo chake kilipokuwa kikikaribia, Yesu aliwapa wanafunzi wake shauri lenye upendo na akasali kwa ajili yao. (10:1–17:26) Tofauti na mwizi au mtekanyara, yeye huingia zizi la kondoo kupitia mlangoni. (10:1-5) Zizi la kondoo lilikuwa boma ambamo kondoo waliwekwa ili walindwe usiku kucha na wezi na wanyama wawindaji. Lilikuwa na kuta za mawe, labda likiwa na matawi yenye miiba juu, na mwingilio wenye kulindwa na bawabu.
Makundi ya mifugo wa wachungaji kadhaa yangeweza kuwekwa katika zizi moja la kondoo, lakini kondoo waliitikia sauti ya mchungaji yule wao hasa. Katika kitabu chake Manners and Customs of Bible Lands, Fred H. Wight asema hivi: “Ihitajiwapo kabisa kutenganisha makundi kadhaa ya kondoo, mchungaji baada ya mwingine husimama na kuita hivi: ‘Tahhoo! Tahhoo!’ au wito kama huo aliouchagua mwenyewe. Kondoo huinua vichwa vyao, na baada ya mpitanopitano wa ujumla, kila mmoja huanza kufuata mchungaji wake mwenyewe. Wao huzoeana kabisa na hali ya sauti ya mchungaji wao wenyewe. Mara nyingi wageni wametumia wito ule ule, lakini majaribio yao kufanya kondoo wawafuate hukosa mafanikio sikuzote.“ Kwa kupendeza, Yesu alisema: “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele.” (10:27, 28) “Kundi dogo” na “kondoo wengine” pia huitikia sauti ya Yesu, hufuata uongozi wake, na kuonea shangwe utunzaji wake mwororo.—Luka 12:32; Yohana 10:16.
Mwana wa Mungu Aliye Mwaminifu Daima
Kristo alikuwa mwaminifu daima kwa Mungu na alikuwa kielelezo akiwa mchungaji mwenye upendo muda wote wa maisha yake ya kidunia. Huruma yake ilidhihirishwa pia katika mionekano ya baada ya kufufuliwa. Hali ya kujali wengine kwa huruma ndiyo iliyosukuma Yesu wakati huo ahimize Petro kulisha kondoo Zake.—18:1–21:25.
Akiwa mhanga wa kutundikwa mtini, Yesu alituwekea sisi kielelezo bora cha uaminifu mpaka kifo. Fedheha moja iliyompata kwa utimizo wa unabii ilikuwa kwamba askari ‘waligawana mavazi yake miongoni mwao wenyewe.’ (Zaburi 22:18) Walipiga kura kuamua ni nani angepata vazi lake la ndani (Kigiriki, khi·tonʹ), lililofumwa bila mshono wa upindo. (19:23, 24, NW) Joho hilo lingeweza kufumwa kwa sufi au kitani likiwa la kitambaa kimoja na lingeweza kuwa jeupe au la rangi mbalimbali. Likiwa bila mikono mara nyingi, lilivaliwa juu ya ngozi ya mwili na kufika magotini au hata kwenye vifundo vya nyayo. Bila shaka, Yesu hakuwa mfuatiaji wa vitu vya kimwili, lakini alivaa vazi hilo la ubora mwingi, joho lake lisilo na mshono wa upindo.
Wakati wa mmoja wa mionekano ya Yesu baada ya kufufuliwa, yeye alisalimu wanafunzi wake kwa maneno haya: “Amani iwe kwenu.” (20:19) Miongoni mwa Wayahudi, hii ilikuwa salamu ya kawaida. (Mathayo 10:12, 13) Kwa wengi, huenda ikawa utumizi wa maneno hayo haukuwa na maana sana. Lakini sivyo kwa habari ya Yesu, kwa maana mapema kidogo alikuwa ameambia wafuasi wake hivi: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa.“ (Yohana 14:27) Amani ambayo Yesu aliwapa wanafunzi wake ilitegemea imani yao katika yeye akiwa Mwana wa Mungu na ikatumika kutuliza mioyo na akili zao.
Vivyo hivyo, sisi twaweza kuionea shangwe “amani ya Mungu.” Na tuthamini sana utulivu huu usiolinganika wenye kutokana na uhusiano wa karibu na Yehova kupitia Mwanaye mpendwa.—Wafilipi 4:6, 7.
[Hisani katika ukurasa wa 25]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.