Je, Wajua?
Je, mfano wa Yesu kuhusu “mbwa wadogo” ulionyesha dharau?
Wakati fulani, Yesu alipokuwa nje ya eneo la Israeli, katika jimbo la Roma huko Siria, mwanamke fulani Mgiriki alienda kumwomba msaada. Yesu alijibu kwa kutoa mfano uliowalinganisha watu wasio Wayahudi na “mbwa wadogo.” Chini ya Sheria ya Musa, mbwa walionwa kuwa wanyama wasio safi. (Mambo ya Walawi 11:27) Lakini je, Yesu alimdharau mwanamke huyo pamoja na watu wengine wasio Wayahudi?
La hasha. Wazo la Yesu, kama alivyowafafanulia wanafunzi wake, lilikuwa ni kwamba wakati huo alitaka kuwasaidia kwanza Wayahudi. Kwa hiyo alitoa mfano kufafanua wazo hilo, na kumwambia hivi mwanamke huyo Mgiriki: “Si sawa kuuchukua mkate wa watoto na kuwatupia mbwa wadogo.” (Mathayo 15:21-26; Marko 7:26) Wagiriki na Waroma waliwaona mbwa kuwa wanyama wazuri na hata waliishi nao ndani ya nyumba na kuwaruhusu wacheze na watoto. Kwa hiyo msemo “mbwa wadogo” ulikuwa na maana nzuri akilini mwa mwanamke huyo. Mwanamke huyo Mgiriki alielewa kile ambacho Yesu alimaanisha, naye akajibu hivi: “Ndiyo, Bwana; lakini kwa kweli hao mbwa wadogo hula sehemu ya makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza ya mabwana zao.” Yesu alimpongeza kwa imani yake na akamponya binti ya mwanamke huyo.—Mathayo 15:27, 28.
Je, kweli mtume Paulo alitoa ushauri mzuri alipopendekeza wasitishe safari yao ya baharini?
Meli ambayo Paulo alipanda kwenda Italia ilikuwa ikikabiliana na upepo mkali. Walipotia nanga mahali fulani, mtume Paulo alipendekeza kwamba safari isitishwe. (Matendo 27:9-12) Je, pendekezo hilo lilikuwa na msingi wowote?
Mabaharia wa kale walijua vizuri kwamba ilikuwa hatari kusafiri katika bahari ya Mediterania wakati wa majira ya baridi. Kuanzia Novemba 15 hadi Machi 15 hivi, haikuwezekana kabisa kusafiri katika bahari hiyo. Lakini safari ambayo Paulo alikuwa akiizungumzia ilikuwa ni ya mwezi wa Septemba au Oktoba. Katika kitabu chake cha Epitome of Military Science, Mwandishi Mroma, Vegetius (karne ya nne W.K.), aliandika hivi kuhusu safari katika bahari hiyo: “Kuna miezi ambayo ni mizuri kusafiri, mingine si salama sana, na mingine haiwezekani kabisa.” Vegetius alisema kwamba ilikuwa ni salama kusafiri kuanzia Mei 27 hadi Septemba 14, lakini wakati ambao si salama sana, au hatari kabisa, ni kuanzia Septemba 15 hadi Novemba 11 na Machi 11 hadi Mei 26. Bila shaka Paulo, ambaye alikuwa msafiri mwenye uzoefu, alijua vizuri mambo hayo. Inaelekea nahodha pamoja na mmiliki wa meli hiyo walijua pia mambo hayo lakini wakapuuza ushauri wa Paulo. Matokeo ni kwamba meli hiyo ilivunjika.—Matendo 27:13-44.