Watu wa Yehova Waimarishwa Katika Imani
“Makundi yakaendelea kufanywa imara katika imani na kuongezeka hesabu siku kwa siku.”—MATENDO 16:5, NW.
1. Mungu alimtumiaje mtume Paulo?
YEHOVA MUNGU alimtumia Sauli wa Tarso kama “chombo kiteule.” Akiwa mtume Paulo, ‘aliteswa kwa mengi.’ Lakini kupitia kazi yake na ya wengine, tengenezo la Yehova liliona shangwe ya kuwa na umoja na mpanuko mzuri ajabu.—Matendo 9:15, 16.
2. Kwa nini litakuwa jambo la manufaa kufikiria Matendo 13:1–16:5?
2 Watu Wasio Wayahudi walikuwa wakiwa Wakristo kwa hesabu zenye kuongezeka, na mkutano muhimu wa baraza lenye kuongoza ulisaidia sana kuendeleza mwungamano miongoni mwa watu wa Mungu na kuwaimarisha katika imani. Itanufaisha sana kufikiria matukio haya na mengine yaliyoandikwa kwenye Matendo 13:1–16:5, kwa maana sasa Mashahidi wa Yehova wanapata ukuzi na baraka za kiroho za jinsi hiyo. (Isaya 60:22) (Katika funzo la faragha la makala ambazo zahusu Matendo katika toleo hili, twadokeza kwamba wewe usome vifungu vitokavyo katika kitabu hicho ambavyo vimeonyeshwa kwa herufi nyeusi.)
Wamisionari Wafanya Kitendo
3. Ni kazi gani iliyofanywa na “manabii na walimu” huko Antiokia?
3 Wanaume waliotumwa nje na kundi katika Antiokia, Siria (Shamu), walisaidia waamini kuwa imara katika imani. (13:1-5) Katika Antiokia walikuwamo “manabii na waalimu” Barnaba, Simeoni (Nigeri), Lukio wa Kirene, Manaeni, na Sauli wa Tarso. Manabii walieleza Neno la Mungu na wakatabiri matukio, hali walimu walitoa maagizo katika Maandiko na katika maisha ya kumcha Mungu. (1 Wakorintho 13:8; 14:4) Barnaba na Sauli walipokea mgawo maalumu. Wakimchukua Marko binamu ya Barnaba, walienda Saiprasi (Kipro). (Wakolosai 4:10) Walihubiri katika masinagogi katika bandari ya mashariki ya Salami, lakini hakuna maandishi ya kuonyesha kwamba Wayahudi waliitikia vema. Kwa kuwa watu wa jinsi hiyo walikuwa na hali nzuri ya vitu vya kimwili, mbona wamhitaji Mesiya?
4. Ilitendeka nini wamisionari walipoendelea kuhubiri katika Saiprasi (Kipro)?
4 Mungu alibariki kazi nyingine ya ushahidi katika Saiprasi. (13:6-12, NW) Huko Pafo, wamisionari hao walikabili yule mchawi Myahudi aliye nabii bandia Bar-Yesu (Elima). Alipojaribu kuzuia Liwali Sergio Paulo asisikie neno la Mungu, Sauli alijawa na roho takatifu akasema: ‘Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, ewe mwana wa Ibilisi, ewe adui wa kila lililo la uadilifu, je! hutaacha kuzipotosha njia zifaazo za Yehova?’ Kisha, mkono wa Mungu wa adhabu ukampofusha Elima kwa muda, na Sergio Paulo “akawa mwamini, kwa kuwa alistaajabia fundisho la Yehova.”
5, 6. (a) Paulo alipohutubu katika sinagogi huko Antiokia ya Pisidia, alisema nini juu ya Yesu? (b) Hotuba ya Paulo ilikuwa na tokeo gani?
5 Kutoka Saiprasi, kikundi hicho kiling’oa nanga kwenda jiji la Perga katika Esia Ndogo. Halafu Paulo na Barnaba wakaenda upande wa kaskazini kupitia vipito vya milima, yaelekea ni ‘katika hatari kutoka kwenye mito na waotea-njiani,’ hadi Antiokia, Pisidia. (2 Wakorintho 11:25, 26, NW) Huko Paulo akahutubu katika sinagogi. (13:13-41) Alipitia habari za mishughuliko ya Mungu pamoja na Israeli na kumtambulisha Yesu mzao wa Daudi kuwa ndiye Mwokozi. Ingawa watawala Wayahudi walikuwa wametaka Yesu auawe, ahadi iliyofanywa kwa babu zao ilitimizwa Mungu alipomfufua. (Zaburi 2:7; 16:10; Isaya 55:3) Paulo alionya wasikiaji wake wasidharau zawadi ya Mungu ya wokovu kupitia Kristo.—Habakuki 1:5, Septuagint.
6 Hotuba ya Paulo iliamsha upendezi, kama vile zifanyavyo hotuba za watu wote zitolewazo na Mashahidi wa Yehova leo. (13:42-52, NW) Katika Sabato iliyofuata karibu jiji lote lilikusanyika kusikia neno la Yehova, na hiyo ikawajaza Wayahudi wivu. Naam, katika juma moja tu, yaonekana Wamisionari hao walikuwa wamegeuza watu wengi zaidi Wasio Wayahudi kuliko wale waliogeuzwa na Wayahudi hao muda wa maisha yao yote! Kwa kuwa Wayahudi hao walimpinga Paulo kwa makufuru, ulikuwa wakati wa nuru ya kiroho kung’aa mahali pengine, nao wakaambiwa hivi: ‘Kwa kuwa mnalitupilia mbali neno la Mungu na hamjihukumu wenyewe kuwa mwastahiki uhai wa milele, sisi twageukia mataifa.’—Isaya 49:6.
7. Paulo na Barnaba waliitikia mnyanyaso jinsi gani?
7 Sasa Wasio Wayahudi walianza kushangilia, na wote wale wenye mwelekeo ufaao kwa uhai wa milele wakawa waamini. Hata hivyo, neno la Yehova lilipokuwa likipelekwa sehemu zote za nchi, Wayahudi waliwachochea wanawake wenye kusifika (yaelekea ili wabane waume zao au wengine) na wanaume wakuu ili wanyanyase Paulo na Barnaba na kuwatupa nje ya mipaka yao. Lakini hiyo haikuwazuia wamisionari hao. ‘Walikung’uta tu mavumbi katika nyayo dhidi yao’ na kwenda hadi Ikonio (Konya ya ki-siku-hizi), hilo likiwa jiji kuu katika mkoa wa Kiroma wa Galatia. (Luka 9:5; 10:11) Basi, namna gani wanafunzi walioachwa katika Antiokia ya Pisidia? Wakiisha kuimarishwa katika imani, waliendelea ‘kujazwa shangwe na roho takatifu.’ Hiyo yatusaidia kuona kwamba upinzani hauhitaji kuzuia maendeleo ya kiroho.
Imara Katika Imani Kujapokuwa na Mnyanyaso
8. Ni nini lililotendeka kutokana na ushahidi wenye mafanikio katika Ikonio?
8 Paulo na Barnaba wenyewe walithibitika kuwa imara katika imani kujapokuwa na mnyanyaso. (14:1-7) Kwa kuitikia ushahidi wao katika sinagogi katika Ikonio, Wayahudi na Wagiriki wengi wakawa waamini. Wayahudi wasioamini walipochochea Wasio Wayahudi dhidi ya waamini wapya, wafanya kazi hao wawili walisema kijasiri kwa mamlaka ya Mungu, naye akaonyesha kibali chake kwa kuwatia nguvu za kufanya ishara. Hiyo iligawanya wafanya ghasia hao, baadhi yao wakiwa upande wa Wayahudi na wengine upande wa mitume. Mitume hawakuwa waoga, lakini walipopata habari juu ya njama ya kuwapiga kwa mawe, waliondoka kwa hekima ili wakahubiri katika Likaonia, jimbo la Esia Ndogo kusini mwa Galatia. Kwa kuwa wenye busara, mara nyingi sisi pia twaweza kubaki tukiwa watendaji katika huduma kujapokuwa na upinzani.—Mathayo 10:23.
9, 10. (a) Wakaaji wa Listra waliitikiaje kuponywa kwa mwanamume kilema? (b) Paulo na Barnaba waliitikia hali jinsi gani huko Listra?
9 Halafu jiji la Listra la Likaonia likapata ushahidi. (14:8-18) Huko Paulo aliponya mwanamume aliyekuwa kilema tangu kuzaliwa. Bila kung’amua kwamba Yehova ndiye aliyekuwa na daraka la mwujiza huo, umati ukapaaza sauti hivi: “Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu”! Kwa kuwa hilo lilisemwa katika ulimi (lugha) wa Kilikaonia, Barnaba na Paulo hawakujua lililokuwa likitukia. Kwa kuwa Paulo ndiye aliyeongoza katika kusema, watu walimwona kuwa Herme (yule mjumbe mfasaha wa miungu) na kufikiri kwamba Barnaba alikuwa Zeu, mungu mkuu wa Kigiriki.
10 Kuhani wa Zeu hata alileta mafahali (ng’ombe ndume) na makoja ya maua ili kuwatolea Paulo na Barnaba dhabihu. Yaelekea kwamba kwa kusema Kigiriki kilichoeleweka kwa wingi au kwa kutumia mkalimani, wageni hao walieleza haraka kwamba wao pia walikuwa wanadamu wenye udhaifu mbalimbali wa kibinadamu na kwamba walikuwa wakijulisha rasmi habari njema ili watu wageuke kutoka “mambo haya ya ubatili” (miungu au sanamu zisizo na uhai) wamwelekee Mungu aliye hai. (1 Wafalme 16:13; Zaburi 115:3-9; 146:6) Ndiyo, hapo zamani Mungu aliyaruhusu mataifa (lakini si Waebrania) wafuate njia yao wenyewe, ingawa hakujiacha bila ushahidi wa kuwako kwake na wema wake ‘kwa kuwapa mvua na nyakati za mavuno, akishibisha mioyo yao chakula na furaha.’ (Zaburi 147:8) Kujapokuwa na usababu wa jinsi hiyo, Barnaba na Paulo waliuzuia umati kwa shida usiwatolee dhabihu. Hata hivyo, wamisionari hao hawakukubali heshima ya kupita kiasi kuwa miungu, wala hawakutumia mamlaka hiyo kuweka msingi wa Ukristo katika eneo hilo. Hicho ni kielelezo kizuri, hasa ikiwa sisi tuna mbetuko wa kutamani sifa ya kupita kiasi kwa mambo ambayo Yehova huturuhusu tutimize katika huduma yake!
11. Twaweza kujifunza nini kutokana na taarifa hii: “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”?
11 Kwa ghafula, mnyanyaso ukachomoza kwa fujo nyingi. (14:19-28) Jinsi gani? Wakishawishwa na Wayahudi kutoka Antiokia ya Pisidia na Ikonio, umati ukampiga Paulo kwa mawe na kumburuta nje ya jiji, wakifikiri amekufa. (2 Wakorintho 11:24, 25) Lakini wanafunzi walipomzunguka, aliinuka akaingia Listra bila kuonwa, yawezekana wakati wa giza. Siku iliyofuata, yeye na Barnaba wakaenda Derbe, ambako wengi kiasi wakawa wanafunzi. Walipozuru tena Listra, Ikonio, na Antiokia, wamisionari hao waliwaimarisha wanafunzi, wakawatia moyo wabaki katika imani, na kusema: “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.” Sisi Wakristo twatarajia pia kupatwa na dhiki na haitupasi tujaribu kuziepa kwa kuacha matakwa ya imani yetu. (2 Timotheo 3:12) Wakati huo, wazee waliwekwa katika makundi yaliyoandikiwa barua ya Paulo kwa Wagalatia.
12. Ilipomalizika safari ya kwanza ya kimisionari ya Paulo, wamisionari wawili hao walifanya nini?
12 Kwa kupitia Pisidia, Paulo na Barnaba wakasema lile neno katika Perge, jiji lenye sifa la Pamfilia. Baada ya muda, wakarudi Antiokia, Siria. Sasa safari ya kwanza ya Paulo ikiwa imemalizika, wamisionari wawili hao wakayapasha makundi habari za “mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani.” Wakati fulani ulitumiwa kuwa pamoja na wanafunzi katika Antiokia, na bila shaka hiyo ilisaidia sana kuwaimarisha katika imani. Ziara za waangalizi wanaosafiri leo zina matokeo ya kiroho kama hayo.
Suala Muhimu Latatuliwa
13. Ikiwa Ukristo haungegawanyika uwe vikundi viwili vyenye kufarakana vya Waebrania na wasio Wayahudi, ni nini kilichohitajiwa?
13 Uimara katika imani ulihitaji mwungamano wa wazo. (1 Wakorintho 1:10) Ikiwa Ukristo haungegawanyika uwe vikundi vyenye kufarakana vya Waebrania na watu Wasio Wayahudi, baraza lenye kuongoza lilihitaji kuamua kama ilikuwa au haikuwa lazima watu Wasio Wayahudi wenye kumiminika ndani ya tengenezo la Mungu washike Sheria ya Musa na kutahiriwa. (15:1-5) Wanaume fulani kutoka Yudea walikuwa tayari wamesafiri hadi Antiokia ya Siria na wakawa wameanza kufundisha waamini Wasio Wayahudi huko kwamba wasipotahiriwa, hawange-weza kuokolewa. (Kutoka 12:48) Kwa hiyo, Paulo, Barnaba, na wengine walitumwa kwa mitume na wazee katika Yerusalemu. Hata huko, waamini ambao hapo kwanza walikuwa Mafarisayo wenye akili za kufuatilia miandiko ya sheria walisisitiza kwamba ilikuwa lazima Wasio Wayahudi watahiriwe na kuishika Sheria.
14. (a) Ingawa kubishana kulitukia mkutanoni katika Yerusalemu, ni kielelezo gani chema kilichowekwa? (b) Ni nini kilichokuwa kiini cha usababu wa Petro katika pindi hiyo?
14 Mkutano ulifanywa ili kuhakikisha mapenzi ya Mungu. (15:6-11, NW) Ndiyo, kubishana kulitukia, lakini hakukuwa na ugomvi wakati wanaume wenye masadikisho imara walipokuwa wakieleza maoni yao—kielelezo kizuri kwa wazee leo! Baada ya muda Petro akasema: ‘Mungu alichagua kwamba kupitia kinywa changu Wasio Wayahudi [kama Kornelio] wasikie habari njema na kuamini. Alitoa ushahidi kwa kuwapa wao roho takatifu na hakufanya upambanufu kati yetu na wao. [Matendo 10:44-47] Kwa hiyo mbona nyinyi mnamtahini Mungu kwa kuweka nira juu ya shingo yao [wajibu wa kuishika Sheria] ambayo wala sisi wala babu zetu hawangeweza kuihimili? Sisi [Wayahudi kulingana na mnofu] twatumaini kuokolewa kupitia fadhili zisizostahiliwa za Bwana Yesu kwa njia ile ile kama watu hao.’ Ukubali wa Mungu wa watu wasiotahiriwa Wasio Wayahudi ulionyesha kwamba tohara na kushika Sheria hayakuwa matakwa ya wokovu.—Wagalatia 5:1.
15. Ni mambo gani ya msingi aliyoyatoa Yakobo, naye alidokeza kuwaandikia nini Wakristo Wasio Wayahudi?
15 Kundi lilinyamaza Petro alipomalizia, lakini mengi zaidi yangesemwa. (15:12-21) Barnaba na Paulo walisimulia juu ya ishara ambazo Mungu alifanya kupitia kwao miongoni mwa Wasio Wayahudi. Yakobo ndugu-nusu wa Yesu, akiwa ndiye mwenyekiti wakati huo, alisema hivi: ‘Simeoni [jina la Petro la Kiebrania] ameeleza jinsi Mungu alivyogeuza uangalifu wake kuelekea mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.’ Yakobo alionyesha kwamba kujengwa tena kwa “nyumba ya [kibanda cha, NW] Daudi” (kusimamishwa tena kwa umaliki katika ukoo wa Daudi) kulikuwa kukitimizwa kwa mkusanyo wa wanafunzi wa Yesu (warithi wa Ufalme) kutoka miongoni mwa Wayahudi na Wasio Wayahudi pia. (Amosi 9:11, 12, Septuagint; Warumi 8:17) Kwa kuwa ni Mungu aliyekusudia hilo, wanafunzi wapaswa kulikubali. Yakobo alishauri kuwaandikia Wakristo Wasio Wayahudi ili washike mwiko wa (1) vitu vyenye kuchafuliwa kwa sanamu, (2) uasherati, (3) damu na kitu kilichonyongwa. Makatazo haya yalikuwa katika miandiko ya Musa iliyosomwa katika masinagogi kila siku ya Sabato.—Mwanzo 9:3, 4; 12:15-17; 35:2, 4.
16. Barua ya baraza lenye kuongoza la karne ya kwanza hutoa mwongozo juu ya mambo gani matatu hadi leo hii?
16 Baraza lenye kuongoza sasa lilipeleka barua kwa Wakristo wasio Wayahudi katika Antiokia, Siria, na Kilikia. (15:22-35, NW) Roho takatifu na waandikaji wa barua hiyo waliitisha kushika mwiko wa vitu vilivyodhabihiwa kwa sanamu; damu (yenye kuliwa kwa ukawaida na watu fulani); vitu vilivyonyongwa bila kuondoa damu yavyo (wapagani wengi waliiona nyama ya jinsi hiyo kuwa mlo maalumu); na uasherati (Kigiriki, por·neiʹa, likimaanisha ngono haramu nje ya ndoa ya Kimaandiko.) Kwa kushika mwiko hivyo, wangefanikiwa kiroho, kama vile Mashahidi wa Yehova wafanikiwa sasa kwa sababu wao hufuata “mambo haya ya lazima.” Maneno “Afya njema kwenu!” yalikuwa ni sawa na kusema “Wasalamu,” na haipasi kukatwa shauri kwamba kwa msingi matakwa haya yalihusiana na hatua za kiafya. Barua hiyo iliposomwa katika Antiokia, kundi lilishangilia kitia-moyo ilichoandaa. Wakati huo, watu wa Mungu katika Antiokia waliimarishwa pia katika imani na maneno yenye kutia moyo ya Paulo, Sila, Barnaba, na wengine. Sisi pia na tutafute njia za kuwatia moyo na kuwajenga waamini wenzetu.
Safari ya Pili ya Kimisionari Yaanza
17. (a) Ni tatizo gani lililotokea wakati safari ya pili ya kimisionari iliponuiwa? (b) Paulo na Barnaba walishughulikiaje ubishi wao?
17 Tatizo fulani lilitokea wakati safari ya pili ya kimisionari iliponuiwa. (15:36-41, NW) Paulo alidokeza kwamba yeye na Barnaba wazuru tena makundi katika Saiprasi na Esia Ndogo. Barnaba alikubali lakini akataka waende pamoja na Marko binamu yake. Paulo hakukubali kwa sababu wakiwa katika Pamfilia Marko alikuwa amewaacha akaenda zake. Ndipo “mfoko mkali wa kasirani” ukatukia. Lakini wala Paulo wala Barnaba hawakutafuta kuthibitisha haki yao binafsi kwa kujaribu kuhusisha wazee wengine au baraza lenye kuongoza katika jambo lao la faraghani. Ni kielelezo kizuri kama nini!
18. Mtengano wa Paulo na Barnaba ulikuwa na tokeo gani, nasi twaweza kunufaikaje na kituko hicho?
18 Hata hivyo, ubishi huu ulisababisha mtengano. Barnaba alimchukua Marko wakaenda pamoja Saiprasi. Paulo, pamoja na Sila akiwa mshirika wake, “walipitia Siria na Kilikia, wakiyaimarisha makundi.” Huenda Barnaba akawa alivutwa na mahusiano ya kifamilia, lakini angalipaswa kuukubali utume na uteule wa Paulo kuwa “chombo kichaguliwa.” (Matendo 9:15, NW) Namna gani sisi? Kisa hicho chapasa kutukazia uhitaji wa kutambua mamlaka ya kitheokrasi na kufanya ushirikiano kamili na “mtumwa mwaminifu mwenye akili”!—Mathayo 24:45-47.
Maendeleo Katika Amani
19. Vijana Wakristo wa kisasa wana kielelezo gani katika Timotheo?
19 Ubishi huu haukuruhusiwa uathiri amani ya kundi. Watu wa Mungu waliendelea kuimarishwa katika imani. (16:1-5, NW) Paulo na Sila walienda Derbe na kusonga mbele hadi Listra. Huko aliishi Timotheo, mwana wa yule mwamini Myahudi Eunike na mume wake Mgiriki asiyeamini. Timotheo alikuwa mchanga, kwa maana hata miaka 18 au 20 baadaye, bado aliambiwa hivi: “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako.” (1 Timotheo 4:12) Kwa kuwa “aliripotiwa vema na akina ndugu katika Listra na [umbali wa kilometa kama 29 katika] Ikonio,” alijulikana vema kwa huduma yake nzuri na sifa za kimungu. Vijana Wakristo leo wapaswa kutafuta msaada wa Yehova ili wajenge sifa nzuri kama hiyo. Paulo alimtahiri Timotheo kwa sababu wangekuwa wakienda kwenye nyumba na masinagogi ya Wayahudi waliojua kwamba baba ya Timotheo alikuwa mtu asiye Myahudi, na mtume hakutaka lolote la kuzuia kuwafikia wanaume na wanawake Wayahudi waliohitaji kujifunza juu ya Mesiya. Bila kuvunja kanuni za Biblia, leo pia Mashahidi wa Yehova hufanya wawezayo ili kufanya habari njema zikubalike kwa namna zote za watu.—1 Wakorintho 9:19-23.
20. Kufuata barua ya baraza lenye kuongoza la karne ya kwanza kulikuwa na tokeo gani, nawe wafikiri jambo hili lapasa kutuathirije sisi?
20 Huku Timotheo akiwa hadimu, Paulo na Sila waliwapelekea wanafunzi maagizo ya baraza lenye kuongoza ili wayashike. Na tokeo likawa nini? Luka aliandika hivi, yaonekana akirejezea Siria, Kilikia, na Galatia: “Makundi yakaendelea kufanywa imara katika imani na kuongezeka hesabu siku kwa siku.” Ndiyo, kufuata barua ya baraza lenye kuongoza kulitokeza mwungamano na ufanisi wa kiroho. Lo, ni kielelezo kizuri kama nini kwa nyakati zetu za hatari, ambapo watu wa Yehova wahitaji kubaki wakiwa wameungamana na kuwa imara katika imani!
Wewe Ungejibuje?
◻ Paulo na Barnaba waliitikiaje mnyanyaso?
◻ Kwaweza kuwa na somo gani kutokana na taarifa hii: “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”?
◻ Twapata shauri gani kutokana na yale mambo matatu yaliyo katika barua iliyopelekwa na baraza lenye kuongoza la karne ya kwanza?
◻ Mambo yaliyoimarisha mashahidi wa Yehova wa karne ya kwanza yatumikaje kwetu leo?