Tembea Katika Hofu kwa Yehova
“Kwa kadiri [kundi lilivyotembea] katika hofu kwa Yehova na katika faraja ya roho takatifu liliendelea kuzidika.”—MATENDO 9:31, NW.
1, 2. (a) Ni nini lililotendeka kundi la Kikristo lilipoingia katika kipindi cha amani? (b) Ingawa Yehova huruhusu mnyanyaso, yeye hufanya nini kingine?
MWANAFUNZI mmoja alikabili mtihani mkubwa kabisa. Je! angedumisha ukamilifu kwa Mungu! Ndiyo, bila shaka! Yeye alikuwa ametembea katika hofu kwa Mungu, akiwa na kicho kwa Mfanyi wake, na angekufa akiwa shahidi mwaminifu wa Yehova.
2 Mshika ukamilifu huyo mwenye kuhofu Mungu alikuwa Stefano, ‘mtu aliyejaa imani na roho takatifu.’ (Matendo 6:5, NW) Kuuawa kwake kulianzisha wimbi la mnyanyaso, lakini baada ya hapo kundi katika sehemu zote za Yudea, Galilaya, na Samaria liliingia katika kipindi cha amani na likajengwa kiroho. Zaidi ya hilo, “lilipokuwa likitembea katika hofu kwa Yehova na katika faraja ya roho takatifu liliendelea kuzidika.” (Matendo 9:31, NW) Mashahidi wa Yehova leo waweza kuwa na uhakika kwamba Mungu atatubariki hata kama twapata amani au mnyanyaso, kama ionyeshwavyo katika Matendo sura ya 6 hadi ya 12. Kwa hiyo acheni tutembee katika hofu yenye heshima nyingi kwa Mungu wakati tunyanyaswapo au tutumie ushwari wowote wa kutokuwapo mnyanyaso uwe wa kutuendeleza kiroho na kumtumikia kwa utendaji mwingi zaidi.—Kumbukumbu 32:11, 12; 33:27.
Waaminifu Hadi Mwisho
3. Ni tatizo gani lililoshindwa katika Yerusalemu, na jinsi gani?
3 Hata matatizo yakitokea nyakati za amani, kutengeneza mambo vizuri kwaweza kusaidia kuyatatua. (6:1-7, NW) Wayahudi wenye kusema Kigiriki katika Yerusalemu walilalamika kwamba wajane wao hawakuwa wakiangaliwa katika mgawanyo wa chakula kila siku huku waamini Wayahudi wenye kusema Kiebrania wakipendelewa. Tatizo hili lilitatuliwa wakati mitume walipoweka wanaume saba waangalie ‘shughuli hii yenye kuhitajiwa.’ Mmoja wao alikuwa Stefano.
4. Stefano alitendaje kuelekea mashtaka bandia?
4 Hata hivyo, muda si muda Stefano mwenye kuhofu Mungu akakabili mtihani. (6:8-15) Wanaume fulani waliinuka wakabishana na Stefano. Baadhi yao walikuwa wa ‘Sinagogi la Mahuru,’ labda Wayahudi waliotekwa na Waroma na baadaye wakawekwa huru, au waongofu Wayahudi waliokuwa wamekuwa watumwa wakati mmoja. Kwa kushindwa kujimudu dhidi ya hekima na roho ambayo Stefano alisema kwayo, adui zake walimpeleka kwenye Sanhedrini. Huko mashahidi bandia wakasema: ‘Sisi tulisikia mtu huyu akisema kwamba Yesu ataliharibu hekalu na kubadili desturi za Musa zilizopokezanwa.’ Na bado, hata wapinzani wake wangeweza kuona kwamba Stefano hakuwa mtenda kosa bali alikuwa na sura tulivu ya malaika, mjumbe wa Mungu mwenye uhakika wa kutegemezwa naye. Ulikuwa uso wenye kutofautiana kama nini na nyuso zao, zenye kujaa uovu kwa sababu walijikabidhi kwa Shetani!
5. Ni mambo gani ambayo Stefano alitokeza akitoa ushahidi?
5 Alipoulizwa maswali na Kayafa Kuhani wa Juu, Stefano alitoa ushahidi usio na hofu. (7:1-53, NW) Pitio lake la historia ya Kiisraeli lilionyesha kwamba kusudi la Mungu lilikuwa kuiweka kando Sheria na utumishi wa hekaluni Mesiya ajapo. Stefano alisema kwamba Musa, yule mkombozi ambaye kila Myahudi alidai kumheshimu, alikataliwa na Waisraeli, kama vile hata sasa wao hawakukubali Mmoja huyo mwenye kuleta ukombozi mkubwa zaidi. Kwa kusema kwamba Mungu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, Stefano alionyesha kwamba hekalu na mfumo walo wa ibada lingepitilia mbali. Lakini kwa kuwa mahakimu wao hawakuhofu Mungu wala hawakutaka kujua mapenzi Yake, Stefano alisema: ‘Enyi wenye shingo ngumu, sikuzote mnapinga roho takatifu. Ni nabii yupi ambaye baba zenu hawakumnyanyasa? Waliwaua wale waliotabiri kuja kwa yule Mwadilifu, ambaye nyinyi mmekuwa wasaliti na wauaji wake.’
6. (a) Kabla ya kifo chake, Stefano alipata maono gani yenye kuimarisha imani? (b) Kwa nini Stefano angeweza kusema hivi kwa kufaa: “Bwana Yesu, pokea roho yangu”?
6 Taarifa ya Stefano isiyo na hofu iliongoza kwenye kuuawa kwake. (7:54-60) Mahakimu walifoka kwa hasira kwa ufichuzi huu wa hatia yao katika kifo cha Yesu. Lakini lo, imani ya Stefano iliimarishwa kama nini ‘alipokaza macho mbinguni akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono Wake wa kuume’! Sasa Stefano angeweza kukabili adui zake kwa uhakika wa kwamba alikuwa amefanya mapenzi ya Mungu. Ingawa Mashahidi wa Yehova hawapati njozi, sisi twaweza kuwa na utulivu huo mwingi wenye kutoka kwa Mungu tunyanyaswapo. Baada ya kutupa Stefano nje ya Yerusalemu adui zake walianza kumpiga kwa mawe, naye akatoa nasihi hii: “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” Hiyo ilifaa kwa sababu Mungu alikuwa amempa Yesu mamlaka ya kuinua wengine kwenye uhai. (Yohana 5:26; 6:40; 11:25, 26) Akiwa amepiga magoti, Stefano akapaaza kilio hivi: “Bwana [Yehova, NW], usiwahesabie dhambi hii.” Halafu akalala usingizi katika kifo akiwa mfia-imani, kama vile wafuasi wengi sana wa Yesu wamefanya tangu hapo, hata katika nyakati za ki-siku-hizi.
Mnyanyaso Waeneza Habari Njema
7. Tokeo la mnyanyaso lilikuwa nini?
7 Kwa kweli kifo cha Stefano kilikuwa na tokeo la kueneza habari njema. (8:1-4) Mnyanyaso ulitapanya wanafunzi wote isipokuwa mitume katika sehemu zote za Yudea na Samaria. Sauli, aliyetoa kibali cha kuuawa kwa Stefano, aliparuza kundi kama hayawani, akivamia nyumba moja baada ya nyingine ili aburute wafuasi wa Yesu wakatiwe gerezani. Wanafunzi wenye kutapanywa walipoendelea kuhubiri, mpango wa Shetani wa kuwakomesha wapiga mbiu ya Ufalme wenye kumhofu Mungu kwa kuwanyanyasa ulivurugwa. Leo, pia, mara nyingi mnyanyaso umeeneza habari njema au ukavuta uangalifu wa watu kwenye kazi ya kuhubiri Ufalme.
8. (a) Ni nini lililotukia kama tokeo la kuhubiri kulikofanywa katika Samaria? (b) Petro alitumiaje ufunguo wa pili ambao Yesu alikuwa amemkabidhi?
8 Filipo mweneza-evanjeli alienda Samaria ‘kumhubiri Kristo.’ (8:5-25) Shangwe kubwa ilienea sana katika jiji hilo wakati habari njema zilipokuwa zikipigiwa mbiu, roho wachafu wakiondoshwa, na watu kuponywa. Mitume katika Yerusalemu walituma Petro na Yohana kwenda Samaria, nao waliposali na kuweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, wanafunzi hao wapya walipokea roho takatifu. Simoni aliyebatizwa karibuni, ambaye hapo kwanza alikuwa mfanya-mizungu ya kiuchawi, alijaribu kuinunua mamlaka hii lakini Petro akasema: ‘Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe. Moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.’ Alipoambiwa atubu na kumtolea Yehova dua ya kuomba msamaha, aliwaomba mitume wasali kwa ajili yake. Hiyo yapasa kusukuma wote wenye kuhofu Yehova leo wasali wapate msaada wa kimungu katika kuulinda moyo salama. (Mithali 4:23) (Kisa hicho ndicho kilichotokeza neno “usimoni,” “kuuza au kununua cheo cha kanisa au pendeleo la kanisa.” Petro na Yohana walipiga mbiu ya habari njema katika vijiji vingi vya Samaria. Hivyo, Petro alitumia ufunguo wa pili ambao Yesu alimpa ili afungue mlango wa maarifa na fursa ya kuingia katika Ufalme wa kimbingu.—Mathayo 16:19.
9. Mwethiopia ambaye Filipo alimtolea ushahidi alikuwa nani, na kwa nini mwanamume huyo angeweza kubatizwa?
9 Ndipo malaika wa Mungu akampa Filipo mgawo mpya. (8:26-40) “Towashi” mmoja, ofisa mwenye kusimamia hazina ya Kandake malkia wa Ethiopia, alikuwa katika gari la kukokotwa akitoka Yerusalemu kwenda Gaza. Yeye hakuwa towashi wa kimwili, mwenye kuzuiliwa asiingie katika kundi la Kiyahudi, bali alikuwa ameenda Yerusalemu kuabudu akiwa mwongofu aliyetahiriwa. (Kumbukumbu 23:1) Filipo alikuta towashi huyo akisoma kutoka kitabu cha Isaya. Alipoalikwa apande juu ya gari hilo lenye kukokotwa, Filipo alizungumza unabii wa Isaya “akamhubiri habari njema za Yesu.” (Isaya 53:7, 8) Muda si muda Mwethiopia huyo akapaaza sauti kwa mshangao: “Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?” Hakuna kilichomzuia, kwa kuwa alijua juu ya Mungu na sasa alikuwa na imani katika Kristo. Kwa hiyo Filipo akambatiza Mwethiopia huyo, kisha akashika njia kwenda zake huku akishangilia. Je! kuna chochote ambacho chakuzuia wewe usibatizwe?
Mnyanyasi Ageuzwa
10, 11. Ni jambo gani lililopata Sauli wa Tarso katika barabara ya kwenda Dameski na muda mfupi baada ya hapo?
10 Kwa sasa, Sauli alitafuta kuwafanya wafuasi wa Yesu wakane imani yao chini ya tisho la kifungo gerezani au kifo. (9:1-18a, NW) Kuhani wa juu (yaelekea ni Kayafa) alimpa barua za kupeleka kwenye masinagogi katika Dameski zikimpa mamlaka ya kuwaleta Yerusalemu wakiwa wamefungwa wanaume na wanawake wa “Njia hii,” au namna ya maisha yenye kutegemea kielelezo cha Kristo. Adhuhuri hivi karibu na Dameski mwangaza ulimweka kutoka mbinguni na sauti ikauliza: “Sauli, mbona unaninyanyasa?” Wale walio na Sauli walisikia “mvumo wa sauti” lakini hawakuelewa lililosemwa. (Linganisha Matendo 22:6, 9.) Ufunuo huo wa kisehemu juu ya Yesu aliyetukuzwa ulitosha kumpofusha Sauli. Mungu alimtumia mwanafunzi Anania kurudisha mwono wake.
11 Baada ya ubatizo wake, huyo aliyekuwa mnyanyasi hapo kwanza akawa kitu cha kunyanyaswa. (9:18b-25) Wayahudi katika Dameski walitaka kumwondolea mbali Sauli. Hata hivyo, wakati wa usiku wanafunzi walimshusha kupitia mwanya ukutani, yaelekea akiwa katika kapu la kusokotwa kwa kamba au vijiti vilivyofunganishwa. (2 Wakorintho 11:32, 33) Huenda ikawa huo mwanya ulikuwa dirisha la makao ya mwanafunzi fulani lililojengwa ukutani. Hakikuwa kitendo cha woga kuwaepa adui na kuendelea kuhubiri.
12. (a) Ni jambo gani lililopata Sauli katika Yerusalemu? (b) Kundi liliendeleaje?
12 Katika Yerusalemu, Barnaba alisaidia wanafunzi wamkubali Sauli kuwa mwamini mwenzi. (9:26-31, NW) Huko Paulo alibishana bila hofu na Wayahudi wenye kusema Kigiriki, waliojaribu pia kumwondolea mbali. Kwa kugundua hilo, akina ndugu walimpeleka Kaisaria na kumwambia aende zake Tarso, mji wa nyumbani kwake katika Kilikia. Ndipo kundi katika sehemu zote za Yudea, Galilaya, na Samaria ‘likaingia katika kipindi cha amani, likijengwa’ kiroho. Lilipokuwa ‘likitembea katika hofu kwa Yehova na faraja ya roho takatifu, likaendelea kuzidika.’ Hiki ni kielelezo kizuri kama nini kipasacho kufuatwa na makundi yote leo ikiwa yatapokea baraka ya Yehova!
Wasio Wayahudi Wawa Waamini!
13. Ni miujiza gani ambayo Mungu alimwezesha Petro kufanya huko Lida na Yafa?
13 Petro pia alikuwa akiendelea kuwa mwenye shughuli. (9:32-43) Huko Lida (sasa Lodi) katika Uwanda wa Sharoni, alimponya Aenea aliyepooza. Maponyo hayo yalisababisha wengi wamgeukie Bwana. Katika Yafa, Tabitha (Dorkasi) yule mwanafunzi mpendwa aliugua akafa. Petro alipowasili, wajane wenye kulia machozi walimwonyesha mavazi ambayo Dorkasi alikuwa ameshona na ambayo huenda wakawa walikuwa wameyavaa. Yeye alimrudisha Dorkasi kwenye uhai, na habari za hilo zilipoenea, wengi wakawa waamini. Petro alikaa katika Yafa pamoja na Simoni mtengeneza ngozi, ambaye nyumba yake ilikuwa kando ya bahari. Watengeneza ngozi walilowesha ngozi za wanyama katika bahari na kuzitibu kwa chokaa kabla ya kuziparuza nywele. Ngozi zilizokauka ziligeuzwa kuwa za kushonea kwa kuzitia dawa kwa umajimaji kutoka mimea fulani.
14. (a) Kornelio alikuwa nani? (b) Ni jambo gani lililokuwa kweli juu ya sala za Kornelio?
14 Wakati huo (36 W.K.), kulikuwako tukio mashuhuri mahali pengine. (10:1-8) Katika Kaisaria aliishi yule mtu mcha Mungu Korne-lio Asiye Myahudi, amiri Mroma mwenye kuamuru wanaume mia mmoja. Yeye ‘aliongoza kikosi cha Kiitalia,’ yaonekana kikiwa mjumliko wa askari wapya waliotolewa miongoni mwa raia Waroma na mahuru katika Italia. Ingawa Kornelio alimhofu Mungu, yeye hakuwa mwongofu Myahudi. Katika njozi, malaika alimwambia kwamba sala zake zilikuwa “zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” Hata ingawa Kornelio hakuwa amejiweka wakfu kwa Yehova wakati huo, alipokea jibu kwa sala yake. Lakini kama vile malaika alivyoelekeza, yeye alipeleka utume ili Petro akaitwe.
15. Ni jambo gani lililotukia Petro alipokuwa akisali juu ya dari ya nyumba ya Simoni?
15 Wakati uo huo, Petro alikuwa na njozi alipokuwa akisali juu ya dari ya nyumba ya Simoni. (10:9-23) Katika usingizi wenye njozi, aliona chombo kama shuka kikishuka kutoka mbinguni kimejaa viumbe wachafu wenye miguu minne, vitu vitambaaji, na ndege. Alipoagizwa achinje na kula, Petro alisema hakuwa amepata kula chochote kilicho najisi. “Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi,” akaambiwa. Njozi hiyo ilimfadhaisha Petro, lakini alifuata mwelekezo wa roho. Hivyo, yeye na ndugu sita Wayahudi waliandamana na wajumbe wa Kornelio.—Matendo 11:12.
16, 17. (a) Petro aliwaambia nini Kornelio na wale waliokusanyika kwenye nyumba yake? (b) Ni jambo gani lililotukia Petro alipokuwa bado akinena?
16 Sasa watu wa kwanza Wasio Wayahudi walikuwa karibu kusikia habari njema. (10:24-43) Petro na washirika wake walipowasili katika Kaisaria, Kornelio, watu wa ukoo wake, na rafiki walio wandani zake walikuwa wakingoja. Kornelio alianguka miguuni pa Petro, lakini kwa unyenyekevu mtume akakataa kusujudiwa hivyo. Alisema juu ya jinsi Yehova alivyompaka Yesu mafuta kwa roho takatifu na nguvu awe Mesiya na akaeleza kwamba kila mtu mwenye kutia imani katika huyo hupata msamaha wa dhambi.
17 Sasa Yehova akachukua hatua. (10:44-48) Petro alipokuwa angali anasema, Mungu aliwapa roho takatifu waamini hao Wasio Wayahudi. Papo hapo, wakazaliwa na roho ya Mungu na kuvuviwa waseme lugha za kigeni na kumtukuza yeye. Kwa hiyo, kwa kufaa walibatizwa katika jina la Yesu Kristo. Ndivyo ikawa kwamba Petro alitumia ufunguo wa tatu kuwafungulia wenye kuhofu Mungu Wasio Wayahudi mlango wa maarifa na wa fursa ya kuingia katika Ufalme wa kimbingu.—Mathayo 16:19.
18. Ndugu Wayahudi waliitikiaje Petro alipoeleza kwamba Wasio Wayahudi ‘walibatizwa kwa roho takatifu’?
18 Baadaye, katika Yerusalemu, wenye kuunga mkono tohara walishindana na Petro. (11:1-18, NW) Alipoeleza jinsi Wasio Wayahudi ‘walivyobatizwa kwa roho takatifu,’ ndugu zake Wayahudi walikubali kuacha maoni yao wakamtukuza Mungu, wakisema: “Haya, basi, Mungu ametunukia toba kwa kusudi la uhai kwa watu wa mataifa pia.” Sisi pia twapaswa kuwa waitikivu tueleweshwapo mapenzi ya kimungu.
Kundi la Wasio Wayahudi Laanzishwa
19. Ilikuwaje wanafunzi wakaja kuitwa Wakristo?
19 Sasa kundi la kwanza la Wasio Wayahudi likaanzishwa. (11:19-26, NW) Wanafunzi walipotawanywa na dhiki iliyotokea juu ya Stefano, watu fulani walienda Antiokia, Siria, iliyojulikana sana kwa ibada chafu na ufisadi wa maadili. Walipokuwa wakisema habari njema kwa watu wenye kusema Kigiriki huko, “mkono wa Yehova ulikuwa pamoja nao,” na wengi wakawa waamini. Barnaba na Sauli walifundisha huko kwa mwaka mmoja, na “ilikuwa kwanza katika Antiokia kwamba wanafunzi wakaitwa Wakristo kwa majaliwa ya kimungu.” Bila shaka Yehova alielekeza kwamba waitwe hivyo, kwa kuwa neno la Kigiriki khre·ma·tiʹzo humaanisha “kuitwa kwa majaliwa ya kimungu” na sikuzote hutumiwa Kimaandiko kuhusiana na kitokacho kwa Mungu.
20. Agabo alitabiri nini, na kundi la Antiokia liliitikiaje?
20 Pia manabii wenye kuhofu Mungu walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. (11:27-30) Mmoja alikuwa Agabo, alionyesha “kupitia roho kwamba njaa kubwa ilikuwa karibu kuja juu ya dunia nzima yenye kukaliwa.” Unabii huo ulitimizwa wakati wa utawala wa Klaudio maliki Mroma (41-54 W.K.), na mwa-nahistoria Yosefo hurejezea “njaa kubwa” hii. (Jewish Antiquities, XX, 51 [ii, 5]; XX, 101 [v, 2]) Kwa kusukumwa na upendo, kundi la Antiokia lilipeleka mchango kwa ndugu wahitaji katika Yudea.—Yohana 13:35.
Mnyanyaso Ni wa Bure Tu
21. Ni hatua gani ambayo Herode Agripa I alichukua dhidi ya Petro, lakini tokeo likiwa nini?
21 Kipindi cha amani kilimalizika Herode Agrippa I alipoanza kunyanyasa wenye kuhofu Yehova katika Yerusalemu. (12:1-11) Herode alimwondolea mbali Yakobo kwa upanga, labda akamkata kichwa akiwa ndiye mtume wa kwanza kufia imani. Kwa kuona kwamba jambo hilo liliwapendeza Wayahudi, Herode alimtia Petro gerezani. Yaonekana mtume alifunganishwa na askari kila upande kwa mnyororo, huku wengine wakilinda seli yake. Herode alipanga kumwua baada ya Sikukuu-Kupitwa na siku za keki zisizochachishwa (Nisani 14-21), lakini sala za kundi kwa ajili yake zikajibiwa kwa wakati ufaao kabisa, kama vile zetu zijiwabavyo mara nyingi. Hilo lilitukia malaika wa Mungu alipomweka mtume huru kimwujiza.
22. Ni nini lililotukia Petro alipoenda kwenye nyumba ya mama ya Marko, Mariamu?
22 Muda si muda Petro akawa nyumbani kwa Mariamu (mama ya Yohana Marko), ambapo yaonekana palikuwa mahali pa mikutano ya Kikristo. (12:12-19) Akiwa gizani, kijakazi Roda alitambua sauti ya Petro lakini akamwacha kwenye mwingilio wa lango lililofungwa. Kwanza huenda ikawa wanafunzi walifikiri kwamba Mungu alikuwa ametuma mjumbe wa kimalaika mwenye kuwakilisha Petro na kusema kwa sauti kama yake. Hata hivyo, walipokubali Petro aingie ndani aliwaambia wakaripoti kwa Yakobo na akina ndugu (labda wazee) juu ya kukombolewa kwake. Ndipo akaondoka na kwenda zake siri-siri bila kufunua alikokuwa akielekea ili kuepuka kuhatarisha wao au yeye mwenyewe iwapo angeulizwa-ulizwa maswali. Herode hakufua dafu kwa kumtafuta Petro, na walinzi waliadhibiwa, labda hata wakauawa.
23. Utawala wa Herode Agrippa I ulimalizikaje, nasi twaweza kujifunza nini kutokana na hilo?
23 Katika 44 W.K. utawala wa Herode Agrippa I ulimalizika kwa ghafula katika Kaisaria alipokuwa na umri wa miaka 54. (12:20-25, NW) Alikuwa katika mori wa kupigana dhidi ya Wafoenike wa Tiro na Sidoni, waliohonga Blasto mtumishi wake ili apange kikao ambacho wangeweza kukubali matakwa ya amani. Katika “siku iliyowekwa” (pia ikiwa ni msherehekeo wa kuheshimu Kaisari Klaudio), Herode alijivika nguo za kifalme, akakalia kiti cha hukumu, na kuanza kutoa hotuba ya watu wote. Kwa kuitikia, wasikilizaji wakapaaza sauti hivi: “Sauti ya mungu, wala si ya mwanadamu!” Papo hapo, malaika wa Yehova akampiga “kwa sababu hakumpa Mungu utukufu.” Herode ‘aliliwa na funza akatokwa na pumzi.’ Kielelezo hiki chenye onyo na kitusukume tuendelee kutembea katika hofu kwa Yehova, tukiepuka kiburi kabisa na kumpa yeye utukufu kwa mambo ambayo sisi hufanya tukiwa watu wake.
24. Makala ya wakati ujao itaonyesha nini kuhusu mpanuko?
24 Mnyanyaso ujapoletwa na Herode, “neno la Yehova liliendelea kukua na kuenea.” Kwa uhakika, kama vile makala ya wakati ujao itakavyoonyesha, wanafunzi wangeweza kutarajia mpanuko zaidi. Kwa nini? Kwa sababu ‘walitembea katika hofu kwa Yehova.’
Wewe Ungejibuje?
◻ Stefano alionyeshaje kwamba alihofu Yehova, kama vile wengi wa watumishi wa Mungu wamefanya tangu wakati huo?
◻ Kifo cha Stefano kilikuwa na tokeo gani juu ya utendaji wa kuhubiri Ufalme, na je! hilo lina ulinganifu wa ki-siku-hizi?
◻ Mnyanyasi Sauli wa Tarso alikujaje kuwa mwenye kuhofu Yehova?
◻ Waamini wa kwanza Wasio Wayahudi walikuwa nani?
◻ Matendo sura ya 12 huonyeshaje kwamba mnyanyaso hauzuii wenye kuhofu Yehova?
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Mwangaza ulimweka kutoka mbinguni na sauti ikauliza: “Sauli, mbona unaninyanyasa?”