Piga Mbiu ya Ufalme wa Yehova kwa Ujasiri!
“Alikuwa akiwapokea wote wale waliomjia ndani, akiwahubiri ufalme wa Mungu.”—MATENDO 28:30, 31, NW.
1, 2. Mtume Paulo alikuwa na uthibitisho gani wa tegemezo la kimungu, naye aliweka kielelezo gani?
YEHOVA huwategemeza sikuzote wapiga mbiu ya Ufalme. Hiyo ilikuwa kweli kama nini juu ya mtume Paulo! Akiwa na tegemezo la kimungu, alienda mbele ya watawala, akavumilia kitendo cha wafanya ghasia, naye akapiga mbiu ya Ufalme wa Yehova kwa ujasiri.
2 Hata akiwa mfungwa-gereza katika Roma, Paulo “alikuwa akiwapokea wote wale waliomjia ndani, akiwahubiri ufalme wa Mungu.” (Matendo 28:30, 31, NW) Ni kielelezo kizuri kama nini kwa Mashahidi wa Yehova leo! Sisi twaweza kujifunza mengi kutokana na huduma ya Paulo kama ilivyoripotiwa na Luka katika sura za mwisho za kitabu cha Biblia cha Matendo.—20:1–28:31.
Waamini Wenzi Wajengwa
3. Ni nini lililotukia Troa, na ni ulinganifu gani uwezao kufanywa na siku yetu?
3 Baada ya ghasia katika Efeso kutulia, Paulo aliendelea na safari yake ya tatu ya kimisionari. (20:1-12) Hata hivyo, alipokuwa karibu kung’oa nanga aende Siria alipata habari kwamba Wayahudi walikuwa wametunga hila dhidi yake. Kwa kuwa huenda wakawa walikuwa wamepanga kupanda meli ile ile wamwue Paulo, alipitia Makedonia. Huko Troa, alikaa juma moja akijenga waamini wenzi kama vile waangalizi wenye kusafiri miongoni mwa Mashahidi wa Yehova hufanya sasa. Usiku uliotangulia kuondoka kwake, Paulo alirefusha hotuba yake mpaka usiku-kati. Eutiko, akiwa ameketi kwenye dirisha, yaonekana alikuwa amechoka sana kutokana na jitihada za siku hiyo. Alilala fofofo akaporomoka kutoka sakafu ya tatu na kufa, lakini Paulo alimrudishia uhai. Ni lazima hilo liwe lilisababisha shangwe sana! Basi, fikiria shangwe itakayotokea wakati mamilioni wengi wafufuliwapo katika ulimwengu mpya unaokuja.—Yohana 5:28, 29.
4. Kwa habari ya huduma, Paulo aliwafundisha nini wazee Waefeso?
4 Akiwa njiani kwenda Yerusalemu, Paulo alikutana huko Mileto na wazee wa Efeso. (20:13-21, NW) Aliwakumbusha kwamba alikuwa amewafundisha “nyumba kwa nyumba” na kwamba ‘alitoa ushahidi kikamili kwa wote Wayahudi na Wagiriki juu ya toba kuelekea Mungu na imani katika Bwana wetu Yesu.’ Wale ambao hatimaye walikuja kuwa wazee walikuwa wametubu, na walikuwa na imani. Pia mtume alikuwa amekuwa akiwazoeza kupiga mbiu ya Ufalme kwa ujasiri kwa wasio waamini katika huduma ya nyumba kwa nyumba kama ile ambayo hufanywa na Mashahidi wa Yehova leo.
5. (a) Paulo aliwekaje kielelezo kuhusu kuelekezwa na roho takatifu? (b) Kwa nini wazee walihitaji ‘kutunza kundi lote’?
5 Paulo aliweka kielelezo katika kukubali mwelekezo wa roho takatifu ya Mungu. (20:22-30) ‘Akiwa amefungwa rohoni,’ au akihisi wajibu wa kufuata mwongozo wayo, mtume angeenda Yerusalemu, ingawa vifungo na dhiki vilimngoja huko. Alithamini uhai, lakini kudumisha ukamilifu kwa Mungu lilikuwa ndilo jambo la maana kabisa kwake, kama vile lipasavyo kuwa kwetu. Paulo aliwahimiza wazee ‘watunze lile kundi lote ambalo roho takatifu ilikuwa imewaweka wawe waangalizi ndani yalo.’ Baada ya ‘kuondoka kwake’ (kwa wazi katika kifo), “mbwa-mwitu wakali [wenye kuonea, NW]” ‘hawangelihurumia kundi.’ Watu hao wangeinuka kutoka miongoni mwa wazee wenyewe, na wanafunzi wasio na utambuzi wangekubali mafundisho yao yenye kupotoka.—2 Wathesalonike 2:6.
6. (a) Kwa nini Paulo angeweza kuwakabidhi wazee mikononi mwa Mungu akiwa na uhakika? (b) Paulo alifuataje kanuni ya Matendo 20:35?
6 Wazee walihitaji kubaki chonjo kiroho ili kulinda dhidi ya uasi-imani. (20:31-38, NW) Mtume huyo alikuwa amewafundisha Maandiko ya Kiebrania na mafundisho ya Yesu, yaliyo na nguvu za utakaso ambayo yangeweza kuwasaidia waupokee Ufalme wa kimbingu, “urithi ulio miongoni mwa watakaswa wote.” Kwa kufanya kazi ili aandae riziki kwa ajili yake mwenyewe na washirika wake, Paulo aliwatia moyo wazee hao wawe pia wafanya kazi wenye bidii. (Matendo 18:1-3; 1 Wathesalonike 2:9) Tukifuatia mwendo kama huo na kusaidia wengine wapate uhai wa milele, tutathamini maneno haya ya Yesu: “Kuna furaha nyingi katika kutoa kuliko katika kupokea.” Wazo la taarifa hii hupatikana katika zile Gospeli lakini hunukuliwa na Paulo peke yake, ambaye huenda akawa alilipokea kwa mdomo au kwa uvuvio. Twaweza kuwa na shangwe ya furaha nyingi ikiwa sisi ni wenye kujidhabihu kama Paulo. Naam, yeye alikuwa amejitoa sana hivi kwamba kuondoka kwake kuliwahuzunisha sana wazee Waefeso!
Acha Mapenzi ya Yehova Yatendeke
7. Paulo aliwekaje kielelezo katika kujitiisha kwa mapenzi ya Mungu?
7 Safari ya tatu ya Paulo ya kimisionari ilipokuwa ikikaribia kumalizika (karibu 56 W.K.), yeye aliweka kielelezo kizuri katika kujitiisha kwa mapenzi ya Mungu. (21:1-14, NW) Katika Kaisaria yeye na waandamani wake walikaa pamoja na Filipo, ambaye binti zake wanne walio mabikira ‘walitoa unabii,’ wakitabiri matukio kwa roho takatifu. Huko nabii Mkristo Agabo akafunga mikono na nyayo zake mwenyewe kwa ukanda wa Paulo na kusukumwa na roho kusema kwamba Wayahudi wangemfunga mwenye ukanda huo katika Yerusalemu na kumtia mikononi mwa Wasio Wayahudi. “Niko tayari si kufungwa tu bali pia kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu,” akasema Paulo. Wanafunzi wakaafikiana naye, wakisema: “Acha mapenzi ya Yehova yatendeke.”
8. Nyakati fulani tukiona ni vigumu kupokea ushauri mwema, tungeweza kukumbuka nini?
8 Paulo aliwaambia wazee katika Yerusalemu mambo ambayo Mungu alifanya miongoni mwa Wasio Wayahudi kupitia huduma yake. (21:15-26, NW) Wakati wowote sisi tukiona ni vigumu kupokea ushauri mwema, twaweza kukumbuka jinsi Paulo alivyoukubali. Ili athibitishe kwamba hakuwa akifundisha Wayahudi katika mabara ya Wasio Wayahudi “uasi-imani wa kumwacha Musa,” alitii shauri la wazee kwamba asafishwe kisherehe na kulipa gharama zake mwenyewe na za wanaume wengine wanne. Ingawa kifo cha Yesu kiliiondoa Sheria, Paulo hakufanya kosa lolote kwa kutekeleza sehemu zayo zilizohusu nadhiri.—Warumi 7:12-14.
Aghasiwa Lakini Hatishiki
9. Kwa habari ya jeuri ya wafanya ghasia, kuna ulinganifu gani kati ya maono ya Paulo na yale ya Mashahidi wa Yehova leo?
9 Mara nyingi Mashahidi wa Yehova wameshika ukamilifu kwa Mungu kwa kukabiliana na jeuri ya wafanya ghasia. (Kwa kielelezo, ona Kitabu cha Mwaka 1982-85 cha Mashahidi wa Yehova, kurasa 110-6.) Vivyo hivyo Wayahudi kutoka Esia Ndogo walichochea kitendo cha wafanya ghasia dhidi ya Paulo. (21:27-40) Kwa kumwona Trofimo Mwefeso akiwa pamoja naye, walimshtaki mtume kwa ubandia juu ya kunajisi hekalu kwa kuingiza Wagiriki humo. Paulo alikuwa karibu kuuawa wakati ofisa-mtetezi Mroma Klaudio Lisia na watu wake walipokandamiza fujo hiyo! Kama ilivyotabiriwa (lakini ikasababishwa na Wayahudi), Lisia aliagiza Paulo afungwe minyororo. (Matendo 21:11) Mtume alikuwa karibu kupelekwa ndani ya makao ya askari yenye kuungana na ua wa hekalu wakati Lisia alipopata habari kwamba Paulo si mfitini serikali bali ni Myahudi aliyeruhusiwa kuingia eneo la hekalu. Alipopata ruhusa ya kusema, Paulo alihutubia watu hao kwa Kiebrania.
10. Hotuba ya Paulo ilipokewaje na Wayahudi katika Yerusalemu, na kwa nini yeye hakupigwa mijeledi?
10 Paulo alitoa ushahidi jasiri. (22:1-30) Alijitambulisha kuwa Myahudi aliyefundishwa na Gamalieli mwenye kustahiwa sana. Mtume akaeleza kwamba alipokuwa njiani kwenda Dameski kunyanyasa wafuasi wa Ile Njia, alikuwa amepofuka kwa kumwona Yesu Kristo aliyetukuzwa, lakini Anania akarudisha mwono wake. Baadaye Bwana alikuwa amemwambia Paulo hivi: “Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.” Maneno hayo yaliwasha moto kama cheche iliyoangukia msitu. Kwa kupiga kelele kwamba Paulo hakufaa kuishi, umati ulitupa-tupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi hewani kwa kasirani. Kwa hiyo Lisia akaagiza Paulo apelekwe kwenye makao ya askari akachunguzwe kwa kupigwa mijeledi ili ijulikane kwa nini Wayahudi walikuwa dhidi yake. Kupigwa mijeledi (kwa chombo chenye nyugwe za ngozi zenye mafundo au zilizokazwa imara kwa vipande vya metali [chuma] au mifupa) kulizuiwa Paulo alipouliza hivi: ‘Je! ni halali kumpiga mtu aliye Mroma naye hajahukumiwa bado?’ Alipojua kwamba Paulo alikuwa raia Mroma, Lisia akawa mwenye hofu na kumpeleka mbele ya Sanhedrini ajue kwa nini alikuwa akishtakiwa na Wayahudi.
11. Paulo alikuwa Farisayo katika jambo gani?
11 Paulo alipofungua utetezi wake mbele ya Sanhedrini kwa kusema kwamba alikuwa ‘amejiendesha mbele za Mungu kwa dhamiri iliyo safi kikamilifu,’ Anania Kuhani wa Juu aliagiza achapwe. (23:1-10, NW) Paulo akasema, “Mungu atakupiga wewe, wewe ukuta uliopakwa chokaa,” akidokeza ukuta uonekanao mwema lakini karibuni utabomoka-bomoka. “Je! wewe unatukana kuhani wa juu?” watu fulani wakauliza. Kwa sababu macho hayakuwa mazuri, huenda ikawa Paulo hakumtambua Anania. Lakini kwa kuona kwamba baraza lilikuwa mjumliko wa Mafarisayo na Masadukayo, Paulo akasema: ‘Mimi ni Farisayo mwenye kuhukumiwa kuhusu tumaini la ufufuo.’ Jambo hilo liliigawanya Sanhedrini, kwa maana Mafarisayo waliamini ufufuo hali Masadukayo hawakuuamini. Mgawanyiko mkubwa sana ulitokea hivi kwamba Lisia akalazimika kumponyosha mtume.
12. Paulo aliponyokaje njama iliyotungwa juu ya uhai wake katika Yerusalemu?
12 Ndipo Paulo akaepuka njama iliyotungiwa uhai wake. (23:11-35) Wayahudi arobaini walikuwa wameapa wasile au wasinywe mpaka wamwue. Mpwa wa Paulo aliripoti hilo kwake na kwa Lisia. Akiwa chini ya ulinzi wa kijeshi, mtume alipelekwa kwa Gavana Antonio Feliki huko Kaisaria, mji mkuu wa usimamizi wa Kiroma katika Yudea. Baada ya kuahidi kumpa Paulo usikizi, Feliki aliendelea kumweka chini ya ulinzi katika jumba la Praitoria la Herode Mkuu, makao makuu ya gavana.
Ujasiri Mbele ya Watawala
13. Paulo alimpa Feliki ushahidi juu ya nini, na kwa tokeo gani?
13 Muda si muda mtume akajitetea dhidi ya mashtaka bandia na kumtolea Feliki ushahidi kwa ujasiri. (24:1-27, NW) Akiwa mbele ya washtaki Wayahudi, Paulo alionyesha kwamba hakuwa amechochea wafanya ghasia. Alisema kwamba aliyaamini mambo yaliyoonyeshwa wazi katika Sheria na Manabii na kutumaini katika “ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu pia.” Paulo alikuwa ameenda Yerusalemu akiwa na “zawadi za rehema” (michango kwa ajili ya wafuasi wa Yesu ambao huenda umaskini wao ukawa ulitokana na mnyanyaso) na akawa amesafishwa kisherehe. Ingawa Feliki aliahirisha hukumu, baadaye Paulo aliwahubiri yeye na Drusila mke wake (binti ya Herode Agripa 1) juu ya Kristo, uadilifu, kujidhibiti, na hukumu inayokuja. Kwa kuogopeshwa na maongeo hayo, Feliki alimwacha Paulo aende zake. Hata hivyo, baadaye alipeleka habari mara nyingi ili mtume aje, huku akitumaini kupata hongo lakini wapi. Feliki alijua kwamba Paulo hakuwa na hatia lakini akamwacha akiwa mfungwa, akitumaini kupata hisani za Wayahudi. Miaka miwili baadaye, mwandamizi wa Feliki katika cheo akawa Porkio Festo.
14. Paulo alitumia kwa faida uandalizi gani wa kisheria alipokuja mbele ya Festo, nawe waona ulinganifu gani katika jambo hili?
14 Paulo alifanya utetezi jasiri mbele ya Festo pia. (25:1-12, NW) Ikiwa mtume alistahili kifo, yeye hangetafuta udhuru, lakini hakuna binadamu ambaye angeweza kumtia mikononi mwa Wayahudi kwa kuwafanyia hisani. “Mimi naomba rufani kwa Kaisari!” akasema Paulo, akitumia haki ya raia wa Kiroma ya kufanyiwa kesi katika Roma (wakati huo mbele ya Nero). Akiisha kupewa ombi la rufani, Paulo ‘angetoa ushahidi katika Roma,’ kama ilivyotabiriwa. (Matendo 23:11) Mashahidi wa Yehova pia huyatumia kwa faida maandalizi ya ‘kuzitetea na kuzithibitisha habari njema kisheria.’—Wafilipi 1:7, NW.
15. (a) Ni unabii gani uliotimizwa Paulo alipokuja mbele ya Mfalme Agripa na Kaisari? (b) Sauli ‘alipigaje teke dhidi ya michokoo’?
15 Mfalme Herode Agripa 2 wa kaskazini mwa Yudea na Bernike dada yake (ambaye alihusiana naye kwa ngono haramu ya kiukoo) alimsikia Paulo alipokuwa akimzuru Festo huko Kaisaria. (25:13–26:23, NW) Kwa kuwatolea ushahidi Agripa na Kaisari, Paulo alitimiza unabii wa kwamba yeye angepeleka jina la Bwana kwa wafalme. (Matendo 9:15) Akimwambia Agripa lililokuwa limetukia katika barabara ya kwenda Dameski, Paulo alitamka kwamba Yesu alisema hivi: “Kuendelea kupiga teke dhidi ya michokoo kwafanya mambo yawe magumu kwako.” Kama vile fahali mwenye kichwa kigumu hujiumiza mwenyewe katika kukinza michomo ya mchokoo, ndivyo Sauli alivyokuwa amejiumiza kwa kupigana dhidi ya wafuasi wa Yesu, waliokuwa na tegemezo la Mungu.
16. Festo na Agripa waliitikiaje ushuhuda wa Paulo?
16 Festo na Agripa waliitikiaje? (26:24-32, NW) Kwa kutoweza kuuelewa ufufuo na kustaajabia usadikisho wa Paulo, Festo alisema: “Kisomo kingi kinakusukuma ndani ya kichaa!” Vivyo hivyo, watu fulani sasa hushtaki Mashahidi wa Yehova kuwa wenye kichaa, ingawa kwa kweli wao ni kama Paulo katika ‘kutamka semi za ukweli na za utimamu wa akili.’ “Katika muda mfupi wewe ungenivuta kwa maneno ili niwe Mkristo,” akasema Agripa, naye akamaliza usikizi huo lakini akakiri kwamba Paulo angaliweza kufunguliwa kama hakuwa ameomba rufani kwa Kaisari.
Hatari za Baharini
17. Wewe ungeelezaje hatari zilizokabiliwa baharini wakati wa safari ya Paulo ya kwenda Roma?
17 Safari ya kwenda Roma ilimweka Paulo katika hali ya kuweza kupatwa na “hatari za baharini.” (2 Wakorintho 11:24-27) Ofisa wa jeshi jina lake Yulio ndiye aliyekabidhiwa kuangalia wafungwa wenye kung’oa nanga kutoka Kaisaria kwenda Roma. (27:1-26) Meli yao ilipotua Sidoni, Paulo aliruhusiwa kuzuru waamini, nao wakamburudisha kiroho. (Linganisha 3 Yohana 14.) Huko Mira katika Esia Ndogo, Yulio aliwafanya wafungwa hao wapande meli ya nafaka yenye kuelekea Italia. Kujapokuwako pepo kali za mbisho, walifanikiwa kufikia Bandari Nzuri karibu na jiji la Krete la Lasea. Baada ya kuondoka huko wakiwa njiani kwenda Foinike (Finiksi NW), tufani ya kaskazini-mashariki iliibamba meli. Kwa kuhofu kukwama chini katika zile Sirti (michanga-topea) nje ya pwani kaskazini mwa Afrika, mabaharia hawa ‘wakashusha vyombo,’ labda matanga na milingoti. Baadaye kiwiliwili cha meli kilizungushiwa kamba hivi kwamba viungo vya meli havingeachana. Ikiwa bado yarushwa-rushwa na tufani siku iliyofuata, meli ilipunguziwa uzito kwa kutupa shehena baharini. Siku ya tatu, walitupilia mbali vifaa vya kutegemeza meli (matanga au vyombo vya akiba). Tumaini lilipoonekana kufifia, malaika alimtokea Paulo na kumwambia asihofu, kwa maana angesimama mbele ya Kaisari. Kilikuwa kitulizo kilichoje mtume aliposema kwamba wasafiri wote wangetupwa pwani katika kisiwa fulani!
18. Ni jambo gani ambalo lilitendeka mwishowe kwa Paulo na abiria wenzake?
18 Abiria hao waliokoka. (27:27-44) Wakati wa usiku-kati katika siku ya 14, mabaharia walihisi kwamba bara lilikuwa karibu. Vipimo vya bildi vilithibitisha hivyo, na nanga zikashushwa ili kukimbia msiba juu ya miamba. Kwa himizo la Paulo, wanaume wote 276 wakala chakula. Halafu meli ikapunguziwa uzito kwa kuitupa ngano baharini. Kulipopambazuka, mabaharia hao walizikata nanga, wakafungulia makasia, na kupandisha tanga la mbele kwenye upepo. Chombo kikapwelea juu ya fungu, na tezi likaanza kuvunjika vipande vipande. Lakini kila mtu alifanikiwa kufika bara.
19. Ni nini lililopata Paulo juu ya Melita, naye huko aliwafanyia wengine jambo gani?
19 Wakiwa wamelowana na kuchoka sana, hao waliovunjikiwa na meli wakajikuta katika Melita, ambako watu wa kisiwani waliwaonyesha “fadhili za kibinadamu zaidi ya zile za kawaida.” (28:1-16, NW) Hata hivyo, Paulo alipokuwa akiweka vijiti juu ya moto, lile joto lilihuisha nyoka-vipiri aliyekuwa amelala hoi naye akajizonga-zonga juu ya mkono wake. (Sasa hakuna nyoka wenye sumu katika Melita, lakini huyu alikuwa “kiumbe mwenye sumu.”) Wamelita walifikiri Paulo alikuwa mwuaji hivi kwamba “haki ya kisasi” haingemruhusu aishi, lakini alipokosa kuanguka chini akiwa mfu au kufura, wakasema alikuwa mungu. Baadaye Paulo aliponya watu wengi, kutia na baba ya Publio, ofisa mkuu wa Melita. Miezi mitatu baadaye, Paulo, Luka, na Aristarko wakaondoka kwa kupanda meli yenye alama ya “Wana wa Zeu” (Castor na Pollux, miungu mapacha iliyosemekana kuwa ilipendelea wasafiri-maji). Ilipotua Puteoli, Yulio akasonga mbele pamoja na mlindwa wake. Paulo akampa Mungu asante na kujipa moyo mkuu wakati Wakristo kutoka ule mji mkuu wa Kiroma kwenye Soko la Apio na Mikahawa Mitatu kando ya Njia ya Apia. Mwishowe, katika Roma, Paulo akaruhusiwa kukaa akiwa peke yake, ingawa kwa kulindwa na askari mmoja.
Endelea Kupiga Mbiu ya
Ufalme wa Yehova!
20. Paulo alijishughulisha na utendaji gani katika makao yake katika Roma?
20 Akiwa katika makao yake katika Roma, Paulo alipiga mbiu ya Ufalme wa Yehova kwa ujasiri. (28:17-31) Aliwaambia hivi wanaume wakuu Wayahudi: “Kwa sababu ya tumaini la Israeli mimi nina mnyororo huu kunizunguka.” Tumaini hilo lilihusisha kumkubali Mesiya, jambo ambalo ni lazima sisi pia tuwe tayari kulitesekea. (Wafilipi 1:29) Ingawa walio wengi wa Wayahudi hao hawakuamini, watu wengi Wasio Wayahudi na walio mabaki ya Kiyahudi walikuwa na hali ifaayo ya moyoni. (Isaya 6:9, 10) Kwa miaka miwili (karibu 59-61, W.K.) Paulo aliwapokea wote wale waliomjia, ‘akiwahubiri ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yanayohusu Bwana Yesu Kristo kwa uhuru mkubwa kabisa wa usemi, bila kizuizi.’ (NW)
21. Hadi mwisho wa maisha yake ya kidunia, Paulo aliweka kielelezo gani?
21 Yaonekana Nero alimtangaza Paulo kuwa hana hatia na akamfungua. Halafu mtume akafanya upya kazi yake kwa kushirikiana na Timotheo na Tito. Hata hivyo, alitiwa gerezani tena katika Roma (karibu 65 W.K.) na yaelekea alifia imani mikononi mwa Nero. (2 Timotheo 4:6-8) Lakini hadi mwisho, Paulo aliweka kielelezo kizuri akiwa mpiga mbiu ya Ufalme aliye na moyo mkuu. Wote wale waliojiweka wakfu kwa Mungu katika siku za mwisho hizi na wapige mbiu ya Ufalme wa Yehova wakiwa na roho hiyo hiyo!
Wewe Ungejibuje?
◻ Ni mazoezi gani ya kihuduma ambayo Paulo aliwapa wazee Waefeso?
◻ Paulo aliwekaje kielelezo cha kujitiisha kwa mapenzi ya Mungu?
◻ Kwa habari ya jeuri ya wafanya ghasia, kuna ufanani gani kati ya maono ya Paulo na yale ya Mashahidi wa Yehova leo?
◻ Ni uandalizi gani wa kisheria ambao Paulo aliutumia kwa faida alipokuwa mbele ya Gavana Festo, na hilo lina ulinganifu gani wa ki-siku-hizi?
◻ Paulo alijishughulisha na utendaji gani katika makao yake katika Roma, akiweka kielelezo gani?