Kwa Nini Sisi Twahitaji Maarifa Sahihi
“Ndiyo sababu sisi pia, tangu siku ile tulipoyasikia hayo, hatujaacha kutoa sala kwa ajili yenu na kuomba kwamba mjawe na maarifa sahihi ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa kiroho.”—WAKOLOSAI 1:9, NW.
1. Toa kielezi cha tofauti kati ya maarifa ya ujumla tu na yale yaliyo sahihi.
KARIBU kila mmoja ajua saa ya mkononi, lakini ni wangapi ambao wajua jinsi yafanya kazi? Huenda ukawa una wazo la ujumla tu kuhusu jinsi yafanya kazi, lakini je! wewe ungeweza kutenganisha-tenganisha sehemu za saa, uitengeneze, na kuiunganisha tena? Hakika mtengeneza saa angeweza kufanya hivyo. Kwa nini? Kwa sababu ana maarifa mapana yaliyo sahihi kuhusu jinsi saa ya mkononi hufanya kazi. Na hiyo yatoa kielezi juu ya tofauti iliyopo kati ya maarifa ya ujumla tu na yale yaliyo sahihi kuhusu habari fulani.
2. Umeona tofauti gani kati ya aina hizo mbili za maarifa katika uwanja wa dini?
2 Mamilioni ya watu wana wazo la ujumla tu kuhusu Mungu. Wao husema kwamba wana imani katika Mungu, ingawa mara nyingi vitendo vyao huonyesha dai lao kuwa uwongo. Nyakati fulani misionari mmoja alikuwa akiuliza mwenye-nyumba hivi: “Kwa kuwa wewe ni Mkatoliki, ni lazima uwe unaamini katika Mungu, sivyo?” Na jibu lililokuwa likitolewa, kwa ishara yenye kuelekezwa kwenye mbingu, ni hili: “Eeh, mimi naamini kwamba ni lazima kuwe kuna mtu fulani kule juu.” Je! wewe ungeyaita hayo kuwa maarifa sahihi na ufahamu mpana juu ya Mungu? Sivyo. Na mara nyingi tokeo la ufahamu huo wa kijuu-juu tu ni kwamba mwenendo wa wale wanaodai kuwa ni Wakristo si wa Kikristo. (Linganisha Tito 1:16.) Hali yenye kutokezwa na jambo hilo iko kama ilivyoelezwa na Paulo: “Kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa.”—Warumi 1:28.
3. Tokeo huwa nini watu wakataapo maarifa sahihi kuhusu penzi la Mungu?
3 Ukosefu huo wa maarifa sahihi ulitokeza nini katika karne ya kwanza? Watu walikuwa wanafanya “yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema.” Ukosefu wao wa maarifa sahihi ulimaanisha kwamba mioyo yao haikuwa na msukumo wa kuelekea vitendo vyenye uadilifu.—Warumi 1:28-31; Mithali 2:2, 10.
Tofauti Ni Nini?
4, 5. Kulingana na wanachuo Wagiriki, ni baadhi ya tofauti gani zilizopo kati ya gno·sis na e·piʹgno·sis?
4 Tofauti hii kati ya maarifa ya ujumla tu na yale yaliyo sahihi yadokezwa katika Maandiko ya Kigiriki. Kigiriki cha awali hunena juu ya gnoʹsis, maarifa, na E·piʹgno·sis, maarifa sahihi. Neno lile la kwanza, kulingana na mwanachuo Mgiriki W. E. Vine, lamaanisha “hasa kutafuta kujua, kuulizia-ulizia mambo, kukagua,” zaidi sana kuhusu ukweli wa kiroho wa habari za Maandiko.”
5 E·piʹgno·sis, kulingana na Thayer mwana-chuo Mgiriki, lamaanisha “maarifa sahihi yaliyo sawasawa kabisa.” Na katika namna ile ya kitenzi, lamaanisha “kuzoeana kikamili kabisa na kitu, kujua kikamili kabisa; kujua kwa usahihi, kujua vyema.” W. E. Vine ataarifu kwamba e·piʹgno·sis, “laonyesha maarifa yaliyo barabara au maarifa kamili, utambuzi, upambanuzi.” Yeye aongeza kwamba latoa maana ya “utambuzi, upambanuzi, wenye maarifa kamili zaidi au yaliyo kamili, kushiriki kwa mjuaji kwa kadiri kubwa zaidi katika jambo alijualo, kwa njia hiyo likimtolea uvutano kwa nguvu nyingi zaidi.” (Italiki ni zetu.) Kama tutakavyoona, usemi huu wa mwisho ni muhimu sana kwa Mkristo.
6. Ni waandikaji gani wa Biblia hutumia maneno ya kusema “maarifa” na “maarifa sahihi,” na kwa nini maarifa sahihi ni ya maana?
6 Ni waandikaji wawili tu wa Biblia ambao hutumia neno la Kigiriki e-piʹgno-sis. Wao ni Paulo na Petro, ambao hutumia neno hilo jumla ya mara 20.a Mbali na Luka, wao tu ndio hutumia lile neno gnoʹsis, huku Paulo akilitumia mara 23 na Petro 4. Kwa hiyo miandiko yao ni mwongozo wenye thamani kubwa kuhusu umaana wa kuwa na maarifa sahihi kwa tazamio la kupata wokovu. Kama vile Paulo alivyotaarifu kwa Timotheo: “Hili ni jema na lakubalika machoni pa Mwokozi wetu, Mungu, ambaye mapenzi yake ni kwamba namna zote za watu waokolewe na kuja kwenye maarifa yaliyo sahihi ya ukweli.” —1 Timotheo 2:3, 4, NW.
Kwa Nini Maarifa Sahihi Ni ya Maana
7. (a) Ili yawe yenye thamani, ni lazima maarifa yatuathiri sisi jinsi gani? (b) Kuna hatari gani tusipojali kuwa na maarifa?
7 Kwa hiyo, kupata maarifa sahihi ya ukweli kama yafundishwavyo katika Biblia ni ufunguo mmoja wa kupata wokovu. Hata hivyo, ni lazima maarifa hayo yaufikie moyo, kile kiti cha msukumo. Hilo haliwezi kuwa jambo la kujaza-jaza maarifa au masomo akilini bila matendo. Zaidi ya hilo, maarifa ya ukweli yakiisha kupatwa ni lazima yatumiwe na kujaziwa-jaziwa. Kwa nini? Kwa sababu kumbukumbu lingeweza kuwa dhaifu na lenye kasoro kama musuli usiotumiwa, na hapo sisi tungeweza kwa urahisi kuachilia hali yetu ya kiroho na kuanza kupeperuka na kuyumba-yumba katika imani yetu. Tungeweza kupoteza mshiko wetu imara juu ya “maarifa hususa kuhusu Mungu.” Muda si muda, kuyumba-yumba huku kungeweza kuonekana katika uwezo mnyonge wa kufikiri na hata mwenendo usio wa Kikristo.—Mithali 2:5, NW; Waebrania 2:1.
8. Sulemani aliona thamani gani katika hekima na maarifa?
8 Basi, twathamini ni kwa nini wakati Sulemani alipokuwa mwaminifu alithamini sana hekima, utambuzi, na uwezo wa kufikiri. Yeye aliandika hivi: “Wakati hekima iingiapo ndani ya moyo wako na maarifa yenyewe yawapo yenye kufurahisha nafsi yako hususa, uwezo wenyewe wa kufikiri utaendelea kulinda juu yako wewe, utambuzi wenyewe utakulinda wewe salama, kukukomboa wewe kutoka kwenye njia iliyo mbaya.”b (Mithali 2:10-12, NW) Maneno haya yadokeza kwamba ni lazima tukuze tamaa yenye juhudi ya kutafuta maarifa sahihi, ambayo yaweza kuathiri moyo na nafsi yenyewe. Zaidi ya hilo, huo ni msingi wa kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri. Na kwa nini huo ni wa maana sana leo?
9. Ni nani walio baadhi ya maadui wa hali ya kiroho ya Kikristo?
9 Tunaishi katika “siku za mwisho” ambapo, kama vile Paulo alivyosema katika unabii, ‘zimekuja nyakati za mkazo’ au “wakati wa matata.” (2 Timotheo 3:1, Revised Standard Version; The New English Bible) Inaendelea kuwa vigumu zaidi na zaidi kudumisha uaminifu wetu wa kimaadili katika ulimwengu huu ulioshuka tabia. Adabu, thamani za kiadili, na viwango vya Kikristo hudharauliwa sana na kubezwa. Imani ya Mashahidi wa Yehova yashambuliwa kutoka pande zote —na makasisi wa Jumuiya ya Wakristo wenye kuchukia ujumbe wa Ufalme ambao twapeleka nyumba kwa nyumba, na waasi-imani ambao hufanya njama na makasisi wa Jumuiya ya Wakristo, na wenye mamlaka wa kitiba ambao hutaka kutulazimisha sisi na watoto wetu tutiwe damu mishipani, na wanasayansi ambao hukataa kuamini kwamba kuna Mungu na kwamba vitu viliumbwa, na wale ambao hujaribu kutushurutisha turidhiane nao kuhusu msimamo wetu wa kutokuwamo. Upinzani wote huu hutungamanishwa na Shetani, aliye mtawala wa giza na ujinga, adui wa maarifa sahihi.—2 Wakorintho 4:3-6; Waefeso 4:17, 18; 6:11, 12.
10. Ni mibano gani huenda ikaongezeka dhidi yetu, na twahitaji nini ili kuikinza?
10 Huenda mibano ikaongezeka katika maisha ya kila siku ili kutolea Mkristo uvutano wa kutenda mambo ambayo wengine wanafanya, yawe ni kutumia dawa za kulevya, kunywa bila kiasi, kuzoea ukosefu wa adili na jeuri, kuiba, kusema uwongo, kupunja, kuacha shule, au kutafuta tu maisha ya raha za ubinafsi. Ndiyo sababu maarifa sahihi ni muhimu. Maarifa yaliyo kamili zaidi juu ya Neno na kusudi la Mungu yaweza kutoa uvutano thabiti zaidi ulio na matokeo mazuri juu ya fikira na vitendo vyetu.—Warumi 12:1, 2.
Mwana Mpotevu wa Ki-Siku-Hizi
11, 12. Ni ono gani la maisha halisi ambalo latoa kielezi cha upumbavu wa kukataa maarifa sahihi ya ukweli?
11 Twaweza kuonyesha kielezi cha jambo hili kwa kutoa kisa cha maisha halisi kuhusu mwanamume kijana ambaye upendo wake kuhusu ukweli ulitahiniwa alipokuwa na umri wa karibu miaka 14, tayari akiwa Mkristo aliyebatizwa. Kama ilivyo kuhusu vijana wengi, yeye alipenda michezo, hasa mpira wa miguu. Lakini kulikuwako tatizo. Shule yao ilicheza mpira wa miguu usiku ule ule ambao kundi lilikuwa na mikutano. Hali yake ya kiroho haikuwa imara kiasi cha kutosha kumfanya akadirie kwamba mpira wa miguu ulikuwa wa thamani ya kijuujuu tu ukilinganishwa na thamani yenye kudumu ya kuhudhuria mikutano ya Kikristo pamoja na mama yake mjane na ndugu na dada yake mchanga. Kwa hiyo yeye akaacha kutenda kulingana na maarifa sahihi na kuamua kuuacha ukweli. Hatimaye, alitengwa na ushirika. Baadaye, alisonga mbele na kufanya utumishi wa kijeshi, ambako alihusika na dawa za kulevya.
12 Katika 1986, mwanamume huyu kijana aliruhusiwa kuacha jeshi, akarudiwa na fahamu zake, na kumwandikia barua rafiki mmoja wa jamaa aliyekuwa ametumikia katika halmashauri ya hukumu iliyomtenga na ushirika. Humo alitaarifu hivi: “Nafurahi kuweza kukuambia habari fulani za maana: Mimi nimerudia ukweli. . . . Nimepata kutambua jambo lile ambalo mtume Paulo alisema kwenye 2 Wakorintho 4:4, kwamba kuna mungu wa mfumo huu wa mambo anayepofusha akili. Kwa muda mrefu, mimi nimekuwa kipofu kiroho nikawa siyaoni mambo yaliyokuwa yakitendeka kunizunguka. Nilipoacha ukweli, sikujua nilivyokuwa nikijasiria kuingia hatarini. Lakini asante kwa Yehova Mungu kwamba baada ya muda nimeweza kuthamini waziwazi kwamba nilikosea kufuata mwendo wangu mbaya.”—Linganisha Luka 15:11-24.
13. Ni tokeo gani zuri laweza kuwapata watu fulani ambao wameanguka kando ya njia, ikiwa watatubu kikweli? (2 Timotheo 2:24-26)
13 Mwanamume huyu kijana amerudia kijia cha maarifa sahihi. Sasa yeye aweza ‘kutembea kwa njia ambayo yamstahiki Yehova kwa lengo la kumfurahisha kikamili.’ Yeye aweza pia ‘kuendelea kuzaa tunda katika kila kazi njema na kuongezeka katika maarifa sahihi ya Mungu’ huku akifuatia ushirika pamoja na kundi la Kikristo. Naye amekuwa baraka yenye kuburudisha kama nini kwa jamaa yake kwa kuwa tena mfuasi wa Kristo! Je! wewe wajua vielelezo vingine vya jinsi hiyo?—Wakolosai 1:9, 10, NW; Mathayo 11:28-30.
Matokeo Mabaya Sana ya Kutojali Hali ya Kiroho
14. (a) Ili kuepuka kuangukia mbali, ni lazima tufanye nini? (b) Ni jambo gani limepata Wakristo fulani?
14 Twaweza kujifunza somo gani kutokana na kisa hiki na vingine vya jinsi hii? Kwamba tukiisha kupata maarifa sahihi ya ukweli, twahitaji daima kuwa tukiirekebisha upya mikondo ya kiroho ya fikira zenye kuzunguka akilini mwetu ili tusianguke. Huenda maliasili zetu za kiroho zikadhoofika tukipuuza funzo la kibinafsi na la jamaa, mikutano ya Kikristo, na huduma. Halafu huenda ikawaje? Mkristo ambaye hapo kwanza alikuwa imara huenda akapeperuka awe mbali na imani, labda hata atumbukie katika mwenendo wenye makosa, kama ukosefu wa adili, au ateleze kwenye utelezi wa mashaka na wa kupashwa habari mbaya zenye kumwingiza katika uasi-imani. (Waebrania 2:1; 3:12; 6:11, 12) Kwa upumbavu, watu fulani hata wamerudia mafundisho ya Kibabuloni ya Utatu na kutokufa kwa nafsi!
15. Ni onyo gani ambalo Petro alitoa kuhusu kuangukia mbali?
15 Hakika maneno ya Petro yafaa: “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki [uadilifu, NW], kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.”—2 Petro 2:20-22.
16. (a) Watu fulani wameongozwaje vibaya katika nyakati za majuzi? (b) Wenye kuongozwa vibaya wametumbukia katika vitendo gani vya mwenendo?
16 Mara nyingi wale ambao hukataa maarifa sahihi ya ukweli huchagua kijia cha kujitafutia faida zao wenyewe. Hawakubali tena lile daraka la kuhudhuria mikutano ya Kikristo kwa ukawaida wala kushiriki katika huduma ya nyumba kwa nyumba. Baadhi yao hata hurudia kuvuta sigareti! Wengine huwa wenye furaha kwamba hawalazimiki tena kuwa tofauti kuhusu suala la kutokuwamo kwa Kikristo na utumizi mbaya wa damu. Looo, uhuru gani huo! Sasa wao waweza hata kukipigia kura kimoja cha vyama vya kisiasa vya “hayawani-mwitu.” (Ufunuo 13:1, 7, NW) Hivyo, wakiwa nafsi zenye kuyumba-yumba, baadhi yao hata wamekiacha kile kijia kinyoofu cha maarifa sahihi kwa kutongozwa na kuongozwa vibaya na wale ambao, ‘wajapowaahidia uhuru, wao wenyewe ni watumwa wa uharibifu.’—2 Petro 2:15-19.
17. Kuna hatari gani kwa wale ambao huangukia mbali kutoka maarifa sahihi ya ukweli?
17 Watu hao wasipotubu na kurudia ukweli, wao wajifunua wazi waweze kupatwa na hukumu ambayo Paulo alieleza: “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi [maarifa sahihi, 7 NW] ya ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu kwenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.” Ni jambo lisilo la hekima na la muono mfupi kama nini kuachilia mbali maarifa sahihi kuhusu Yehova Mungu na Kristo Yesu ili kufuata mafundisho ya uasi-imani ya Jumuiya ya Wakristo!—Waebrania 6:4-6; 10-26, 27.
Bidii Pamoja na Maarifa Sahihi
18. Kulingana na Paulo, kwa nini makasisi wa Kiyahudi walishindwa kumkubali Kristo?
18 Kwa uhakika makasisi Wayahudi wa siku ya Paulo walikuwa na maarifa kuhusu Maandiko ya Kiebrania. Lakini je! yalikuwa maarifa sahihi? Je! yaliwavuta kumwelekea Kristo akiwa ndiye Mesiya aliyeahidiwa? Paulo alibisha kwamba wao walikuwa wakishughulikia sana kuthibitisha uadilifu wao wenyewe kwa kutumia Sheria hivi kwamba hawakutaka kujitiisha kwa “Kristo [ambaye] ndiye mwisho wa Sheria.” Kwa hiyo Paulo angeweza kusema hivi juu yao: “Kwa maana mimi natoa ushahidi juu yao kwamba wana bidii kwa ajili ya Mungu; lakini si kulingana na maarifa sahihi.”—Warumi 10:1-4, NW.
19, 20. (a) Twaweza kupataje maarifa sahihi? (b) Ni maswali gani yabakia kujibiwa?
19 Kwa hiyo sisi twaweza kupataje haya maarifa sahihi? Kwa kujifunza kibinafsi na kutafakari, pamoja na kusali na kuhudhuria mikutano. Hiyo yamaanisha kujazia daima nguvu zilizokwisha katika betri zetu za kiroho, kwa njia ya ufananisho. Hatuwezi kuthubutu kutegemea maarifa yale tu tuliyopata tulipokubali ukweli. Ni lazima tuendelee kutwaa chakula kigumu cha kiroho, maarifa sahihi, kwa funzo la kibinafsi lenye kudhamiria mambo kwa bidii. Hivyo shauri la Paulo lafaa: “Chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya. Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na,wa kuwa na imani kwa Mungu . . . Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.”—Waebrania 5:14–6:3.
20 Sasa maswali ni, Ni vyombo gani tulivyo navyo ili kutusaidia tupate maarifa sahihi? Na kwa sababu ya maisha zetu zenye shughuli, ni wakati gani tuwezapo kujifunza Neno la Mungu? Makala inayofuata itazungumza habari hii na nyingine zenye kuhusiana nayo.
[Maelezo ya Chini]
a Kama ilivyoorodheshwa katika Comprehensive Concordance of the New World Translation of the Holy Scriptures, ukurasa 17; pia Filemoni 6 (Ona The Kingdom Interlinear Translation of the Greek Scriptures.).
b Ili kupata uelewevu bora juu ya namna-namna za maana ya maneno “maarifa” (“knowledge”) “uwezo wa kufikiri” (“thinking ability”), “hekima” (“wisdom”), na mengine yenye kupatikana katika Mithali, ona Insight on the Scriptures, Buku 2, kurasa 180, 1094, 1189, kilichopigwa chapa kwa Kiingereza na Watch Tower Bible and Tract Society of New York, Inc.
Maswali ya Kujibu
◻ Ni nini tofauti kati ya “Maarifa” na “maarifa sahihi”?
◻ Kwa nini maarifa sahihi ni ya maana sana katika hizi siku za mwisho?
◻ Watu fulani wangeweza kushawishwaje waanguke mbali kutoka kwenye ukweli?
◻ Petro atupa sisi onyo gani kuhusu kukataa maarifa sahihi?
◻ Ni lazima sisi tufanye nini ili tupate na tudumishe maarifa sahihi?