Maisha na Huduma ya Yesu
Majaribio Zaidi ya Kuua Yesu
KWA kuwa ni wakati wa kipupwe, Yesu anatembea katika eneo lenye kinga linalojulikana kuwa ukumbi wa Sulemani. Ni kando-kando ya hekalu. Hapo Wayahudi wanamzunguka na kuanza kusema: “Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi.”
“Naliwaambia,” Yesu anajibu, “lakini ninyi hamsadiki [hamwitikadi, NW].” Yesu hakuwa amewaambia moja kwa moja kwamba ndiye Kristo, kama vile alivyokuwa amemwambia mwanamke Msamaria kwenye kisima. Hata hivyo, kwa kweli alikuwa amefunua utambulisho wake alipowaeleza kwamba alikuwa ametoka kwenye makao ya juu na alikuwa amekuwako kabla ya Abrahamu.
Hata hivyo, Yesu anataka watu wakate wenyewe shauri la kwamba yeye ndiye Kristo kwa kulinganisha utendaji wake pamoja na yale ambayo Biblia ilitabiri Kristo angeyafanya. Ndiyo sababu hapo mapema kidogo aliagiza wanafunzi wake wasiambie yeyote kwamba yeye ndiye Kristo. Na ndiyo sababu sasa yeye anaendelea kuwaambia hivi Wayahudi hao wakinzani: “Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki [hamwitikadi, NW].”
Kwa nini wao hawaitikadi? Je! ni kwa sababu ya kukosa ithibati kwamba Yesu ndiye Kristo? Sivyo, bali kwa sababu ambayo Yesu anatoa anapowaambia hivi: “Hammo miongoni mwa kondoo wangu. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”
Ndipo Yesu anapofasili uhusiano wake wa karibu pamoja na Baba yake, akieleza hivi: “Mimi na Baba tu umoja.” Kwa kuwa Yesu yupo duniani na Baba yake yuko mbinguni, kwa uwazi yeye hasemi kwamba yeye na Baba yake ni mmoja kihalisi, au kimwili. Badala ya hivyo, anamaanisha kwamba wao ni mmoja katika kusudi au wamo katika muungamano.
Kwa kutiwa kasirani na maneno ya Yesu, Wayahudi wanaokota mawe wamuue, hata kama vile walivyofanya miezi kadhaa mapema, wakati wa Sikukuu ya Vibanda. Akiwaelekezea uso kishujaa hao wanaotaka kumuua, Yesu anasema: “Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?”
“Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe,” wao wanajibu, “bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.” Kwa kuwa Yesu hakudai kamwe kuwa mungu [NW], kwa nini Wayahudi wanasema jambo hilo?
Ithibati inaonyesha ni kwa sababu Yesu anajihesabu mwenyewe kuwa na nguvu ambazo wao wanaitikadi ni za Mungu peke yake. Mathalani, ni sasa tu kwamba yeye amesema hivi juu ya “kondoo,” “Nami nawapa uzima wa milele,” jambo ambalo hakuna mwanadamu anaweza kufanya. Hata hivyo, Wayahudi wanakosa kuona uhakika wa kwamba Yesu anakiri kuwa alipokea mamlaka kutoka kwa Baba yake.
Kwamba Yesu anadai kuwa mpungufu kuliko Mungu, yeye anaonyesha hivyo baada ya hapo kwa kuuliza hivi: “Je! haikuandikwa katika torati yenu [kwenye Zaburi 82:6] ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?” Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); je! yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu?”
Ndiyo, kwa kuwa Maandiko yanawaita “miungu” hata mahakimu wa kibinadamu wasio haki, ni kasoro gani ambayo Wayahudi hawa wanaweza kupata kwa Yesu kwa sababu ya kusema, “Mimi ni Mwana wa Mungu”? Yesu anaongezea hivi: “Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu [katika muungano pamoja na mimi, NW], nami ni ndani ya Baba [katika muungano pamoja na Baba, NW].”
Yesu anaposema hilo, Wayahudi wanajaribu kumkamata. Lakini yeye anakimbia, hata kama vile alivyofanya mapema kidogo kwenye Sikukuu ya Vibanda. Yeye anasafiri kuondoka Yerusalemu na kuvuka ng’ambo ya Mto Yordani mahali ambako Yohana alianza kubatiza karibu miaka minne mapema. Inaonekana kwamba mahali hapo si mbali kutoka kwenye ufuo wa kusini wa Bahari ya Galilaya, safari ya siku mbili hivi kutoka Yerusalemu.
Watu wengi wanamjia Yesu mahali hapo na kuanza kusema: “Yohana kwa kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohana katika habari zake huyu yalikuwa kweli.” Hivyo wengi wanatia imani katika Yesu hapa. Yohana 10:22-42; 4:26; 8:23, 58; Mathayo 16:20.
♦ Yesu anataka watu wamtambue yeye kuwa ndiye Kristo kwa kutumia njia gani?
♦ Ni jinsi gani Yesu na Baba yake walivyo mmoja?
♦ Ithibati inaonyesha ni kwa nini Wayahudi wanasema Yesu anajifanya mwenyewe kuwa mungu?
♦ Nukuu la Yesu kutoka kwenye Zaburi linaonyesha jinsi gani kwamba yeye hadai kuwa sawa na Mungu?