Maisha na Huduma ya Yesu
Wasamaria Wengi Wanaamini
WANAPORUDI kutoka Sikari wakiwa na chakula, wanafunzi wanamkuta Yesu kisimani walipomwacha. Lakini sasa anasema na mwanamke Msamaria. Mwanamke huyo anaondoka wakati wanafunzi wanapofika, anaacha mtungi wake, na kuelekea mjini.
Kwa kupendezwa sana na mambo aliyoambiwa na Yesu, mwanamke anawaambia watu mjini hivi: “Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda.” Halafu, kwa kutumia njia ya kuamsha hamu yao ya kutaka kupashwa habari, anauliza: “Je! haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?” Ulizo hilo linatimiza kusudi lake—watu hao wanaenda wakajionee wenyewe.
Kwa wakati huo, wanafunzi wanamhiza Yesu ale chakula ambacho wamenunua mjini. Lakini yeye anajibu: “Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.”
“Je! mtu [amemletea] chakula?” wanafunzi wanaulizana. Yesu anaeleza: ‘Chakula changu ni kwamba mimi niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno?’ Lakini akielekeza kwenye mavuno ya kiroho, Yesu anasema: ‘Tayari avunaye anapokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele.’
Labda Yesu tayari aliweza kuona matokeo makubwa ambayo yangetokana na ushuhuda uliotolewa na mwanamke huyo Msamaria—ya kwamba wengi walikuwa wakimwamini kwa sababu ya ushuhuda wake mwanamke. Wakati watu wa Sikari wanapomjia pale kisimani, wanamwomba akae aendelee kusema nao kidogo. Yesu anaukubali mwaliko huo na kukaa muda wa siku mbili.
Wasamaria wanapomsikiliza Yesu, wengine wengi wanamwamini. Ndipo wanapomwambia mwanamke yule: “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.” Kwa uhakika mwanamke huyo Msamaria ni mfano mzuri sana wa jinsi sisi tunaweza kutoa ushuhuda juu ya Kristo kwa kuamsha hamu ya wasikilizaji ya kutaka kuchunguza habari zaidi!
Kumbuka kwamba sasa imebaki miezi minne kabla ya mavuno—kwa wazi mavuno ya shayiri—ambayo katika Palestina yanatukia katika majira ya masika. Kwa hiyo labda sasa ni Novemba au Desemba. Hiyo maana yake ni kwamba baada ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 30 W.K., Yesu na wanafunzi wake walikaa miezi minane hivi katika Yudea wakifundisha na kubatiza. Sasa wanaondoka kwenda kwenye eneo la nyumbani kwao la Gailaya. Ni mambo gani yanayowangoja huko? Yohana 4:27-42.
◆ Mwanamke Msamaria anatoa ushuhuda gani na matokeo yanakuwa nini?
◆ Chakula cha Yesu kinahusianaje na mavuno?
◆ Tunaweza kujuaje urefu wa huduma ya Yesu katika Yudea baada ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 30 W.K.?
[Picha ya ukurasa nzima katika ukurasa wa 25]