Maisha na Huduma ya Yesu
Mtawala Anayetamaniwa Mwenye Nguvu Zaidi ya Wanadamu
WAKATI Yesu anapolisha maelfu kwa mwujiza, watu wanastaajabu. “Huyo kwa uhakika ndiye yule nabii ambaye alikuwa aje ndani ya ulimwengu,” wao wanasema. Wao wanakata shauri si kwamba tu Yesu lazima ndiye nabii aliye mkubwa kuliko Musa bali pia yeye angeweza kuwa mtawala wa kutamanika sana. Kwa hiyo, wanafanya mpango wamkamate na kumfanya mfalme.
Hata hivyo, Yesu anajua jambo wanalopangia. Kwa hiyo anafanya haraka aepuke kushurutishwa nao kuingia katika cheo hicho. Yeye anawaambia makutano waende zao, amelazimisha wanafunzi wake waingie katika mashua yao na kurudi wakielekea Kapernaumu, na ndipo anapoingia mlimani peke yake kusali. Usiku huo Yesu anakuwa pale yeye peke yake kabisa.
Muda mfupi kabla ya mapambazuko Yesu anatazama kule nje akiwa mahali hapo palipoinuka na kuona mawimbi yakichafuliwa-chafuliwa katika bahari na upepo wenye nguvu. Katika nuru ya mwezi unaokaribia kuwa mpevu, kwa kuwa sikukuu ya Kupitwa inakaribia, Yesu aiona mashua huko wanafunzi wake wakijitahidi sana kusonga mbele dhidi ya mawimbi yale. Wanaume hao wanapiga makasia kwa nguvu zao zote.
Kuona hivyo, Yesu anashuka mlimani na kuanza kutembea kuielekea mashua akipita juu ya mawimbi. Anapomaliza umbali wa maili karibu tatu au nne hivi, yeye anafikia wanafunzi wake. Hata hivyo, yeye aendelea kutembea tu kana kwamba atawapita mahali walipo. Wanapomwona, wanapaaza sauti: “Ni mzuka!”
Yesu aitika hivi kwa kufariji: “Ni mimi; msiwe na hofu.”
Lakini Petro anasema: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru mimi nikujie wewe juu ya maji haya.”
“Njoo!” Yesu anajibu.
Papo hapo, Petro anatoka mashuani, anatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini anapoitazama dhoruba ya upepo, Petro anaingiwa na woga, na anapoanza kuzama, anapaaza sauti hivi: “Bwana, niokoe mimi!”
Akinyoosha mkono wake bila kukawia, Yesu anamshika, akisema: “Wewe uliye na imani kidogo, mbona wewe umeliachia shaka nafasi?”
Baada ya Petro na Yesu kurudi ndani ya mashua, upepo ule unaacha kuvuma, na wanafunzi wanastaajabu. Lakini je! inawapasa kufanya hivyo? Kama wao wangaliishika “maana ya mikate ile” kwa kuthamini ule mwujiza mkubwa ambao Yesu alifanya saa chache kabla ya hapo wa kulisha maelfu kwa mikate mitano tu na samaki wawili wadogo, basi lisingalipasa kuonekana kana kwamba ni jambo la kustaajabisha sana kwamba yeye angeweza kutembea juu ya maji na kufanya upepo utulie. Hata hivyo, sasa wanafunzi wanamsujudia Yesu na kusema: “Wewe kweli kweli ni Mwana wa Mungu.”
Baada ya muda mfupi wanafika Genesareti, uwanda wa kupendeza ulio na mazao karibu na Kapernaumu. Hapo wanitia mashua nanga. Lakini wanapoenda nchi kavu, watu wanamtambua Yesu na kwenda ndani ya nchi yote inayozunguka eneo hilo, wakitafuta wale walio wagonjwa. Wanapoletwa wakiwa katika machela zao na kugusa tu upindo wa vazi la nje la Yesu, wanaponyeshwa kabisa.
Siku inayofuata kutano lililoshuhudia ulishaji wa kimwujiza wa maelfu ya watu linagunduwa kwamba Yesu ameondoka. Kwa hiyo wakati mashua ndogo-ndogo zinapowasili kutoka Tiberia, wao wanzipanda na kutweka tanga kwenda Kapernaumu kwa kumtafuta Yesu. Wanapompata, wanamwuliza: “Rabi, wewe ulifika hapa lini?” Jibu la Yesu litafunua mambo wazi sana. Yohana 6:14-25; Mathayo 14:22-36; Marko 6:45-56, NW.
◆ Baada ya Yesu kulisha maelfu kwa mwujiza, watu wanataka kumfanya nini?
◆ Yesu anaona nini akiwa katika mlima ambako yeye amejitenga awe peke yake, na ndipo yeye anapofanya nini?
◆ Kwa sababu gani wanafunzi hawapaswi kustaajabishwa na mambo hayo?
◆ Ni jambo gani linalotukia baada ya wao kufika nchi kavu?
[Picha ya ukurasa nzima katika ukurasa wa 9]